Waridi wa BBC: 'Sikutaka kuolewa kuhofia kuwa mzigo kwa mume wangu'

ggg

Chanzo cha picha, Neema Ibrahim Chizenga

  • Author, Na Veronica Mapunda
  • Nafasi, BBC Dar es Salaam

Mcheshi aliyejawa na tabasamu kubwa usoni kwake.

Neema Chizenga almaarufu ‘Mama Chai’, mjasiriamali mwenye ulemavu wa mguu, anayepambana kupigania ndoto zake kwa kujituma katika ujasiriamali na kuondokana na utegemezi katika maisha.

Anajulikana zaidi kama ‘Neema Chai’ kutokana na aina ya majani ya chai anayotengeneza, ambayo yamepenya sokoni katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

“Chai yangu mimi si chai ndogo ya kimchezo mchezo mpaka mawaziri wameshakunywa, mpaka Ikulu nimeshapeleka chai yangu,” Neema anaeleza.

Ni mlemavu ambaye kuomba kwake ni mwiko.

“Sipendi kujibweteka na wala sipendi kukaa, nikikaa nakaa kwa machungu sina mtaji lakini sipendi kujitia unyonge kwa sababu ni mlemavu”.

Lakini nyuma ya tabasamu lake, kuna simulizi iliyojaa simanzi kutokana na ulemavu wake alioupata akiwa msichana mdogo mwenye ndoto kubwa.

Familia

”Mimi binafsi sijaolewa ila niliamua kutoolewa”

Neema anasema ana watoto watatu ambao aliwahudumia pekee yake bila msaada wa mzazi mwenzie na aliamua kuishi mwenyewe bila mwenza ili kuepuka usumbufu ambao angempatia mwenza wake kwa kuwa yeye ni mlemavu.

‘’Sikutaka tu kuolewa ila mimi ni kungwi, ninatoa huduma ya somo kwa mabinti ambao wanataka kuolewa.

Unaweza kuniuliza ninafundishaje maisha ambayo siyaishi?

Niligundua kuwa nina kipaji cha kufundisha kama somo na kutoa ushauri ambao wakizingatia wanafanikiwa, na si kama najisifia ila huo ndiyo ukweli wenyewe.

Niligundua kuwa nina kipaji cha kutoa ushauri kwa wasichana kujua namna ya kuishi na mume, usafi na namna ya kumpikia mume na mengine mengi yanayohusu majukumu ya mke.

Maisha kabla ya Ulemavu

Neema alizaliwa mwaka 1984 mkoani Tanga, Tanzania bila ulemavu wowote mwilini na kufanikiwa kupata elimu yake msingi mkoani Tanga hadi alipohitimu elimu ya msingi.

‘’Nilikuwa binti mrembo, mchapakazi na mpenda michezo na kinara wa kuimba shuleni. Kila aliyekuwa karibu yangu alivutiwa na ucheshi wangu.

‘Nilitamani kuwa mfanyabiashara mkubwa lakini ndoto hizo zilianza kufifia baada ya kuanza kupooza kidogo kidogo wakati ninaanza elimu ya sekondari katika shule ya sekondari ya Jangwani Jijini Dar es Salaam.’’

‘’Nilianza kupooza ghafla bila kujua sababu”

Na alipofika kidato cha pili mguu mmoja haukuweza kufanya kazi, hivyo ilimbidi awe anatembea kwa kuchechemea. Mwaka 1999 mguu ulipooza kabisa licha ya kuhangaika kupata matibabu hospitalini bila mafanikio.

“Daktari aliniambia nina kitu kwenye goti, hivyo alipendekeza nifanyiwe upasuaji kukitoa, lakini kabla ya upasuaji goti liligeuka na kufanya kuwa ngumu kufanyiwa upasuaji”

Pamoja na kupata ulemavu, Neema alifanikiwa kumaliza kidato cha nne na kufanikiwa kupangiwa kusoma ualimu lakini hakuwa na matumiani tena.

ggg

Chanzo cha picha, Neema Ibrahim Chizenga

Kukata tamaa

“Nilipoanza kupooza nilikuwa nalia sana, nikawaza sijui nijiue, kitendo cha kutoka nje kilikuwa kinaniumiza sana”

Kukata tamaa ndicho kilichokuwa kichwani mwake, lakini sauti ya aliyekuwa mwalimu mkuu wake akimwambia ulemavu ni sehemu ya maisha kauli ambayo ilimuamsha kutoka usingizini. Maana hata familia yake kuna wakati alikuwa anaona kuwa wamechoka kumhudumia.

Kilikuwa kipindi ambacho binti yeyote anatamani kuonekana mrembo lakini kwake hali ilikuwa tofauti na kulikuwa na ugumu wa kufanya kila kitu.

„”Nianza maisha mapya kabisa, maisha ya utegemezi yalikuwa yananiumiza sana”

Ubunifu waleta sura mpya katika maisha

Kwa sasa Neema anajivunia na kujipambanua kuwa ni mbunifu na mpambanaji ambaye analeta tofauti katika jamii yake.

Alianza kujishugulisha kutengeneza maua, kuandaa mboga ambazo alizisindika na kuweza kudumu hadi mwaka mzima bila kuharibika na utengenezaji wa pilipili. Hadi kufikia hatua ya kufundisha watu wengine jinsi ya kuandaa bidhaa hizo.

Licha ya safari hiyo ya kujaribu kufanya ujasiriamali mbalimbali, ujasiriamali wa viungo vya chai ndiyo umempa umaarufu mkubwa na yeye akaamua kushughulika na chai tu.

‘’Mapenzi yangu kwa chai ndiyo yaliyonivutia, kujaribu ubunifu wa kipekee wa kuja na chai ya aina yake, kuitwa ‘Mama Chai’ ni fahari kwangu.”

Anasema pamoja na ulemavu, amekuwa akiweka juhudi katika kupata mafanikio ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakimrudisha nyuma kwa kuchukua bidhaa zake kwa ahadi ya kwenda kumuuzia na kutafuta masoko lakini wengi wamekuwa wakikimbia na ‘mizigo’.

“Mimi kutokana na ulemavu wangu siwezi kuzunguka wala kutembea kwenda kuuza, hivyo huwapa watu ambao wengine hawarudi tena”

Ujasiriamali wa viungo vya chai ulimpa fursa pia ya kufungua ofisi yake binafsi ambapo alikuwa akipanga bidhaa zake na kuuzia watu wengi.

ggg

Chanzo cha picha, Neema Ibrahim Chizenga

Harakati za biashara

Licha ya ujuzi huo ambao pia ulimpatia fursa ya kufundisha wajasiriamali wengine katika Shirika la viwanda vidogo vidogo (SIDO), ofisi yake sasa imebaki kama gofu akishindwa hata kwenda kufuta vumbi.

Miundombinu imekuwa moja ya changamoto kubwa inayomrudisha nyuma ikiwa ni pamoja na usafiri. Neema anakiri kuanguka kwa mtaji kumeua bishara yake kwa sasa na kushindwa hata kwenda kufungua ofisi yake iliyopo eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.

Anasema hali yake ya ulemavu inamnyima fursa ya kusonga mbele kwani kufuatia hali ya hewa ya mvua inayoendelea inamuwia vigumu kutembea kwa magongo hadi eneo la umbali wa kilomita zaidi ya 15 ilipo ofisi yake.

ggg

Chanzo cha picha, Neema Ibrahim Chizenga

“Mvua imeniathiri sana, siwezi kutoka kwenda kutafuta, hivyo najikuta nakula hadi fedha ya mtaji kwa kukaa tu ndani”

“Mimi Mungu anipe miguu miwili, macho mawili hata beseni la mboga ntabeba. Ninawalaumu wale Mungu amewapa vitu vyote viko makini halafu anakwambia nina shida”

Anasema hapendi kusaidiwa wala kukaa bila kufanya kazi na kujituma ndiyo msingi wake na endapo atapata mtaji anauhakika atafika mbali ikiwa ni pamoja na kufungua kiwanda kikubwa cha ujasiriamali kwani viungo vyake vya chai vina soko kubwa.

Anajipambanua kwamba kuomba kwake ni mwiko, na kupambana kwake kumevifanya viungo vyake vya chai kuuliziwa kwa wingi lakini uzalishaji ni kama umesimama.

“Mimi ni mnyonge lakini si mnyonge sana kwa sababu napambana sana”