Vita vya Sudan: RSF kuunda serikali yao kuna maana gani?

rf

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Abdul Rahim Hamdan Dagalo (kulia), naibu kamanda wa RSF akiwa ameambatana na mwenyekiti wa waasi wa SPLA-Kaskazini, Abdelaziz al-Hilu (kushoto) kabla ya mpango wao wa kutia saini Mkataba wa kuunda serikali jijini Nairobi, Kenya.
  • Author, Akisa Wandera
  • Nafasi, BBC

Wanamgambo wa Rapid Forces (RSF) na makundi washirika ya kisiasa na yenye silaha wametia saini mkataba wa kuanzisha serikali katika maeneo wanayoyadhibiti.

Kundi hilo, ambalo sasa linajiita Sudan Founding Alliance, linadai linataka taifa hilo jipya liwe la kisekula, kidemokrasia, na la ugatuzi, lililojengwa juu ya "uhuru, usawa na haki."

Hatua hii inazua wasiwasi kuhusu madhara yanayoweza kutokea kwa nchi ambayo tayari imeharibiwa na migogoro. Sudan iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 2023, kati ya Jeshi la Sudan na Rapid Forces.

Kutiwa saini kwa mkataba huo kulifanyika faraghani katika mji mkuu wa Kenya, licha ya upinzani kutoka kwa kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Abdel Fattah Al Burhan.

Miongoni mwa waliotia saini ni Abdel Rahim Dagalo, Naibu kiongozi wa RSF na kaka wa kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye hakuwepo. Alikuwepo pia Abdelaziz al-Hilu, kiongozi wa Sudan People's Liberation Movement-North (SPLM-N), kundi linalodhibiti sehemu za majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile.

Pia unaweza kusoma

Nchi katika machafuko

fc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Moto ukiwaka katika eneo la soko la mifugo huko al-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini mwa Sudan, Septemba 1, 2023, baada ya mashambulizi yaliyofanywa na RSF.

RSF iliundwa kutoka kwa wanamgambo wa Janjaweed ambao hapo awali walipigana kwa niaba ya serikali ya Sudan na wanaongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti. RSF inadhibiti sehemu muhimu za Sudan, ikiwa ni pamoja na Darfur, sehemu za Khartoum, Kordofan, na Blue Nile.

Huku kukiwa na mzozo ambao tayari umeua zaidi ya watu 60,000, haijuulikani kwa namna gani wataweza kutoa huduma za kimsingi za kiserikali kama vile kulipa mishahara, kukusanya kodi, kutoa maji, pamoja na huduma za afya na elimu kwa raia.

"Watu wengi huko Darfur hawana uhakika kuhusu serikali hii, kwa sababu kundi hili halina mpango uliopangwa wa kusimamia masuala ya kiraia au taasisi za utumishi wa umma," anasema Musbah Eisah, mtetezi wa haki za binadamu anayefanya kazi huko Darfur.

Mzozo huo umewalazimu watu milioni 12 kukimbia makazi yao. Maelfu ya raia wameuawa, huku RSF na jeshi wakituhumiwa kufanya ukatili.

Muundo wa serikali ya RSF

fvc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanawake na watoto wamesimama kwenye foleni ndefu, wakisubiri kujisajili kwa ajili ya msaada huko Agari, Kusini mwa Kordofan.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyomo kwenye serikali mpya, ni mfumo wa utawala wa serikali wa ngazi nne, unaojumuisha serikali ya shirikisho, kikanda, majimbo na serikali za mitaa.

Pia inapendekeza Bunge la Kitaifa lenye vyombo viwili vya kutunga sheria, yaani Seneti na Baraza la Wawakilishi, pamoja na tume ya kikatiba iliyopewa jukumu la kuandaa katiba ya mpito.

Mkataba huo pia unabatilisha maamuzi yote yaliyofanywa chini ya serikali iliopo, isipokuwa tangazo la uhuru wa Sudan la 1956.

RSF imepata uungwaji mkono kutoka kwa makundi kadhaa ya kisiasa ikiwa ni pamoja na Umoja wa Vikosi vya Kiraia vya Kidemokrasia (Taqaddum), ambalo linawakilisha vyama vingi vidogo vidogo vya kisiasa, pamoja na Sudan People's Liberation Movement-North (SPLM-N), makundi yenye ushawishi katika mikoa ya kusini na magharibi na National UMMA Party, mjumuiko wa makundi makongwe ya upinzani nchini Sudan vyama vya upinzani.

RSF inatumai serikali hiyo itasaidia kupanua wigo wake wa kisiasa na kupata uhalali wa ndani na kimataifa.

Lakini wataalamu wana maoni tofauti: "Vyama na mavuguvugu haya yanayoongozwa na RSF, hayana ushawishi wowote, ama ndani au kimataifa." anasema Musbah Eisah.

Majibu ya Sudan kwa mkutano huu, ni kumrudisha nyumbani balozi wake nchini Kenya, na kuituhumu Nairobi kuunga mkono harakati za RSF.

Kenya imejitetea kwa kusema, inaunga mkono juhudi za amani pekee kwa kutoa jukwaa lisiloegemea upande wowote ili kufanya mazungumzo, kwani ni utamaduni wake wa muda mrefu wa kuwezesha mazungumzo katika eneo hilo.

Hata hivyo, Nairobi imekumbwa na ukosoaji mkubwa, huku wengi wakimshutumu Rais William Ruto kwa kusaidia RSF katika kuiyumbisha zaidi Sudan.

Katika taarifa yake kwenye X (zamani Twitter), Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Marekani, Seneta Jim Risch ameandika, "Mwaka jana, niliongoza juhudi katika Bunge la Congress kutambua ukatili unaofanywa na RSF nchini Sudan, ambao umechangia vifo vya zaidi ya watu 150,000 kuwa ni mauaji ya kimbari. Na kuanzia mwezi Januari hiyo ndio ikawa sera ya Marekani. Sasa, Kenya, mshirika wa Marekani, inaisaidia RSF kuhalalisha mauaji yao ya kimbari kwa madai ya kuleta amani Sudan. Ni Jaribio la kuficha ukweli na halitamaliza mauaji hayo."

RSF imerudishwa nyuma katika maeneo muhimu, hasa Khartoum Kaskazini na Omdurman, miji miwili kati ya mitatu katika eneo la mji mkuu wa Khartoum.

Jeshi la Sudan linatarajia kuuteka tena mji mkuu huo na kuunda serikali yake.

Mtafiti na mchambuzi wa sera wa Sudan, Hamid Khalafalla anasema, "baada ya RSF kupoteza maeneo muhimu katika wiki za hivi karibuni, imegundua kuwa inahitaji kubadilisha mkakati wao. Ikiwa wataingia kwenye mazungumzo sasa, nguvu zao za kujadiliana zimedhoofika, jambo ambalo linaweza kusababisha matokeo yasiyofaa kwao."

Sababu za kiuchumi

fdc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Raia wa Sudan wakisherehekea huko Meroe katika Jimbo la Kaskazini mwa nchi hiyo Januari 11, 2025, baada ya jeshi kutangaza kulikomboa eneo la Al-Jazira katika jimbo la Wad Madani, kutoka kwa RSF.

Udhibiti wa RSF wa rasilimali muhimu ni sababu kuu ya kukuwa kwa ushawishi wao na nguvu zao nchini Sudan. Moja ya rasilimali zao kubwa ni migodi ya dhahabu huko Darfur.

Sudan ni mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika, na migodi hii ni muhimu kwa uchumi wa nchi hiyo. Inawapa faida kubwa ya kifedha, na kufadhili shughuli zao za kijeshi.

Zaidi ya dhahabu, RSF pia inashikilia baadhi ya maeneo ya mafuta ya Sudan, hasa katika mikoa ya Kordofan Kusini na Blue Nile.

Ingawaje jeshi la Sudan linadhibiti maeneo makubwa zaidi yanayozalisha mafuta, uwepo wa RSF kwenye maeneo haya bado unawaruhusu kupata faida kutokana na mauzo ya mafuta.

"Tangu mzozo uanze, uchimbaji wa dhahabu na madini umeshamiri." Hamid anasema, "pande zote mbili zina himaya za kiuchumi, lakini waathirika wa kweli ni watu wa Sudan, ambao rasilimali zao zinauzwa nje ya nchi kinyume cha sheria."

Athari za kikanda

Serikali kama hiyo imeibuka katika maeneo mbalimbali ya migogoro, kama vile Libya ambako serikali mbili hasimu ziliundwa baada ya kuanguka kwa Muamar Gaddafi mwaka 2011. Nchi hiyo iligawanyika kati ya serikali ya Tripoli, inayoungwa mkono na makundi yenye silaha, na serikali ya Tobruk, inayoungwa mkono kimataifa, hasa na Misri na UAE.

Licha ya juhudi za kimataifa za kuleta amani, serikali hizi pinzani hazikuweza kutawala kwa amani, na hali ilizidi kuwa mbaya na kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu, na kusababisha kukosekana kwa utulivu na usalama.

Shida kubwa kwa RSF itakuwa ni kupata uungwaji mkono kimataifa. Wataalamu wanasema uamuzi wa kuandaa mikutano jijini Nairobi ni jaribio la kutafuta uungwaji mkono kikanda na kimataifa kwa sababu bila hilo, serikali inayopendekezwa inaweza kufa.

Kwa hali ilivyo, viongozi kadhaa wa RSF, haswa Bw Dagalo, wanakabiliwa na vikwazo vya kimataifa kwa kuhusika kwao katika mzozo unaoendelea.

Vikwazo hivi ni pamoja na marufuku ya kusafiri kwenda Marekani na kuzuiwa mali yao yoyote iliyoko Marekani. Umoja wa Ulaya pia umeweka marufuku ya kusafiri na kuzuia mali za viongozi wa RSF.

Mzozo huo sasa unakaribia miaka miwili, huku zaidi ya watu milioni 12 wakiyahama makazi yao na kuzidisha mzozo wa kibinadamu.