'Nyumbani ni eneo hatari zaidi kwa wanawake na wasichana' - Utafiti

- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
Huku siku 16 za uanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia zikiendelea, takwimu za kuogofya zinaonyesha kuwa ukatili wa kijinsia unajitokeza kwa wingi katika familia na jamii, mahali ambapo wanapaswa kujisikia salama.
Haya ni kutokana na kuongezeka kwa mauaji ya kikatikli dhidi ya wanawake yaliyotekelezwa na watu wa karibu kama vile wapenzi.
Kulingana na katibu mkuu wa masuala ya jinsia nchini Kenya, Anne Wang’ombe wanawake walio katika ndoa na walio na umri kati ya miaka 45 hadi 49 wanadhulumika zaidi kijinsia ikilinganishwa na wenzao wa kiume.
Visa 97 vya mauaji ya wanawake vimeripotiwa ndani ya miezi mitatu nchini Kenya huku visa vya wanawake wanaofika hospitalini kupata matibabu baada ya kudhulumiwa vikiongezeka hadi 4000.
Hali ni mbaya pia kimataifa.
Ripoti mpya inaonyesha kuwa zaidi ya wanawake 50,000 na wasichana waliuawa na wapenzi wao au wanafamilia mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko kutoka kwa 48,800 waliouawa 2022.
Ukatili huu unadhibitishwa na mashirika ya Umoja wa mataifa kama vile UN Women na UNODC, na umeonekana katika maeneo mengi duniani.
Unyanyasaji wa kingono wa wanawake
Hali ya kutisha pia inaendelea nchini Haiti, Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch inasema zaidi ya wanawake 4000 wamenyanyaswa kingono nchini Haiti katika kipindi cha miezi kumi mwaka huu.
Na huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wanawake wanakumbana na madhila makubwa zaidi katika migogoro ya kivita, ambapo vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia vinatumika kama silaha za vita.
Wanawake na wasichana wanadhalilishwa na kulazimishwa kuondoka kwenye makazi yao, wakiwa wahanga wa mashambulizi ya kikatili kutoka kwa vikundi vya waasi na majeshi ya kitaifa.
Bruno Lemarquis Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu, Mratibu Mkazi wa Misaada ya Kibinadamu ameweka wazi kwamba umoja wa mataifa umeanzisha mpango wa kukomesha ukatili dhidi ya wanawake ifikapo 2030.
Akisisitiza kuwa siku 16 za uanaharakati ni fursa ya kuweka upya ahadi za Umoja wa Mataifa kudai uwajibikaji kutoka kwa watu wanaotoa maamuzi.
'‘Unyanyasaji wa kutisha wa kijinsia hutumika kama silaha katika vita mashariki mwa DRC ambapo miili ya wanawake na wasichana inatumika kama viwanja vya vita hali hii ambayo inatia kizunguzungu na shuhuda zinaumiza na hatupaswi kuzoea tabia ya kukaa kimya mbele ya vitendo vya kivita, hatupaswi kuzoea lazima tupambane nao”Bruno anasema.
Kama anavyoeleza muathiriwa wa unyanyasaji huo unaosababishwa na vita vya mashariki ya DRC..
‘Nilipata ile shida alafu nimebakia na watoto 11 hivi hapa ninasumbuka sana juu ya vita,.. walitubaka na hata ubakaji bado unaendelea tunaomba amani hapa chilombo watuonee macho ya huruma watupiganie tuone vile wataturegesha nyumbani kwetu”alisema muathiriwa huyo
Hayo yakijiri Prisca Luanda, mshauri wa gavana wa Kivu Kaskazini, alisisitiza haja ya serikali na washirika wake kuimarisha hatua za ulinzi na haki kwa wanawake na wasichana walioathirika na vita. Alisema kuwa ni muhimu kuongeza juhudi katika kuhakikisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, hasa kwa kuimarisha mifumo ya kisheria na kutoa msaada kwa waathirika.
‘Vitendo hivi vimesababishwa na mambo kadhaa na vinaathiri wanawake na wasichana ikiwa serikali na washirika wetu lazima uimarishe vitendo vya ulinzi.”alisema Prisca.
Haya yanaripotiwa mashariki mwa jamhuri ya Kongo wakati pia wanawake wanataka kushirikishwa kwa uongozi ili kuleta amani DRC.

Chanzo cha picha, Reuters
Ripoti hiyo iliyotolewa wiki hii na Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli wa Umoja wa Mataifa, inafichua kiwango cha kutisha cha unyanyasaji wa kingono unaokumba mzozo wa Sudan uliodumu kwa miezi 18.
Utekaji nyara kwa ajili ya utumwa wa kingono umeripotiwa kuwa jambo la kawaida, huku waathiriwa wakianzia wasichana wenye umri wa miaka minane hadi kwa wanawake.
"Hakuna mahali salama nchini Sudan sasa," alisema Mohamed Chande Othman, mwenyekiti wa ujumbe huo, akionyesha ukosefu wa usalama ambao umeenea nchini humo tangu mzozo huo ulipozuka Aprili 2023.
Huku mikakati ikibuniwa na kutekelezwa ya kupambana dhidi ya ukatili wa jinsia ya kike bado visa vya kuogofya vinaendelea kuwaandama wanawake wengi ulimwenguni.
Nchini Kenya visa vya mauaji ya wanawake vimezidi huku rais William Ruto akiahidi shilingi milioni 100 kwa kampeni ya 'safe homes safe spaces”, yaani nyumba salama sehemu salama, akielekeza mahakama iwaadhibu vikali kisheria wanaoshukiwa.
Kampeni dhidi ya ukatili wa wanawake

Chanzo cha picha, Erika Brichta
Kwengineko, Mikesha imefanyika huko West Sussex kama sehemu ya kampeni ya kimataifa ya kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake.
Matukio hayo ya Chichester na Horsham yaliandaliwa na Taasisi ya Wanawake (WI), ikiwa ni sehemu ya Siku ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake.
Koja la maua ilionyeshwa ikiwa na majina ya wanawake kutoka Sussex ambao walikufa katika hali tatanishi miaka mitano iliyopita.
Ikizungumza na idhaa ya BBC WI ilisema unyanyasaji dhidi ya wanawake unaweza kuzuilika na takwimu zilikuwa "za kutisha".
Matukio ya Jumatatu ya tarehe 25 mwezi Novemba mwaka huu yalikuwa sehemu ya siku 16 za uanaharakati, na zitamalizika siku ya Kimataifa ya Haki za Kibinadamu tarehe 10 Desemba.
"Ikiwa wanaume watavaa utepe mweupe kusema unyanyasaji unaotokea nyumbani hauko kwa jina lao, hivyo ni vizuri," Bi Brichta alisema.
"Ikiwa wanawake wanavaa ua la machungwa, ambalo ni rangi ya Umoja wa Mataifa, hiyo pia inaonyesha uungwaji mkono wao."
Alisema wanawake wanaweza pia kujitolea katika kusaidiana iwapo mmoja wao ni muathiriwa wa dhulma za kijiinsia.
Aliongeza: "Tulikuwa na wawakilishi kutoka Safe In Sussex katika mikesha yote miwili, na tumekuwa tukichangisha pesa kwa ajili yao. Wanahitaji fedha sana."
Wanaharakati wamekuwa wakiadhimisha tarehe 25 Novemba kama Siku ya kimataifa ya kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake tangu 1981.
Tarehe hii ilichaguliwa kuwaenzi akina dada Mirabal, wanaharakati watatu wa kisiasa kutoka Jamhuri ya Dominika ambao waliuawa kikatili mwaka 1960 kwa amri ya mtawala wa nchi hiyo, Rafael Trujillo (1930-1961).
Imehaririwa na Seif Abdalla