Waridi wa BBC: 'Walinambia nimerogwa kisa kuzaa watoto wenye changamoto za kiafya'

..

Chanzo cha picha, Susan Mukoyi

Maelezo ya picha, Susan Mukoyi, mwalimu wa shule ya sekondari Ukombozi jijini Dar es Salaam.

"Baadhi ya watu waliniambia huenda nimerogwa, wapo baadhi ya watu walikataza watoto wao wasicheze na wangu wakidhani huenda wataambukizwa kifafa," anaeleza Susan Mukoyi, ambaye ni mama wa watoto wanne, mkazi wa jiji la Dar es Salaam.

Anasema ubaguzi na kunyanyapaliwa na baadhi ya watu katika jamii havikumzuia kushirikiana na mumewe kuwapatia watoto wake malezi bora.

Susan ambaye ni mwalimu wa sekondari jijini Dar es Salaam anajitambulisha kama shujaa wa kipekee, kutokana na kuwalea watoto wake watatu wenye maradhi tofauti akiwemo mwenye changamoto ya moyo, mwenye tatizo la kifafa pamoja na mwingine ambaye sasa ni marehemu aliyezaliwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Wataalamu walimueleza kuwa sababu ya changamoto hiyo ni kuwa hakuzingatia baadhi ya dawa muhimu katika kipindi cha ujauzito wake.

Uzawa wake

Katika hali isiyo ya kawaida, Susan anasema alijifungua mtoto wake wa kwanza vizuri bila tatizo lolote, isipokuwa mtoto wake wa pili ambaye alizaliwa na changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi, alifariki dunia miezi michache baadaye.

Mwaka 2021 alibahatika kujifungua mtoto wake wa nne ambaye alikuwa na changamoto ya moyo. Alianza kuwa na dalili za homa ya mapafu, baada ya kufanya vipimo ilibainika kuwa ana tundu kwenye moyo.

Changamoto hiyo ilipelekea familia ya Susan iliyokuwa ikiishi jijini Arusha, Kaskazini mwa Tanzania kuhamia Dar es Salaam ili kuwa karibu na hospitali ambazo watoto wao wawili walikuwa wakipokea matibabu.

..

Chanzo cha picha, Susan Mukoyi

Maelezo ya picha, Susan na mumewe

'Mume wangu ni faraja yangu nyakati zote'

Wakati wakiyapitia hayo, anasema alipata faraja na msaada mkubwa kutoka kwa mume wake na wafanyakazi wenzake, ambao mara nyingi walimsaidia hasa watoto walipougua kwa muda mrefu mfululizo.

Mama huyo anasema,"Nimewahi kulazwa na watoto hospitalini kwa nyakati tofauti wakiwa mahututi, walimu wenzangu walinisaidia kisaikolojia na hata kunitolea baadhi ya taarifa za dharura ilipobidi…

"…ninakumbuka nilimuuliza mwanangu, kwanini huwaombi wenzako wakusaidie pale usipoelewa? alinijibu kuwa hakuna anayetaka kumkaribia na kuongeza kwamba watoto walimuacha peke yake," anasimulia huku akieleza kuwa mara kadhaa walimuogopa mwanae alipoanguka kwa kifafa.

Unaweza pia kusoma

'Ninajivunia wanangu wanapendana'

..

Chanzo cha picha, Susan Mukoyi

Susan anasema kutokana na kuwafundisha watoto wake kusaidiana na kupendana imemfanya kuwa mama mwenye furaha na amani.

Anasema, "Binti yangu ambaye ana changamoto ya kifafa ana umri wa miaka 13 sasa, anaelewa changamoto ya moyo ya mdogo wake wa mwisho.Wote wanapokea matibabu kwa nyakati tofauti na kwa sasa ninaona nafuu katika maisha yao tofauti na hali ilivyokuwa miaka kadhaa nyuma."

Susan anasema sasa ameanza kuzungumza na wazazi ambao wana watoto wenye changamoto za kiafya kwa kuwatia moyo kwani anaamini kila mtoto ana uwezo wa kufanikiwa, bila kujali changamoto alizonazo.

"Ninatamani kila mtu aelewe kuhusu changamoto hizi mfano kifafa ili inapotokea mtu ameanguka wamsaidie badala ya kumuogopa wakidhani wataambukizwa, ni fikra potofu," anashauri.

Uelewa mdogo wa baadhi ya watu

Susan anasema bado baadhi ya watu katika jamii hawana uelewa mzuri kuhusu changamoto za kiafya na kujikuta wakihusisha na imani potofu.

Anasema," Ninapenda kuendelea kuwaelimisha..."

Unaweza pia kusoma

Imehaririwa na Alfred Lasteck