Vita vya Sudan: BBC imepenyeza simu katika mji wa el-Fasher ili kufichua njaa na hofu

Chanzo cha picha, Hafiza
- Author, Heba Bitar
- Nafasi, Uchunguzi wa BBC, el-Geneina
"Hakuacha neno lolote la mwisho. Alikuwa ameshakufa alipokuja kuchukuliwa," anasema Hafiza kwa sauti ya chini, wakati anaelezea jinsi mama yake alivyouawa katika jiji lililozingirwa huko Darfur, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, vilivyoanza miaka miwili iliyopita.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 21 ameeleza jinsi maisha ya familia yake yalivyobadilika baada na kifo cha mama yake, kupitia moja ya simu kadhaa ambazo BBC ilifanikiwa kuzipeleka kwa watu waliokuwa wamekwama katikati ya mapigano huko El-Fasher.
Kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara, mji wa el-Fasher umetengwa na ulimwengu wa nje kwa mwaka mzima, na hivyo kufanya kuwa vigumu kwa waandishi wa habari kuingia. Kwa sababu za kiusalama, tunatumia tu majina ya kwanza ya watu ambao walikubali kurekodi maisha yao kupitia simu za BBC.
Hafiza anaeleza jinsi alivyojikuta ghafla akiwajibika kwa mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitano na wasichana wawili wadogo.
Baba yao alifariki kabla ya kuanza kwa vita hivyo, ambavyo vimehusisha wanamgambo wa Rapid Forces (RSF) na Jeshi la Nchi, na kusababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu duniani.
Hafiza aliyepoteza Mamake

Chanzo cha picha, Hafiza
Mji anao ishi Hafiza ndio mji mkubwa wa mwisho kudhibitiwa na wanajeshi katika eneo la magharibi mwa Sudan la Darfur, na umezingirwa na RSF kwa muda wa miezi 12 iliyopita.
Agosti 2024, kombora liligonga soko ambapo mama yake alikuwa amekwenda kuuza bidhaa za nyumbani.
"Huzuni ni kubwa sana, bado siwezi kwenda eneo lake la kazi," anasema Hafiza katika moja ya ujumbe wake wa kwanza wa video baada ya kupokea simu yake, muda mfupi baada ya kifo cha mama yake.
"Natumia muda mwingi kulia peke yangu nyumbani."
Pande zote mbili katika vita zimeshutumiwa kwa uhalifu wa kivita na kuwalenga raia kimakusudi - jambo ambalo wanalikanusha.
RSF pia ilikanusha shutuma kutoka kwa Marekani na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwamba imefanya mauaji ya halaiki dhidi ya jamii zisizo za Kiarabu katika maeneo mengine ya Darfur baada ya kutwaa udhibiti wa maeneo hayo.
RSF inadhibiti njia za kuingia na kutoka katika jiji na wakati mwingine inaruhusu raia kuondoka, kwa hivyo Hafiza aliweza kuwapeleka ndugu zake kukaa na familia nyingine katika eneo lisilo na mapigano.
Lakini yeye alibaki katika mji huo akijaribu kutafuta pesa za kuwahudumia.
Katika jumbe zake, anaelezea siku za kusambaza blanketi na maji kwa watu waliohamishwa, kusaidia kupika na kusaidia kikundi cha uhamasishaji wa kupima saratani ya matiti kwa malipo ya pesa kidogo kumsaidia kuishi.
Usiku anakuwa peke yake.
"Nakumbuka sehemu ambazo mama na ndugu walikuwa wakikaa, nahisi kuvunjika moyo," anaongeza.
Mostafa aliyepoteza nyumba

Karibu katika kila video ambazo Mostafa mwenye umri wa miaka 32 alitutumia, milio ya risasi inaweza kusikika kwa nyuma.
Siku moja, baada ya kuitembelea familia yake, alirudi na kukuta nyumba yake katikati mwa jiji imepigwa na makombora - paa na kuta zimeharibiwa - na imeporwa kila kilichobaki.
"Nyumba nyingi katika mtaa wetu zimeporwa," anasema, akiilaumu RSF.
"Hakuna sehemu salama katika mji wa el-Fasher," anasema. "Hata kambi za wakimbizi zinapigwa mabomu.
"Kifo kinaweza kumpata mtu yeyote, wakati wowote, bila ya onyo ... kwa risasi, makombora, njaa au kiu."
Katika ujumbe mwingine, anazungumzia ukosefu wa maji safi, akielezea jinsi watu wanavyokunywa kutoka kwenye vyanzo vilivyochafuliwa na maji taka.
Mostafa na Manahel mwenye umri wa miaka 26, ambaye pia alipokea simu ya BBC, walijitolea kupika katika jiko la jumuiya kwa michango kutoka watu wa Sudan wanaoishi kwingineko.
Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu njaa katika mji huo, jambo ambalo tayari limetokea katika kambi ya karibu ya Zamzam, ambayo ni makazi ya zaidi ya watu 500,000 waliokimbia makazi yao.
Watu wengi hawawezi kufika sokoni "na wakienda, bidhaa ni bei ya juu", anaelezea Manahel.
"Kila familia ni sawa - hakuna tajiri au maskini. Watu hawawezi kumudu mahitaji ya msingi kama vile chakula."
Manahel na familia yake

Chanzo cha picha, Manahel
Vita vilipoanza, Manahel alikuwa amemaliza chuo kikuu, alisomea Sharia na Sheria.
Mapigano yalipofikia el-Fasher, alihama na mama yake na ndugu zake sita kwenda katika mji salama, mbali zaidi na mstari wa mbele wa mapigano.
"Unapoteza nyumba yako, kila kitu unachomiliki, unajikuta katika sehemu mpya bila chochote," anasema.
Lakini baba yake alikataa kuondoka nyumbani kwao. Baadhi ya majirani walimkabidhi mali zao, naye akaamua kubaki ili kuzilinda - uamuzi ambao uligharimu maisha yake.
Anasema aliuawa na kombora la RSF Septemba 2024.
20,000 wameuawa au kujeruhiwa

Chanzo cha picha, Manahel
Tangu kuzingirwa mwaka mmoja uliopita, karibu watu 2,000 wameuawa au kujeruhiwa huko El-Fasher, kulingana na UN.
Baada ya jua kutua, ukosefu wa umeme hufanya nyakati za usiku kuwa za kutisha kwa wakazi milioni moja wa El-Fasher.
Watu walio na nishati ya jua au betri wanaogopa kuwasha taa kwa sababu "wanaweza kuonekana na droni," anaelezea Manahel.
Kuna nyakati hatukuweza kuwasiliana naye au wengine kwa siku kadhaa kwa sababu hawakuwa na intaneti.
"Kama msichana, ninaweza kubakwa," Hafiza anasema katika moja ya jumbe zake.
Yeye, Manahel na Mostafa wote wanatoka jamii zisizo za Kiarabu na hofu yao inatokana na kile kilichotokea katika miji mingine ambayo RSF imeitwaa, hasa el-Geneina, maili 250 (400km) magharibi mwa el-Fasher.
El-Geneina, kuzingirwa na mauaji

Mwaka 2023 Sudan ilishuhudia mauaji ya kutisha, kwa misingi ya kikabila, ambayo Marekani na matiafa mengine wanasema yalifikia kuwa ni mauaji ya kimbari.
Wapiganaji wa RSF na wanamgambo washirika wa Kiarabu wanadaiwa kuwalenga watu kutoka makabila yasiyo ya Kiarabu, kama vile Massalit - lakini RSF imekanusha hilo.
Mwanamke wa Kimassali niliyekutana naye katika kambi ya wakimbizi mpakani mwa Chad alielezea jinsi alivyobakwa na genge la wapiganaji wa RSF na hakuweza kutembea kwa karibu wiki mbili, UN imesema wasichana wenye umri wa miaka 14 walibakwa.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kati ya watu 10,000 na 15,000 waliuawa huko el-Geneina pekee mwaka 2023. Nusu ya wakazi wake wa zamani - ni miongoni mwa wale wanaoishi katika kambi za wakimbizi nchini Chad.
Wanahabari wachache wameweza kuingia el-Geneina. Baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo na serikali ya kiraia ya jiji hilo, timu ya BBC iliruhusiwa kutembelea mwezi Desemba 2024.
Timu ya BBC

Tulipewa walinzi kutoka ofisi ya gavana na tuliruhusiwa tu kuona walichotaka kutuonyesha.
Ilikuwa wazi kwamba RSF inadhibiti mji huo. Niliwaona wapiganaji wao wakishika doria barabarani kwa magari yenye silaha na kufanya mazungumzo mafupi na baadhi yao.
Haikuchukua muda kutambua jinsi walivyouona mzozo huo kwa njia tofauti. Kamanda wao alisisitiza hakuna raia kama Hafiza, Mostafa na Manahel wanaoishi el-Fasher.
"Mtu anayekaa kwenye eneo la vita anashiriki vita, hakuna raia, wote wanatoka jeshini," alisema.
Alidai mji wa el-Geneina sasa una amani na wakazi wake wengi - "karibu 90%" - wamerejea. "Nyumba ambazo hapo awali zilikuwa tupu sasa zimekaliwa tena."
Lakini maelfu ya wakaaji wa jiji hilo bado wanaishi kama wakimbizi huko Chad, na niliona vitongoji vingi vilivyoachwa vitupu na kuharibiwa tulipokuwa tukizunguka.
Walitupeleka kwenye soko la mboga lenye shughuli nyingi, ambako niliwauliza watu kuhusu maisha yao. Kila nilipomuuliza mtu swali, niliona wanamtazama mlinzi kabla ya kujibu na kusema kila kitu kiko "sawa."
Licha ya kusema kuwa bei ya bidhaa iko juu. Lakini mlinzi wangu mara kwa mara alinong'ona sikioni, akisema watu wanatia chumvi juu ya bei.
Tulimaliza safari yetu kwa mahojiano na Tijani Karshoum, gavana wa Darfur Magharibi ambaye mtangulizi wake aliuawa Mei 2023 baada ya kuishutumu RSF kwa kutekeleza mauaji ya halaiki.
Ni mahojiano yake ya kwanza tangu 2023, na alisisitiza yeye ni raia asiyeegemea upande wowote katika machafuko ya El-Geneina.
"Tumefungua ukurasa mpya na kauli mbiu ya amani, kuishi pamoja, kusonga mbele," alisema, akiongeza kuwa takwimu za majeruhi za Umoja wa Mataifa "zimetiwa chumvi."
Pia katika chumba hicho kulikuwa na mtu ambaye ni mwakilishi wa RSF.
Takriban wiki mbili baada ya kuzungumza na Karshoum, Umoja wa Ulaya ulimwekea vikwazo, ukisema "anahusika katika shambulio baya" dhidi ya mtangulizi wake na "alihusika katika kupanga, kuelekeza au kufanya... ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na aina nyingine mbaya za unyanyasaji wa kingono na kijinsia, na utekaji nyara."
Nilimfuata ili kupata majibu yake kwa tuhuma hizi, akasema: "Kwa kuwa mimi ni mtuhumiwa wa jambo hili, naamini kauli yoyote kutoka kwangu itakosa uaminifu."
Lakini alisema "kamwe hakuwa sehemu ya mzozo wa kikabila na alibaki nyumbani wakati wa mapigano" na kuongeza kuwa hakuhusika katika ukiukaji wowote wa sheria za kibinadamu.
"Mashtaka ya mauaji, utekaji nyara au ubakaji lazima yashughulikiwe kupitia uchunguzi huru" ambao atatoa ushirikiano," anasema Karshoum.
Kuondoa el-Fasher

Chanzo cha picha, Mostafa
Hafiza, Mostafa na Manahel waliona maisha huko el-Fasher ni magumu kuvumilia na mwezi Novemba 2024 wote watatu waliondoka katika mji huo na kwenda katika miji ya karibu.
Huku jeshi likiudhibiti tena mji mkuu, Khartoum, mwezi Machi. Darfur linasalia kuwa eneo la mwisho ambalo wanamgambo bado wanadhibiti kwa kiasi kikubwa - na hilo limeufanya mji wa el-Fasher kuwa uwanja wa vita vikali.
"El-Fasher inatisha," Manahel alisema huku akipakia vitu vyake.
"Tunaondoka bila kujua hatima yetu. Je, tutarudi tena el-Fasher? Vita hivi vitaisha lini? Hatujui kitakachotokea."