Je,Guardiola ameshindwa kuongoza Man city?

Guardiola

Chanzo cha picha, Reuters

  • Author, Mariam Mjahid
  • Nafasi, BBC Swahili

Manchester City ambayo imeshinda kombe la EPL mara nne mfululizo chini ya ukufunzi wa Pep Guardiola imekuwa na msururu wa matokeo duni kwani haijashinda katika mechi sita za mwisho ikipoteza mechi tano kati yazo.

Jumapili iliyopita ilicharazwa mabao manne bila jibu nyumbani dhidi ya Tottenham Hotspur.

Na itakuwa na kibarua kigumu jumapili ijayo ambapo itasafiri hadi Anfield kupambana na viongozi wa ligi Liverpool.

Guardiola alionekana wazi amegadhabishwa kwa kutoka sare ya mabao matatu na Feyenoord baada ya timu yake kuongoza na mabao matatu katika kipindi cha kwanza.

Hata hivyo,Pep Guardiola, amesema wachezaji wake wanahuzuni kutokana na mfululizo wa kupoteza mechi tano, lakini ana matumaini kugeuza hali hiyo.

Kupoteza 4-0 nyumbani kwa Tottenham kulikuwa pigo kubwa siku chache tu baada ya Guardiola kusaini mkataba mpya wa miaka miwili kwenye klabu.

Ilikuwa ni kipigo kikali zaidi kwa City nyumbani tangu mwaka 2003 na mara ya kwanza kupoteza mechi tano mfululizo tangu 2006, kabla ya Sheikh Mansour kuanza kipindi chake cha mafanikio makubwa kama mmiliki.

Guardiola hajawahi kupoteza mechi tano mfululizo katika kipindi chote cha kazi yake ya ukufunzi.

Hali hiyo pia inawaacha City nyuma kwa pointi nane dhidi ya viongozi wa Premier League, Liverpool, kufuatia ushindi wa 3-2 dhidi ya Southampton Jumapili.

“Nawamini wachezaji hawa zaidi kuliko wakati wowote ule,” alisema Guardiola.

“Sijawahi kuona mchezaji katika maisha yangu anayetamani kufanya vibaya au kutoa uchezaji mbaya kwa mashabiki au kwa klabu. Hakuna anayetaka hivyo.

“Wakati wanapokuwa mbele ya watu 60,000 wanataka kucheza vizuri. Lakini kwa sababu nyingi, inawakwaza.”

Guardiola

Chanzo cha picha, BBC Sport

Masaibu ya Guardiola

Aliyekuwa meneja wa Barcelona alikuwa na alama kadhaa kwenye paji la uso baada ya mechi hiyo kukamilika alipokuwa akifanya mahojiano na idhaa ya Amazon Prime.

Alipoulizwa na ripota katika kongamano hilo alilokuwa amehudhuria kuhusiana na alama yake puani,Guardiola alijibu:” Nilijikwaruza na kucha ya kidole changu.”

Baadaye akafanya mzaha kuwa alitaka “kujiumiza“ kufuatia timu yake kuwa na matokeo yasioridhisha,na kucheka huku akiondoka kwa jukwaa.

Man City hawajakuwa na matokeo mazuri tangu tarehe 26 Oktoba mwaka huu,baada ya kufurahia ushindi wa kubahatisha wa bao 1-0 dhidi ya Southampton ambao walikuwa wanasuasua.

Tangu kufungwa mabao 17 katika mechi sita walizozicheza,ni takwimu za kushangaza ukizingatia mafanikio yao chini ya mkufunzi Guardiola yaliyojikita katika safu imara ya ulinzi.

“sijui kama ni tatizo la akili,”alisema Guardiola.

“kipindi cha kwanza kilikuwa sawa kwa 3-0 .Ulikuwa ni mchezo mzuri,lakini tukafungwa mabao Zaidi ishara kuwa hatukuwa sawa.Tulijitolea kipindi cha kwanza ,na nguvu zikatuishia ,ndio maana ilikuwa ni vigumu.

"Hiyo ndio hali ilivyo.Tulicheza vizuri lakini hatungewaachia.."

Wachezaji wawili wa Manchester City, Phil Foden (kushoto) na Erling Haaland baada ya kuchapwa 4-0 nyumbani na Tottenham.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wachezaji wawili wa Manchester City, Phil Foden (kushoto) na Erling Haaland baada ya kuchapwa 4-0 nyumbani na Tottenham.

Kwanini Manchester City inadidimia?

City ina kibarua kigumu kama wanataka kuepuka michezo ya mikondo miwili mwezi Februari ili kuingia katika orodha ya timu 16.

Itawabidi wamalize katika nafasi ya nane bora ili kupata kibali cha kuingia moja kwa moja katika hatua ya muondoano lakini wakae nafasi ya 15 baada ya mechi ya Jumanne.

Ingawa wanaweza kushuka hata chini baada ya mechi za Jumatano.

City inasubiri kucheza na timu mbili ambazo zina safu nzuri kama vile Juventus tarehe 11 December na Paris St-Germain tarehe 22 mwezi Januari kabla ya kuwaalika Brugge tarehe 29 Januari mwaka ujao.

"Kwa sasa siko tayari kufikiria kuhusu hayo{haja ya kushinda michuano mitatu ya mwisho ili kuwa katika nafasi ya nane bora]," Guardiola alisema.

"Tunapaswa kujiandaa vyema kwa mchuano ujao.Iwapo tutashindwa kushinda michuano itakuwa vigumu kwetu."

Kocha wa Mabingwa wa EPL Manchester City Pep Guardiola amesema kwamba hakuwa na nia ya kumuudhi mtu yeyote kufuatia matamshi aliyotoa akieleza alama alizokuwa nazo usoni baada ya mechi ya UCL dhidi ya Feyenoord siku ya Jumanne.

Akisema kuwa anatambua kuna watu wengi wanaokumbwa na matatizo ya afya ya akili na hangetaka mtu yeyote adhurike

Kwa sasa, Liverpool inaaongoza and jedwali la EPL ikiwa na alama 31 huku City ikiwa ya pili kwa alama 23

Je,Manchester City itaweza kutamba tena?

Ikiwa timu inayoongozwa na Arne Slot tayari iko kifua mbele kwa pointi nane, pengo linaweza kuwa pointi 11 ifikapo mwishoni mwa wikendi ijayo.

Ni mara moja tu ambapo timu imekuwa na uongozi mkubwa zaidi baada ya michezo 12 - Manchester United mwaka 1993-94, ambao walishinda ubingwa.

Kompyuta ya kisayansi ya Opta bado inaipa Manchester City asilimia 22.2% ya kutetea ubingwa wao.

Alipoulizwa moja kwa moja kama pointi 11 zitakuwa nyingi kupunguza, Guardiola alisema kwa uthabiti: “Ndio, ni kweli.

“Lakini hatufikirii kushinda au kupoteza [ubingwa], hatupo katika hali ya kufikiria kuhusu kile kitakachotokea mwishoni mwa msimu. Ikiwa mwishowe hatushindi, ni kwa sababu hatustahili.

“Sasa unaelewa jinsi ilivyokuwa vigumu kile tulichokifanya.”

Hata hivyo ,Manchester City Wanajitahidi kukabiliana na kumkosa Rodri, kiungo bora wa ulinzi duniani na mshindi wa Ballon d'Or.