Kwa nini India na Pakistan zilitenganishwa?

Kila jioni tangu mwaka 1959, Wanajeshi wa India na Pakistani wameshusha bendera zao kwa pamoja kwenye kivuko cha mpaka cha Wagah

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kila jioni tangu mwaka 1959, wanajeshi wa India na Pakistani wameshusha bendera zao kwa pamoja kwenye kivuko cha mpaka cha Wagah

Mnamo Agosti 1947, Uingereza iliipatia India uhuru wake.

Eneo ambalo ilikuwa imetawala iligawanywa, kuwa India na jimbo jipya la Pakistani (na Pakistan ya Mashariki baadaye ikawa Bangladesh).

Hii ilizua ongezeko la ghasia ambapo takriban watu milioni 15 walikimbia makazi yao, na inakadiriwa watu milioni moja walipoteza maisha yao.

India na Pakistan zimesalia kuwa mahasimu tangu wakati huo.

Kwanini utenganishaji ulifanyika?

Mnamo 1946, Uingereza ilitangaza kuwa itaipatia India uhuru.

Haingeweza tena kusimamia nchi na ilitaka kuondoka haraka iwezekanavyo.

Makamu wa mwisho, Lord Louis Mountbatten, aliweka tarehe hiyo kuwa tarehe 15 Agosti, 1947.

Kwa wakati huo, 25% ya watu wa India walikuwa waumini wa Kiislamu.

Waliobaki wengi wao walikuwa Wahindu. Idadi ya watu pia ilikuwa na Wakalasinga, Wabudha na washiriki wa dini zingine ndogo.

Viongozi wa uhuru wa India Jawaharlal Nehru na Mohandas Gandhi wakizungumza pamoja katika miaka ya 1940

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanaharakati wakuu wa kupigania uhuru Jawaharlal Nehru (kushoto) na Mohandas Gandhi (kulia) walitaka India ambayo inakumbatia imani zote.
Pia unaweza kusoma:

"Waingereza walitumia dini kama chombo cha kuwagawanya watu nchini India katika makundi," anasema Profesa Navtej Purewal, Mshiriki wa Baraza la Utafiti wa Sanaa na Kibinadamu wa India.

"Kwa mfano, waliandaa orodha tofauti za wapiga kura Waislamu na Wahindu katika chaguzi za mitaa.

Kulikuwa na viti vilivyotengwa kwa ajili ya wanasiasa Waislamu, na viti vilivyotengwa kwa ajili ya Wahindu. Dini ikawa hoja ya siasa."

"Ilipoonekana uwezekano kwamba India itapata uhuru, anasema Dk Gareth Price katika taasisi ya sera ya mambo ya nje ya Chatham House yenye makao yake makuu nchini Uingereza, "Wahindi wengi wa Kiislamu waliingiwa na wasiwasi kuhusu kuishi katika nchi inayotawaliwa na Wahindu wengi," "Walidhani wangezidiwa," anasema.

"Walianza kuunga mkono viongozi wa kisiasa ambao walifanya kampeni kwa ajili ya nchi tofauti ya Waislamu."

Mohandas Gandhi na Jawaharlal Nehru, viongozi wa vuguvugu la uhuru wa Congress, walisema wanataka India iliyoungana ambayo inakumbatia imani zote.

Muhammad Ali Jinnah seen arguing with Mohandas Gandhi about partition outside Jinnah's house in 1939

Chanzo cha picha, Getty Images

Hata hivyo, Muhammad Ali Jinnah, kiongozi wa Jumuiya ya Waislamu wote wa India, alidai kugawanywa kwa maeneo hayo kama sehemu ya suluhu la uhuru.

"Ingechukua muda mrefu kufikia makubaliano kuhusu jinsi India iliyoungana ingefanya kazi," anasema Dk Price.

"Kugawanywa huko kulionekana kuwa suluhisho la haraka na rahisi."

Inafikiriwa watu 2,000 walikufa katika mauaji ya Calcutta ya 1946, wakati Wahindu na Waislamu walipigana mitaani.

Chanzo cha picha, Huw Evans Picture Agency

Maelezo ya picha, Inasadikiwa kuwa watu 2,000 walikufa katika mauaji ya Calcutta ya 1946, wakati Wahindu na Waislamu walipigana mitaani.

Hatua hiyo ilisababisha mateso kiasi gani?

Mipaka mipya kati ya India na Pakistan iliwekwa mwaka 1947 na mtumishi wa serikali ya Uingereza. Sir Cyril Radcliffe.

Aligawanya bara dogo la India kwa takribani sehemu ya kati na kusini ambapo Wahindu waliunda wengi, na sehemu mbili kaskazini-magharibi na kaskazini-mashariki ambapo Waislamu waliunda wengi.

Hata hivyo, kulikuwa na jumuiya za Wahindu na Waislamu zilizotawanyika kote katika India ya Uingereza.

Hii ilimaanisha kuwa baada ya kugawanyika, takriban watu milioni 15 walisafiri - mara nyingi mamia ya maili - kuvuka mipaka mpya iliyoundwa.

Katika visa vingi, watu walifukuzwa nje ya nyumba zao na vurugu za kijamii. Mfano wa kwanza wa hii ulikuwa Mauaji ya Calcutta ya 1946, ambapo takriban watu 2,000 waliuawa.

"Jumuiya ya Waislamu iliunda wanamgambo, na vivyo hivyo na vikundi vya Kihindu vya mrengo wa kulia," anasema Dk Eleanor Newbigin, mhadhiri mkuu katika historia ya Asia Kusini katika SOAS, Chuo Kikuu cha London.

"Makundi ya kigaidi yangefukuza watu nje ya vijiji vyao, ili kupata udhibiti zaidi kwa upande wao."

Je, matokeo ya kugawanywa huko ilikuwa nini?

Tangu kugawanywa huko India na Pakistan zimepigana mara kwa mara kuhusu ni nani atakayechukua udhibiti wa mkoa wa Kashmir.

Wamepigana mara mbili juu yake (mwaka 1947-8 na 1965), na pia walipigana katika mgogoro wa Kargil wa 1999 huko Kashmir.

Nchi zote mbili zinadai jimbo hilo kuwa lao, na kwa sasa zinasimamia sehemu zake tofauti.

India pia ilipigana na Pakistan mwaka 1971, ilipoingilia kati kuunga mkono Pakistan Mashariki (sasa Bangladesh) katika vita vyake vya uhuru dhidi ya Pakistan.

Chini ya 2% ya wakazi wa Pakistan sasa ni Wahindu. "Pakistani imekuwa ya Kiislamu zaidi na zaidi," anasema Dk Price, "Hiyo ni kwa sababu wengi wa wakazi wake sasa ni Waislamu, na kuna Wahindu wachache sana waliosalia huko."

"Na India sasa inakuja zaidi chini ya ushawishi wa utaifa wa Kihindu."

 Sehemu za Amritsar ziliharibiwa na kuwa vifusi wakati wa ghasia mwaka 1947. Waislamu walitaka jiji hilo liwe sehemu ya Pakistan na Wahindu walitaka libaki India.

Chanzo cha picha, Getty Images

"Urithi wa kugawanya ni wa kufadhaisha," anasema Dk Newbigin. "Imeunda dini kubwa zenye nguvu katika nchi zote mbili.

Wachache wamekuwa wadogo na walio hatarini zaidi kuliko walivyokuwa hapo awali."

Ugawaji unaweza kuepukwa, anasema Profesa Navtej Purewal.

"Inawezekana mwaka 1947 kuunda India iliyoungana. Ingeweza kuwa shirikisho legelege la majimbo, ikiwa ni pamoja na majimbo ambayo Waislamu walikuwa wengi," anasema.

"Lakini Gandhi na Nehru wote walisisitiza kuwa na serikali ya umoja, inayodhibitiwa kutoka katikati.

Kwa kweli hawakuzingatia jinsi Waislamu walio wachache wangeweza kuishi ndani ya aina hiyo ya nchi."