WARIDI WA BBC: ‘‘Hatimaye nimepata mpenzi nikiwa na miaka 60”

.

Chanzo cha picha, Lucy Ibura

  • Author, Anne Ngugi
  • Nafasi, BBC Swahili

Lucy Iburu, mama na bibi wa miaka 60 kutoka nchini Kenya, kamwe tabasamu halimtoki mdomoni kisa, ni baada ya kufunga ndoa takatifu mwezi uliopita wa Julai mwaka 2023.

Lucy anawanyamazisha wenye maoni kinzani ya kwamba mama au bibi wa rika lake, hana nafasi ya kuwa kwenye mapenzi. Mwenyewe anasema – ‘kila kiungo ambacho kimeumbwa na Mwenyezi Mungu, kina umuhimu. Kwa hivyo anauliza swali; ‘je, ni kwanini niumbwe na hisia za kupenda?’

Vilevile, anasema hakuna kiungo cha binadamu ambacho kinaweza kuitwa cha kizee, kisa kusonga kwa miaka.

‘‘Ni makosa kwa mtu kuwa na maoni kwamba mimi ni mzee sana na kwa hiyo, haoni ni kwanini niwe kwenye mahusiano ya mapenzi katika umri wangu wa miaka 60,” anasema Lucy.

Je, alikutana vipi na barafu wa moyo wake?

fdfdfd

Chanzo cha picha, Lucy Ibura

Kwa zaidi ya miaka 8 Lucy Iburu alikuwa akifanya kazi nchini Saudi Arabia, kama mfanyakazi wa ndani. Kwakuwa ana ukomavu katika kazi za ndani, yeye na Wakenya wengine ambao wanafanya kazi ughaibuni hususani nchini Saudi Arabia, waliunda makundi ya kuwasaidia kuwasiliana wakiwa nje ya nchi yao katika mitandao ya kijami.

Katika pilika pilika hizo mmoja wa swahiba wa Lucy, ambaye alikuwa anafahamu kuwa mama huyu anatafuta mume wa kufunga naye ndoa, alimweleza kuwa amekutana na mwanaume mmoja ambaye anadhani wangefaana.

Lucy anaeleza, yeye na swahiba wake walikuwa na urafiki wa karibu sana kiasi cha kuelezana siri zao. Hivyo Lucy hakuona kama ni jambo la ajabu kwa rafiki yake wa kike kumuunganisha na mwanamme ambaye wangejenga urafiki ambao pengine ungeishia kwenye ndoa.

Mpango huo uliishia kwa Lucy kukutanishwa na mwanamme huyo kwa njia ya mtandao wa kijami. Kuanzia wakati huo ndio safari ya mahaba ya wawili hao ilianza, safari ambayo hatimaye ndoa takatifu ilifungwa mwezi uliopita.

Mapenzi katika umri wa miaka 60

.

Chanzo cha picha, Lucy Ibura

Lucy anasema, moyo unapopenda unapenda. Japo mahaba kati yake na mume wake yalianza yeye akiwa nchini Saudi Arabia na mume akiwa nchini Kenya. Umbali haukuzuia mapenzi yao kumea kwa kasi.

Huku akicheka, Lucy anasema, ‘wakati mmoja nilimuuliza mume wangu kwa njia ya simu, ‘Je, huna wasiwasi kwamba hujui umbo langu na muonekano wangu kamili na tayari umeanza kunipenda?’

Kwa mujibu wa Lucy, mume wake alijibu kuwa, mawasiliano ya moyo yana macho yake na hana haja ya kumuona ili kuhakiki kabla ya kukata kauli ya kufunga pingu za maisha nayeye.

Anasema mahari pamoja na mambo mengine ambayo yalitakikana kulingana na mila za jamii ya Agikuyu - jamii yake Lucy, yalitimizwa na mume mtarajiwa kabla ya hata wawili hao kuonana kwa mara ya kwanza.

Walipokutana kwa mara ya kwanza, hisia na mahaba yao vilikuwa moto moto. Uchumba wao ulikuwa wa mwaka mmoja, kwa mujibu wa mama huyu. Siku zimefunguka kwa njia ya kipekee na mapenzi hufanya kila jambo kuwa jipya.

Lucy pamoja na mume wake sasa wanajitahidi mno kuhakikisha - wanaunganisha familia zao mbili. Lucy alikuwa kwenye mahusiano mengine ambayo sio ya ndoa hapo awali na kujaaliwa watoto na vile vile mume wake.

Mume wake alikuwa amefunga ndoa hapo awali na kwa bahati mbaya mke wake alifariki mwaka 2002. Alitumia muda mwingi kuwalea watoto. Na sasa wanaona jukumu kubwa kando na mapenzi ni kuhakikisha - watoto wa Lucy na wa mume wake wanatangamana na kupendana.

Lucy anaeleza, amekuwa kwenye ndoa zisizo rasmi kwa zaidi ya mara nne na wanaume tofauti. Kila wakati alijikuta ameachwa au hata yeye mwenyewe kuondoka, kutokana na sababu mmoja au nyengine.

Ushauri wake

ererr

Chanzo cha picha, Lucy Ibura

Anasema moja ya mahusiano yake ya hapo awali, aliishi na mwanamme aliyekuwa mpenzi wake kwa miaka 15 na uhusiano huo ulimpa somo kubwa sana, panapohusika ulimwengu wa mapenzi. Pia, amejifunza kwanini wakati mwengine watu hujikuta wamechoka kukaa na mwenza mmoja.

Lucy anafafanua kwa kusema, hilo hutokea kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa wapenzi. Kwa mfano, marafiki au jamii ya karibu au wakati mwengine tangu mwanzo wahusika katika mapenzi wanakosa darubini au mwelekeo wa kiini haswa cha kuwa pamoja.

Fauka ya hayo, anaeleza siku hizi watu wamekosa uvumilivu hasa inapotokea mpenzi mmoja ameishiwa na pesa au mali au hata amepatwa na udhuru. Wengi huondoka na kuchoka kusimama pamoja na wapenzi wao na hivyo kuingia katika mahusiano mapya.

Lucy anatoa wasia hasa kwa wanawake ambao wanaishi bila wenza baada ya kukaa kwenye ndoa ambazo zinafahamika kama ‘‘come we stay.” Yaani ndoa ambazo hazija rasimishwa, kuwa wasikate tamaa.

Kwa sasa Lucy anasema wangali kwenye fungate na mume wake na kwake mapenzi hayana umri.