Jinsi PSG na Inter wanavyobadili dhana ya 'ligi ya wakulima'

UEFA

Chanzo cha picha, UEFA

  • Author, Sean Kearns
  • Nafasi, BBC Sport

Wakati Paris St-Germain (PSG) na Inter Milan watakapoingia uwanjani Allianz Arena jijini Munich, Ujerumani Mei 31, 2025 itakuwa ni fainali ya Ligi ya mabingwa ya kwanza katika miaka 21 ambayo haishirikishi klabu kutoka ligi kuu England (EPL), Ligi ya Ujerumani (Bundesliga) au ile ya Hispania (La Liga).

Angalau klabu moja ya Uingereza, Ujerumani au Hispania imekuwa ikiingia kwenye fainali ya ligi ya mabingwa tangu Porto chini ya Jose Mourinho ilipoishinda Monaco kwenye fainali ya mwaka 2004. Mabingwa 14 waliopita wa michuano hii wametoka katika mojawapo ya mataifa hayo matatu ama ligi hizo tatu, jambo lililopelekea mashabiki wengi mara nyingi kupuuza ubora wa ligi nyingine Ulaya.

Meneja wa PSG, Luis Enrique, alirejelea hilo kwa mzaha baada ya timu yake kuifunga Arsenal kwenye nusu fainali, akisema: "'Ligi ya wakulima, si ndiyo? Sisi ndio ligi ya wakulima!

Neno hilo hutumiwa na mashabiki wa soka hasa kutoka Uingereza kupuuza ligi zingine za nchi za Ulaya, ambapo ubora wa soka unachukuliwa kuwa dhaifu kuliko ule wa Ligi kuu ya England (EPL)

Ingawa PSG na Inter zimeonyesha kitu tofauti kuhusu dhana hiyo kwa kuingia fainali ya Mabingwa Ulaya.

Hili inamaanisha nini kuhusu timu hizo na ligi zao za ndani na nguvu inayochukuliwa kuwa EPL ni bora zaidi?

Kuachana na 'Galacticos'

PSG

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Lionel Messi, Kylian Mbappe na Neymar walicheza pamoja PSG kwa misimu miwili

Ni Luis Enrique pekee ndiye anayejua kama kweli aliamini maneno yake aliposema PSG ingekuwa bora zaidi bila Kylian Mbappe. Nahodha huyo wa Ufaransa, ambaye ndiye mfungaji bora wa klabu wa muda wote, alikuwa ametoa hadharani uamuzi wake wa kuondoka Mei 2024 wakati Luis Enrique aliposema timu yake ingekuwa bora zaidi, katika eneo la ushambuliaji na ulinzi.

"PSG itaendelea kuwa timu kubwa na tutazidi kuwa bora. Tutaleta wachezaji wenye akili timamu na wachezaji wanaokwendana na klabu, ndivyo maisha yanavyokwenda," alisema Luis Enrique. Miezi12 baadaye wachache wangepinga utabiri wa Luis Enrique baada ya timu yake kushinda taji la ligi kuu Ufaransa (Ligue 1) zikiwa zimesalia mechi sita na bila kupoteza mchezo.

Urahisi waliotumia kushinda taji la ndani na uhaba wa upinzani mkali ungeweza kuonekana kama kitu hasi katika kujenga mafanikio barani Ulaya. Marseille, mwaka 1993, inabaki kuwa mabingwa pekee wa Ufaransa waliotwaa taji la Ligi ya Mabingwa.

Baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi ya Mabingwa mwaka 2020, PSG ilifika nusu fainali mara mbili na robo fainali mara mbili katika miaka minne iliyofuata. Lakini kulikuwa na kukubalika kufuatia kuteuliwa kwa Luis Enrique mwaka 2023 kwamba kitu fulani kilipaswa kubadilika kama wangetaka kuvuka mstari kuingia fainali na kutwaa ubingwa.

Msimu huo wa joto mshambuliaji Lionel Messi aliondoka kujiunga na Inter Miami na Neymar akauzwa kwenda klabu ya Saudi Arabia Al-Hilal. Hii iliashiria mwanzo wa mwisho wa enzi ya 'Galactico', huku kuondoka kwa Mbappe miezi 12 baadaye kulimaliza 'Galactico kwa maana ya mastaa wakubwa waliokuwepo. Bila wao, Luis Enrique alijenga timu inayocheza kwa kasi, presha ya juu kwa taswira yake, ikitegemea ushirikiano wa timu badala ya mchezaji mmoja mmoja.

Barani Ulaya msimu huu PSG ilianza vibaya na kumaliza hatua ya makundi katika nafasi ya 15. Lakini, wakiongozwa na mchezaji mpya walio msajili Januari, Khvicha Kvaratskhelia, PSG wamevichapa vilabu vinne vya Uingereza, Manchester City, Liverpool, Aston Villa na Arsenal katika mashindano hayo.

Uzoefu ni muhimu kwa Inter

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Inter ina wazoefu wengi kikosini

Ushindi wa Inter katika nusu fainali dhidi ya Barcelona utaoingizwa kama mojawapo ya mechi mbili bora zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa. Barcelona, wakiongozwa na Lamine Yamal mwenye umri wa miaka 17, walizidiwa na uzoefu na ujuzi wa Inter Milan ya Simone Inzaghi.

Inzaghi alikuwa na wachezaji 10 wenye umri zaidi ya miaka 25 katika kikosi cha kwanza katika mechi dhidi ya Barca, huku Barcelona wakiwa na wachezaji sita tu wenye umri wa zaidi ya miaka 25. sco Acerbi, 37, akawa mfungaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa alipofunga bao la kusawazisha dakika ya 93 na kupeleka mechi kwenye muda wa ziada huko San Siro.

Yan Sommer, 36, alijiunga na Inter kwa pauni milioni 5 kufuatia uhamisho wa Andre Onana wa pauni milioni 44 kwenda Manchester United mnamo 2023. Kipa huyo wa Uswisi aliokoa michomno kadhaa kuisaida Inter katika mchezo huo kabla ya bao la kushangaza la Acerbi. Viungo Henrikh Mkhitaryan na Hakan Calhanoglu wana jumla ya umri wa miaka 67.

Kama PSG, Inter wamekabiliwa na maoni ya kubeza kutoka kwa mashabiki wanaodharau ubora wa ligi ya Italia, Serie A. Lakini timu ya Inzaghi iliwaondoa Bayern Munich katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa hatua ya makundi, wakipoteza mechi moja tu kati ya nane.

Mabingwa hao wa Serie A katika misimu miwili kati ya minne iliyopita, Inter wameshinda Kombe la Uropa mara tatu, hivi karibuni mnamo 2010 chini ya Mourinho.

Changamoto mabingwa Ulaya, lakini mafanikio katika michuano ya Europa na Conference

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chelsea ni mabingwa wapya wa Conference League

Arsenal walikuwa timu pekee ya Uingereza kufikia nne bora ya Ligi ya Mabingwa, lakini fainali ya Ligi ya Europa imewakutanisha Manchester United na Tottenham Hotspurs, ambapo Spurs walishinda bao 1-0 na kutwaa taji hilo huko Bilbao Mei 21, Hispania.

Tottenham, washindi mara mbili wa Kombe la UEFA, walitwaa Ligi ya Europa kwa mara ya kwanza tangu 1984, huku United wakiwa wameshinda mara ya mwisho mwaka 2017 na kumaliza nafasi ya pili miaka minne baadaye.

Katika Ligi ya Europa Conference, Chelsea, washindi mara mbili wa Ligi ya Mabingwa, wametwaa taji la Europa Conference wiki hii na kuwa klabu ya kwanza duniani kushinda Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Europa na Ligi ya Europa Conference.