Jeshi kudhibiti tena Ikulu kubadili muelekeo wa vita vya Sudan?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Barbara Plett Usher
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka Port Sudan
Taswira za wanajeshi wakisherehekea huko Khartoum zinaashiria hatua kubwa katika mashambulizi ambayo yamewezesha Jeshi la Sudan (SAF) kurejesha maeneo mengi katika miezi ya hivi karibuni.
SAF ilipoteza udhibiti wa mji mkuu mwanzoni mwa vita na imekuwa ikipambana kwa miaka miwili kuurejesha kutoka kwa Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF).
Sasa wamechukua tena Ikulu ya Rais na wanaamini wako kwenye njia ya kurejesha mji mzima. Lakini bado wako mbali na kushinda vita.
Jengo hilo, likiwemo Ikulu ya Kihistoria ya Republican, ni ishara ya mamlaka na enzi, muhimu kwa serikali inayoongozwa na jeshi na hadithi yao kama watawala halali wanaopambana na "kikundi cha kigaidi."
Huu pia ni ushindi wa kimkakati.
Baada ya kusafisha vitongoji vya nje vya Khartoum, jeshi limechukua sehemu kubwa ya jiji, likiwafurusha wapiganaji wa RSF kutoka maeneo muhimu kama majengo ya serikali na kuwasogeza mbali na Makao Makuu ya Jeshi, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi.
Hii inamaanisha kuwa RSF imepoteza udhibiti wa mji mkuu, ingawa wapiganaji wake bado wapo Khartoum.
Lakini haijulikani ni kwa kiasi gani mstari wa mbele umehamia. Wapiganaji wa RSF bado wanasambaa katikati ya jiji na wanadhibiti sehemu ya uwanja wa ndege. Pia wanashikilia maeneo kusini mwa Ikulu.
Mapigano makali yanatarajiwa kuendelea huku jeshi likijaribu kuwazunguka vikosi vya RSF vilivyobaki. Kikosi cha wanamgambo tayari kimeonyesha kuwa kinaweza kupigana hata katika hali dhaifu, baada ya kufanya shambulio la ndege isiyo na rubani katika Ikulu lililoua wanahabari wa Sudan na maafisa wa jeshi.
Ushindi kamili wa jeshi katika mji mkuu unaweza kubadili mwelekeo wa vita au kuimarisha mgawanyiko wa maeneo kati ya pande mbili hasimu.

Chanzo cha picha, Getty Images
RSF, inayoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, inadhibiti sehemu kubwa ya eneo la Darfur magharibi mwa Sudan na baadhi ya maeneo kusini.
Serikali inayoungwa mkono na jeshi, inayoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, inadhibiti sehemu za mashariki na kaskazini mwa Sudan.
Wanaume hawa wawili waliwahi kushirikiana na kufanya mapinduzi pamoja kabla ya mgogoro wa mamlaka kati yao kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Aprili 2023.
Udhibiti kamili wa Khartoum unaweza kusaidia jeshi kukamilisha kutwaa maeneo ya katikati mwa Sudan, ambako limefanikiwa kuyachukua tena kutoka RSF katika miezi ya hivi karibuni.
Hali hii inaweza pia kutoa msukumo kwa SAF kujaribu kuikabili RSF katika ngome yake ya Darfur, hasa katika mji wa El Fasher, ambao umekuwa katika mzingiro wa RSF kwa karibu mwaka mmoja.
Lakini wachambuzi wengi wanaamini kuna hatari ya Sudan kugawanyika kwa hali halisi, huku pande zote mbili na washirika wao wakijiimarisha katika maeneo yao ya ushawishi.
RSF inajaribu kuunda serikali mbadala katika maeneo inayoongoza, na mwezi uliopita, ilikusanya makundi washirika kusaini hati ya kisiasa na katiba huko Nairobi.
Lengo lake lilikuwa kuonyesha kuwa, licha ya kushindwa kwenye uwanja wa vita, bado ni nguvu inayohitaji kuzingatiwa – na kwamba nia yake ya kutawala Sudan bado haijabadilika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia wa Sudan wameathirika pakubwa na vita hivi vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vimesababisha vifo, uharibifu mkubwa, na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Umoja wa Mataifa umeelezea hali nchini Sudan kama janga baya zaidi la kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kukimbia makazi yao na mamilioni wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku sehemu za nchi zikielekea kwenye njaa.
Khartoum ni mojawapo ya maeneo yanayotarajiwa kufikia hali ya njaa hivi karibuni, kutokana na uporaji mkubwa unaofanywa na wanajeshi wa RSF na vikwazo vya msaada vilivyowekwa na serikali ya Sudan. Hivyo, mabadiliko ya mamlaka katika jiji hilo yanaweza kuleta tofauti kubwa katika hali ya kibinadamu.
Lakini kwa watu wengi wa Sudan, hii ina maana kuwa hakuna mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kwa sasa.
Pande zote mbili zimeshutumiwa kwa kuzuia misaada ya dharura, wakitumia hali hiyo kama silaha ya vita, kulingana na maafisa wa Umoja wa Mataifa. Na zote zimeshtakiwa kwa uhalifu wa kivita, ingawa RSF imeshtumiwa zaidi kwa makosa ya ubakaji wa halaiki na mauaji ya kimbari.
Jeshi litakuwa na matumaini kuwa kurejesha Ikulu ya Rais kutakuwa hatua muhimu kuelekea ushindi mkubwa wa kijeshi.
Lakini ingawa SAF inaonekana kuwa na kasi kwa sasa, ni vigumu kwa upande wowote kushinda vita kwa namna itakayowaruhusu kutawala Sudan nzima, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya International Crisis Group.
Hata hivyo, pande zote mbili zimedhamiria kuendelea kupigana kwa ajili ya maeneo yaliyosalia, na juhudi za kufufua mazungumzo ya amani hadi sasa zimeshindwa.