Mzozo wa Sudan: Unayofaa kujua baada ya jeshi la Sudan kuiteka tena ikulu ya Rais


Wanajeshi wawili wakijipiga picha kuotia simu huku mwanamume aliyevaa shati ya kijani wakiwa nyuma yake katika ikulu ya Rais

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Sudan wakiwa ndani ya ikulu ya Rais iliyoko Khartoum

Wanajeshi wa Sudana wamesema wapiganaji wake wamedhibiti Ikulu ya Rais iliyoko katikati mwa eneo la Khartoum.

Katika wiki za hivi majuzi wanajeshi wa Sudam walikuwa wamezidisha mapigano dhidi ya wanamgambo wa RSF katika mji mkuu wa Sudan, baada ya kushindwa kudhibiti miji mingi tangu vita vianze mwaka 2023.

Haya ndio mambo unapaswa kujua kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Sudan.

Sudan iko upande gani ya Ulimwengu?

Ramani ya eneo la Khartoum ya Sudan, inayoonyesha eneo la Ikulu ya Rais, pamoja na ramani ya Afrika inayojumuisha Ethiopia kama jirani ya kusini mwa Sudan.
Maelezo ya picha, Ramani ya eneo la Khartoum ya Sudan, inayoonyesha eneo la Ikulu ya Rais, pamoja na ramani ya Afrika inayojumuisha Ethiopia kama jirani ya kusini mwa Sudan.

Sudan iko kaskazini-mashariki mwa Afrika na ni mojawapo ya nchi kubwa zaidi barani, ikiwa na ukubwa wa karibu kilomita za mraba milioni 1.9 (milioni 734 za maili za mraba).

Sudan inapakana na nchi 7: Sudan Kusini, Misri, Libya, Chad, Eritrea, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Nchi hii yenye Waislamu wengi ina idadi ya watu zaidi ya milioni 50.

Hata kabla ya vita, Sudan ilikuwa mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.

Zaidi ya miaka miwili tangu kuanza kwa vita, nchi hii inakabiliwa na uhaba wa chakula, maji, dawa na mafuta.

Zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini humo wanakutana na uhaba mkubwa wa chakula, kulingana na ripoti ya UNHCR ya mapema mwaka huu.

Tangu mapigano yaanze, zaidi ya watu milioni 12.5 wameachwa bila makazi.

Kwanini Sudan inashuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe?

Halime Adam Moussa, mkimbizi wa Sudan ambaye anatafuta hifadhi nchini Chad kwa mara ya pili, akisubiri pamoja na wakimbizi wengine kupokea msaada wa  chakula kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), karibu na mpaka kati ya Sudan na Chad huko Koufroun, Chad, tarehe 9 Mei 2023, huku wakimbizi wengine wakiketi kwenye eneo la wazi nyuma yake.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Halime Adam Moussa, mkimbizi wa Sudan ambaye anatafuta hifadhi nchini Chad kwa mara ya pili, akisubiri pamoja na wakimbizi wengine kupokea msaada wa chakula kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), karibu na mpaka kati ya Sudan na Chad huko Koufroun, Chad, tarehe 9 Mei 2023, huku wakimbizi wengine wakiketi kwenye eneo la wazi nyuma yake.

Baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021, baraza la majenerali lilichukua hatamu za uongozi nchini Sudan, likiongozwa na majenerali wawili walio katikati ya mzozo huu:

  • Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa jeshi na ni Rais wa nchi
  • Na naibu wake, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, kiongozi wa waasi wa (RSF), ambaye pia anajulikana kama "Hemedti".

Wawili hao walikosa kukubaliana na mwelekeo wa nchi na pendekezo la kuhamia utawala wa kiraia.

Vikwazo vikuu vilijumuisha mipango ya kuingiza wanajeshi wa RSF 100,000 katika jeshi kuu, na ni nani ataongoza kikosi hicho kipya.

Wasiwasi ilikuwa kwamba majenerali hawa wawili walikuwa wanataka kubaki madarakani na kutaka kudumisha ushawishi wao.

Pia unaweza kusoma:

Ni nani anatawala Ikulu ya Rais na kwanini ni muhimu kuidhibiti?

Wanajeshi wanne wakisherehekea huku wakipiga picha  ndani ya ikulu ya Rais mjini Khartoum

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Vikosi vya serikali vilitangaza tarehe 21 Machi walikuwa wamechukua udhibiti wa ikulu ya Rais

Kabla ya vita kuanza mwaka 2023, wakati pande hizo mbili walikuwa wakishirikiana na kuwa na uhusiano mwema , Wanajeshi wa Sudan wailipatia jukumu RSF kulinda baadhi ya taasisi muhimu huko Khartoum, kama vile uwanja wa ndege, makao makuu ya jeshi, majengo ya vyombo vikuu vya habari, na ikulu ya Rais.

Wakati vita vilipoanza, RSF walikuwa tayari wanadhibiti ikulu hiyo.

Walishikilia hadi jeshi la Sudan wiki jana kutangaza kuwa limedhibiti ikulu hiyo iliyoko Khartoum.

Ikulu hiyo inachukuliwa kama "ishara ya uhuru wa Sudan," .

Kwa umuhimu inayokuwa nayo kudhibiti Ikulu ya Rais ambayo sasa imeharibiwa ni ishara na sio vile kimkakati ikiashiria ushindi kwa wanajeshi wa Sudan dhidiya waasi wa RSF.

Imeongezea maeneo ambayo wanajeshi wa Sudan wamedhibiti kwa mara nyingine katika wiki za hivi majuzi, na inatoa ishara kuwa wanajeshi wa Sudan wanakaribia kudhibiti jiji la Khartoum kikamilifu.

Picha ya televisheni ya Sudan ikiobyesha msemaji wa eshi Nabil Abdallah akitangaza kudhibitiwa kwa ikulu ya Rais

Chanzo cha picha, Sudan TV

Maelezo ya picha, Msemaji wa jeshi Nabil Abdallah alitangaza kutekwa kwa ikulu ya Rais kupitia runinga ya serikali

Je wanamgambo wa RSF ni akina nani?

Wapiganaji wa RSF wakiwa wameketi kwenye gari lililokuwa na bunduki inayoonyesha risasi katika jiji la Nyala, kusini mwa Darfur, tarehe 3 Mei 2015.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waasi wa RSF wakiendelea na mishemishe zao

RSF ilianzishwa mwaka 2013, ikiwa na mizizi katika kundi maarufu la Janjaweed, ambalo lilipigana na waasi eneo la Darfur.

Kundi hili limeshutumiwa kwa kutekeleza mauaji ya kikabila dhidi ya watu wa Darfur wasio na asili ya Kiarabu.

Tangu wakati huo, Jenerali Dagalo ameunda kikosi cha kijeshi chenye nguvu, ambacho kinatumika kutuliza mizozo nchini Yemen na Libya.

Aidha, ameanzisha maslahi ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kudhibiti baadhi ya migodi ya dhahabu nchini Sudan.

Kabla ya vita hivi vinavyoendelea kuchipuka, RSF wamelaumiwa kwa kutekeleza dhulma dhidi ya haki za kibinadamu, ikiwemo mauaji ya waandamanaji 120 mwezi Juni 2019.

Umoja wa Mataifa umeshutumu vikali RSF na wanajeshi wa Sudan kwa kutoheshimu haki za kibinadamu katika vita hivi vya wenyewe kwa wenyewe.

Waasi hawa ambao sio wanajeshi wa Sudan wameonekana kuwa kichechea cha utovu wa usalama nchini humo.

Je, RSF wanatarajiwa kufanya nini sasa?

Waasi wa RSF watatu wamevaa magwanda ya kijeshi wakiwa wameshikilia bunduki

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Picha ya waasi wa RSF

Saa chache baada ya jeshi la Sudan kutangaza kuteka tena ikulu ya Rais, RSF ilizindua shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye ikulu.

Shambulio hilo la anga limeripotiwa kuwaua watu kadhaa, wakiwemo waandishi watatu wa habari wa televisheni ya taifa ya Sudan.

Msemaji huyo wa RSF alisema baadaye katika taarifa yake kwenye Telegram kwamba vita vya kuwania ikulu bado vitaendelea na "bado wako karibu na eneo hilo.

Jeshi la wanamgambo lilisema lilifanya "operesheni ya kijeshi" ndani ya ikulu, na kuua "maadui 89".

RSF pia ilisema iliharibu magari mbalimbali ya kijeshi na kusisitiza kwamba "wataendelea kupigana".

Ni maeneo gani muhimu ambayo RSF bado inadhibiti?

Moshi ukifuka kutoka kwenye barabara  ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum huku moto ukiwaka na moshi ukitanda juu ya anga ya Khartoum tarehe 17 Aprili 2023.

Chanzo cha picha, Reuters

Mji mkuu wa pande tatu wa Sudan una miji mikuu mitatu; Khartoum, Bahri (kaskazini mwa Khartoum) na Omdurman.

Miji hiyo miwili Bahri na Omdurman iko chini ya udhibiti wa jeshi, wakati mapigano yanaendelea Khartoum, ambapo RSF bado iko madarakani katika baadhi ya maeneo ya kimkakati.

Taasisi muhimu iliyoachwa chini ya udhibiti wa RSF huko Khartoum ni uwanja wa ndege wa kimataifa.

Ingawa haifanyi kazi, lakini ina umuhimu wake katika mzozo huu wa madaraka.


Moshi ukiongezeka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum wakati mapigano yakiendelea katika mji mkuu wa Sudan tarehe 16 Aprili 2023 kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya RSF

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum bado umefungwa kufuatia mapigano ya mwaka 2013

Eneo kubwa la umuhimu wa kimkakati linaloshikiliwa na RSF ni Bwawa la Jebel Aulia.

Kwa kuzingatia eneo lake linalounganisha sehemu ya magharibi ya Sudan, ikiwa ni pamoja na Darfur, hadi katikati mwa nchi, bwawa hilo ni njia muhimu ya ugavi kwa RSF, na inaweza kutoa njia yao ya kutoka Khartoum.

RSF pia bado inadhibiti eneo la kimkakati la Al-Mogran, ambapo mto wa Blue Nile unaungana na White Nile, katikati mwa Khartoum.

Kisiwa cha Tuti kinafikiriwa kuwa eneo rahisi jeshi la Sudan kudhibiti tena.

Eneo hilo liko kati ya miji mitatu ya mji mkuu, na imezingirwa na RSF tangu vita vilipozuka.

Hali ilivyo nchini Sudan?


Ramani inayoonyesha vikundi vinavyodhibiti Sudan, ikiangazia Jeshi la Sudan, Vikosi vya RSF na vikundi Vingine
Maelezo ya picha, Ramani inayoonyesha vikundi vinavyodhibiti Sudan, ikiangazia Jeshi la Sudan, Vikosi vya RSF na vikundi Vingine

Uwiano wa mamlaka sasa unaegemea upande wa jeshi, baada ya kufanya maendeleo dhidi ya RSF katika miezi ya hivi karibuni.

Tangu Mwezi Septemba 2024, jeshi liliiondoa RSF katika maeneo muhimu.

Hasa ni miji mikuu miwili katika mji mkuu: Bahri na sehemu kubwa ya Omdurman, pamoja na jimbo la Al-Jazeera.

Jeshi lina faida ya kuwa na nguvu za anga na silaha ambazo RSF inakosa.

Muungano pia una jukumu katika vita hivi.

Wakati kamanda wa RSF wa eneo la Al-Jazeera, Jenerali Abu Aqla Kaikal, alipojitenga na jeshi, alivipa vikosi vya serikali kudhibiti jimbo hilo.

Walakini, RSF bado ina safu ya silaha na jeshi kubwa la mapigano.

RSF bado inadhibiti maeneo makubwa ya nchi, ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa ya eneo la magharibi la Darfur, ambalo limekumbwa na ghasia mbaya zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Je, mataifa mengine yanahusika katika vita hivi?

Majengo yaliyoharibiwa katika barabara isiyo na watu na vifusi vilivyotapakaa chini huko Omdurman

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Miji kama vile Omdurman iligeuzwa kuwa mahame kutokana na vita vya mara kwa mara

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema RSF imekuwa ikiungwa mkono na mataifa jirani ya Afrika, zikiwemo Chad, Libya na Sudan Kusini katika muda wote wa vita.

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umeshutumiwa kwa kuipatia silaha RSF, lakini taifa hilo la Ghuba limekanusha kuhusika kwa vyovyote vile.

Mnamo 2024, Uingereza na Marekani zilitaka UAE kukoma kuunga mkono pande zinazopigana za Sudan.

Pia kuna ripoti kwamba ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran zimesaidia jeshi laRSF kurejesha maeneo karibu na Khartoum.


Picha ya ndege zisizo na rubani

Chanzo cha picha, X / @war_noir

Maelezo ya picha, Jeshi la Sudan limekamata ndege zisizo na rubani zinazotumiwa na RSF, ambazo mtaalamu wa silaha katika shirika la Amnesty International aliiambia BBC mwaka 2024 kuwa kuna uwezekano mkubwa zilitengenezwa na serikali ya kigeni.

Uchunguzi wa BBC mnamo 2024 ulipata ushahidi kwamba jeshi laSudan lilikuwa na usambazaji wa silaha kutoka Iran, nyingi zikiwa ni ndege zisizo na rubani.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na BBC News Arabic, waziri wa mambo ya nje wa Sudan, Ali Yousef Al Sharif, alisema: "Majeshi ya magharibi yaliweka kizuizi kwa Sudan," ambayo iliwasukuma kugeukia nchi yoyote kununua silaha.

Al Sharif pia alizungumza kuhusu baadhi ya mipango inayohusiana na kuanzisha "kituo cha ugavi wa majini" kwa meli za kijeshi za Urusi kwenye pwani ya Sudan inayotazamana na Bahari Nyekundu.

Alikataa kuiita "kambi ya jeshi la majini" na alikataa ukosoaji wa makubaliano yanayoipa Urusi nafasi ya kufikia nchi yake.

Je, ni madai gani ya mauaji ya halaiki huko Darfur?

Msururu wa raia wa Sudan wanaokimbia mzozo wa Murnei katika jimbo la Darfur nchini Sudan wanavuka mpaka kati ya Sudan na Chad tarehe 4 Agosti 2023.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Raia wa Sudan waliokimbia vita katika jimbo la Darfur nchini Sudan wanavuka mpaka kati ya Sudan na Chad mwezi Agosti 2023.

Mnamo mwaka wa 2023, BBC iliona ushahidi mpya wa mauaji ya kikabila huko Darfur, ambayo mauaji hayo yamelaumiwa na wanamgambo ambao ni sehemu ya - au wanashirikiana na - RSF.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka jana kutoka shirika linaloangazia haki za kibinadamu la Human Rights Watch lilisema

Uingereza,Umoja wa Mataifa,Marekani na mashirika mengine wamesema raia walioko majimboni wanalengwa kutokana na asili yao.


Watu wakipeperusha bendera ya Sudan wakisherehekea mjini Khartoum

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Waandamanaji wanaounga mkono viongozi wa kiraia wamekuwa wakijitokeza katika mitaa ya mji mkuu

Vile vile, Ubakaji unatumiwa kama aina ya vita yasema UN huku wapiganaji wakidhulumu kingono wanawake wasio na asili ya kiarabu na matusi wakati wanapotekeleza ukatili huo, wakisema kuwa watawalazimisha "kupata watoto wenye asili ya kiarabu"".

Kulingana na mtaalam wa masuala ya mauaji ya kimbari wa Umoja wa Taifa UN Alice Wairimu aliiambia BBC kuwa Darfur imeendelea kushuhudia ongezeko la mauaji hayo wakati ulimwengu unaangazia vita vya Ukraine na Gaza.

Mauaji yanayoendelea sasa kwa muda yamejikita katika mzozo wa rasilimali kati ya wakulima wa jamii za asili ya kiarabu na wafugaji wa jamii zisizo na asili ya kiarabu.

Waasi wa RSF wamekanusha vikali kwa mauaji ya kimbari yanayolenga makabila fulani Darfur wakisema haihusiki na kile wanachokitaja ni ''mzozo wa kikabila".

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi