Trump aishutumu China kwa 'kukiuka' mapatano ya ushuru
Rais wa Marekani Donald Trump ameishutumu China kwa kukiuka makubaliano ya wiki mbili ya kusitisha ushuru wa forodha - ishara kwamba mvutano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani unaweza kuongezeka tena.
Muhtasari
- Mtaalamu wa kuruka kwa mwavuli anusurika kifo baada ya kupaa hadi ndani ya mawingu
- Kesi ya timu ya matibabu ya Maradona yasitishwa
- Wanamuziki watano wauawa na genge la uhalifu Mexico
- Ushuru wa Trump unaweza kuendelea kwa sasa - mahakama ya rufaa
- Ukosefu wa usalama washuhudiwa Gaza huku raia wakitafuta chakula
- Sean 'Diddy' Combs alimbaka na kumshambulia msaidizi wake wa zamani - mahakamani
- Hamas kukataa mpango mpya wa kusitisha mapigano Gaza
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Mazungumzo ya biashara ya China yamekwama, waziri wa fedha wa Marekani asema
Chanzo cha picha, PA Media / Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump ameishutumu China kwa kukiuka makubaliano ya wiki mbili ya kusitisha ushuru wa forodha - ishara kwamba mvutano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani unaweza kuongezeka tena.
Washington na Beijing zilikubaliana kupunguza kwa muda ushuru wa Piga-nikupige baada ya mazungumzo huko Geneva mapema mwezi huu.
Trump alisema Ijumaa katika chapisho kwenye mtandao wa Truth kwamba ushuru umeiacha China katika "hatari kubwa ya kiuchumi", kabla ya nchi hizo kufanya "mkataba wa haraka".
Hata hivyo alisema China "imekiuka kabisa makubaliano yake na sisi", bila kueleza jinsi gani.
Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Jamieson Greer baadaye alisema China haikuwa ikiondoa vizuizi visivyo vya ushuru kwa njia ambayo ilikuwa imekubaliwa. Beijing bado haijajibu madai hayo.
Unaweza kusoma;
Watu 110 wafariki kutokana na mafuriko Nigeria
Chanzo cha picha, Mikail Musa
Maelezo ya picha, Zaidi ya nyumba 50 zimesombwa na maji Takriban watu 110 wamefariki kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa katikati mwa Nigeria, maafisa wameiambia BBC.
Mvua hiyo ilinyesha kwa saa kadhaa, alisema mkuu wa mamlaka inayosimamia masuala ya dharura wkatika Jimbo la Niger (Nsema), Abullahi Baba-Arah.
Aliongeza kuwa "maji ya mafuriko yalisomba zaidi ya nyumba 50 za makazi". Kulingana na Nsema, wilaya za Tiffin Maza na Anguwan Hausawa za mji wa Mokwa ziliathirika zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Mokwa, Muhammad Shaba Aliyu, alisema ni zaidi ya "miaka 60" tangu jamii kukumbwa na mafuriko ya aina hii.
“Naomba serikali ituusaidia kukabiliana na janga hili,” Bw Aliyu alisema.
Operesheni ya kuwatafuta na kuwaokoa manusura bado inaendelea huku watu kadhaa wakiwa hatarini, mamlaka inasema.
Mvuvi wa eneo hilo aliliambia shirika la habari la AFP kwamba ameachwa bila makao. "Sina pa kulala. Nyumba yangu imebomoka," Danjuma Shaba alisema.
Maeneo mengi ya kaskazini mwa Nigeria yalipata mvua kubwa na mafuriko mwaka 2024 ambayo yalisababisha vifo, watu kuhama makazi yao huku miundombinu ikiharibiwa vibaya.
Ukraine inasubiri pendekezo la amani la Urusi kabla ya mazungumzo ya Istanbul
Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi inasema itatuma wajumbe wake mjini Istanbul Jumatatu ijayo kwa ajili ya duru ya pili ya mazungumzo ya amani na Ukraine.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema kuwa masharti ya Moscow ya kufikiwa kwa makubaliano ya muda yanaandaliwa na yatajadiliwa nchini Uturuki.
Ukraine imesema bado imejitolea kufanya mazungumzo lakini haitatuma ujumbe hadi itakapopokea maelezo ya pendekezo la Urusi la kusitisha mapigano.
Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya wajumbe wa ngazi ya chini wa Urusi na Ukraine ilifanyika mapema mwezi huu, na kusababisha pande zote mbili kuwarudisha mamia ya wafungwa katika upokezanaji mkubwa zaidi tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha alisema Ukraine tayari imetuma "mruwaza yake ya hatua za baadaye" kwa Urusi, akiongeza kuwa Moscow "lazima ikubali usitishaji vita bila masharti" ili kutoa njia ya mazungumzo yaliyo na tija.
Soma pia:
Israel yamshutumu Macron kwa kuwa katika 'vita dhidi ya taifa la Kiyahudi'
Chanzo cha picha, EPA
Wizara ya mambo ya nje ya Israel imemjibu Emmanuel Macron, ikimtuhumu rais wa Ufaransa kuwa kwenye "vita dhidi ya taifa la Kiyahudi".
Hapo awali Macron alisema "itabidi kuimarisha msimamo wetu wa pamoja" ikiwa Israel haitafanya jitihada zaidi kukabiliana na hali ya kibinadamu huko Gaza.
Katika majibu yenye maneno makali kwenye ukurasa wa X, wizara hiyo inaandika: "Ukweli haumpendezi Macron. Hakuna kizuizi cha kibinadamu.
Huo ni uwongo mtupu. "Israel kwa sasa inawezesha kuingia kwa msaada Gaza kupitia juhudi mbili sambamba," inasema, ikitoa mfano wa misaada inayoingia kupitia Umoja wa Mataifa na Mfuko wa Kibinadamu wa Gaza.
Katika siku za hivi karibuni Umoja wa Mataifa umeendelea kushinikiza msaada zaidi kuruhusiwa kuingia Gaza, kufuatia kupunguzwa kwa kizuizi cha wiki 11.
Mapema siku ya Ijumaa, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu iliishutumu Israel kwa kuzuia idadi kubwa ya misaada kuingia Gaza.
Unaweza kusoma;
Pendekezo la kusitisha mapigano lashindwa kukidhi matakwa ya Hamas, afisa asema
Chanzo cha picha, Reuters
Afisa wa Hamas Basem Naim, anasema Hamas imepokea "jibu rasmi" kutoka Israel kwa pendekezo lililotolewa na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff.
Jibu hilo la Waisraeli, Naim anasema, "linashindwa kukidhi matakwa yoyote ya haki na uhalali kwa watu wetu, miongoni mwao ni kusitishwa mara moja kwa uhasama na kumalizika kwa maafa ya kibinadamu yanayotokea Gaza".
Lakini, anaongeza, "Uongozi wa Hamas kwa sasa unafanya mapitio ya kina na ya kuwajibika ya pendekezo jipya".
"Tathmini hii inaongozwa na hisia ya kina ya uwajibikaji wa kitaifa na dhamira thabiti ya kulinda haki na mustakabali wa watu wa Palestina katika ardhi yake," Naim anaeleza.
Unaweza kusoma;
Ndege iliyombeba rais wa Liberia yatua ghafla
Chanzo cha picha, FrontPage Africa
Safari za ndege zilisitishwa kwa muda katika uwanja mkuu wa ndege wa Liberia Alhamisi usiku baada ya ndege ya kibinafsi iliyokuwa imembeba Rais Joseph Boakai kukumbwa na hitilafu na kulazimika kutua ghafla.
Sehemu ya gia ya kutua ya ndege ya rais iliharibika ilipokaribia uwanja wa ndege, mamlaka ya uwanja wa ndege ilisema.
Kisa hicho, ambacho kilizua hofu katika uwanja huo wa ndege, kilisababisha safari zote za ndege zilizopangwa usiku huo kuahirishwa, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Rais Boakai, ambaye alikuwa akirejea kutoka safarini nchini Nigeria na wasaidizi wake, aliondolewa katika eneo la tukio, huku mamlaka ikianza uchunguzi.
Picha za ndege iliyokwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts (RIA) zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, na kusababisha wasiwasi kuhusu usalama wa rais.
Chanzo cha picha, Executive Mansion - Liberia / Facebook
Vyombo vya habari nchini humo, vikinukuu mamlaka ya uwanja wa ndege, vilisema tairi moja ya ndege hiyo ilipasuka ilipotua na kuicha ikiwa imekwama kwenye njia ya ndege kurukia.
Katika taarifa, Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Liberia (LAA) ilithibitisha "tukio hilo la kushutua" iliyohusisha ndege ya rais.
Mamlaka hiyo aidha ilipuuzilia mbali madai kuwa tukio hilo lilisababishwa na hali mbaya ya njia ya kurukia ndege.
Mtaalamu wa kuruka kwa mwavuli anusurika kifo baada ya kupaa hadi ndani ya mawingu
Chanzo cha picha, Social Media
Mtaalamu wa kuruka kwa mwavuli wa China amenusurika kifo kwa kurushwa kibahati mbaya umbali wa mita 8,500 (futi 27,800) angani kaskazini-magharibi mwa China, kulingana na ripoti ya vyombo vya habari vya serikali.
Peng Yujiang, 55, alikuwa akifanya majaribio ya vifaa vipya akiwa mita 3,000 juu ya usawa wa bahari, katika milima ya Qilian, wakati mkondo wa upepo usio wa kawaida ulipomvuta takriban mita 5,000 juu hadi kwenye mawingu.
Katika video iliyosambaa TikTok Bw Peng anaonekana akijaribu kudhibiti mwavuli, uso wake na sehemu kubwa ya mwili wake ikiwa imefunikwa kwa vijipande vya barafu.
"Ilikuwa tukio la kutisha... Kila kitu kilikuwa cheupe. Sikuweza kuona mwelekeo wowote. Bila dira, nisingejua ni njia gani nilikuwa nikienda. Nilidhani nilikuwa nikiruka moja kwa moja, lakini ukweli ni kwamba, nilikuwa nikizunguka," aliambia China Media Group.
Bw Peng alinusurika kifo kwa tundu ya sindano kwa sababu oksijeni ni kidogo sana katika mwinuko huo - chini kidogo kuliko kilele cha Mlima Everest. Joto pia linaweza kushuka hadi -40C.
"Nilitaka kushuka haraka, lakini sikuweza. Niliinuliwa juu zaidi na zaidi hadi nikajiona nimefika ndani ya mawingu," alisema.
Bw Peng, ambaye amekuwa akiruka kwa mwavuli kwa miaka minne na nusu, alisema huenda alipoteza fahamu wakati anashuka kurudi chini.
Hata hivyo, mamlaka ya Cina inachunguza tukio hilo na Bw Peng amesimamishwa kazi kwa muda wa miezi sita kwa sababu mwavuli huo haukuwa umeidhinishwa, ripoti ya shirika la serikali la Global Times iliripoti.
Pia unaweza kusoma:
Kesi ya timu ya matibabu ya Maradona yasitishwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Maradona mwaka 2019. Kesi ya wahudumu wa afya ya Diego Maradona haiwezi kuendelea nchini Argentina baada ya kubainika kuwa jaji aliyehusika katika kesi hiyo alishiriki katika makala kuihusu.
Hakimu anayesimamia kesi hiyo iliyoanza Machi 11 na ilitarajiwa kuendelea hadi Julai, alisema italazimika kuanza tena.
Wanachama saba wa timu ya matibabu ya Maradona walishtakiwa kwa mauaji ya kizembe yanayohusiana na kifo cha mwanasoka huyo wa zamani mnamo mwaka 2020.
Hata hivyo, wamekanusha madai hayo.
Mmoja wa majaji watatu wasimamizi, Julieta Makintach, alijiuzulu wiki hii.
Maradona, kiungo wa zamani wa Napoli na Argentina, alikuwa akipata nafuu nyumbani kwake Buenos Aires kutokana na upasuaji wa ubongo wa kuganda kwa damu mnamo mwezi Novemba 2020 alipofariki kutokana na mshtuko wa moyo, akiwa na umri wa miaka 60.
Miongoni mwa timu ya matibabu ni mtaalamu wa mfumo wa neva, daktari na muuguzi wa usiku.
Wanadai mwanasoka huyo aliyestaafu alikataa matibabu zaidi na alipaswa kukaa nyumbani kwa muda mrefu baada ya upasuaji wake.
Iwapo watapatikana na hatia, wanakabiliwa na kifungo cha kati ya miaka minane hadi 25 jela.
Soma zaidi:
Wanamuziki watano wauawa na genge la uhalifu Mexico
Chanzo cha picha, AFP
Wanamuziki watano waliotoweka katika mji wa Reynosa nchini Mexico, karibu na mpaka wa Marekani, waliuawa na washukiwa wa kundi la madawa ya kulevya, mamlaka ya Mexico imesema.
Watu tisa wanaodaiwa kuwa wanachama wa genge la Gulf wamekamatwa kwa tuhuma za mauaji, kulingana na Irving Barrios Mojica, mwanasheria mkuu wa jimbo la Tamaulipas nchini Mexico.
Wanamuziki hao - wanaojulikana kama Grupo Fugitivo - walitekwa nyara walipokuwa wakisafiri kwa hafla ya faragha tarehe 25 Mei, Barrios Mojica alisema. Muda mfupi baadaye, jamaa zao waliripoti kupokea madai ya kuwataka watoe fidia.
Wachunguzi wanajaribu kubaini sababu za mauaji hayo.
Wanamuziki hao walikuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 40, na mara nyingi walifanya maonyesho kwenye karamu za mitaani.
Silaha tisa na magari mawili pia yalikamatwa wakati wa msako.
Haijabainika mara moja ikiwa kikundi hicho kililengwa kwa sababu ya muziki wao, au walinaswa na vurugu ambazo zimeikumba Tamaulipas kwa muda mrefu, ambapo genge la Gulf limetawala kwa kiasi kikubwa.
Utawala wa Trump umetaja genge la Gulf, pamoja na vikundi vingine vya uhalifu kuwa "shirika la kigaidi la kimataifa".
Mnamo mwezi Januari, ubalozi wa Marekani nchini Mexico ulitoa ushauri wa usafiri wa kiwango cha 4, kiwango cha juu zaidi, na kuwaonya raia wake kutosafiri katika miji kadhaa ya Mexico, ikiwa ni pamoja na Reynosa.
Soma zaidi:
Ushuru wa Trump unaweza kuendelea kwa sasa - mahakama ya rufaa
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump anaweza kuendelea kukusanya ushuru wa bidhaa zinazoingia kutoka nje ya nchi kwa sasa, mahakama ya rufaa imesema, siku moja baada ya mahakama ya kibiashara kutoa uamuzi kuwa ushuru mkubwa ulioanzishwa na rais huyo katika nchi mbalimbali ni kinyume cha sheria.
Mahakama ya rufaa ilikubali ombi kutoka Ikulu ya White House la kusitisha kwa muda agizo la mahakama ya chini, ambayo ilitoa uamuzi kuwa Trump alikiuka mamlaka yake kwa kuanzisha ushuru huo.
Uamuzi wa Jumatano kutoka kwa Mahakama ya Biashara ya Kimataifa ya Marekani uliwakasirisha maafisa wa Trump, ambao waliutaja kuwa mfano wa unyanyasaji wa mahakama.
Wafanyabiashara wadogo wadogo na kundi la maafisa wa serikali walipinga hatua za kuanzisha ushuru mkubwa zilizochukuliwa na Trump, ambazo zimetikisa utaratibu wa kiuchumi duniani.
Soma zaidi:
Ukosefu wa usalama washuhudiwa Gaza huku raia wakitafuta chakula
Chanzo cha picha, Reuters
Matukio ya ghasia, ukosefu wa usalama, na uporaji yanashuhudiwa katika mji mkuu wa kaskazini wa Gaza, ambapo Wapalestina wanatafuta kwa udi na uvumba chakula na imekuwa vigumu kwa misaada kupatikana.
Wizara ya mambo ya ndani inayoongozwa na Hamas ilisema maafisa wake saba wa polisi waliotumwa sokoni katika mji wa Gaza siku ya Alhamisi waliuawa na mashambulizi ya anga ya Israel walipokuwa wakijaribu kurejesha utulivu na kukabiliana na kile kilichoitwa "uporaji".
Jeshi la Israel halijazungumzia tukio hilo, lakini lilisema limeshambulia maeneo kadhaa "lengwa ya kigaidi" kote Gaza katika siku iliyopita.
Madaktari wa eneo na waokoaji walisema takriban watu 44 waliuawa katika eneo lote siku ya Alhamisi, wakiwemo 23 katika kambi ya wakimbizi ya Bureij.
Soma zaidi:
Sean 'Diddy' Combs alimbaka na kumshambulia msaidizi wake wa zamani - mahakamani
Chanzo cha picha, Reuters
Aliyekuwa msaidizi wa msanii maarufu wa rapu Sean "Diddy" Combs ameiambia mahakama ya New York kwamba alinyanyaswa na Diddy kingono mara kwa mara alipokuwa ameajiriwa naye kwa miaka minane.
Shahidi huyo - ambaye alitoa ushahidi wake bila kutambulika kwa kutumia jina bandia la "Mia" - pia alisema huku akibubujikwa na machozi kuwa aliishi kwa hofu kubwa alipokuwa akifanya kazi kwa Bw Combs.
Mwanamuziki huyo alitazama akiwa upande wa mshtakiwa huku mikono yake ikiwa imekunjwa mapajani wakati shahidi huyo anaelezea juu ya hofu yake ya kudhurika ikiwa angeripoti madai ya unyanyasaji aliokuwa anapitia.
Bw Combs, 55, amekanusha mashtaka aliyofunguliwa na serikali ya kupanga njama, kutekeleza ulanguzi wa ngono, na usafirishaji ili kujihusisha na ukahaba.
Onyo: Simulizi hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuona ya kuhuzunisha
"Singeweza kumkatalia,…" alisema. "Sikuweza kumwambia hapana kwa lolote."
Timu ya wanasheria ya Bw Combs bado haijapata nafasi ya kumhoji Mia, au kujibu madai yake.
Yeye ni shahidi wa pili katika kesi hiyo kudai kuwa Bw Combs alimnyanyasa kingono, pamoja na mpenzi wa zamani wa Bw Combs, Casandra Ventura
Soma zaidi:
Hamas kukataa mpango mpya wa kusitisha mapigano Gaza
Chanzo cha picha, Reuters
Afisa mwandamizi wa Hamas ameiambia BBC kuwa kundi hilo la Palestina litakataa pendekezo la hivi karibuni la Marekani la kusitisha mapigano Gaza lenye kutaka liwaachilie mateka.
Ikulu ya White House ilisema siku ya Alhamisi kwamba Israel "imetia saini" mpango wa mjumbe wa Marekani Steve Witkoff na kwamba inasubiri jibu rasmi kutoka kwa Hamas.
Vyombo vya habari vya Israel vimenukuu maafisa wa Israel wakisema kuwa Hamas itaachilia mateka 10 walio hai na miili ya mateka 18 waliokufa katika awamu mbili ili kubadilishana na kusitisha mapigano kwa siku 60 na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina katika jela za Israel.
Afisa huyo wa Hamas alisema pendekezo hilo halijakidhi matakwa ya msingi, ikiwa ni pamoja na kukomesha vita, na kwamba italijibu kwa wakati ufaao.
Serikali ya Israel haijasema lolote, lakini Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliripotiwa kuziambia familia za mateka siku ya Alhamisi kwamba alikubali mpango wa Witkoff.
Israel iliiwekea vikwazo Gaza na kuanza tena mashambulizi yake ya kijeshi dhidi ya Hamas tarehe 18 Machi kufuatia kusambaratika kwa makubaliano ya miezi miwili ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani, Qatar na Misri.
Ilisema ilitaka kuweka shinikizo kwa Hamas kuwaachilia mateka 58 ambao bado inawashikilia huku takriban 20 kati yao wakiaminika kuwa hai.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 30/05/2025.