Kuomba radhi kwa Marais Ruto na Museveni ni mwanzo mpya au danganya toto?

Chanzo cha picha, William Samoei Ruto/Facebook
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka Nairobi
Wiki hii imeshuhudia matukio ambayo ni nadra sana kutokea, Marais William Ruto wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda wameomba msamaha hadharani kwa makosa ambayo yametendeka katika nchi zao.
Mtazamo wa wengi, kuomba radhi ni miongoni mwa mambo magumu sana kusema ama iwe kosa lako binafsi au kwa niaba ya wengine.
Watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti kuhusu 'kuomba radhi', kuna wale wanaoweza kuelewa hatua hiyo labda pengine kama njia ya kujirudi, lakini upande wa pili wa shilingi, wako wanaoweza kuchukulia hatua hiyo kama mapungufu.
Lakini vipi kuhusu msaha unatolewa na rais. Ukweli ni kwamba, hii pia inaweza kutosheleza hitaji lile lile, la msamaha unaotelewa na mtu binafsi.
Lakini nini hasa kilitokea kwa marais William Ruto wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda?
Vigogo wa Kenya na Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Yoweri Museveni na mkewe kwa pamoja wiki hii walikiri kuwepo kwa mapungufu katika uongozi, kutokea kwa ufisadi na kuomba msamaha kwa makosa ambayo yametokea katika kipindi cha uongozi wao.
"Kama viongozi wakuu wa National Resistance Movement (NRM), tunawajibika kwa makosa yote tuliyofanya sisi wenyewe, mawakala wetu na wawakilishi wetu. Kwa hiyo, tunasimama hapa kutubu na kuomba radhi hasa wananchi wa Buganda na nchi nzima. Tunaomba urejesho na upendeleo.

Chanzo cha picha, AFP
Nchini Kenya, Jumatano, Mei 28, 2025 wakati wa hotuba yake kwa taifa katika hafla ya maombi ya kitaifa ambayo huleta pamoja viongozi wa serikali, Rais Ruto aliomba msamaha kwa Wakenya na mataifa jirani.
Katika hotuba yake, Ruto alisema ikiwa kuna jinsi viongozi wamewaendea visivyo vijana wa Gen Z, basi anaomba radhi.
"Kwa watoto wetu, ikiwa kumekuwa na makosa yoyote, tunaomba msamaha," rais aliwaambia vijana wa nchi hiyo, maarufu kama Gen Z, ambao wamekuwa mwiba katika utawala wake.
Hii ilikuwa mara ya kwanza rais kuomba msamaha kwa vijana, kufuatia mwaka wa mvutano kati ya serikali yake na vizazi vya Gen Z na Millennia.
Rais Ruto hakuishia hapo, pia aliyaomba radhi mataifa jirani ya Uganda na Tanzania katika hatua ambayo inaonekana kama juhudi za kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo ya Afrika Mashariki.
"Jirani zetu wa Tanzania kama tumewakosea kwa namna yoyote tunaomba radhi, wenzetu wa Uganda ikiwa kuna jambo ambalo Wakenya wamefanya ambalo sio sahihi tunawaomba radhi," alisema Rais Ruto.
Rais pia aliwahimiza Wakenya kuishi kwa amani licha ya tofauti zao za kisiasa, akisisitiza hitaji la kujenga taifa lenye umoja na amani.
Akinukuu Kitabu cha Zaburi 133, Ruto alisema: "Neno la Mungu linasema jinsi ilivyo muhimu kwa watu kuishi kwa umoja".
"Tunataka kutembea hii safari pamoja, kujenga mahusiano kwa misingi ya kuheshimiana na kuelewana."
Wanakosolewa kwa nini?
Kwa muda mrefu, Uganda imekuwa ikikosolewa kwa demokrasia inyoendelea kudidimia na kukandamiza upinzani na ukosefu wa haki za binadamu.
Tukirejelea hotuba yake, Museveni aliomba radhi jamii ya Buganda kwa makosa ambayo yametokea.
Baadaye, msemaji wa ufalme wa Buganda Bw Israel Kizibwe Kitooke, alimtaka rais huyo kukumbuka aliyoahidi. Pia walitoa wito wa kuangaziwa kwa suala la unyakuzi wa ardhi, utekaji nyara na mengine yasiofurahisha ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini Uganda.
Wakichanganua hotuba ya rais, baadhi ya wachanganuzi walizungumzia kile walichokiita ukatili wakimlenga mwanasiasa wa Upinzani Kizza Besigye ambaye bado anahangaika gerezani tangu alipokamatwa akiwa jijini Nairobi nchini Kenya na kusafirishwa Uganda.

Chanzo cha picha, Reuters
Majuma kadhaa yaliyopita, picha za kudhoofika kwa mpinzani wake Besigye ambaye alikuwa daktari wake binafsi zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikibainika kwamba alikuwa kwenye mgomo wa kususia chakula.
Mpinzani mwingine ambaye amejipata matatani mara nyingi nchini Uganda ni Robert Kyagulanyi maarufuku kwa jina lake la usanii Bobi Wine.
Kwasasa, ndiye kiongozi wa chama cha National Unity Platfform baada ya kuchaguliwa kama mgombea wa urais wa chama hicho.
Bobi Wine amekuwa akilengwa na ukandamizaji wa serikali.
Utawala wa rais Museveni uliwahi kumzuia kutofanya matamasha na kupiga marufuku umma kutovaa kofia nyekundu ambazo zilishirikishwa na nembo ya Peoples power, kikundi alichokianzisha.
Ni miongoni mwa wale waliokamatwa kwenye msako wa serikali, na pia aliwahi kushtakiwa kwa uhaini na kumiliki silaha.
Kuna kipindi kukamatwa kwa Bobi Wine kulisababisha maandamano ya kitaifa ambapo watu wasiopungua 54 waliuawa.
Kama inavyoshuhudiwa kwa Besigye, wakati Bobi wine alipokuwa gerezani kwa siku kumi alipigwa vibaya na maafisa wa usalama wa serikali kiasi cha hata kushindwa kutembea.
Kulingana na mtazamo wa wengi, ukijitokeza kumpinga Rais Museveni, kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kujipata mashakani chini ya utawala wake.
Nchini Kenya, Ruto hivi karibuni amekuwa na wakati mgumu kukabiliana na vijana ambao mara kadhaa wameonyesha kupinga hatua zinazochukuliwa chini ya utawala wake.
Mfano, vijana walikuwa mstari wa mbele kupinga mswada wa fedha 2024 jijini Nairobi, na kusababisha maandamano makubwa kote nchini kuwahi kushuhudiwa katika miaka hivi karibuni.
Matokeo yake vijana wengi walipoteza maisha, kutekwa nyara na wengine wengi wakiwa hawajulikani walipo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pia suala la wanaharakati kukamatwa sio geni nchini Kenya.
Mwanaharakati Boniface Mwangi amewahi kujikuta mikononi mwa polisi mara kadhaa. Kuna kipindi alichukuliwa kutoka nyumbani kwake na watu waliovalia nguo za raia lakini baadaye ilisemekana kwamba amekamatwa kwa kosa la kusababisha vurugu.
William Ruto ameomba msamaha Tanzania na Uganda kwa kile ambacho kilionekana kuwa mvutano kati ya Kenya na nchi hizo kwenye mitandao ya kijami.
Baadhi ya Wakenya wamekuwa wakimlenga Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuatia hatua ya hivi majuzi ya kufurushwa kwa wanaharakati Boniface Mwangi.
Yeye pamoja na mwenzake Agather Atuhaire walizuiliwa kwa siku kadhaa nchini Tanzania kabla ya kuachiliwa huru, walipokuwa wameenda kushuhudia kusikilizwa kwa kesi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu ambaye aliwekwa kizuizini.
Wawili hao walidai kuwa waliteswa, kabla ya kuachwa mpakani na vikosi vya usalama vya Tanzania, jambo lililokosolewa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu katika eneo hilo.
Hata hivyo, Tanzania bado haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo ya mateso lakini awali Rais Samia alikuwa ameonya kwamba hatawaruhusu wanaharakati kutoka nchi jirani "kuingilia" masuala ya nchi yake na kusababisha "machafuko".
Kauli ya Rais Samia iliibua majibizano makali kati ya raia nchi hizo mbili za Afrika Mashariki huku watumiaji wa mtandao wakiwa katika mzozo wa muda mrefu kuhusu siasa za kikanda na uanaharakati.
Wanamaanisha walichosema au ni danganya toto?
Msahama wa Rais William Ruto nchini Kenya umepokelewa kwa hisia mseto. Vijana waliozungumza na televisheni ya Citizen nchini humo, walisema kwamba wamepokea msamaha wa rais lakini walimtaka atafute suluhu kwa masuala yaliyoibuliwa.
Hata hivyo, kwenye mitandao ya kijami kuna wale ambao wameendelea kuwa na mawazo tofauti.

Chanzo cha picha, X

Chanzo cha picha, X
Upinzani pia umetaka msamaha wa William Ruto kwendana na vitendo na kukamata wale waliotekeleza utekaji nyara.
Katibu mkuu wa chama cha People's Liberation Asha Bashir, alisema wakati mabadiliko alioonyesha yanakaribishwa, "tunastahili kumkumbusha rais kuwa ikiwa msamaha unastahili kumaanisha kitu cha msingi, lazima uandamane na matokeo chanya kwa raia wa Kenya."
"Wale ambao bado hawajulikani walipo, wanaouguza majeraha, msamaha huo hautoshi na ni lazima uwendane na vitendo," Aliongeza Asha Bashir.
Nchini Uganda, raia wengi walionekana kwenye mitandao wa kijamii wakipuuza msamaha huo na kuashiria kuwa mchezo wa kisiasa uliokosa nia ya kweli au mabadiliko ya kumaanisha.

Chanzo cha picha, BBC NEWS
Kiongozi wa upinzani Bobi Wine, alikataa ombi la msamaha.
Akizungumza katika mji wa Gulu, aliishutumu serikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Alisema kuwa msamaha wa kweli lazima uanze na kukomesha ukandamizaji, akiongeza kuwa hakuna mazungumzo yanayoweza kutokea wakati raia wanabaki kuwa waathirika wa vurugu za serikali.
"Wakati anaomba msamaha, ndugu zetu wako gerezani wanateswa. Dada zetu wanabakwa. Watu wetu bado wanapokonywa ardhi zao... wakati ninasimama hapa, ninasema kwa Museveni, msamaha haukubaliki."
Wengine walikuwa na wingi wa matumaini kwamba huu huenda ukawa ndio mwanzo mpya.

Chanzo cha picha, X
Yote tisa, kumi, hakuna jambo zuri kama mtu kugundua hapa kuna tatizo na kuomba msamaha, ndivyo maisha yanavyokwenda hata majumbani.
Hii ni hatua moja ya kuponesha mioyo iliyojeruhiwa, na kutoa hakikisho kwamba makosa hayatatokea tena.
Inasaidia pia kuanza tena mahusiano kwa namna ya kuyaboresha zaidi na kurejesha nia njema kama ilitoweka.
Lakini ikiwa msahama wa vingozi wa Uganda na Kenya ulitolewa kwa kumaanisha ni suala la kusubiri na kufuatilia nini kitatokea baada ya hapo.