Waridi wa BBC: Licha ya muonekano wangu najivunia kuwa mwanamke

mm
Maelezo ya picha, Loveness Tarimo, mtunisha misuli
  • Author, Martha Saranga
  • Nafasi, BBC Swahili
  • Akiripoti kutoka Tanzania

"Ndoto yangu kubwa ilikuwa kuwa mchezaji mpira lakini ilikwama kipindi ambacho wazazi hawakuelewa kuwa kuna haja ya kuendeleza vipaji,walikasirika kila nilipotoka shule na kiatu kimeharibika kwa sababu ya kucheza mpira wakati mimi ni binti, kwanini nicheze mpira’’

Loveness Stanley Tarimo 38 ,anasema anapenda kutambulika kama mwanamke wa kawaida kabisa anayejipenda na asiye na majivuno. Muonekano wake haumbadilishi jinsia yake na anajivunia kuwa alivyo.

Loveness amezaliwa katika familia ya watoto wa kike watatu na mmoja wa kiume huko mkoani Kilimanjaro.

‘’Mimi nimetokea kwenye familia ya kawaida ya kikristo kabisa ya wacha Mungu,ingawa mimi ninaonekana kama niko tofauti kidogo,’’anaeleza Loveness huku akicheka.

pia unaweza kusoma
mm

Nilipokuwa mtoto nilichukia kuitwa 'jike dume'

Baada ya kumaliza darasa la saba katika shule ya msingi Kijenge, Arusha Loveness hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari kwa kushindwa kupata ufaulu mzuri na wazazi hawakuwa na uwezo wa kumuendeleza katika shule za kulipia.

Hivyo aliamua kujikita zaidi kwenye michezo jambo alilofurahia sana katika kipindi chote.

Ingawa mazingira ya mpira wa miguu yakiwa ya chini sana kwa upande wake aliamua kuachana na mchezo huo kwani haukumlipa akaamua kujiunga na kujifunza mazoezi ya kujenga mwili.

‘’Maisha ya shule yalikuwa mazuri sana kwangu muda mwingi nilipenda kucheza mpira. Watoto wenzangu walinishangaa kwanini kila mara nilipokwenda uwanjani nilivaa sketi ya shule na kaptura kwa ndani ili nicheze mpira kwa uhuru’’anaeleza akitabasamu

Loveness anasema zipo nyakati hakufurahia wakati wa utoto wake akieleza namna baadhi ya wanafunzi walivyokuwa wakimtania kwa kumuita majina kama 'Tomboy' au jike dume kwa sababu tu alipenda kuongozana na wavulana, "Nilikuwa nikiitwa hivyo ninaenda chumbani ninalia".

‘’Hata nikihitaji kitu sasa hivi siwezi kuomba msichana,ni rahisi sana kumuomba mwanaume kuliko mwanamke."

Pamoja na kuwa tofauti kwa muonekano wa jamii, anajivunia kuwa hakuwahi kuwavunjia heshima wazazi wake, na wanajivunia kuwa na mtoto kama yeye.

mm

Muonekano wangu unanipa fursa katika kazi yangu

mm

Chanzo cha picha, Loveness Instagram

Loveness anasema haikuwa rahisi kujenga mwili kuwa na misuli namna hii.

Ni takribani miaka 10 sasa tangu alipoanza kufanya mazoezi ya kujenga misuli,na sasa anafurahia muonekano wake kwani unampa utofauti na wanawake wengine,anajisikia mrembo zaidi.

Anasikitishwa na namna baadhi ya watu wasivyomtathmini na kumpa majina kama Tom boy na mtu ambaye amekataa jinsi yake, anasema inamshangaza haelewi tatizo nini.

‘’Kipindi cha nyuma kweli ilinisumbua lakini sasa hivi ninazidi kupenda nilivyo kwani hakuna kitu kizuri kama kujikubali.

Kwa maisha ya sasa hivi ukisema uhangaike na kila mtu ili akuelewe utasumbuka sana. Siwezi kuwalazimisha watu kunielewa nimeachana nao".

Muonekano wake umempa fursa ya kujiingizia kipato kwa kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali ambao wamekuwa wakimfikia na kuwafundisha.

‘’Namshukuru Mungu nimekuwa nikipata sana wateja ambao wengi ni wanawake kidogo imeniongezea kipato’’

Idadi ya walimu wa mazoezi wa kike kuwa ndogo, kwa Loveness imekuwa fursa, "Wateja wangu wengi wa kuwafundisha mazoezi ni wanawake waislamu, wahindi na waarabu kwasababu ya imani yao wanaona ni bora wanichague mimi mwanamke kuliko kufundishwa na mwanaume. Wameshaniamini mimi ni jinsi ya kike na muonekano wangu hauwapi wasiwasi wowote, "Loveness anaeleza.

Loveness anasema ‘’Unajua wenzetu kidogo haiwasumbui kwani michezo hii ya wanawake kuwa na misuli mikubwa kwao ipo,lakini kwa hasa watanzania kushangaa nawaelewa tu’’

Kwanini amechagua muonekano huu na sio wa kike?

"Nilivutiwa na dada mmoja mkenya anaitwa Eveline, yeye anaongoza kwa watunisha misuli wanawake nchini Kenya,’’Loveness anasimulia.

Imezoeleka hata katika maeneo mengine duniani wapo watunisha misuli wa kike wenye kuvalia vitu vya kike kama mavazi, hereni, kusuka au kufuga nywele ndefu na kujipodoa?

Loveness anasema 'kibongobongo' ili kutunza muonekano wa kike ni gharama sana,"nimechagua kuwa hivi kwa sababu ya mambo mengi huko kwa wenzetu ujue wana wafadhili, wana maisha mazuri, wana pesa sio kama sisi tunakula ugali maharage, alafu kuwa na nywele au kujipodoa sio kigezo pekee cha kuwa mrembo,’’anaeleza huku akiangua kicheko.

Loveness anasema rafiki zake wengi ni wanaume hana mashosti akimaanisha hana marafiki wa kike.

Loveness huku akicheka anasema kwamba hana khanga wala kitenge na hajawahi kuvaa viatu virefu vya kike (high hills)..

Familia yake inamuunga mkono na kujivunia kwa kile anachokifanya na namna alivyoamua kuwa na muonekano wa kujazia misuli.

Ndugu zangu wananipa moyo sana hata sasa natarajia kwenda kwenye mashindano ya kutunisha misuli ya Afrika mashariki Oktoba 12 huko Nairobi wananiunga mkono sana ili kufanikisha azma yangu ya kuwakilisha Tanzania katika mashindano hayo.

Katika mashindano ya kutunisha misuli Afrika mashariki mwaka juzi alishika nafasi ya pili, mwaka jana nafasi ya sita, safari hii anajipanga ashike nafasi ya kwanza.

mm

Chanzo cha picha, Loveness

Mwaka 2019 Loveness alitunukiwa taji la miss Fitness Tanzania alijiskia vizuri kwani iliashiria kwamba anaweza kutimiza ndoto yake hiyo ya kuwa mwanamke mtunisha misuli bingwa mwenye mafanikio ndani ya nchi na nje ya Tanzania.

Loveness anasema watu wenye muonekano kama wake wanatafutwa sana, hivyo yeye hawazingatii sana wanaomdhihaki na kumuita majina ya kuudhi mtandaoni.

Kwa sasa Loveness anasema anaye mpenzi tayari na masuala ya kuoana ni majaliwa ya Mungu.

Anasema akijaaliwa Watoto sawa atafurahi ni Jambo jema la kawaida.

‘’Nimeamua kuwa na huyo mtu kwa sababau ameweza kunikubali jinsi nilivyo,kwa sababu yeye tumekutana gym’’

Siri kubwa ambayo yeye na watu wengi wanaopenda kufanya mazoezi ni hawapendi kugombana, 'sijawahi kugombana na mtu au kumpiga mtu kwa sababu ya ugomvi.'

Hata hivyo Loveness alithibitisha kuwa huwa anapata kazi za ulinzi(bodyguard ) haswa za wanawake mfano niliitwa kuwa mlinzi na nikafanya kazi nzuri kabisa lakini sikuwahi kumpiga mtu.

mm

'Usichopenda kufanyiwa na wewe usifanyie wengine'

Kuna wakati sikuelewa watu walionibeza na kuniita majina, nilijiskia vibaya hata kulia lakini baadae nimekuja kuelewa na kujifunza kwamba huwezi kuwafurahisha watu wote.

‘’Lakini usichopenda kufanyiwa na wewe usifanyie wengine, jamii itambue kwamba na mimi nilizaliwa, nina wazazi wangu ambao walinizaa na wananipenda na kuniombea mema, sifurahishwi na namna natupiwa maneno ya kejeli matusi na fikra potofu mtandaoni’’

Loveness anasema anafurahia na kujivunia alivyo kwani Mungu amemuumba hivyo na anaishi anavyotaka yeye.

Loveness anawaambia watu wanaoona anaharibu muonekano wake wa kike anapenda kuwaambia wamuache alivyo kwani kwake anaona ni kipaji alichojaaliwa na kinamletea mafanikio.

Kwa wanaopenda kuwa kama yeye wasiogope kuingia kwenye mchezo huo ingawa bado wanahitaji kuungwa mkono na wadau na serikali.

''Kuvaa suruali na kufanya mazoezi kuwa mkakamavu sio kitu kibaya. Haiwezekani sote tukafanana na kwangu mimi nimechagua kuwa wa kipekee na upekee wangu ndio huu katika muonekano wangu''.

Anajiona akiendelea kujifunza na kusonga mbele katika elimu ya mazoezi ambayo anasema inabadilika kila siku.

Ndoto yake ya baadae ni kupambana kufanikisha kuwa na kituo chake cha mafunzo ya mazoezi ya ujenzi wa mwili na masuala ya lishe haswa kwa wanawake wanaopenda kujenga misuli.

Anasema ndoto ambazo hazifanyiwi kazi ni ngumu kutokea.

Pia unaweza kusoma

Imehaririwa na Esther Namuhisa na kuchapishwa na Seif Abdalla