Waridi wa BBC: 'Nilionywa kutowatuma watoto wa wengine kisa tu sina wangu'

Shamila Mwakinjula

Chanzo cha picha, Shamila Mwakinjula

  • Author, Martha Saranga
  • Nafasi, BBC Dar es Salaam

Kwa muda mrefu sana Shamila Mwakinjula amekuwa akihangaika kupata matibabu na kufanyiwa uchunguzi wa afya yake ya uzazi yeye pamoja na mumewe.

Wataalamu wa afya ya uzazi katika hospitali mbalimbali alizokwenda walimwambia hana tatizo lolote na afya yake ilikuwa njema lakini hakuweza kushika ujauzito.

‘Mume wangu alibahatika kupata watoto nje, basi mwanamke aliyezaa naye alipewa mamlaka yote juu ya kila kitu pale nyumbani’, anasema Shamila.

Hali hiyo ilimfanya kuhangaika sana kutafuta tiba katika sehemu mbalimbali.

”Hakuna tiba ambayo sikujaribu, hospitali, mitishamba, tiba mbadala na hata maombezi katika majumba ya ibada na waganga wa kienyeji’

Alipewa masharti mbalimbali ya ajabu katika kutafuta tiba, anasema: Nilipewa masharti ya kunywa dawa nikiwa chooni au katikati ya umati wa watu kama msibani..yote ni katika kuhangaika tu nipate uzao wa tumbo langu, anaelezea.

Anasema alijitahidi kadiri awezavyo ili apate mtoto kwani aliona kama anadharauliwa.

”Mimi niliambiwa hali yangu ni mgumba niko vizuri katika viungo vyangu vya uzazi lakini siwezi kupata mtoto’’anasema Shamila.

Historia

Shamila Mwakinjula

Chanzo cha picha, Shamila Mwakinjula

Shamila Makwinjula alizaliwa Januari 7, 1973 katika familia ya kawaida huko kijiji cha Mtimbila mkoani Morogoro umbali wa kilomita 200 magharibi mwa jiji kuu la kibiashara la Tanzania, Dar es Salaam.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi hakubahatika kuendelea na elimu ya sekondari.

Alipotimiza umri wa miaka 23 alipata mchumba na kuolewa ndoa ya kwanza, akiwa na furaha na matarajio mengi ikiwemo kupata watoto wanne hadi watano.

‘Unapoenda kwenye ndoa yako unatarajia kabisa uitwe mama wa watoto kwa kadiri Mungu alivyokujaalia, lakini nilishangaa tu miaka inaenda sipati mtoto, baada ya miaka mitatu niliachika’ anaeleza Bi Shamila.

Alifanikiwa kufunga ndoa ya pili mwaka 1995 na alidumu kwa miaka 11, hadi ilipofika mwaka 2006.

”Changamoto ilikuwa kubwa sana nikaachwa tena na tangu hapo niliamua sitaingia tena katika ndoa.’’

Soma pia:

Changamoto ya manyanyaso

Anasema: waliofahamu hali yangu ya kutokupata watoto walikuwa wakininyanyasa kisaikolojia ikiwa ni pamoja na kuonywa kutowatuma watoto wa watu kisa tu sina wangu.

Anasema alizuiwa hadi kutumia baadhi ya vitu ”Ninakumbuka nilipigwa na mume wangu hadi nikazimia kisa nilichukua baiskeli kwenda kuchotea maji”

”Nilihadithiwa kwamba nilibebwa kwenye kitanda cha kamba hadi hospitali kule Malinyi ambako nililazwa wodi ya wagonjwa mahututi’'.

Shamila anaeleza kwamba watu hawajui kuwa ugumba ama kukosa mtoto si kukosa nguvu za kufanya kazi, ama kukosa akili na hapendezwi na unyanyapaa aliokuwa akifanyiwa.

”Nilikuwa nampenda mume wangu sitamani kuachika, nilijikuta natamani kuiba mtoto mchanga Dar es Salaam nirudi naye kijiji kusema nimejifungua”.

Niliachana na uamuzi huo baada ya kuwaza kuwa si kitendo kizuri kuiba mtoto wa mtu, nikajiuliza ingekuwaje kama ningebainika?

Mwaka 2006 alikata tamaa kabisa akasema hataolewa tena wala kutafuta mtoto.

Ilibidi kuwatafuta watu wenye hali kama yake kuunganisha nguvu ili kuionesha jamii unyanyasaji na unyanyapaa kunavyoathiri kisaikolojia.

”Tunaumia na tunatamani kuthaminiwa kwani tunaweza kukosa uzazi lakini tukawa na mchango chanya katika jamii kwa kushiriki katika malezi na shughuli za kiuchumi”.

Alifikiria kuanzisha chama cha wagumba nchini ili kutambulika na kupatiwa stahiki wanazostahili.

”Wapo wenzetu kutokana na kushindwa kupata watoto katika ndoa wamepoteza haki ya kurithi mali walizochuma na waume zao”

Anaelezea kuwa wapo wagumba ambao wamepitia unyanyasaji wa ajabu ikiwemo vipigo na hata kupata ulemavu.

Anasema anakumbuka kipindi alichojitosa kuwania udiwani wa kata yake ‘nilishuhudia watu wakisimama jukwaani na kusema wewe hujazaa hujawahi kuwa na mtoto una machungu gani ya kuweza kutuongoza na kujali?’

Chama cha Wagumba Tanzania

Shamila Mwakinjula

Chanzo cha picha, Shamila Mwakinjula

Wengi walikipokea vizuri kwa nchini Tanzania ambapo wanawake kwa wanaume wamejiunga kutoka mikoa tofauti.

‘'Hadi sasa tupo wagumba na tasa jumla 307,hao saba ni wanaume wagumba ambao nao walikwisha hangaika na kushindwa kupata watoto’'.

Chama hiki pia hufundisha namna ya kuvumilia kama mtu hajapata mtoto na kutothubutu kuwaza kuiba mtoto wa mtu mwingine ili uongope kuwa ni wako.

Anasema chama ni cha tasa na mgumba, mgumba anaweza akazaa kama akipata matibabu sahihi.

Mwingine ni tasa, ambaye hiyo hali anazaliwa nayo ya kutoweza kupata mtoto.

Kupitia hiki chama sasa tunajifunza kujitambua na kujikubali na kuisaidia jamii kwa kuipa elimu iache unyanyapaa.

Anasimulia kwa Mfano ‘’kuna mtu sasa anahitaji mume amechoka upweke lakini akiwaza unyanyapaa anajikuta anaogopa’’

Kupitia chama hiki tunajitahidi kujikwamua kiuchumi kwa shughuli mbalimbali.

Hutumia wataalamu wa Saikolojia kuwasaidia wanawake na wanaume wanaojitokeza kujiunga na chama.

Mafanikio

Bi Shamila anasema anajivunia kujiamini na kuweza kuanzisha chama ili kusaidia wagumba wenzake.

Anasema sasa hivi anafuraha anatamani kuona jamii ikimuunga mkono ili kuwafanya wagumba na tasa walioko kwenye jamii kuwa na furaha kama ilivyo kwa watu wengine.

‘’Napenda kuona wakiishi kwa furaha na hata wakifa, basi wafe wakiwa na furaha’’

Malengo ya baadaye

Shamila Mwakinjula

Bi Shamila anasema anatamani kufungua kituo cha kulea wazee wagumba, ambao wapo na wanaishi katika mazingira magumu kwa sababu tu hawakuwahi kuwa na watoto wa kuwajali na kuwathamini.

‘’Mimi ninasema haya kwa kuwa nimeishi katika vipigo, dharau na kejeli kiasi kwamba sikutamani tena kurudi kwenye ndoa ya namna ile’’ anaeleza.

Ni jambo la kufurahisha kwamba serikali ya Tanzania imetambua tatizo la ugumba kwamba lipo Tanzania, na kuona umuhimu wa kuleta huduma ya upandikizaji.

”Tunafurahi sana kuona wizara ya afya imeahidi kushughulikia hilo, nami ninaomba watusaidie gharama ziwe nafuu na rafiki ili kuwaruhusu kila wanaotamani kupata huduma hiyo wapate”