India-Pakistan: Fahamu nguvu za kijeshi za mataifa haya yaliyo na mzozo

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kikosi cha Usalama Mipakani cha India kimeanzisha operesheni kubwa ya kuwasaka wahusika wa shambulio la Pahalgam huko Kashmir.

Jeshi la India limefanya mashambulizi dhidi ya Pakistan na eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Islamabad mapema Jumatano asubuhi, likidai kushambulia "maeneo tisa" ya magaidi.

Pakistan inadai ni maeneo sita ndio yaliyoshambuliwa na inasema ilifanikiwa kuangusha ndege tano za kivita za India, ripoti ambayo New Delhi bado haijathibitisha.

Mvutano huu ni sehemu ya mvutano wa muda mrefu ambao umegharimu maisha ya maelfu ya watu. Mizizi wa mvutano huu ulianza zaidi ya miongo saba nyuma. Pale India na Pakistan zote zilipoanza madai ya udhibiti wa eneo lote la Kashmir.

Kufuatia shambulio hilo, Pakistan imesema India imefanya "kitendo cha wazi cha kutangaza vita" na kuapa kulipiza kisasi.

Uwezo wao wa kijeshi ukoje?

Pia unaweza kusoma

Nguvu ya Jeshi la India

dx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kombora la Agni lililowekwa kwenye lori, ni kombora la masafa ya kati lililotengenezwa India.

Kulingana na Global Fire Power, kuna pengo la nafasi nane kati ya India na Pakistan katika orodha ya nchi zilizo na nguvu kubwa zaidi za kijeshi mwaka 2025.

India inashika nafasi ya nne kati ya nchi 145, huku Pakistan ikiwa nafasi ya 12. Jeshi la India ni moja ya jeshi kubwa ulimwenguni, lina karibu wanajeshi milioni 2.2.

India ina vifaru 4,201, magari ya kivita milioni 1.5, vifaru vya mizinga 100, mizinga 3,975 na magari ya kurushia roketi 264.

Jeshi la Anga la India lina wafanyakazi zaidi ya 300,000 na jumla ya ndege 2,229, zikiwemo ndege za kivita 513 na ndege 270 za usafirishaji.

Ndege zake za kivita zinajumuisha ndege 130 za mashambulizi, ndege 351 za mafunzo, na ndege sita za kuongeza mafuta. Jeshi hilo lina jumla ya helikopta 899, ambapo 80 ni helikopta za mashambulizi.

Jeshi la Wanamaji la India, kwa upande wake, lina wafanyakazi 142,000 na jumla ya meli 293, zikiwemo manowari mbili za kubeba ndege na nyambizi 18.

Kwa upande wa vifaa, Jeshi la India lina viwanja vya ndege 311, bandari 56, na kilomita 65,000 za njia za reli.

Nguvu ya Jeshi la Pakistan

c

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Pakistani wakipiga doria karibu na msikiti ulioharibika, baada ya shambulio la India karibu na Lahore, Pakistani, Mei 7, 2025.

Kulingana na Global Fire Power, Jeshi la Pakistani lina takribani wanajeshi 1,311,000, kati ya hayo wanajeshi 124,000 ni wa jeshi la majini na wanajeshi 78,000 wa jeshi la anga.

Pakistan ina jumla ya ndege 1,399, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita 418, ndege 64 za usafirishaji, na ndege 565 za mafunzo. Ina helikopta 373, pamoja na helikopta 57 za kushambulia.

Ina vifaru 2,627, magari ya kivita 17,516, vifaru vya mizinga 662, mizinga 2,629, na magari ya kurushia makombora 600.

Jeshi la Wanamaji la Pakistan, kwa upande wake, lina jumla ya meli za kivita 121, ikiwa ni pamoja, nyambizi nane, na meli 69 za doria.

Kwa upande wa vifaa, ina viwanja vya ndege 116, bandari tatu, na kilomita 11,900 za reli.

Nyuklia na Droni

fc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, India imetia saini mkataba wa kununua ndege 31 zisizo na rubani aina ya Predator kutoka Marekani zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.5.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2024 iliyochapishwa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), India ina vichwa 172 vya nyuklia, huku Pakistan ikiwa na 170.

SIPRI inadai Pakistan inatayarisha silaha za nyuklia kwa uwezekano wa vita na India, wakati New Delhi imejikita zaidi katika kutayarisha silaha za masafa marefu.

Shakeel Akhtar, mwandishi wa habari wa BBC Uurdu, anasema India na Pakistan zimekuwa zikiongeza uzalishaji wa droni katika miaka ya hivi karibuni.

Alieleza katika makala iliyochapishwa Novemba mwaka jana kwamba nchi zote mbili hazijanunua tu droni, lakini pia zimeunda teknolojia yao ya kufuatilia, kupeleleza na kushambulia droni za adui.

Mchambuzi wa masuala ya ulinzi Rahul Bedi anakadiria kuwa India itakuwa na droni 5,000 katika kipindi cha miaka miwili hadi minne ijayo.

Anasema Pakistan ina "droni chache kuliko India," lakini droni inazomiliki zina uwezo tofauti na ni chapa kati ya 10 hadi 11 tofauti.

Oktoba mwaka jana, India ilitia saini mkataba na Marekani kununua ndege zisizo na rubani 31 za Predator zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.5.

Pia wamenunua mabomu na makombora yanayoongozwa na mionzi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 500. Silaha hizi zinaweza kutumika kushambulia kwa kutumia droni.

Kulingana na Rahul Bedi, Pakistan inaagiza ndege zisizo na rubani nyingi kutoka Türkiye na China, lakini pia imenunua ndege zisizo na rubani za Ujerumani na Italia.

Islamabad pia imetengeneza ndege zake zisizo na rubani kama vile Barraq na Shahpar.

Makombora ya balistiki

dx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, India imeunda makombora ya BrahMos na BrahMos-2 kwa ushirikiano na Urusi.

"India ni mojawapo ya nchi chache ambazo zina mfumo wa ulinzi wa anga wa kuzuia makombora ya balestiki," anaandika mchambuzi wa masuala ya ulinzi Harrison Cass kwenye tovuti ya The National Interest.

India ina aina mbili ya mifumo ya ulinzi wa anga. Ya kwanza ni Prithvi, na wa pili ni AAD unaojulikana pia kama Ashwin Ballistic Missile Interceptor. Mfumo wa kuzuia makombora ya balestiki nchini India una uwezo wa kuzuia mashambulizi ya makombora kutoka umbali wa angalau kilomita 5,000.

New Delhi pia imeunda makombora ya BrahMos na BrahMos-2 ya haipasoniki kwa ushirikiano na Urusi, ambayo yanaweza kurushwa kutoka ardhini, anga, bahari, na nyambizi.

Na ingawa nchi zote mbili zimeboresha uwezo wao, tofauti na India, Pakistan haina makombora ya balestiki kufika bara jingine.

Wachambuzi wengi wa masuala ya ulinzi wanaamini huenda Pakistan haihitaji makombora hayo, kwa sababu makombora ya Pakistan yana uwezo wa kufikia malengo ya kikanda."