Mawakili wa Tundu Lissu wapiga hodi Umoja wa Mataifa

Mawakili wa Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania aliyepo mahabusu, Tundu Lissu jana Ijumaa waliwasilisha malalamiko yao kwa Jopo Kazi la Umoja wa Mataifa wakipinga kuendelea kushikiliwa kwake katika jitihada za kuongeza shinikizo la kimataifa la kutaka aachiwe huru, linaripoti shirika la habari la Uingereza Reuters.
Lissu, ambaye ni mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, na mshindi wa pili katika uchaguzi wa rais wa 2020, alikamatwa mwezi uliopita na kushtakiwa kwa uhaini, shitaka ambalo akikutwa na hatia hukumu yake ni kifo, kutokana na kudaiwa kutoa wito kwa wafuasi wake kuzuia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Msemaji wa serikali ya Tanzania hakujibu mara moja ombi la Reuters kutaka maoni yake.
Wakati Rais Samia Suluhu Hassan amepata sifa kwa kupunguza ukandamizaji wa kisiasa hususani kwa vyama vya upinzania na viongozi wao, amekabiliwa na maswali kuhusu utekaji nyara wa wakosoaji wa serikali katika miezi ya hivi karibuni. Utekaji nyara huo haujatolewa maelezo thabiti na viongozi wa serikali.
Rais Samia, ambaye atagombea kiti cha urais katika uchaguzi wa Oktoba, amesema serikali yake inaheshimu haki za binadamu na kuagiza uchunguzi ufanyike kuhusu utekaji nyara unaoripotiwa.

Chanzo cha picha, AFP
Wakili wa kimataifa wa Lissu, Robert Amsterdam, alisema malalamiko ya siri kwa jopo kazi la Umoja wa Mataifa, ambalo linatoa maoni lakini halina nguvu ya utekelezaji, ni sehemu ya kampeni ya shinikizo kubwa.
Mwezi huu Bunge la Ulaya lilipitisha azimio la kupinga kukamatwa kwa Lissu na kwamba kulichochewa kisiasa, na Amsterdam alisema kwamba ataiomba Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuweka vikwazo.
"Hata kwa waendesha mashtaka, majaji, polisi - watu wote ambao wanahusika katika kesi hii ya uwongo wangefahamu kwamba wanapaswa kulinda maslahi yao nchini Amerika," Amsterdam aliiambia Reuters.
Katika kujibu azimio la Bunge la Ulaya, wizara ya mambo ya nje ya Tanzania ilisema ukosoaji wa nje kuhusu kesi hiyo ulitokana na "taarifa zisizo kamili au za kuegemea upande fulani".
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni yake.
Lissu, ambaye alipigwa risasi 16 katika shambulio la mwaka Septemba 2017 katika eneo la makazi ya viongozi mjini Dodoma, na ambalo hakuna mtuhumiwa aliyewahi kufunguliwa mashtaka, atafikishwa mahakamani tena Jumatatu Juni 2.
Kabla ya kufikishwa mahakamani wiki iliyopita, mamlaka zilimshikilia mwanaharakati rai awa Kenya na mwanaharakati wa haki za Uganda ambao walikuwa wameingia Tanzania kuhudhuria kusikilizwa kwa shauri dhidi ya Lissu.
Walitelekezwa siku kadhaa baadaye jirani na na mipaka ya nchi zao. Mwanaharakati wa Kenya, Boniface Mwangi, alisema wote wawili waliteswa vibaya wakiwa mahabusu.
Maafisa wa Tanzania hawajajibu maombi ya maoni yao kuhusu madai hayo.
Rais Samia amewaonya watu wa nje dhidi ya "kuvamia na kuingilia mambo yetu"

Chanzo cha picha, Getty Images
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024), Rais Samia alisema kuna mwenendo unaoibuka wa baadhi ya wanaharakati kuvuka mipaka na kuingilia masuala ya ndani ya nchi, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.
"Tusiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region (kanda) yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku," alisema Rais Samia.
Kauli hiyo ilikuja siku moja baada ya wakili mashuhuri wa Kenya na aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria, Martha Karua, pamoja na Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga na wanaharakati wengine wawili, kuzuiwa kuingia nchini Tanzania.
Walikuwa wamewasili kushuhudia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu, ambayo imeendelea leo katika Mahakama ya Kisutu.
Kwa mujibu wa Karua, alifurushwa na kurudishwa Kenya kwa lengo la kumzuia kuhudhuria kesi hiyo. Mutunga na wenzake pia walielezwa kuwa walizuiwa katika uwanja wa ndege kabla ya kurejeshwa nchini kwao.
Kauli ya Rais Samia ilionekana kutoa mwelekeo wa msimamo wa serikali ya Tanzania kuhusu suala hilo.
"Sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika watu wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu, aliongeza Rais Samia.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya, Korir Sing'oei, alisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu na ushirikiano wa kikanda.
Hata hivyo, tofauti na ilivyotarajiwa, baada ya kauli hizo hali ya mambo haikupoa badala yake kulitokea kauli zenye lugha kali za baadhi ya wabunge wa Tanzania wakati wakchangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi huku baadhi ya wabunge wa Kenya wakijibu kwa ukali
Nako katika mitandao ya kijamii kulikuwa na mjadala na malumbano makali kwa pande zote mbuli hadi Rais wa Kenya, William Ruto alipoziomba radhi Tanzania na Uganda.
Imetafsiriwa na Florian Kaijage