Kwa nini mikataba mingi mikubwa ya amani inasimamiwa na Saudi Arabia na Qatar?

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Saudi Arabia iliandaa mazungumzo Februari 2025 na wanadiplomasia wa Marekani na Urusi kuhusu kusitisha vita nchini Ukraine.

Siku ya Jumanne (11/3), mamlaka kutoka Marekani na Ukraine zinatarajiwa kukutana nchini Saudi Arabia kwa mazungumzo ambayo yanaweza kusababisha makubaliano ya amani na Urusi.

Nchi hiyo ilichaguliwa kwa sababu ya uhusiano kati ya mtawala wake mkuu, Mwanamfalme Mohammed bin Salman, alionao na Rais Vladimir Putin wa Urusi na Rais wa Marekani Donald Trump.

Serikali ya Saudia inasema itachukua jukumu kubwa ka kupatanisha pande zinazozozana.

Jirani wa Saudi Arabia, Qatar, pia imekuwa maarufu duniani kwa kuunga mkono harakati za amani katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Kwa nini Saudi Arabia inataka kufanya makubaliano ya amani?

...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Saudi Arabia iliingilia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen kwa mashambulizi ya anga na mizinga dhidi ya waasi wa Houthi

Saudi Arabia imepitisha jukumu la kusimamia makubaliano ya amani baada ya miaka kadhaa iliyofahamika kutumia njia uchokozi zaidi.

Mnamo mwaka 2015, nchi hiyo iliingilia kati vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen ili kuunga mkono serikali, kufanya mashambulizi ya anga na mizinga dhidi ya waasi wa Houthi.

Mnamo mwaka wa 2017, serikali ya Lebanon iliishutumu Saudi Arabia kwa kumzuilia Waziri Mkuu wa Lebanon Saad al-Hariri katika jaribio la kumlazimisha kujiuzulu.

Mnamo 2018, mwandishi wa habari Jamal Khashoggi - mkosoaji wa serikali ya Saudi - aliuawa na maafisa wa serikali katika ubalozi wa Saudi huko Istanbul.

"Awali uongozi wa Mohamed bin Salman ulisababisha makabiliano," alisema Paul Salem wa Taasisi ya Mashariki ya Kati huko Washington DC.

"Hata hivyo, uongozi umeamua kuwa kufanya vyema zaidi kwa kusimamia upatikanaji wa mikataba ya amani kuliko kuongezeka kwa migogoro," aliambia BBC.

Saudi Arabia imepitisha mikataba ya amani ili kuboresha uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati, anasema Elizabeth Dent wa Taasisi ya Washington, taasisi yenye makao yake makuu nchini Marekani inayoshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati.

"Hii ni sehemu muhimu ya mkakati wao - kukomesha utegemezi wao kwa mauzo ya mafuta na kuvutia biashara za kigeni kusaidia kukuza sekta mpya za kiuchumi," aliiambia BBC.

Je, Saudi Arabia imefanikiwa kwa kiasi gani katika kusimamia makubaliano ya amani?

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Saudi Arabia ilipitisha Mkataba wa Taif 1989 ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon

Historia ya Saudi Arabia kama mpenda amani katika eneo la Mashariki ya Kati ilianzia miongo kadhaa iliyopita.

Mnamo mwaka 1989, nchi hiyo ilisimamia mazungumzo kati ya pande zinazopigana nchini Lebanon ambayo yalipelekea Mkataba wa Taif na kusitishwa kwa mapigano mwaka 1990.

Hii ilimaliza miaka 15 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Mnamo 2007, Saudi Arabia ilipitisha Mkataba wa Mecca, ambao ulimaliza uhasama kati ya vikundi vya Wapalestina vya Hamas na Fatah.

Hivi karibuni, huku Mwanamfalme Mohammed bin Salman akiwa mtawala, Saudi Arabia ilichukua tena jukumu la kutafuta amani.

Tangu 2022, Saudi Arabia imekuwa katika mazungumzo na waasi wa Houthi nchini Yemen kujaribu kufikia usitishaji mapigano nchini humo.

Pia inaandaa mazungumzo ya muda mrefu kati ya pande hizo mbili katika mzozo wa Sudan - watawala wa kijeshi wa nchi hiyo, Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan, na kundi la waasi la Rapid Forces.

Saudi Arabia pia ilisimamia makubaliano ya 2022 kati ya Urusi na Ukraine ambapo zaidi ya wafungwa 250 wa vita waliokamatwa katika mzozo kati ya nchi hizo mbili walirejeshwa kwao.

Je, Qatar imeendeleza mikataba gani ya amani?

Qatar ilikuwa mpatanishi mkuu katika jopo la wawakilishi kutoka mataifa (ikiwemo Misri na Marekani) iliyofanikisha usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas mnamo Januari 2025.

Mnamo 2020, Qatar iliandaa makubaliano ya amani kati ya Taliban na Marekani ili kumaliza vita vya miaka 18 nchini Afghanistan, na Marekani na washirika wake kuondoa majeshi yao na Taliban kuchukua udhibiti wa nchi.

Mnamo 2010, nchi hiyo pia ilipanga usitishaji mapigano kati ya serikali na waasi wa Houthi nchini Yemen - makubaliano hayo yalivunjika baadaye.

Qatar pia imesimamia mikataba ya amani barani Afrika, ikiwa ni pamoja na usitishaji vita wa 2022 kati ya serikali ya Chad na makumi ya makundi ya upinzani.

Nyingine ilikuwa makubaliano ya amani ya mwaka 2010 kati ya serikali ya Sudan na makundi yenye silaha katika jimbo la magharibi la Darfur.

Mnamo mwaka wa 2008, serikali ya Qatar ilipitisha makubaliano kati ya makundi hasimu nchini Lebanon wakati uhasama kati yao ulipotishia kuzuka vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa nini Qatar inataka kuwa msuluhishi wa mizozo?

...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Qatar inashirikiana eneo kubwa la gesi la North Dome/Pars Kusini na Iran na imekuwa shauku yake kushirikiana na nchi hiyo.

Qatar ilianza kutekeleza jukumu kubwa la usuluhishi wa amani chini ya Hamad bin Khalifa al-Thani, ambaye alikua kamanda wa kijeshi wa nchi hiyo mwaka 1995 (na alikua madarakani hadi 2013).

Sababu kuu ya hili ni kwamba Qatar ilitaka kuendeleza hifadhi ya gesi katika Ghuba iitwayo North Dome/South Pars, ambayo iligunduliwa mwaka 1990.

Kwa sababu ya hifadhi hiyo inayozunguka maeneo ya maji ya eneo la Qatar na Iran, Qatar ilihitaji kushirikiana na Iran ili kufanikisha mradi huo – ingawa Iran ilikuwa adui wa Saudi Arabia wakati huo, anasema HA Hellyer wa Royal United Services Institute huko London, Uingereza.

"Walipogundua hifadhi ya gesi, Qatar ilifahamu kwamba inahitajika kutengeneza namna ya kujitegemea," alieleza BBC.

Qatar ilichagua kubeba jukumu la upatanishi wa amani, mtaalamu anasema, kwa sababu "kuwa na uhusiano mzuri na mataifa mengi kunajenga mtandao wa mataifa ambao unaweza kukusaidia na kukuunga mkono."

Jukumu la Qatar kama msuluhishi wa amani limejumuishwa katika Katiba iliyopitishwa mwaka 2004.

"Qatar imechagua kuwa na uhusiano wa kimataifa kama moja ya alama zake za kitaifa," anasema Salem.

Je, Saudi Arabia na Qatar zinatofautiana vipi kama wapatanishi wa amani?

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Qatar iliikasirisha Saudi Arabia kwa kuwaunga mkono wanasiasa wa Ikhwanul Muslimin wakati wa Mapinduzi ya Kiarabu, kama vile Mohamed Morsi, ambaye alikua rais wa Misri mwaka 2012 kabla ya kuondolewa mwaka mmoja baadaye.

Qatar mara nyingi huchaguliwa kama nchi ya kusuluhisha mizozo kwa sababu ina uhusiano na makundi ambayo Saudi Arabia na mataifa mengine hayashughulikii.

"Qatar haina chuki dhidi ya makundi ya Kiislamu - kama vile Muslim Brotherhood, Hamas, na Taliban - kama ilivyo kwa Saudi Arabia," anasema Salem.

Anasema kwamba uhusiano ambao Qatar ilikuwa nao na Taliban uliwasaidia kuziba pengo kati ya Taliban na Marekani, na uhusiano ambao ilikuwa nao na Hamas na Israel ulisaidia Qatar kusuluhisha mapigano kati ya pande hizo mbili.

"Saudi Arabia inashughulika na kesi ya Orthodox, Qatar inashughulika na wasiokuwa wa Orthodox," anasema Elizabeth Dent.

Hata hivyo, Qatar ilikasirisha Saudi Arabia kwa kuunga mkono makundi kama Muslim Brotherhood, ambayo serikali ya Saudi Arabia inayaona kama tishio kwa utawala wake.

"Wakati wa Mapinduzi ya Kiarabu [ya 2010 na 2011], Qatar iliunga mkono bila sharti makundi ya upinzani katika nchi kama Syria na Libya," anasema Dent. "Iliweka msimamo wake wazi."

Hii ilisababisha "mgawanyiko wa Ghuba" mwaka 2017, ambapo Saudi Arabia na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati yalivunja uhusiano na Qatar.

"Baada ya kufarakana, Qatar haikujihusisha kwenye harakati zaidi za mazungumzo yake na makundi ya kigaidi bila kwanza kushirikishana na majirani zake," anasema Dent. "Sasa, ni nchi isiyo na upande."

Aidha Qatar na Saudi Arabia hawana mgogoro kuhusu nani atakayekuwa msuluhishi wa makubaliano ya amani, anasema Hellyer.

"Qatar haitaki kushindana na Saudi Arabia siku hizi, na Saudi Arabia haitaki kushughulikia kesi za Qatar," anasema.

"Kwa bahati mbaya, bado kuna migogoro mingi duniani ambayo inawashughulisha."