Vijue vyuo vikuu kumi bora Afrika 2025

r

Chanzo cha picha, UNICON

Kwa mujibu wa jarida la elimu kutoka Uingereza la Times Higher Education, vyuo vikuu bora barani Afrika vimetoka katika nchi 19 katika orodha yao ya 2025 kati ya zaidi ya vyuo vikuu 2,000 kutoka nchi 115. Kwa ujumla, Misri na Algeria ndizo nchi mbili za Afrika zilizotoa vyuo vingi katika orodha hiyo, zikiwa na vyuo vikuu 35 na 26 kila moja.

Lakini nusu ya vyuo vikuu 10 bora barani Afrika imejazwa na vyuo vikuu kutoka Afrika Kusini, na vyuo vikuu 14 vya Afrika Kusini vimetajwa katika orodha ya vyuo 2000+. Nchi ya Misri, Ghana, Nigeria, Uganda na Afrika Kusini ziko katika orodha ya vyuo vikuu 1000 bora kimataifa.

Mgawanyo huu wa vyuo kwa mujibu wa Times Higher Education hupimwa kwa kutazama mambo 18 yakiwemo ufundishaji, mazingira ya utafiti, ubora wa utafiti, mtazamo wa kimataifa, kuaminika kwao na wanafunzi, wataalamu na serikali, kuyataja kwa uchache.

Ikiwa sasa Marekani imesitisha miadi ya viza za wanafunzi kutoka Afrika wanaotaka kwenda kusoma huko na nchi kama Uingereza na zingine za Ulaya zikiongeza masharti ya viza za wanafunzi wa kigeni, macho yanaweza kuelekezwa kwenye vyuo vya ndani barani Afrika.

Ifuatayo ni orodha ya vyuo vikuu kumi bora barani Afrika kwa mwaka 2025 kwa mujibu wa jarida la Times Higher Education. Orodha hii inaanza kutokea chuo cha kwanza hadi cha kumi:

Pia unaweza kusoma

1. Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini

f

Chanzo cha picha, Adrian Frith

Maelezo ya picha, Ndio chuo kikuu kikongwe zaidi Afrika Kusini

Chuo hiki kilianzishwa mwaka 1829, ndio chuo kikuu kikongwe zaidi Afrika Kusini na cha pili kwa ukongwe barani Afrika, nyuma ya Chuo Kikuu cha Sierra Leone, ambacho kilianzishwa miaka miwili mapema.

Chuo hiki ni cha 180 duniani, kina idara nyingi za kufundisha, kama vile biashara, uhandisi, mazingira, afya, sayansi ya jamii, sayansi na sheria. Chuo hiki kimejitolea kuleta mabadiliko ya kijamii kupitia miradi ambayo hushughulikia maswala ya fursa na uwezo wa wanafunzi.

2. Chuo Kikuu cha Stellenbosch, Afrika Kusini

V

Chanzo cha picha, Flickr

Maelezo ya picha, Chuo kikuu cha Stellenbosch

Chuo Kikuu cha Stellenbosch kiko katika Rasi ya Magharibi ya Afrika Kusini, kilomita 50 kutoka Cape Town. Mji wa Stelenbosch umeenea majengo ya tangu ukoloni wa Uholanzi.

Katika orodha ya kidunia kipo kati ya 301-350. Ufundishaji katika chuo hiki umegawanywa katika kampasi nne, na moja kuu iko Stellenbosch na zingine katika maeneo ya karibu. Wanafunzi hutumia Kiingereza na Kiafrikana kufanyia mitihani na kazi za darasani, ingawa lugha kuu ya kufundishia ni Kiafrikana.

3. Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Afrika Kusini

g

Chanzo cha picha, Wikipedia

Maelezo ya picha, Nelson Mandela alisoma katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand

Chuo Kikuu cha Witwatersrand - au Chuo Kikuu cha Wits, kama kinavyojulikana kipo Johannesburg. Kilianzishwa kama taasisi ya uchimbaji madini; eneo hilo ndilo lenye dhahabu nyingi zaidi kuliko eneo lolote duniani.

Katika orodha ya kimataifa kiko kati ya 301-350. Chuo hicho kilikuwa sana mwishoni mwa karne ya 20, na kimepanuka na kuwa na majengo mengi mapya. Wakati huo pia kilikuwa ni kipindi cha kupinga sera za ubaguzi wa rangi, na viongozi wengi mashuhuri weusi walihitimu hapo.

Baba wa taifa wa Afrika Kusini, Nelson Mandela alisoma katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand (Wits). Alikuwa mwanafunzi wa sheria kuanzia 1943 hadi 1949.

4. Chuo Kikuu cha Mohammed VI Polytechnic, Morocco

FC

Chanzo cha picha, O

Maelezo ya picha, Chuo hiki sehemu ya mradi wa Jiji la Kijani

Kilianzishwa 2016, Chuo Kikuu cha Mohamed VI Polytechnic ni chuo binafsi katika jiji la Benguerir, Morocco. Chuo hiki sehemu ya mradi wa (Jiji la Kijani) Green City uliozinduliwa na Mfalme Mohamed VI mwaka 2009, jiji la kukuza utafiti na elimu kwa nchi.

Katika orodha ya kimataifa kipo 401-500. Chuo hicho kimegawanywa katika idara tano; sayansi na teknolojia, uchumi, sayansi ya kijamii, biashara na usimamizi na matibabu. Kila idara inajumuisha taasisi kadhaa na kozi mbali mbali.

5. Chuo Kikuu cha Johannesburg, Afrika Kusini

GV

Chanzo cha picha, virtual

Maelezo ya picha, Chuo Kikuu cha Johannesburg (UJ) ni cha umma

Chuo Kikuu cha Johannesburg (UJ) ni cha umma, kipo Johannesburg, Afrika Kusini. Kilianzishwa 2005 kama muunganisho wa taasisi tatu, ya Chuo kikuu cha Rand Afrikaans, Technikon Witwatersrand, na kampasi ya Soweto na East Rand za chuo kikuu cha Vista.

Katika orodha ya kimataifa kipo 401-500. Taasisi hii ni mojawapo ya vyuo vikuu vikubwa nchini Afrika Kusini miongoni mwa vyuo vikuu 26 vya umma vinavyounda mfumo wa elimu ya juu. UJ ina idadi ya wanafunzi zaidi ya 50,000, ambapo zaidi ya 3,000 ni wanafunzi wa kimataifa kutoka nchi 80.

6. Chuo Kikuu cha E-JUST, Misri

GV

Chanzo cha picha, E-JUST

Maelezo ya picha, Kilianzishwa mwaka 2009 huko Alexandria, Misri

Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Misri-Japan (E-JUST), kilianzishwa mwaka 2009 huko Alexandria, Misri, kama mradi kati ya serikali ya Misri na Japan. Chuo hicho kilipokea wanafunzi wake wa kwanza mwaka mmoja baadaye, 2010.

Katika orodha ya kimataifa kipo 501-600. Chuo hicho kinafadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japani na Muungano wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Japani, pia kinaendeshwa na ufadhili wa serikali ya Misri.

7. Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal, Afrika Kusini

f

Chanzo cha picha, UKZN

Maelezo ya picha, Kipo karibu na fukwe ya Bahari ya Hindi, katika jiji la Durban

Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal kipo Durban, mashariki mwa Afrika Kusini, kilianzishwa mwaka 2004 kufuatia kuunganishwa kwa Chuo Kikuu cha Durban-Westville na Chuo Kikuu cha Natal, baada ya mpango wa serikali wa kupunguza idadi ya vyuo vikuu Afrika Kusini.

Katika orodha ya kimataifa kipo kati ya 501-600. Chuo hicho kina kampasi tano. Kipo karibu na fukwe ya Bahari ya Hindi, katika jiji la Durban - jiji la pili kwa ukubwa nchini Afrika Kusini. Kampasi ya Pietermaritzburg ndiyo pekee ambayo haipo karibu na fukwe ya bahari.

8. Chuo Kikuu cha Marekani Cairo, Misri

fc

Chanzo cha picha, smapse

Maelezo ya picha, Hapo awali kilikuwa ni kwa ajili ya wanafunzi wa kiume tu

Chuo Kikuu cha Marekani huko Cairo kilianzishwa 1919 na Wamishenari wa Marekani huko Misri, ilikuwa ni misheni ya Kiprotestanti iliyofadhiliwa na Kanisa la United Presbyterian la Amerika Kaskazini, kama chuo kikuu cha lugha ya Kiingereza na shule ya maandalizi.

Kimataifa kipo kati ya 601-800. Hapo awali kilikuwa ni kwa ajili ya wanafunzi wa kiume. Kilisajili mwanafunzi wake wa kwanza wa kike 1928. Chuo hicho kinafundisha programu zake kwa mtindo wa Marekani katika viwango vya shahada ya kwanza, ya pili na viwango vingine.

9. Chuo Kikuu cha Future, Misri

CX

Chanzo cha picha, FUE

Maelezo ya picha, Ni chuo binafsi kilicho katika mtaa wa 90, New Cairo, Misri

Chuo Kikuu cha Future (FUE), Misri ni chuo binafsi kilicho katika mtaa wa 90, New Cairo, Misri na kilianzishwa 2006. Kila kitivo ni taasisi inayojitegemea yenye mali na vifaa vyake. Vitivo vina jukumu la kuchagua wanafunzi, kwa mujibu wa kanuni za chuo.

Kimataifa kipo kati ya 601-800. Taarifa rasmi ya chuo hicho inasema, FUE ni bora katika ufundishaji, utafiti na huduma, kinajitahidi kutoa elimu bora, ya hali ya juu ambayo inawatayarisha wahitimu kuwa viongozi wa siku zijazo.

10. Chuo Kikuu cha Kafr El Sheikh, Misri

x

Chanzo cha picha, Kafr

Maelezo ya picha, Kafr El Sheikh kilianzishwa mwaka 2006, kipo katika mji wa Kafr El Sheikh katika eneo la Nile Delta.

Chuo Kikuu cha Kafr El Sheikh kilianzishwa mwaka 2006, kipo katika mji wa Kafr El Sheikh katika eneo la Nile Delta. Kina idadi ya wanafunzi karibu 30,000 na wafanyakazi 1,500. Pia ni mwenyeji wa taasisi tatu za utafiti: Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nano, Taasisi ya Ugunduzi na Maendeleo ya Dawa na Taasisi ya Uuguzi.

Kimataifa kipo 601 – 800. Kafrel sheikh ni chuo kikuu cha pili ambacho ni rafiki wa mazingira katika Ulimwengu wa Kiarabu, kulingana na mfumo wa viwango vya Global Green Metric. Pia kina sifa kitaifa kama kituo cha utafiti, kikishika nafasi ya nne kati ya vyuo vikuu vya nchi hiyo.