'Walitupiga na kutubaka barabarani hadharani'

Chanzo cha picha, Reuters
Wanawake na wasichana katika jimbo la Darfur nchini Sudan wako katika hatari ya kukabiliwa na ukatili wa kingono, shirika la matibabu lisilokuwa na mipaka Médecins Sans Frontières (MSF) limeonya.
Kiwango cha kweli cha mgogoro huu kinasalia kuwa kigumu kuainisha, kwani huduma zinabaki kuwa chache na watu wanakabiliwa na vizuizi katika kutafuta matibabu au kuzungumzia shida zao.
Hata hivyo manusura wote wanaozungumza na timu za MSF huko Darfur na kuvuka mpaka nchini Chad wanazungumzia kuhusu hadithi za kutisha za unyanyasaji wa kikatili na ubakaji.
Wanaume na wavulana pia wapo katika hatari, kwa kuwa kiwango cha mateso ni cha kupita kiasi
"Wanawake na wasichana hawajisikii salama mahala popote. Wanashambuliwa katika nyumba zao wenyewe, wanapokimbia vurugu, kupata chakula, kukusanya kuni au kufanya kazi mashambani.
Wanatuambia wanahisi wamenaswa," anasema Claire San Filippo, mratibu wa dharura wa MSF.
"Mashambulizi haya ni mabaya na ya kikatili, mara nyingi yanahusisha wahalifu wengi.
Hii lazima ikome. Unyanyasaji wa kijinsia sio matokeo ya asili au ya kuepukika ya vita, inaweza kujumuisha uhalifu wa kivita, aina ya mateso, na uhalifu dhidi ya binadamu.
Pande zinazopigana lazima ziwawajibishe wapiganaji wao na kuwalinda watu kutokana na ghasia hizi mbaya.
Huduma kwa waathirika lazima ziongezwe mara moja, ili waathirika wapate matibabu na huduma ya kisaikolojia wanayohitaji sana."
Unyanyasaji wa kijinsia umeenea sana huko Darfur hivi kwamba watu wengi hawaezi kuepuka kuzungumzia suala hilo.
Unyanyasaji wa kijinsia Darfur

Chanzo cha picha, Reuters
"Kuna watu walikuja usiku kuwabaka wanawake hao na kuchukua kila kitu wakiwemo wanyama, nilisikia baadhi ya wanawake wakibakwa usiku.
Wanaume wao walikuwa wamejificha kwenye vyoo au katika vyumba fulani ambavyo wangeweza kufunga, kama mume wangu na ndugu zangu, la sivyo wangeuawa.
Wanawake hawakujificha kwa sababu ilikuwa tu kupigwa na kubakwa kwa ajili yetu, lakini wanaume wangeuawa," mwanamke mwenye umri wa miaka 27 aliiambia timu ya MSF huko Darfur Magharibi.
Sio tu wakati wa mashambulizi dhidi ya vijiji na miji au wakati wa kuelekea kutafuta usalama ambapo watu wamebakwa na kupigwa.
Usaidizi mdogo wa kibinadamu unawalazimu watu kuhatarisha maisha: watu wanatembea umbali mrefu ili kukidhi mahitaji yao ya kimsingi na kufanya kazi katika maeneo hatari.
Wengine huamua dhidi ya kuchukua hatari hiyo lakini hufutwa kazi na hivyo kupunguza zaidi upatikanaji wao wa maji, chakula na afya.
Hii sio hakikisho la usalama, kwani watu hushambuliwa nhadi majumbani mwao.
MSF ilitoa huduma kwa manusura 659 wa unyanyasaji wa kingono huko Darfur Kusini kati ya Januari 2024 na Machi 2025
- 86% waliripoti kuwa walibakwa
- Asilimia 94 ya walionusurika walikuwa wanawake na wasichana
- 56% walisema walivamiwa na mtu ambaye si raia (na mwanajeshi, polisi au vikosi vingine vya usalama au vikundi visivyo vya serikali)
- 55% waliripoti ukatili wa ziada wa kimwili wakati wa shambulio hilo
- 34% walikabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia walipokuwa wakifanya kazi au wakisafiri kwenda mashambani.
- 31% walikuwa chini ya 18, 29% walikuwa vijana (wenye umri kati ya 10 na 19), 7% walikuwa chini ya umri wa miaka 10 na 2.6% walikuwa chini ya miaka 5.
Takwimu hizi za kutatanisha zina uwezekano wa kukadiria kiwango halisi cha unyanyasaji wa kingono huko Darfur Kusini.
Hali ni sawa katika maeneo mengine ambapo MSF inaweza kutoa huduma kwa waathirika kama vile Mashariki ya Chad, ambayo kwa sasa inahifadhi zaidi ya wakimbizi 800,000 wa Sudan.
Mjini Adre karibu nusu ya manusura 44 waliotibiwa na MSF tangu Januari 2025 walikuwa watoto.
Katika Mkoa wa Wadi Fira, manusura 94 walitibiwa kati ya Januari na Machi 2025, 81 wakiwa na umri wa chini ya miaka 18.
Ushuhuda wa wagonjwa na watoa huduma mashariki mwa Chad na Darfur, Sudan unathibitisha hili.

Chanzo cha picha, Reuters
'Abakwa na wanaume watatu'
Mwanaume mmoja aliiambia timu ya MSF huko Murnei, Darfur Magharibi, "Miezi mitatu iliyopita kulikuwa na msichana mdogo wa umri wa miaka 13 ambaye alibakwa na wanaume watatu…Walimkamata na kumbaka, kisha wakamtelekeza bondeni... Waliwaita baadhi ya watu kumbeba msichana huyo hospitalini. Mimi nilikuwa mmoja wao. Alikuwa msichana mdogo."
Wengi walionusurika wanaripoti kubakwa na zaidi ya mtu mmoja. Huko Metché mashariki mwa Chad, manusura 11 kati ya 24 waliotibiwa kati ya Januari na Machi 2025 walishambuliwa na washambuliaji wengi.
Uzoefu ambao wagonjwa huzungumzia katika maeneo mbalimbali huthibitisha hili. "Tulipowasili Kulbus, tuliona kundi la wanawake watatu wakiwa na baadhi ya wanaume wa RSF [Rapid Forces] wakiwalinda.
RSF pia ilituamuru kukaa nao. Walituambia, 'Ninyi ni wake wa jeshi la Sudan au wasichana wao.' ... Kisha walitupiga, na walitubaka barabarani, hadharani
Kulikuwa na wanaume tisa wa RSF, saba walinibaka. Nilitaka kupoteza kumbukumbu yangu baada ya hapo, "mmoja mwenye umri wa miaka 17 aliyenusurika kubakwa aliiambia MSF.

Chanzo cha picha, Getty Images
'Walinibaka kwasababu ya cheti changu'
Katika baadhi ya matukio, washambuliaji walishutumu moja kwa moja walionusurika kwa kuunga mkono upande mwingine. Mwanamke mmoja alitoa hadithi yake: "Nina cheti cha uuguzi wa huduma ya kwanza. [Walipotusimamisha], RSF iliniomba niwape begi langu.
Walipoona cheti ndani, waliniambia, 'Unataka kuponya jeshi la Sudan, unataka kuponya adui!' Kisha wakachoma cheti changu, na kunichukua ili kunibaka.
Wakawaambia wengine wote wakae sakafuni. Nilikuwa na wanawake wengine, akiwemo dada yangu.
Ni muhimu kwa walionusurika kupata huduma baada ya shambulio hilo, kwani unyanyasaji wa kingono unahitaji dharura ya kiafya.
Unyanyasaji huo na madhara ya haraka na ya kudumu ya kimwili na kisaikolojia ambayo yanaweza kuhatarisha maisha.
Bado walionusurika wanatatizika kupata huduma za matibabu na ulinzi kwa sababu ya ukosefu wa huduma, ufahamu mdogo wa huduma chache zilizopo, gharama kubwa ya kusafiri hadi kwenye vituo, na kusitasita kuzungumza juu ya unyanyasaji kwa sababu ya aibu, hofu ya unyanyapaa au kulipiza kisasi.
"Siwezi kusema chochote kwa jamii kwa sababu itakuwa aibu kwa familia yangu. Kwa hiyo, sikusema chochote kuhusu kile kilichonipata kabla ya leo.
Ninaomba tu msaada wa matibabu sasa. Niliogopa sana kwenda hospitali.
Familia yangu iliniambia, 'Usimwambie mtu yeyote,'" mwanamke mwenye umri wa miaka 27 aliyenusurika aliiambia MSF mashariki mwa Chad.
Mahali ambapo huduma zipo, walionusurika wanahitaji njia za rufaa zilizo wazi na zinazoweza kufikiwa ili kupata usaidizi wanaohitaji.

Chanzo cha picha, AFP
Katika Darfur Kusini, jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan, mwishoni mwa 2024, MSF iliongeza kipengele cha kijamii katika huduma yake kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia.
Wakunga na wahudumu wa afya ya jamii walifunzwa na kuwezeshwa kutoa vidhibiti mimba vya dharura na msaada wa kwanza wa kisaikolojia kwa walionusurika.
Pia waliunga mkono rufaa ya waathirika kwa kliniki za afya ya msingi zinazoungwa mkono na MSF na hospitali za upili kwa ajili ya huduma ya kina.
Tangu kuongezwa kwa mtindo huu wa kijamii, MSF imeona ongezeko kubwa la wanawake na vijana wanaotafuta huduma.
Timu za MSF zinaendelea kuwaona waathirika wapya wa unyanyasaji wa kijinsia.
Huko Tawila, ambako watu wanaendelea kuwasili baada ya mashambulizi katika kambi ya Zamzam na huko Elf Fasher, Darfur Kaskazini, hospitali ilipokea manusura 48 wa ukatili wa kingono kati ya Januari na mwanzoni mwa Mei, wengi wao tangu kuanza kwa mapigano katika kambi ya Zamzam mwezi Aprili.
"Huduma kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia zinakosekana na, kama huduma nyingi za kibinadamu na afya nchini Sudan, lazima ziongezwe haraka.
Watu - wengi wao wakiwa wanawake na wasichana - wanaoteseka kwa unyanyasaji wa kijinsia wanahitaji huduma za matibabu haraka, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kisaikolojia, na huduma za ulinzi.
Huduma lazima iandaliwe mapema ili kupunguza vikwazo vingi vinavyolemea katika unyanyasaji wa kijinsia," anasema. Kauffman, meneja wa matibabu ya dharura wa MSF.
Mashambulizi ya kikatili na ubakaji lazima yakomeshwe, pande zinazopigana lazima zihakikishe kwamba raia wanalindwa, kuheshimu wajibu wao chini ya Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu ya kulinda raia, na huduma za matibabu za kibinadamu kwa walionusurika katika unyanyasaji wa kijinsia lazima ziongezwe haraka huko Darfur na mashariki mwa Chad.
Ushuhuda - Unyanyasaji wa kijinsia wa Darfur
Ilani: Ni muhimu kulinda usiri wa watu ambao walishiriki hadithi zao nasi.
Watu kadhaa walionusurika walionyesha waziwazi hofu yao ya kile ambacho kingetokea kwao ikiwa mtu yeyote angejua walichokuwa wamepitia.
Kwa ulinzi wao, tumechagua kutoonyesha eneo waliopo katika baadhi ya shuhuda zao kwani inaweza kuwawezesha kutambuliwa.
Katika eneo la Darfur, neno Janjaweed wakati mwingine hutumika kuelezea wanamgambo wa makabila fulani na wakati mwingine wale wa RSF.
Kwa vile huu ni ushuhuda unaotolewa kwa maneno ya watu wenyewe, hatujabadilisha masharti yaliyotumika lakini MSF haijathibitisha iwapo vikundi vilivyohusika katika mashambulizi haya ni vya RSF au wanamgambo wengine au la.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ushuhuda wa 1: "Nataka ulinzi sasa; sitaki kubakwa tena"
Mkimbizi wa kike mwenye umri wa miaka 27 aliyehojiwa huko Tine, mashariki mwa Chad:
Tarehe ya ushuhuda: 06/02/2025
Nilipoteza mama yangu wakati wa vita. Siku moja mnamo Juni 2024 nilikuwa nje ya nyumba yangu huko El Fasher.
Niliporudi, bomu lilikuwa limeanguka kwenye nyumba.
Mama pekee ndiye aliyekuwa ndani. Nilijaribu kumpeleka mama hospitali, lakini alifariki kabla hatujafika.
Baada ya hapo nilikaa El Fasher, lakini baba yangu pia alifariki. Nilikwenda kukaa na dada yangu na mumewe.
Niliondoka El Fasher siku 33 zilizopita, nikitafuta mahali salama.
Tuliondoka kwa gari. Barabarani tulisimamishwa na kikundi cha wanamgambo wa RSF. Walijaribu kuniteka nyara, wakanibaka.
Nina cheti cha uuguzi wa huduma ya kwanza. [Walipotuzuia], RSF iliniomba niwape begi langu. Walipoona cheti ndani, waliniambia, "Unataka kuponya jeshi la Sudan, unataka kuponya adui!" Kisha wakachoma cheti changu na kunichukua ili kunibaka.
Wakawaambia wengine wote wakae sakafuni. Nilikuwa na wanawake wengine, akiwemo dada yangu. Walinibaka tu, kwa sababu ya cheti changu. Kisha gari likawasili kuelekea kwetu, likiwa na watu wapatao 17 ndani wakiwa na bunduki, RSF wakatoroka.
Nataka ulinzi sasa; Sitaki kubakwa tena. Siwezi kusema chochote kwa jamii kwa sababu itakuwa aibu kwa familia yangu. Kwa hivyo, sikusema chochote kuhusu kile kilichonipata kabla ya leo. Ninaomba tu msaada wa matibabu sasa. Niliogopa sana kwenda hospitali. Familia yangu iliniambia, "Usimwambie mtu yeyote". Sina uchungu zaidi. Lakini nina ndoto mbaya juu yake.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla