TikTok inavyonufaika kutokana video za ngono zinazohusisha watoto

Picha iliyoundwa inayoonyesha mwanga wa mviringo, simu ya rununu inayoonyesha picha iliyofifia ya msichana anayecheza dansi, na picha  ya sehemu ya nembo ya TikTok.
  • Author, Nalini Sivathasan, Patrick Clahane & Debula Kemoli
  • Nafasi, Uchunguzi wa BBC & Africa Eye

Nchini Kenya mtandao wa kijamii wa TikTok umekuwa ukipata faida kutokana na matangazo ya moja kwa moja yenye maudhui ya ngono inayohusisha vijana wadogo walio na umri wa miaka 15, BBC yaambiwa.

Tulizungumza na wanawake watatu wa Kenya ambao wanasema walianza shughuli hii wakiwa vijana wadogo.

Wanatuambia walitumia mtandao wa Tiktok kujinadi na kuafikiana malipo ya ziada ili wachapishe maudhui ya faragha ambayo yangerushwa kwa mitandao mingine.

TikTok imepiga marufuku kutongozana lakini kampuni hiyo inajua shughuli inafanyika, wasimamizi waambia BBC.

TikTok huchukua takriban asilimia 70% kutoka kwa biashara za chapisho za mubashara, hili tuligundua hapo awali.

Hata hivyo Tiktok iliambia BBC ''hairuhusu unyanyasaji''.

Video za moja kwa moja ni maarufu nchini Kenya katika mtandao wa TikTok- usiku wa manane tumekutana na video nyingi ambazo wanawake wananengua viuno vya kusisimua watazamaji ambao wanafuatilia kote ulimwenguni.

Tahadhari: taarifa inajumuisha maudhui ambayo yanaangazia lugha ya ngono

Mchezaji dansi aliye upande wa kushoto wa skrini ya TikTok na watumiaji ambao wanatazama video ya moja kwa moja kwenye visanduku vilivyo upande wa kulia wa skrini - sura zao zimefichwa  kwa sababu za faragha.
Maelezo ya picha, Picha ya skrini ambayo haionekani vizuri ya video za mubashara za TikTok - baadhi ya waigizaji (kulia) wanaibadilisha kwa zamu na kucheza kwa kukisia kwenye skrini kuu (kushoto)

Ni saa mbili asubuhi jijini Nairobi, na video za mubashara za TikTok zimechacha.

Nyimbo zimeanikiza, watumizi wakipiga soga, huku mwanamke mmoja anaonekana akijielekeza kamera na kuanza kunengua kiuno kutamanisha.

Vikorombezo vya ''zawadi'' vinaanza kujaa kwa skrini.

''Nitumie arafa ukitaka kuona utupu wangu. Tap, Tap, mcheza dansi huyo anarudia. ''Tap, tap,'' ni neno lililozoeleka katika mtandao wa TikTok likiwa na maana watazamaji waonyeshe ishara ya upendo na kuthamini maudhui yako.

Watazamaji wanaelekezwa kutuma arafa ya faragha katika akaunti yake ya TikTok ikiwa wanahitaji kutazama mchezaji dansi huyo akijipiga punyeto, akivua nguo na pia akifanya maonyesho ya ngono akiwa na wanawake wengine.

Katika baadhi ya matangazo ya moja kwa moja tulioyatazama, sajili ya ngono ilitumika kunadi huduma za ngono.

Zawadi kwa njia ya vikorombezo vya kidijitali ambavyo hubadilishwa na kuwa fedha halisi hutumika kama malipo kwa mtandao wa Tiktok- hata hivyo TikTok huondoa vitendo vya ngono na uchi vinavyochapishwa- ili biashara inoge zaidi wanahamia katika mitandao mbadala kutuma video hizo.

''Sio jambo la manufaa la TikTok kuondoa video za kuomba ngono- watu wengi wakizawadiana kwenye matangazo ya moja kwa moja.. ni faida kwa TikTok,'' anasema aliyekuwa msimamizi wa TikTok nchini Kenya kwa jina Jo - akiwa miongoni mwa wasimamizi 40,000 ambao TikTok inasema imewaajiri kote ulimwenguni.

Pia unaweza kusoma:

Tuligundua kuwa TikTok bado inapokea asilimia 70 ya mapato kutoka kwa zawadi za matangazo ya moja kwa moja.

Kampuni hiyo ilikana kuchukua ada kubwa kiasi hicho baada ya sisi kuthibitisha ada hiyo katika uchunguzi wa 2022.

TikTok imekuwa ikifahamu kuhusu unyanyasaji wa watoto katika matangazo ya moja kwa moja tangu mwaka 2022, lakini ilipuuzilia mbali suala hilo kwa sababu "ilifaidi sana" kutokana na hali hiyo, kulingana na madai ya kesi iliyoletwa na jimbo la Utah, Marekani, mwaka jana.

TikTok ilijibu kuwa kesi hiyo - ambayo bado inaendelea - ilipuuzilia mbali "hatua za awali" zilizochukuliwa kuboresha usalama.

Kenya ni kitovu cha unyanyasaji huu, inasema shirika la ChildFund Kenya, ikichochewa kupendelewa na vijana na matumizi makubwa ya mtandao.

Bara la Afrika kwa ujumla lina udhibiti mdogo wa mtandao ikilinganishwa na nchi za Magharibi, iliongeza shirika hilo.

Mifano ya zawadi za TikTok - emoji zinazoonyesha waridi, koni ya aiskrimu na mkono ulioshikilia moyo
Maelezo ya picha, Malipo kwenye TikTok, kwa kawaida kwa shughuli kama vile mafunzo ya urembo, hufanywa kupitia "zawadi" za emoji ambazo zinaweza kubadilishwa kuwa pesa.

Jo, ambaye alifanya kazi kwa Teleperformance - kampuni iliyokodishwa na TikTok kutoa usimamizi wa maudhui - anasema wasimamizi wanapewa mwongozo wa maneno au vitendo vya ngono vilivyopigwa marufuku.

Hata hivyo, mwongozo huu ni finyu, anasema Jo, na hauzingatii maneno ya mtaani au ishara nyingine za uchochezi.

"Unaweza kuona kwa jinsi wanavyosimama, kwa kamera kuwafikia kwenye kifua na mapaja yao [kwa mfano], kuwa wanahamasisha ngono. Wanaweza kutosema chochote, lakini unaweza kuona wanajielekeza kwenye akaunti yao [ya jukwaa lingine], lakini hakuna chochote ninachoweza kufanya."

Msimamizi mwingine wa maudhui wa Teleperformance, ambaye tunamwita Kelvin, anasema usimamizi unadidimia kutokana na ongezeko la utegemezi wa TikTok kwa akili bandia (AI), ambayo anasema haitambui vya kutosha maneno ya ngono ya mtaani.

Jo na Kelvin ni miongoni mwa wasimamizi saba wa maudhui, wa sasa na wazamani, wanaofanya kazi na TikTok, waliotuambia kuhusu wasiwasi wao.

Jo anasema karibu asilimia 80 ya matangazo ya moja kwa moja zilizoripotiwa kwenye mifumo ya wasimamizi wa maudhui zilikuwa za ngono, au za kutangaza huduma za ngono, na TikTok inafahamu ukubwa wa tatizo hili.

Msimamizi, ambaye amevalia fulana iliyo na kofia kumzuia asionekane sura, aonesha ripota wa BBC picha kutoka kwa TikTok
Maelezo ya picha, Mtoa taarifa ambaye jina lake halisi tumelibana anayehudumu kwa kampuni inatengeza maudhui kwa niaba ya TikTok amezungumza na BBC

ChildFund Kenya na mashirika mengine ya msaada wameiambia BBC kwamba watoto wadogo wa umri wa miaka tisa wanahusishwa na shughuli hizi.

Tumezungumza na matineja wa kike na wasichana wadogo wanaosema wanatumia hadi saa sita au saba wakati wa usiku kwenye shughuli hii na kupata wastani wa £30 kwa siku - kiasi kinachotosheleza kulipa chakula na usafiri wa wiki moja.

"Nauza mwili wangu kwenye TikTok. Ninacheza uchi. Nafanya hivyo kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kupata pesa ili kujisaidia," anasema msichana mwenye umri wa miaka 17, ambaye tunamwita Esther.

Anaishi katika kitongoji duni cha Nairobi, ambacho wakazi 3,000 wanatumia choo kimoja.

Anasema pesa hizo humsaidia kununua chakula kwa mtoto wake, na kumsaidia mama yake ambaye amekuwa akishindwa kulipa kodi tangu baba yake alipofariki.

Anasema alikuwa na umri wa miaka 15 alipokuwa anafundishwa kuhusu matangazo ya moja kwa moja ya TikTok na rafiki yake, ambaye alimsaidia kuvuka vikwazo vya umri - kwa kuwa watu wazima wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ndio wanaweza kutumia video za mubashara.

Watumiaji wanahitaji pia angalau wafuasi 1,000 ili kuweza kuanzisha matangazo ya moja kwa moja.

Hivyo, watumiaji wa TikTok wenye wafuasi wengi wanaweza kuwa wakiritimba wa kutongozea - wakiongoza matangazo ya moja kwa moja yanayouza maudhui ya ngono.

Baadhi yao wana akaunti za akiba, zikionyesha kuwa wamepigwa marufuku au maudhui yao yamesitishwa na TikTok hapo awali.

Wanaonekana kujua jinsi ya kuepuka kugunduliwa na wasimamizi wa maudhui wa TikTok, huku wakijenga mvuto wa ngono ili kuvutia wateja.

"Unaponengua kiuno, simama mbali na kamera, vinginevyo akaunti yako itapigwa marufuku," mkiritimba wa ngono anamuarifu kwa sauti mwanamke anayecheza kwa mtindo wa kutingisha viungo kwenye skrini.

Kwa malipo ya kujumuishwa kwenye video za mubashara, wanawake hao wanawapa mabosi wao ambao wanamiliki akaunti hizo sehemu ya mapato yao.

Uhusiano huo ni rahisi kugeuka kuwa wa unyanyasaji, anasema Esther. Anasema mkiritimba wake wa dijitali alitambua wazi alikuwa na umri wa chini ya miaka 18, na alipendelea sana kutumia ''wasichana wachanga''.

Alikuwa akimshinikiza kupata pesa zaidi - kumaanisha kuwa alihitaji kufanya video za mubashara zaidi - na alichukua sehemu kubwa ya mapato yake kuliko alivyotarajia, anasema.

"Hivyo, ikiwa emoji inatumwa yenye thamani ya 35,000 Ksh (£213), yeye anachukua 20,000 Ksh (£121) na wewe unapokea 15,000 Ksh (£91)."

Kumfanyia kazi ilikuwa kama kujifunga "na pingu", anasema. "Wewe ndiye unayeumia kwa sababu yeye anapata sehemu kubwa zaidi na ingawa ni wewe uliye tumika."

"Sophie", si jina lake halisi, ambaye anasema alikuwa na umri wa miaka 15 alipokuwa anaanza matangazo ya moja kwa moja kwenye TikTok, anasema alipokea maombi kutoka kwa wanaume wa Ulaya kwa huduma kwenye jukwaa lingine, akiwemo mmoja mtumiaji kutoka Ujerumani ambaye alimtaka kugusa matiti na sehemu zake za siri kwa pesa.

Sasa akiwa na miaka 18, anajutia kazi yake ya ngono mtandaoni.

Baadhi ya video alizotuma kwa watumiaji kupitia majukwaa mengine zilipakiwa kwenye mitandao ya kijamii bila idhini yake, anasema.

Majirani zake walijua, na kuwatahadharisha vijana wengine wasihusiane naye, aliiambia BBC.

"Wananihusisha na kondoo waliopotea, na vijana wanaambiwa kuwa nitawaongoza vibaya. Mimi ni mpweke mara nyingi."

Baadhi ya wasichana na wanawake tuliowazungumzia wamesema pia walilipwa kukutana na watumiaji wa TikTok kwa ngono ana kwa ana, au walishinikizwa kufanya ngono na mabosi wao wa kidijitali.

TikTok inataka kujiimarisha katika masoko ya Afrika, lakini haijajiri wafanyakazi wa kutosha ili kudhibiti maudhui ipasavyo, walisema wasimamizi wa maudhui Kenya.

Serikali ya Kenya imeonyesha dalili za kukubali tatizo hili - mwaka 2023, Rais William Ruto alifanya mkutano na Mkurugenzi Mtendaji wa TikTok, Shou Zi Chew, kuhimiza uboreshaji wa usimamizi wa maudhui kwenye jukwaa.

Serikali ilisema kampuni hiyo ilikubali kudhibiti vizuri, ikiwa na ofisi ya TikTok nchini Kenya kusaidia kuratibu shughuli.

Lakini wasimamizi tuliowazungumzia walisema, zaidi ya miezi 18 baadaye, hakuna kilichotokea.

Teleperformance ilijibu kuwa wasimamizi wao "hufanya kazi kwa bidii kugundua na kupokea malalamishi kuhusu maudhui yaliyoundwa na watumiaji kulingana na viwango vya jamii na miongozo ya wateja", na kwamba mifumo ya wateja wao haijaandaliwa kuwaruhusu Teleperformance kuondoa maudhui yasiyofaa au kuyaripoti kwa mamlaka za kutekeleza sheria.

Msemaji wa TikTok aliiambia BBC:

"TikTok hairuhusu unyanyasaji. Tunatekeleza sera kali za usalama, ikiwa ni pamoja na sheria madhubuti za maudhui ya matangazo mubashara, usimamizi katika lugha 70, ikiwemo Kiswahili, na tunashirikiana na wataalamu wa ndani na watengenezaji maudhui, ikiwemo Baraza la Usalama la Afrika la jangwa la Sahara, ili kuimarisha mbinu zetu."

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi