Simba SC inafahamu la kufanya ili 'kupindua meza'

g
Maelezo ya picha, Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids
  • Author, Na Florian Kaijage
  • Nafasi, BBC News Swahili
  • Akiripoti kutoka Zanzibar

Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids amesema wachezaji na jopo la ufundi wanafahamu fika wanachopaswa kukifanya katika mchezo wa marejeano wa fainali ya Kombe la Shrikisho Afrika ili kubadili matokeo ya kufungwa magoli 2-0 na RS Berkane katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Mei 17 huko Morocco.

Kocha Davids raia wa Afrika Kusini amewaambia waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kuhusu matayarisho ya mchezo wa Jumapili Mei 25 kwamba mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita uliwapa mafunzo mengi ya namna ya kuwakabili Berkane nyumbani japo amekiri kuwa hautakuwa mchezo mwepesi hata kidogo.

"Berkane ni timu kubwa ina wachezaji wenye uzoefu wa kucheza fainali kuliko wachezaji wetu, lakini tutakabiliana ano vilivyo, ninaamini kila mchezaji akitekeleza majukumu yake na kujituma inawezekana kupata matokeo mazuri, Simba ni timu ambayo imakabiliana na changamoto nyingi na imekwishadhihirisha namna ya kuzikabili vilivyo na kuzishinda, tuna mashabiki wanaoiunga mkono timu yao ipasavyo" alifafanua.

Kadhalika amezungumzia kusikitishwa na mchezo huo kutofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ambako Simba imekuwa ikipata matokeo mazuri tangu aanze kuinoa timu hiyo, yapata miezi kumi iliyopita. Lakini amesema hayo sasa yamepita na kwamba anaamini mashabiki wataendelelea kuiunga mkono timu yao hata wale ambao hawatapa fursa ya kufika uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.

g
Maelezo ya picha, Kocha wa Berkane, Mouini Chaabani

Simba ilishinda michezo yote 6 ya nyumbani msimu huu kuanzia hatua za awali, makundi, robo fainali na nusu fainali. Hata hivyo, Simba ilicheza mchezo wa nyumbani wa nusu fainali dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini kwenye uwanja wa Amaan na kuibuka na ushindi wa 1-0 na kisha kulazimisha sare yab 0-0 katika mchezo wa marejeano ugenini hivyo kutinga fainali.

Alipoulizwa na mwandishi wa BBC kuhusu kufungwa magoli ya haraka ndani ya dakika 16 za kwanza katika mchezo wa Morocco, Davids alisema walitarajia mchezo wa kasi kutoka kwa Bekane na ndivyo ilivyokuwa. "Berkane ni hatari inapocheza nyumbani, timu nyingi zimepigwa goli nyingi pale, Stellenbosch ilifungwa 5, tulikumbwa na kasi hiyo, timu yangu ilikuwan mchezaji mmoja tu, Fabrice Ngoma aliyewahi kucheza mchezo wa fainali kabla, wengine ni vijana. Baadaye tulirekebisha mbinu za mchezo na kuwa washindani halisi, Camara (mlinda lango) aliokoa hatari moja kubwa vinginevyo zingekuwa 3-0, kesho tunakwenda kuwa na mchezo tofauti kabisa.

g
Maelezo ya picha, Nahodha wa Simba, Shomari Kapombe

Nahodha wa Simba, Shomari Kapombe alisema: Tunaambiwa yapata miaka takribani 32 iliyopita Simba ilicheza fainali na kufungwa nyumbani 2-0, wengine hatukuwepo duniani wakati huo lakini tumeambiwa hivyo tunaelewa, tunafahamu hisia za wanachama na wapenzi wa Simba kuhusu hili tunakwenda kucheza kukidhi mahitaji yao, tungependa kucheza Benjamin Mkapa Dar es Salaam lakini uamuzi uliopitishwa wa kucheza Amaan hatuwezi kuupinga na hali iliyopo hapa ya matayarisho na mapokezi tuliyoyapata ni nzuri na sioni tofauti, tupo tayari kupambana.

Mapema akizungumza na waandishi wa habari, kocha mkuu wa RS Berkane Mouin Chaabani, alisema wamejiandaa kikamilifu kuikabili Simba yenye rekodi nzuri ushindi inapocheza uwanja wa nyumbani. "Katika mchezo wa kwanza tungeweza kupata ushindi mnono zaidi ya 2-0, lakini hayo yamepita sasa tunauangalia mchezo wa pili, hatutaki kuzungumzia jambo lolote ambalo ni tatizo au changamoto bali ni kubakia makini na mchezo wa marudiano, iwe mvua iwe jua tunakwenda kupambana. Mchezo utakuwa mgumu lakini tunajiamini kupata matokeo mazuri".

Naye mshambuliaji Mamadou Camara raia wa Senegal aliyeifungia Berkane goli la kuongoza katika mchezo wa kwanza alisema Mawazo yao yote yapo katika mchezo wa fainali. Kuhusu tetesi kuwa zipo klabu za Tanzania zenye nia ya kumsajili, alijibu kuwa kwa sasa akili yote ipo katika mchezo wa fainali akiipambania timu yake ya Berkane.

Maelezo ya video, Kapombe: 'Tunaambiwa miaka 32 iliyopita Simba ilicheza fainali na kufungwa nyumbani 2-0
Unaweza pia kusoma:
h
Maelezo ya picha, Mamadou Camara, mshambuliaji wa Berkane

Novemba 27, 1993, Simba ilifungwa 2-0 nyumbani katika mchezo wa marejeano katika uwanja wa Taifa (Sasa Uhuru) dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast baada ya kulazimisha sare ya 0-0 ugenini. Tangu wakati huo haikuwahi kufika hatua ya fainali ya mashindano ya Afrika hadi msimu huu. Sasa Simba itakuwa ikijiuliza tena na kupambana kuondoa jinamizi hilo na kuwa timu ya pili kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kutwaa ubingwa wa Afrika wa ngazi ya klabu. Klabu pekee kuwahi kutwaa taji ni Gor Mahia ya Kenya mwaka 1987 iliponyakua kombe la washindi dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Mbali na Simba mwaka 1993, Klabu nyingine za CECAFA zilizowahi kucheza fainali bila mafanikio ni Sports Club Villa ya Uganda dhidi ya Esperance ya Tunisia mwka 1991 (Klabu bingwa Afrika), Kenya Breweries (sasa Tusker FC) mwaka 1994 dhidi ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (kombe la washindi), El Merreikh ya Sudan mwaka 2007 ilipofungwa na CS Sfaxien ya Tunisia (Kombe la Shirikisho) na Yanga ya Tanzania iliyopoteza kwa kanuni ya goli la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria mwaka 2023.