Kwanini Saudi Arabia inaandaa mazungumzo ya kusitisha mapigano ya Ukraine?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Sebastian Usher
- Nafasi, BBC Middle East analyst, Jerusalem
Chaguo la utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano ya Ukraine katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riadh imeipa hadhi nchi hiyo kifalme kama mwenyeji wa kidiplomasia.
Nchi hiyo iliwahi kukosolewa vikali kufuatia mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi mwaka 2018 lakini sasa inachukua mkondo wa ustawi wa kidiplomasia kuandaa mazungumzo haya.
Uvumi kuhusu vikwazo vya kimataifa vilivyokuwa vikimzunguka Mohammed bin Salman, Mrithi wa kiti cha kifalme, umeanza kupotea, ingawa bado kuna masuala ya haki za binadamu yanayoibuliwa mara kwa mara katika mikutano ya kimataifa.
Saudi Arabia imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya burudani na michezo ili kujidhihirisha kama nchi muhimu kimataifa na kuipa muonekano mpya.
Aidha, katika medani ya kidiplomasia, uongozi wa Saudia umekuwa ukiongeza nafasi yake, na katika utawala wa Biden, Ufalme wa Saudi ulionyesha kujitenga na utegemezi wake wa zamani kwa Marekani kama mshirika wake mkuu wa kimataifa.
Saudi Arabia ilionyesha wazi kuwa itafuata maslahi yake ya kimsingi, na kuanzisha uhusiano wa karibu na mataifa ambayo yanaonekana kama washindani wa Marekani, kama vile Urusi na China.
Kwa upande mwingine, kurejea kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House kulipokelewa na Saudia kwa furaha kubwa.
Ziara ya Trump ya kwanza ya kigeni katika muhula wake wa kwanza ilikuwa nchini Saudi Arabia, na mtindo wake wa sera za nje unaolenga masuala ya kibiashara unafaa kwa uongozi wa sasa wa Saudi.
Mwanamfalme huyo Salman hajawahi kusamehe au kumsahau Biden pale aliposema Saudi Arabia inapaswa kutengwa kwa kukiuka haki za binadamu.
Moja ya malengo anayotarajia kufikia Trump ni makubaliano ya amani kati ya Saudi Arabia na Israel, ambayo itakuwa ni kilele cha Mikataba ya Abraham aliyoanzisha katika muhula wake wa kwanza.
Hata hivyo, vita vya Gaza vimeingilia kati na huenda vikaongeza masharti ambayo Saudi Arabia itadai katika makubaliano ya amani.
Wasaudi walijitokeza haraka kutangaza kukataa kwao mpango wa Trump kuhusu ''kununua na kuimiliki'' Gaza, ambao ulitaka kuondoa Wapalestina wote na kuijenga Gaza kama kituo cha utalii.
Hii imewasukuma Wasaudi kutafuta mpango mbadala pamoja na mataifa mengine ya Kiarabu, ambao utahakikisha kuwa Wapalestina wanabaki Gaza wakati sehemu hiyo inajengwa upya, na hivyo kutafuta suluhu ya mataifa mawili kwa mgogoro huo.
Kwa upande wa utawala wa Trump, mtazamo wake sasa unaonekana kinyume na wa Saudi Arabia kuhusu siasa za Gaza na Ukingo wa Magharibi uliojaa mizozo.
Jinsi mabadiliko haya yatafanikiwa kutatuliwa ni muhimu kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Saudi Arabia na Marekani.
Kinachojulikana kwa sasa ni kuwa Saudi Arabia haina nia ya kupunguza azma yake ya kuwa nchi muhimu katika diplomasia ya kimataifa, jambo ambalo linathibitisha mwelekeo wake wa kujitokeza kama nguvu kuu katika medani za kisiasa za dunia.

Chanzo cha picha, Russian Foreign Ministry
Azma ya Saudi Arabia kuwa mpatanishi
Ghuba hii ya kiarabu sio mara yake ya kwanza kujipata katika meza ya mazungumzo ya maridhiano imekuwa ikijishughulisha na masuala ya kidiplomasia hasa yanayoathiri mataifa yaliyo katika ukanda wake.
Saudi Arabia pia wamekuwa mstari wa mbele kutatua mgogoro unaoendelea nchini Sudan.
Vile vile ilipendekeza kusitisha kwa mapigano chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa kati ya vikosi vya Yemen na waasi wa Houthi ambao walikuwa wakiungwa mkono na Iran.
Isitoshe, Mwanamfalme Mohammed bin Salman alikuwa kiungo muhimu katika harakati za kuachilia huru wafungwa wa kigeni 10 waliokamatwa Ukraine.
Tukio hili ambalo lilifanyika tarehe 22 mwezi Septemba 2022 lilipelekea kukabidhina mateka wa kivita kati ya Urusi na Ukraine.
Je, huku ni 'kujiosha' kwa kutumia upatanishi?
Huenda taifa hili la kifalme linajipa jukumu la kuandaa mazungumzo ili kusaidia kuboresha taswira ya nchi ambayo imekabiliwa na ukosoaji wa miaka mingi juu ya masomo kama vile:
- ukiukaji wa haki za binadamu
- ukandamizaji wa wanawake
- kuharamisha mapenzi ya jinsia moja
- kizuizi cha uhuru wa kujieleza
- kuendelea kutumia adhabu ya kifo
- mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi mwaka 2018
- kifungo cha wanaharakati kwa upinzani mtandaoni
- kuhusika kwa nchi hiyo katika mzozo wa umwagaji damu nchini Yemen
Wakati wanakampeni wanakubali kwamba kumekuwa na mabadiliko muhimu katika miaka ya hivi karibuni, kwa mfano kuhusu haki za wanawake, pia walisema kumekuwa na ukandamizaji unaoendelea.
Saudi Arabia ilinyonga wafungwa wa tatu kwa wingi zaidi duniani mwaka 2023, na watu mia tatu tayari wameuawa mwaka jana, rekodi iliyotokana na takwimu rasmi.
Mwaka 2024 Manahel al-Otaibi alihukumiwa kifungo cha miaka 11 jela baada ya kutumia mitandao ya kijamii kutaka kukomeshwa kwa sheria zinazosema kuwa wanawake wanahitaji ruhusa ya jamaa wa kiume kuolewa au kusafiri.
Hata hivyo Ukraine haijaalikwa kushiriki katika mazungumzo haya yanayofanyika Riyadh, jambo ambalo limezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Ulaya.
Kuhusu hilo, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rubio alisema mazungumzo hayo yatakuwa "ya kweli" ikiwa yataanza rasmi, lakini akasisitiza kuwa "hatujafikia hatua hiyo bado."
Rubio pia alisema hatarajii mazungumzo haya kumaliza vita mara moja.
Awali mataifa ya Ulaya yamekuwa wapatanishi wa masuala ya uhusiano ya Urusi na Marekani.
Lakini wakati huu Ulaya umepoteza umuhimu wake baada yakujitangaza wazi wanaegemea upande wa Ukraine.
Mazungumzo ya maridhiano yakitarajiwa kuanza Jumanne Rais wa Ukraine Zelensky atakuwa akielekea Saudi Arabia lakini ameweka wazi sio kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano bali safari yake ilipangwa awali.