Kwanini mji huu uko katikati ya vita vya Sudan?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Marco Oriunto
- Nafasi, BBC News
Vita vinavyoendelea kati ya vikosi vya serikali na waasi wenye silaha nchini Sudan vimehamia kwenye mji wa El Fasher, mji mkuu wa Kaskazini mwa Darfur, magharibi mwa nchi.
Ijumaa, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuwa watu 70 waliuawa katika shambulizi lililotekelezwa na Vikosi vya kukabiliana na dharura (RSF) katika hospitali ya mji huu.
Tangu vita vilipoanza mwaka 2023, maelfu ya watu wamepoteza maisha na zaidi ya milioni 10 wamekimbia makwao katika kile Umoja wa Mataifa kinachokiita janga kubwa la kibinadamu duniani.
Lakini, kwa nini El Fasher imekuwa kituo cha vita hivi?
Udhibiti wa kikanda

Darfur ni eneo lenye ukubwa sawa na Hispania na lina idadi kubwa ya watu wa Sudan.
Vikosi vya RSF tayari vinadhibiti majimbo manne kati ya matano ya Darfur.
Kuchukua El Fasher kutawapa udhibiti wa eneo lote la Darfur.
"El Fasher ndiyo mji wa mwisho katika Darfur unaodhibitiwa na jeshi la taifa," anasema mchambuzi wa siasa wa Sudan, Dallia Abdelmoniem.
Ikiwa RSF itadhibiti El Fasher, wataweza kutawala upande wa magharibi wa Sudan.
"Ni vita vikubwa," anasema Abdelmoniem. "[RSF] inaweza kutangaza uhuru au kuhimiza kugawanywa kwa nchi."
Mvutano wa kikabila

Chanzo cha picha, Reuters
El Fasher iko katikati ya mvutano wa kikabila unaoendelea, ambao unahatarisha kugawanya nchi.
Darfur ni makazi kwa jamii kubwa za Waafrika, wakiwemo Wafur, Wazaghawa, na Wamasalit.
Wengi wao wanapinga sera za serikali ya Sudan, wanazoona kuwa ni za kibaguzi dhidi ya watu wasio Waarabu.
Mwaka 2003, mvutano wa kikabila ulisababisha kampeni ya kikatili iliyosimamiwa na serikali dhidi ya jamii za Waafrika.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai iliwashitaki viongozi wa Sudan na Janjaweed, kikundi cha kijeshi kilichosaidiwa na serikali, kwa uhalifu wa kimbari, mateso, na uhalifu wa vita.
Kufikia mwaka 2013, Janjaweed walijitambulisha kama Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Hivi sasa, RSF inataka kudhibiti Darfur.
"Jamii nyingi za Kiafrika zinaishi El Fasher, huku RSF ikiwa inajumuisha hasa makabila ya Kiarabu ya Sudan na wanajeshi wa kulipwa," anasema Abdelmoniem.
"Wanaweza kuanzisha ghasia zaidi. Historia ya RSF inaonesha hawana aibu kufanya hivyo."
Vita vinavyoendelea nchini Sudan vimejaa ukatili kutoka pande zote mbili.
Katika ziara ya hivi karibuni kwenye kambi ya wakimbizi wa Sudan mpakani na Chad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy, alisema alifahamu kuhusu "baadhi ya mambo ya kutisha niliowahi kusikia na kuona maishani mwangu."
"Wanawake na watoto wamekuwa wakihofia maisha yao - wakisimulia visa vya mauaji ya kimbari, kunyanyaswa, kuchomwa moto, unyanyasaji wa kingono dhidi yao na watoto wao. Na kinachotamausha zaidi ni njaa, - mateso yasiyoelezeka."
Kuzozania rasilimali zilizopo

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapigano ya kudhibiti El Fasher pia ni vita ya rasilimali muhimu.
"Uwezo wa uchimbaji madini wa Darfur ni mkubwa," anasema mwandishi wa BBC, Mohanad Hashim.
"Kuna mafuta, urani, maji ya chini ya ardhi, lakini kinachochochea vita hivi ni dhahabu."
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, biashara ya magendo ya dhahabu inadhaniwa kufadhili vita.
Kudhibiti Kaskazini mwa Darfur kupitia El Fasher kunaweza kutoa ufikiaji wa nchi jirani kama Libya na Chad, pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao wanatamani dhahabu.
Kwa mujibu wa nyaraka za Hazina ya Marekani, kiongozi wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, tayari anadhibiti mgodi wa dhahabu wa faida kubwa katika Darfur.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid