Maswali muhimu kuhusu uamuzi wa Fifa kuipatia Saudia jukumu la kuandaa Kombe la Dunia la 2034

Chanzo cha picha, Saudi 2034
Uthibitisho wa Fifa kwamba Saudi Arabia itaandaa Kombe la Dunia la wanaume 2034 - licha ya nchi hiyo kukabiliwa na uchunguzi wa miaka mingi juu ya rekodi yake ya haki za binadamu na mazingira - ni moja ya hatua zenye utata zaidi ambazo bodi inayosimamia soka imewahi kuchukua.
Ingawa wakosoaji wengi wamesikitishwa na matarajio hayo, wachache wanapaswa kushangazwa kutokana na ushawishi ambao uwekezaji mkubwa wa kifalme katika michezo umepata.
Kwa hivyo michuano hiyo inatumika kusaidia kubadilisha sifa ya Saudi Arabia, au inaweza kuwa kichocheo cha mageuzi ya kijamii? Na hii inatuambia nini kuhusu Fifa na soka kwa upana zaidi?
BBC inaangazia maswali muhimu.
Kwa nini huku ni 'kutawazwa', na sio mashindano?
Uthibitisho rasmi wa Kombe la Dunia la Saudia ulikuja katika mkutano wa wa Congress ya Fifa Jumatano alasiri.
Lakini hiyo imeonekana kama utaratibu tu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mnamo Oktoba 2023, iliibuka kuwa ombi la Saudia lingepita bila kupingwa baada ya Australia - mgombea mwingine - kuamua kutoshiriki katika kinyang'anyiro hicho, ikidokeza kwamba ilikuwa kazi bure kufanya hivyo baada ya kupewa muda wa chini ya mwezi mmoja na Fifa kuwasilisha pingamizi yake.
Fifa imetetea mchakato unaofuatiliwa haraka ambao wengi wanahoji kuwa haukuwa na uwazi na uwajibikaji. Lakini wakosoaji wanaamini kuwa ilifungua njia kwa Wasaudi, kwa kuamuru kwamba Kombe la Dunia la 2030 litaandaliwa katika mabara matatu (nchini Hispania, Ureno na Morocco na mechi tatu za kwanza zikifanyika Amerika ya Kusini). Hiyo ilimaanisha kuwa chini ya sera yake ya mzunguko, zabuni kutoka Asia na Oceania pekee ndizo zilizozingatiwa kwa 2034.
Inafaa kufahamika kuwa Saudi Arabia na Fifa, chini ya rais Gianni Infantino, wameendeleza uhusiano wa karibu. Nchi hiyo ilikuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la Vilabu la 2023 , na bodi inayoongoza ina mkataba wa udhamini mzuri na kampuni kubwa ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Saudi Aramco.
Pia kumekuwa na uvumi ulioenea kwamba Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi (PIF) unaweza kufanya uwekezaji mkubwa katika utiririshaji mkubwa wa matangazo utakaofanywa na kampuni ya DAZN ambayo imekubali kutangaza toleo la uzinduzi wa mradi kipenzi wa Infantino - Kombe la Dunia la Vilabu lililopanuliwa msimu ujao wa joto.
Hali ya kutoepukika inayozunguka ombi la Saudi iliimarishwa mwezi uliopita tu na uchapishaji wa usiku wa manane wa ripoti ya tathmini ya Fifa, iliyoandikwa na naibu wa Infantino, katibu mkuu Mattias Grafstrom. Ilikabidhi zabuni hiyo alama ya wastani ya 4.2 kati ya 5, ikiwa ni ya juu zaidi kuwahi kutokea.
Hakuna mkutano wa vyombo vya habari ulifanyika ili kuelezea tathmini nzuri kama hii, wala ukweli kwamba zabuni hiyo ilionekana kuwa na 'hatari chache ' kwa haki za binadamu na 'hatari ndogo' kwa ulinzi wa mazingira, na kuzua hasira kutoka kwa wanakampeni.
Zaidi ya hayo, uidhinishaji ulithibitishwa na matamshi wakati wa Kongamano, badala ya kura, njia pekee ya vyama vya kitaifa vinavyopingana ni kuonyesha upinzani wao ni kutoshiriki.
Wawakilishi wa vyama vyote wanachama 211 waliombwa kuunga mkono ombi la Uhispania, Ureno na Morocco 2030 ambalo halijapingwa na kisha la Saudi 2034 kwa wingi.
Fifa hathivyo inaweza kusema kuwa waandaji wanaweza kuidhinishwa kupitia zabuni ambazo hazijapingwa, wakati mchakato mrefu kati ya nchi mbalimbali unaweza kuwa hatari kwa kubadilishana kura na majaribio ya rushwa, na kwamba kama chombo cha kimataifa wana wajibu wa kupeleka michunao hiyo katika maeneo mapya .
Siku ya Jumanne ilidai wakaguzi wa BDO walikuwa wamehitimisha mchakato huo waliodai "umetekelezwa kwa usawa, uadilifu na uwazi".

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, nchi zingine zimesema nini?
Shirikisho la kandanda la Norway ilijiondoa katika kura hiyo, ikipinga mchakato wa zabuni "unadhoofisha mageuzi ya Fifa ya utawala bora" na "changamoto kwa imani ya Fifa". Imeongeza kuwa miongozo ya Fifa ya uangalizi makini haikufuatwa, "na kuongeza hatari ya ukiukaji wa haki za binadamu".
Mashirikisho mengine yote yaliidhinisha ombi la Saudia. DFB ya Ujerumani ilisema "ilichukulia ukosoaji wa nchi iliyotuma maombi kwa uzito…[lakini] lengo letu ni kufanya kazi pamoja na Fifa kuboresha hali hiyo katika miaka ijayo".
FA ilifuata mkondo huo na kuunga mkono zabuni zote mbili, huku baadhi ya maafisa wakuu wakijulikana kuwa walihofia shutuma za unafiki ikiwa hawangeiunga mkono Saudi Arabia lakini wanataka Uingereza kushiriki.
Uchunguzi mwingi umetoka nje ya mchezo. Mnamo Machi, gazeti la Guardian lilisema limepata ushahidi wa idadi kubwa ya vifo visivyoelezeka vya wafanyikazi wahamiaji wa Bangladesh nchini Saudi Arabia. Nchi hiyo ilitetea kanuni na viwango vyake, lakini Fifa ilishinikizwa kuhakikisha kuna ahadi za mabadiliko kabla ya kuipatia Saudia jukumu la kuandaa michuano hiyo.
Je! Kombe la Dunia la Saudia litakuwaje?
"Ajabu", kulingana na Shirikisho la Soka la Saudi. Zabuni yake ilipendekeza viwanja 15, (pamoja na viwanja vitatu ambavyo vinaendelea kujengwa, na nane ambapo kazi bado haijaanza), katika miji mitano, ikijumuisha kiwanja kimoja moja cha teknolojia ya kisasa (ambacho bado hakijajengwa.
Ripoti ya tathmini ya Fifa inasifu "viwanja mbalimbali vya kuvutia ambavyo, vikijengwa au kurekebishwa, vinaweza kutoa miundombinu ya hali ya juu".
Pia michezo hiyo huenda ikafanyika wakati wa baridi. Lakini kunaweza kuwa na tofauti moja kubwa na mashindano ya nchi jirani ya Qatar, ambayo yalifanyika Novemba-Desemba, 2022.
Mashindano hayo yatafanyika kuanzia mwanzoni mwa Januari ili kukwepa mgongano na mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Ligi ya Premia na ligi zingine kuu za Ulaya zitapinga Kombe la Dunia la msimu wa baridi, kulingana na shirika la habari la PA.
Ingawa ligi za ndani zilisimama katikati ya msimu ili kombe la Dunia la Qatar 2022 kufanyika, upanuzi wa mashindano ya vilabu vya Uropa, na kuongezeka kwa ukubwa wa Kombe la Dunia hadi mashindano ya timu 48, kungemaanisha usumbufu zaidi kwa kalenda ambayo tayari imejaa.
Je, hii inasema nini kuhusu ushawishi wa michezo wa Saudia?
Kwa wengi, kuidhinishwa kwa Kombe la Dunia la Saudia ndio kielelezo kikuu cha nguvu ambayo nchi hiyo sasa inamiliki katika michezo yote, na fursa, usumbufu na mabishano ambayo yameambatana nayo.
Ufalme huo umewekeza mabilioni ya pauni ya kuandaa hafla tangu 2021, wakati mtawala wa nchi hiyo Mwanamfalme wa alipoifanya kuwa sehemu muhimu ya mkakati wake wa 'Ruwaza ya 2030' wa kufanya uchumi wa kisasa na mseto. Ufalme huo tangu wakati huo umekuwa mwenyeji wa michezo ya Formula 1, fainali za kombe la kandanda la Uhispania na Italia, Kombe la Dunia la Klabu, na ndondi za kiwango cha juu, gofu, mbio za farasi na tenisi.
Mfuko wa Uwekezaji wa Umma nchini Saudia pia umezindua msururu wa mashindano ya gofu ya LIV, na kudhibiti vilabu vinne vya Saudi Pro League mbali na kuinunua Newcastle United.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, huku ni 'kujiosha' kwa kutumia michezo?
Wakosoaji wengi wanaona hiki kama kitendo kikubwa zaidi cha kuosha michezo katika historia ya Fifa huku Kombe la Dunia likitumika kusaidia kuboresha taswira ya nchi ambayo imekabiliwa na ukosoaji wa miaka mingi juu ya masomo kama vile:
- ukiukaji wa haki za binadamu
- ukandamizaji wa wanawake
- kuharamisha mapenzi ya jinsia moja
- kizuizi cha uhuru wa kujieleza
- kuendelea kutumia adhabu ya kifo
- mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi mwaka 2018
- kifungo cha wanaharakati kwa upinzani mtandaoni
- kuhusika kwa nchi hiyo katika mzozo wa umwagaji damu nchini Yemen
Wakati wanakampeni wanakubali kwamba kumekuwa na mabadiliko muhimu katika miaka ya hivi karibuni, kwa mfano kuhusu haki za wanawake, pia walisema kumekuwa na ukandamizaji unaoendelea.
Saudi Arabia ilinyonga wafungwa wa tatu kwa wingi zaidi duniani mwaka 2023, na watu mia tatu tayari wameuawa mwaka huu, rekodi iliyotokana na takwimu rasmi. Mwaka huu Manahel al-Otaibi alihukumiwa kifungo cha miaka 11 jela baada ya kutumia mitandao ya kijamii kutaka kukomeshwa kwa sheria zinazosema kuwa wanawake wanahitaji ruhusa ya jamaa wa kiume kuolewa au kusafiri.
Je, Saudi 2034 inaweza kusababisha mabadiliko?
Wengi wanaamini kwamba wakati Qatar ilisimamia Kombe la Dunia salama na la kukumbukwa lililofurahiwa na mashabiki wengi, miaka ya mabishano ambayo ilifunika mashindano hayo juu ya haki za binadamu, sheria za kibaguzi, na usumbufu mkubwa wa kalenda ya kandanda uliosababishwa na Kombe la Dunia la msimu wa baridi wa kwanza sasa inaweza kuwa. mara kwa mara.
Huko nyuma 2010, ushindi wa kushangaza wa Qatar katika kura ya kuamua wenyeji wa 2022 ulichukua uongozi wa Fifa kwa mshangao. Kinyume chake, Infantino anaonekana kuunga mkono wazo la Kombe la Dunia la Saudia. Na kwa kuwa Fifa imeleta sera ya haki za binadamu mwaka wa 2017, kunaweza kuwa na uchunguzi zaidi juu ya uamuzi wake - na ushahidi wowote unaosababisha wafanyakazi kuathiriwa vibaya.
Kama ilivyo kwa Qatar, miundombinu ya Kombe la Dunia la Saudi itajengwa kwa kiasi kikubwa na wafanyikazi wahamiaji kutoka Asia Kusini, na zaidi ya wageni milioni 13 wanaoishi nchini humo, na kiwango cha ujenzi kinachohitajika kimesababisha wasiwasi.
Vipi kuhusu mazingira?
Wanaharakati kwa muda mrefu wamemshutumu msafirishaji mkubwa wa mafuta duniani kwa kuongeza mabadiliko ya hali ya hewa kupitia tasnia yake ya mafuta, na kuzuia hatua za hali ya hewa.
Lakini sasa pia wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu athari za kuandaa mashindano ya timu 48, wakionyesha nishati inayohitajika kwa mifumo ya kupoeza, kuondoa chumvi kwenye maji na miradi ya miundombinu inayotumia kaboni.
Serikali ya Saudia inasema inajitenga na nishati ya mafuta na kujaribu kupunguza upungufu, na imekataa ukosoaji unaotumia michezo kuvuruga rekodi yake ya uendelevu.
Ripoti ya tathmini ya Kombe la Dunia ya Fifa ilisema: "Ingawa kiwango cha ujenzi kitakuwa na athari za kimazingira, zabuni hiyo inatoa msingi mzuri wa kutoa hatua za kukabiliana na changamoto zinazohusiana na mazingira."
Je, hii inatuambia nini kuhusu michezo?
Kombe la Dunia la Saudi linasisitiza mabadiliko ya ajabu katika nguvu za michezo kuelekea Mashariki ya Kati.
Hadi hivi majuzi, wazo la Qatar jirani ya Saudi Arabia kuandaa Kombe la Dunia ndani ya kipindi cha miaka 12 tu lingekuwa lisilowezekana kwa wengi. Lakini kutokana na utajiri wa nchi hizi, na mashirika ya michezo kutaka ukuaji wa kifedha na masoko mapya, hilo lilifanyika kwa haraka.
Saudi Arabia inaweza kusema kuwa haitakuwa mwenyeji wa pekee mwenye utata wa hafla kubwa ya michezo katika miaka ya hivi karibuni. Katika miongo miwili iliyopita, Urusi imekuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia na Olimpiki, na Uchina imekuwa mwenyeji wa Olimpiki za msimu wa joto na msimu wa baridi.
Mahusiano ya watu wa jinsia moja pia ni kinyume cha sheria mwaka wa 2030 kwa waandaji-wenza wa Kombe la Dunia Morocco. Na wanaharakati wa mazingira wameelezea kusikitishwa na uandaaji wa Kombe la Dunia la 2030 katika mabara matatu.
Amnesty pia hivi majuzi imeelezea wasiwasi wake kuhusu haki za binadamu kwa waaandaji wa Kombe la Dunia mwaka wa 2026 Marekani .
Hii Imetafsiriwa na Seif Abdalla