Nywele bandia marufuku 'Miss Ivory Coast'

Chanzo cha picha, COMICI
Nywele za bandia au mawigi yamekuwa yakitawala katika mashindano maarufu ya urembo nchini Ivory Coast kwa miaka mingi.
Hivyo, Washiriki nchini humo hutumia kiasi kikubwa cha fedha kujiandaa kuanzia mavazi hadi mitindo ya nywele huku wachache sana wakichagua muonekano wa asili.
Kwa zaidi ya miongo sita, kumekuwa na mifano miwili tu ya kipekee ya hivi karibuni ya Marlène-Kany Kouassi, aliyeshinda taji la Miss Ivory Coast mwaka 2022 akiwa amependeza kwa nywele zake fupi za asili.
Ushindi wake haukuwa wa kipekee tu nchini Ivory Coast bali hata duniani kote, ambako viwango vya urembo vya Magharibi mara nyingi hutazamwa kama ndivyo vinavyotakiwa na washiriki na hata majaji.
Mabadiliko yameanza kujitokeza taratibu mwezi Disemba mwaka jana, Angélique Angarni Filopon kutoka kisiwa cha Karibiani cha Martinique ambayo ni sehemu ya Ufaransa, alivuma baada ya kutangazwa kuwa Miss , hasa kwa sababu ya umri wake ana miaka 34 na pia kwa sababu alikuwa na nywele fupi za Afro.
Lakini mwaka huu waandaaji wa shindano la Miss Ivory Coast wameamua kufanya mageuzi kuanzia mwanzo kabisa.
Na kupiga marufuku mawigi, nywele za bandia na urefushaji nywele kuanzia hatua za awali za mashindano hayo, ambayo hufanyika katika miji 13 nchini kote pamoja na wale wanaoishi ughaibuni.
"Tunataka washiriki wawe wa asili, iwe ni kwa nywele zilizopakwa dawa au zilizosokotwa, nywele hizo lazima ziwe zao wenyewe. Urembo lazima uwe wa kweli," alisema Victor Yapobi, rais wa kamati ya maandalizi ya Miss Ivory Coast, alipokuwa akizungumza na BBC.

Ivory Coast ndio nchi pekee barani Afrika inayotekeleza marufuku hii katika shindano la kitaifa.
Bwana Yapobi alisema waandaaji wa mashindano hayo nchini Ivory Coast kwa muda mrefu wamekuwa wakijitahidi kuhimiza muonekano wa asili zaidi , kwa mfano kufanya mabadiliko ya muonekano kwa urembo ni marufuku na matumizi ya dawa za kupunguza weusi wa ngozi hayakubaliki.
"Tumeamua mwaka huu kuonyesha uzuri wa asili wa wasichana hawa," alisema.
Mabadiliko mengine pia yameanzishwa, kama kuruhusu wanawake wafupi kidogo kushiriki , kima cha chini sasa ni mita 1.67 (futi 5.4), kuongeza umri wa juu kwa miaka mitatu hadi kufikia miaka 28, na jambo muhimu zaidi kupunguza ada ya ushiriki kuwa dola 30 hadi dola 50.
"Mabadiliko haya ya vigezo yametokana na kuona kuwa wasichana hawa walikuwa wakitumia fedha nyingi sana kushiriki na ilikuwa ikiwalemea kifedha," aliongeza.
BBC ilipohudhuria shindano la awali mjini Daloa, jiji kuu la eneo la magharibi la Haut-Sassandra, mshiriki mmoja alifurahi sana kutokana na kanuni mpya akihisi kwamba zinampa nafasi nzuri zaidi ya kushinda kwa kuwa hapendi kuvaa nywele bandia.

Hatua hiyo iliyolenga kusherehekea uzuri wa asili wa Mwafrika imechochea mjadala mkubwa nchini humo, ambako nywele bandia na za kusuka ni maarufu sana.
Kama chaguo la mitindo, wanawake wengi wanapenda ubunifu unaowezeshwa na wigs na nywele za bandia. Pia hutumika kama "mitindo ya kulinda nywele" yaani kupunguza mvutano na kuvutwa kwa nywele kila siku ambavyo vinaweza kusababisha kukatika.
Hali hii ilionekana kwa baadhi ya washiriki mjini Daloa waliokuwa na maoni kuwa kanuni hiyo imeondoa kipengele cha kujieleza binafsi.
"Mimi ni shabiki wa mawigi. Napenda mawigi" alisema mshiriki na mtaalamu wa urembo Astrid Menekou. Msichana huyo mwenye umri wa miaka 24 aliambia BBC kuwa alishtushwa awali na kanuni ya kupiga marufuku mawigi na nywele za bandia.
"Sikutegemea marufuku hii! Lakini napenda nywele zangu, na hilo ni sawa."
Kanuni hiyo mpya imewafanya washiriki kufikiria zaidi kuhusu dhana ya urembo na imebadili mitazamo ya baadhi yao, kama Laetitia Mouroufie.
"Mwaka jana nilivaa nywele za kusuka kwa sababu nilidhani ndivyo urembo unavyopaswa kuwa," alisema mshiriki huyo mwenye umri wa miaka 25.
"Mwaka huu, najisikia mwenye kujiamini zaidi kwa kuwa mimi mwenyewe."

Iwapo mashindano haya yataweza kubadili mitazamo hata nje ya ulimwengu wa urembo, yanaweza kuwa na athari kubwa kiuchumi.
Mawigi yaliyotengenezwa kwa nywele halisi za binadamu ambayo yanaweza kudumu kwa miaka mingi yakitunzwa vizuri , huuzwa kwa bei ya kati ya dola 200 hadi 4,000, huku zile za plastiki zikiuzwa kwa dola 10 hadi 300.
Sekta ya biashara ya nywele nchini Ivory Coast inakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 300 kwa mwaka, huku mawigi na nywele za kusuka zikichukua sehemu kubwa ya soko hilo.
"Marufuku hii si nzuri kwetu," alisema Ange Sea, mjasiriamali wa saluni mwenye umri wa miaka 30 mjini Daloa, alipoongea na BBC.
"Wanawake wengi wanapenda mawigi. Hii itaathiri biashara yetu na tunapata faida kubwa zaidi tunapofanya kazi za kusuka nywele bandi."
Katika saluni yake, gundi hutumika kuunganisha mawigi kwa uangalifu ili zionekane za asili zaidi na wanawake hutumia saa nyingi wakisuka au kuweka nywele bandia.
Hii inaonyesha jinsi utamaduni wa mawigi umejikita sana Afrika Magharibi, licha ya harakati ya kuenzi nywele za asili miongoni mwa wanawake weusi duniani ambayo imekua kwa kasi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Bidhaa za nywele za asili zimekuwa rahisi kupatikana kwa sasa na watu maarufu wanahamasisha matumizi ya nywele asilia wamejaa mitandaoni kote duniani, wakitoa ushauri kuhusu namna ya kutunza na kutengeneza nywele za asili jambo ambalo linaweza kuchukua muda mwingi.
Hapo awali, ilichukuliwa kuwa si ya kitaalamu mwanamke kuvaa nywele zake za asili, na ilikuwa jambo la kushangaza kuwaona wanawake weusi kwenye runinga kama watangazaji au wakurugenzi wakuu wa mashirika wakiwa na nywele zao halisi.
Kwa mujibu wa Florence Edwige Nanga, mtaalamu wa nywele na ngozi ya kichwa katika jiji kuu la Abidjan, hali hiyo bado ipo nchini Ivory Coast.
"Fungua tu runinga , utaona karibu kila mwanahabari amevaa wig," alisema mtaalamu huyo akizungumza na BBC.
"Urembo huu wa nyongeza una mvuto, lakini pia unaweza kuleta matatizo kama vile kupoteza nywele au maambukizi ya ngozi ya kichwa," alionya.
Kwa kuwa duru za awali za mashindano zimeshaanza, mjadala unaendelea kuhusu kama mashindano ya urembo yanapaswa kuweka kanuni za urembo au wanawake wenyewe waamue namna wanavyotaka kuonekana.
Huenda matokeo yakawa kwamba jamii ya Ivory Coast ikawa tayari kukubali mitazamo yote miwili ya kuvaa nywele asilia au kutumia wigs na nywele za kusuka, kwa mabadiliko kadri mtu anavyopenda.
Bw. Yapobi alisema maoni aliyopokea kuhusu kanuni hizo mpya yamekuwa ya "ajabu sana" na yanaonyesha wazi kuwa yameleta athari chanya.
"Kila mtu anatupa pongezi. Kila mtu, hata kutoka nje ya nchi. Napokea barua pepe na jumbe za WhatsApp kutoka kila mahali wakitupongeza kwa kutaka kurejea kwenye asili yetu."
Alisema hakuna uamuzi uliokuwa umefanyika kuhusu kama marufuku ya kuvaa wig itawahusu washiriki 15 watakaofika fainali ya Miss Ivory Coast 2025.
Tamasha hilo kubwa linatarajiwa kufanyika katika hoteli moja jijini Abidjan mwishoni mwa mwezi Juni na litarushwa moja kwa moja kupitia runinga ya taifa.
"Ikifanikiwa, tutaendelea na kuendeleza mpango huu kwa miaka ijayo," alisema Bw. Yapobi.
Kwa Doria Koré, ambaye alikuja kutangazwa kuwa Miss Haut-Sassandra, taji lake lina maana kubwa zaidi: "Kushinda nikiwa na nywele za asili kunaonesha uzuri wa kweli wa wanawake wa Kiafrika."
Bi Dali alisema anaondoka na kitu chenye thamani kubwa zaidi – kujiamini: "Sijashinda, lakini najivunia. Huyu ndiye mimi."