WARIDI WA BBC : 'Jinsi ugonjwa sugu ulivyo mtihani katika ndoa yangu'

Racheal Otuoma

Chanzo cha picha, Racheal Otuoma

Maelezo ya picha, Licha ya misukosuko katika ndoa ana matumaini
  • Author, Anne Ngugi
  • Nafasi, Multimedia Journalist

Racheal Otuoma ni mkewe Ezekiel Otuoma ambaye ni mmojawapo ya wachezaji wa soka kutoka nchini Kenya . Katika siku za hivi karibuni yeye na mumewe Bwana Otuoma wamekuwa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na ukakamavu ambao mwanamke huyu aliudhihirisha baada ya mumewe kuanza kuugua ugonjwa wa neva unaofahamika kama Motor neurone disease (MND )

Tangu mwaka wa 2020 Racheal anasema kuwa ugonjwa huo ulianza kumuathiri mume wake hadi kufikia kiwango cha kushindwa kutembea na kuathirika kwa sauti , kiasi kwamba mama huyu anasema kuwa mumewe amerejea kuwa kama mtoto mdogo na kwa kila jambo lazima ahudumiwe .

”imekuwa miaka mnne ambayo imejaa changamoto sio haba , kumuona mwanamume ambaye alikuwa ananihudumia kwa yote akiwa hawezi chochote sio rahisi ila ninajikakamua kila siku nikitumai ya kwamba atapona ”anasema Racheal

Ezekiel Otuoma amechezea timu mbalimbali nchini Kenya zikiwemo muhoroni , Ulinzi stars , Western Stima ,FC leopards na Talanta.

Katika kipindi hicho ambacho Ezekiel alikuwa anachezea timu ya Muhoroni ndipo penzi lao lilianza.

Bi Racheal anazungumizia uchumba ambao ulikuwa umejaa bashasha na mapenzi.

Racheal amekuwa akimhudumia mumewe baada ya ugonjwa

Chanzo cha picha, Racheal Otuoma

Maelezo ya picha, Racheal na mumewe Ezekiel aliyekuwa mchezaji soka Kenya .

Je walikutana vipi ?

Racheal anasema kwamba tangu zamani yeye na Ezekiel walikuwa marafiki , anakumbuka wakikutana kwenye sherehe moja ya kusherehekea kuzaliwa kwa rafiki yao mmoja , na hapo ndipo penzi lao lilianzia.

Tarehe 2 May 2015 , Racheal alifunga ndoa na Ezekiel wakati huo akiwa bado ni mchezaji soka nchini Kenya , na maisha yao pamoja yakaanza. Misukosuko katika ndoa ilianza pale Rachel alipopata ujauzito mara mbili , ila watoto wao walifariki kabla ya kuzaliwa.

”Ezekiel alinipenda kweli , na wakati wote alihakikisha kuwa amenipa maisha mazuri , hakuna wakati mimi kama mke wake nilitamani kitu kikamshinda kufanya na kwa hivyo alipoanza dalili za kuwa mngonjwa nilifahamu kuwa ni wakati wangu wa kumtunza ” anasema Racheal.

Ezekiel Otuoma alichezea timu mbalimbali Kenya

Chanzo cha picha, Racheal Otuoma

Maelezo ya picha, Mumewe Racheal akisakata Kabumbu kabla ya ugonjwa

Mahangaiko ya ugonjwa yalivyoanza .

Mwaka wa 2015 ndipo mume wake Racheal alianza kuonyesha dalili za ugonjwa ambao haukuwa unaeleweka , mwanadada huyu anasema kuwa anakumbuka mumewe akisema kuwa anahisi homa.

Ishara nyingine zilikuwa mumewe kupoteza sauti yake na alianza kutembea kwa kuyumba.

”Mume wangu alianza kuonyesha dalili za kudhoofika , mojawapo ya mambo yaliyokuwa yananipa wasiwasi ni kule kupoteza sauti yake , na wakati mwingine alizungumza akiwa anazungumza kwa kuvuta matamshi mtu asiweze kumsikia vizuri ”Racheal anakumbuka.

g

Chanzo cha picha, Racheal Otuoma

Jitihada zetu za kumpeleka katika hospitali mbalimbali ziliishia pale baada ya uchunguzi wa madaktari kuonyesha kuwa Ezekiele alikuwa ana ugonjwa unaofahamika kama motor neurone.

Kulingana na mwanadada huyu tangu wakati walipopewa matokeo hayo, mumewe wake ameendelea kubadilika hasa kwa kuwa Neva zake pamoja na ubongo vinaendele kuathirika kila siku.

”Jitihada zangu za kuhakikisha kuwa amepona zimetupeleka mbali sana , na hata tulipata fursa ya kusafiri hadi India kwa matibabu zaidi , japo hata wakati huu mume wangu ananihitaji kumhudumia kila kitu ”anasema Racheal.

Jitihada za kutafuta maombi

Racheal anasema kuwa baada ya kutafuta matibabu katika hospitali mbalimbali , aliwazia kuingia kwenye vyumba vya ibada kutaka afanyiwe maombi maalum.

Mwanamke huyu anasema kuwa alianza pia kushuku kuwa huenda ugonjwa wa mumewe usiwe wa kawaida , na huenda umesababishwa na watu.

Yeye na mumewe walizuru maeneo mbalimbali nchini Kenya wakiwasaka mapadre na maaskofu wa makanisa makubwa nchini humo katika jitihada za kutafuta majibu ya ugonjwa ambao umemuhangaisha mumewe kwa miaka kadhaa sasa.

Hadi wakati mmoja dada huyu anasema kuwa walisafiri hadi Uganda kwa maombi maalumu, lakini licha ya maombi mumewe hajaonyesha dalili za kupona bali mwili wake umeendelea kudhoofika.

Anakiri kuwa baada ya kuona kuwa hata makanisani hali yake haikubadilika alianza kuikubali hali ya mumewe.

Mara nyingi Racheal ndio mwenye kumtumikia mume wake kwa kila hali kwani ugonjwa wenyewe umemuathiri kiasi kwamba hawezi kufanya lolote peke yake.

”Limekuwa jambo la kusikitisha kumuona mume wangu akiwa na uchungu mbaya hali kadhalika asiweze kufanya chochote bila usaidizi wangu , ananihitaji kwa kila jambo kwani kwa sasa hakuna kitu anachoweza kujifanyia mwenyewe ” anasema Racheal.

Racheal na Ezekiel walifunga ndoa 2015

Chanzo cha picha, Racheal Otuoma

Maelezo ya picha, Racheal siku ya ndoa yao mnamo mei mwaka wa 2015

Ugonjwa wa motor neurone ni nini na dalili zake ni zipi?

Ugonjwa wa motor neuron (MND)ni hali mbaya ambayo huulazimisha ubongo na seli za neva za uti wa mgongo kushindwa kutenda kazi yake.

Ugonjwa huu huathiri ubongo na neva.

Husababisha udhaifu unaozidi kuwa mbaya zaidi kadri muda unavyosonga. Kufikia sasa hakuna tiba ya MND, lakini kuna matibabu ya kusaidia kupunguza athari zinazojitokeza katika maisha ya kila siku ya mtu.

Baadhi ya watu wenye ugonjwa huu huishi nao kwa miaka mingi.

Ugonjwa huu pia mara nyingi huathiri misuli yote hivyo kumfanya mtu kupata changamoto kufanya shughuli za kila siku na sauti kubadilika.

Imehaririwa na Dinah Gahamanyi na Seif Abdalla