Waridi wa BBC: 'Sina uwezo wa kushiriki unyumba'

Chanzo cha picha, Mary Wangari
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Mary Njoki Wangari ni mwanamke mwenye miaka 27 kutoka nchini Kenya.
Maisha yake kwa hivi sasa kama anavyosimulia yamegubikwa na siutafahamu ya siku zijazo , hii ni baada ya kupewa matokeo ya uchunguzi aliofanyiwa katika sehemu ya kizazi chake na kubainika kuwa yeye ni mwanamke anayeishi bila mfuko wa uzazi , mayai (ovari)hali kadhalika njia ya uzazi haiko vizuri.Hali hii ikifahamika kwa kiingereza kama Mayer-Rokitansky-Küster-Ha (MRKH)
Mwaka mmoja na nusu baada ya kupashwa habari hiyo amekubali hali hiyo ila ana shauku ya kuendelea kutafuta matibabu zaidi yatakayomwezesha kupata matibabu ya kutengeneza njia ya uzazi.

Chanzo cha picha, Mary Wangari
Hali hii iligunduliwa vipi ?
Mary alikulia jimbo la Nyandarua nchini Kenya na kama mabinti wengine alikuwa na ndoto za kuwa mama wa watoto, sasa zinasalia kuwa ndoto kwani anakumbuka alipotimiza miaka 12 alikuwa anasubiri kwa hamu na ghamu kupata hedhi kama walivyokuwa wamefunzwa kupitia somo la biolojia kuhusiana na jinsi mabinti hubalehe na kupata mabadiliko mbali mbali mwilini
Kwake anasema kuwa hakuna mabadiliko makubwa aliyoyaona kuanzia alipotimiza miaka 12 hadi 18. Wasiwasi wake mkuu ulianza wakati alipomaliza shule ya sekondari.
“Niliwaona marafiki zangu wengi, tayari walikuwa wamepata hedhi na hata wengine kujaaliwa watoto katika umri mdogo, ila kwangu mwili wangu ulikuwa kama vile binti mdogo ingawa miaka ilikuwa imesonga ”anakumbuka Mary.
Mwanadada huyu anasema kwa kuwa alikulia maeneo ya mashambani alikosa mtu wa kumsaidia kung’amua yaliokuwa yanaendelea ndani ya mwili wake, pia kutokana na unyanyapaa aliogopa kuzungumza kuhusiana na masaibu yake ya kukosa hedhi pamoja na hisia tofauti za kik .
Baada ya kuona miaka inasonga na hakuna mabadiliko makubwa aliyoyaona mwilini mwake aliamua kuanza kutafuta tiba.
Mary anasema kuwa alikwenda kwa madaktari tofauti wabobezi wa tiba ya afya ya uzazi kwa wanawake, wanne kati yao walipata na majibu yaliyo sawa hasa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina tumboni mwake.
“Nilipashwa habari kuwa sina viungo vyote vya uzazi , nilihisi uchungu sana kwani kwa miaka 28 nimeishi duniani sikuwahi kuhisi maumivu yoyote tumboni nilidhani kuwa tatizo langu lingetatuliwa mara mmoja. Sasa nimekubali tu kuwa sina uwezo wa kupata watoto lakini ninatumaini kuwa mengine yatarekebishwa ili nihisi kama wanawake wengine ”anasema Mary.
Masaibu ya kuishi na hali hii katika utu uzima
Mary alifika miaka 28 kabla ya mwisho wa mwaka huu na katika miaka ambayo ameishi kama mtu mzima amepitia mengi hasa kibinafsi kwani ni jambo ambalo ameanza kulizungumzia wazi wazi hivi maajuzi .
Matamanio yake makuu yamekuwa kujaaliwa watoto, ila katika hali anayoishi kwa sasa haiwezekani akajaaliwa watoto .
Tangu Mary alipoanza hatua za kutafuta ukweli amepitia karibu wataalamu wanne ili kuthibitisha na kujitosheleza kuwa ndani ya tumbo lake hana ishara yoyote ya kuwa na via vya uzazi na pia njia ya kizazi ni kweli.
Mojawapo ya changamoto za kuishi na hali hiyo alielezwa hatakuwa na uwezo wa kupata watoto. AmeIkubali hali hiyo ila anatumaini ataweza kupata matibabu ya kutengeneza njia ya uzazi.
Aidha anasema kuwa licha ya kuwa ameelezwa kuwa hatakuwa na uwezo wa kujaaliwa watoto anatumaini kuwa baada ya upasuaji wa kuuunda njia ya uzazi hatimaye atapata mchumba ,kwani hadi sasa hali ya kujamiiana haijawezekana kutokana na hali yake .
''Ile hali ya kuishi na ukimya kuhusiana na hali ninayoishi nayo ndiyo ilinipa msongo wa mawazo , ila baada ya kufunguka ninajihisi mwenye amani , pia ninatumaini kama nilivyoelezwa na matabibu wangu kuwa kuna uwezekano nikapitia operesheni maalumu kuunda njia ya uzazi , ili iwapo nitaingia kwenye ndoa hakutakuwa na matatizo. ” Anasema Mary.

Chanzo cha picha, Mary Wangari
Mayer-Rokitansky-Küster-Ha (MRKH) ni hali gani ?
Kulingana na wataalamu Ugonjwa wa Mayer-Rokitansky-Küster-Ha (MRKH) ni ugonjwa unaoathiri zaidi mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Hali hii husababisha uke na mfuko wa uzazi kutokua vizuri au kutokuwepo, ingawa sehemu za siri za nje huwa ni za kawaida.
Watu walioathirika kwa kawaida hawana hedhi kutokana na kutokuwepo kwa uterasi au mfuko wa uzazi .
Mara nyingi, ishara ya kwanza inayoonekana ya ugonjwa wa MRKH ni kutokuwa na hedhi.
Watu walio na ugonjwa wa MRKH wana muundo wa kromosomu ya kike (46,XX) na ovari zinazofanya kazi kwa kawaida.
Pia wana ukuaji wa kawaida wa matiti na sehemu za siri. Ingawa watu walio na hali hii kwa kawaida hawawezi kubeba mimba, wanaweza kupata watoto kupitia usaidizi wa uzazi.
Wakati viungo vya uzazi pekee vimeathiriwa, hali hiyo huainishwa kama ugonjwa wa MRKH aina ya kwanza.