Tunachokijua kuhusu shambulio la India dhidi ya Pakistan

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Flora Drury
- Nafasi, BBC News
Wiki mbili baada ya shambulizi la kijeshi dhidi ya watalii waliokuwa ziarani katika upande mmoja wa Kashmir unaotawaliwa na India, taifa hilo limezindua msururu wa mashambulizi dhidi ya upande wa pili wa Kashmir unaotawaliwa na Pakistan.
Wizara ya ulinzi ya India ilisema mashambulizi wanayoyataja kama ''operesheni Sindoor'' ilikuwa sehemu ya kulipiza kisasi shambulizi la mwezi Aprili 22 ambalo liliwaua raia 25 wa India na mmoja wa Nepal.
Lakini Pakistan ambayo imekanusha kuhusika kwa shambulio hilo, imeelezea hatua hiyo kuwa "kitendo cha kikatili cha uchokozi kitaadhibiwa vikali", Waziri Mkuu Shehbaz Sharif alinukuliwa kusema.
Lakini je, ni nini hasa kilitokea - na India na Pakistan zilifikaje hapa?
India imeshambulia eneo lipi?
Delhi ilisema mapema asubuhi ya Jumatano kwamba maeneo tisa tofauti yalilengwa katika Kashmir inayosimamiwa na Pakistan.
Ilisema maeneo haya ni "miundombinu ya kigaidi" - mahali ambapo mashambulizi "yalipangwa na kuelekezwa".
Ilisisitiza kuwa haijagonga vituo vyovyote vya kijeshi vya Pakistani, ikisema "vitendo vyake vimezingatia, kupimwa na sio kuchochea vita".
Kulingana na Pakistan, maeneo matatu tofauti yalishambuliwa: Muzaffarabad na Kotli katika eneo la Kashmir inayotawaliwa na Pakistan, na Bahawalpur katika jimbo la Pakistani la Punjab.
Waziri wa Ulinzi wa Pakistan Khawaja Asif aliiambia GeoTV kwamba shambulio hilo lililenga maeneo ya kiraia, na kuongeza kwamba madai ya India ya "kulenga kambi za magaidi" ni ya uwongo.
Ahmed Sharif, msemaji wa jeshi la Pakistan, baadaye aliambia BBC kwamba watu saba, ikiwa ni pamoja na watoto wawili, waliuawa katika shambulizi hilo.
Kwanini India imeanzisha mashambulizi?
Msururu wa mashambulizi yanayoshuhudiwa sasa yanajiri baada ya wiki kadhaa za mvutano unaozidi kupamba moto kati ya India na Pakistan, majirani wawili wenye silaha za nyuklia kutokana na tukio la kusikitisha la mashambulizi ya risasi katika mji wa kitalii wenye mandhari ya kuvutia wa Pahalgam.
Katika tukio hilo la tarehe 22 Aprili, kundi la wapiganaji walivamia eneo hilo na kuua watu 26 kwa njia ya kikatili.
Walionusurika waliripoti kuwa wanaume wa Kihindu walilengwa mahsusi, jambo lililoibua hisia kali za huzuni na hasira nchini India.
Shambulizi hilo limeelezwa kuwa baya zaidi dhidi ya raia katika eneo hilo tangu miaka ishirini iliyopita.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alitoa tamko kali, akiahidi kuwa serikali yake itawafuatilia washukiwa "hadi mwisho wa dunia" na kuwa waliohusika "wataonja adhabu inayozidi hata mawazo yao."
Hata hivyo, licha ya kauli hiyo nzito, India haijataja kundi lolote linaloshukiwa kuhusika, na hadi sasa bado haijulikani wazi ni nani waliohusika.
Polisi wa India, kwa upande wao, wamedai kuwa baadhi ya washambuliaji walikuwa raia wa Pakistan, madai ambayo serikali ya Islamabad imeyakana vikali, ikisisitiza kuwa haina uhusiano wowote na tukio hilo la kigaidi.
Katika kipindi cha wiki mbili baada ya shambulizi hilo, India na Pakistan zimeingia kwenye mzozo wa hatua za kisiasa wakifukuza wanadiplomasia, kusimamisha utoaji wa viza, na hata kufunga mipaka.
Hali hiyo imezua hofu kuwa huenda hali ikafikia mashambulizi ya kuvuka mipaka, kama ilivyoshuhudiwa mwaka 2019 kufuatia shambulizi la Pulwama ambapo wanajeshi 40 wa India waliuawa.
Kwanini Kashmir ni eneo la mgogoro kati ya India na Pakistan?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kashmir imebaki kuwa kiini cha mzozo mkali kati ya India na Pakistan kwa zaidi ya nusu karne.
Ingawa kila nchi inadai eneo hilo kwa ukamilifu, kihistoria limegawanywa na kusimamiwa kwa sehemu na pande zote tangu mgawanyo wa India mwaka 1947, baada ya uhuru kutoka kwa Uingereza.
Tangu wakati huo, nchi hizo zimepigana vita viwili juu ya hatma ya Kashmir.
Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, mashambulizi ya wapiganaji wa kivita yamekuwa kichocheo kikuu cha mvutano.
Tangu mwaka 1989, Kashmir inayodhibitiwa na India imekuwa ikikumbwa na uasi wa silaha dhidi ya utawala wa New Delhi, ambapo mashambulizi huwalenga wanajeshi na raia bila kuchagua.
Shambulizi la Pahalgam ni la kwanza kubwa dhidi ya raia tangu mwaka 2019, wakati serikali ya India ilipofuta Kifungu cha 370 kilichokuwa kikitoa hadhi ya kujitawala kwa sehemu kwa Kashmir.
Uamuzi huo ulizua maandamano makubwa, lakini pia ulifuatiwa na kupungua kwa mashambulizi ya kijeshi na kuongezeka kwa idadi ya watalii.
Hata hivyo, kumbukumbu ya mashambulizi ya zamani bado haijafutika.
Mwaka 2016, India ilizindua mashambulizi ya "kimkakati ya kijeshi" dhidi ya kambi za wapiganaji baada ya wanajeshi wake 19 kuuawa huko Uri.
Na mwaka 2019, mashambulizi ya Pulwama yalisababisha India kufanya mashambulizi ya anga ndani ya Pakistan hatua iliyochochea mapambano ya anga baina ya ndege za kivita za mataifa hayo mawili.
Ingawa matukio haya hayakugeuka vita kamili, dunia imesalia na hofu ya mlipuko mkubwa wa vita, hasa kwa kuzingatia kuwa pande zote zina uwezo wa nyuklia.
Mataifa mbalimbali na jumuiya za kimataifa zimejitahidi kupunguza mvutano huu kwa njia ya kidiplomasia.
Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametaka "kujitahidi kwa kiwango cha juu kujizuia," huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akieleza matumaini kuwa "mapigano yatamalizika haraka iwezekanavyo."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi