Presha 6 zinazoikabili Simba SC dhidi ya Berkane Zanzibar

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Yusuph Mazimu
- Nafasi,
- Akiripoti kutoka Dar es Salaaam
Simba SC inakaribia kucheza moja ya mechi zake kubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo, mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco (RS Berkane) Jumapili hii.
Baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 ugenini kwenye dimba la Berkane, Wekundu hao wa Msimbazi wanahitaji ushindi wa angalau mabao 3-0 ili kugeuza matokeo na kutwaa taji lao la kwanza barani Afrika.
Kocha wa Simba Fadlu Davids anasema; "Tulifungwa mabao mawili ya mapema ambayo yalituzuia, lakini nina matumaini tunaweza bado kufanya vizuri zaidi katika mchezo wa marudiano."
Katika kipindi ambacho mashabiki wa klabu hiyo wamejaa matumaini na msisimko, pia kuna hali ya wasiwasi na presha kubwa inayoizunguka timu hiyo na hasa presha hizi sita.
1. Presha ya kupindua matokeo ya Morocco

Chanzo cha picha, CAF
Simba wanakabiliwa na mlima mrefu kufuta mabao mawili ya ugenini dhidi ya timu ngumu ya Berkane. Katika hatua ya makundi, Berkane walifungwa mechi moja tu kati ya sita, na walionesha uimara wa kujilinda. Hakuna mechi waliyopoteza kwa mabao mawili na zaidi. Kwa Simba, hilo lina maana kuwa lazima wachanganye akili zao, za kuambiwa, nidhamu, ubunifu na kasi ya mashambulizi.
Na dakika 30 za kwanza huenda zikaeleza hatma ya matokeo, iwapo Simba itafanikiwa kupata angalau bao muda katika muda huo.
Mchezo huo unaechezwa saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na hilo linaonekana na wachambuzi wa soka kama linawapa faida Simba kutokana na tofauti ya mazingira ya Morocco inakotoka Berkane na Tanzania.
"Kule mechi huchezwa usiku kwa sababu kwao mchana ni joto kali sana", anasema Ramadhan Mbwaduke, mchambuzi wa soka Tanzania", kuonyesha simba inavyoweza faidika na mchezo huo kuchezwa alasiri.
2. Presha ya kutengeneza historia

Chanzo cha picha, Getty Images
"Kubwa tunalotakiwa kuhakikisha ni kwamba Kombe linabaki Zanzibar", anasema mbunge wa Chumbuni, Ussi Pondeza. Ukibaki ubingwa huu litakuwa jambo la kihistoria
Utakuwa ubingwa wa kwanza kabisa kwa Simba SC katika historia ya michuano ya CAF. Baada ya miaka 31 tangu fainali yao ya mwisho (Kombe la CAF mwaka 1993), hatimaye wamepata nafasi nyingine ya kutinga kilele cha mafanikio ya bara.
Wapinzani wao wa jadi, Yanga SC, waliingia fainali ya michuano hii mwaka 2023 lakini wakakosa taji. Kwa Simba, huu ni wakati wa kuzidi hatua hiyo na kuweka jina lao kwenye historia ya dhahabu ya soka la Afrika Mashariki.
Historia itaandikwa zaidi kutokana na rekodi nzuri ya Berkane. Mara ya mwisho Berkane kufungwa mabao matatu ilikuwa miaka miwili iliyopita na msimu huu haijaruhusu kufungwa mabao mawili katika mchezo wowote wamichuano ya Afrika.
"Berkane ni mpinzani mgumu, anacheza fainali ya tatu katika miaka mitano, anao uzoefu, na ndio alama zinaandikwa kwa njia kama hizi", anasema mchambuzi wa soka, George Job na kuongeza: "Kwa mara ya kwanza (timu) kutoka Tanzania inaweza kutwaa kombe, (Simba) iko kwenye mstari katika kutengeneza historia', anasema Job.
3. Presha ya Uwanja wa Amani, Zanzibar

Chanzo cha picha, CAF
CAF waliamua mechi hii ichezwe Uwanja wa Amani, Zanzibar, baada ya Uwanja wa Mkapa kutokamilika kwa wakati ukarabati unaohitajika kimataifa. Simba walipigania kuutumia Mkapa si kwa sababu ya ukubwa tu, bali rekodi yao nzuri pale: mechi 12 za Afrika, ushindi 8, sare 3, kipigo 1 pekee.
Uwanja wa Amani hauna mvuto ule ule, na idadi ya mashabiki imebanwa kwa uwezo mdogo wa viti na majukwaa. Wakati mashabiki maelfu walikuwa wamejipanga kushuhudia mchezo huu Dar es Salaam, sasa wanajikuta kwenye sintofahamu huku baadhi wakikata tamaa kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda zanzibar.
"Mara nyingi na unaposikia kwa Mkapa hatoki mtu ni kwa sababu ya maandalizi ya benchi la ufundi na preshapresha muda wote kwa ajili ya kusaka ushindi katika mechi za nyumbani, uwepo wa mashabiki na lingine mazingira ya kujiografia', anasema mchambuzi Mbwaduke.
Tamaa ya kutaka mchezo upigwe kwa Mkapa ilikuwa kubwa na siku chache hizi kama haijathibitishwa, macho yalikuwa huko sasa wanalazimika kujielekeza Zanzibar na kushusha presha ya uala la uwanja.
Msemaji wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, anakiri tamaa hiyo lakini haiwakatishi tamaaa, "Tunakubali Benjamin Mkapa ndio ngome yetu lakini hatushindi sababu ya uwanja, tunashinda sababu ya ubora wetu. Uwanja wa Amaan ndio ulitupeleka fainali na sasa ndio utatupa ubingwa'.
4. Presha ya kulipa deni kwa Rais Mwinyi

Chanzo cha picha, Mo dewji
Rais wa Zanzibar, Hussein Ally Mwinyi atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huu wa fainali dhidi nya RS Berkane pale Zanzibar na kwa mazingira hayo ataishabikia Simba, kama shabiki namba moja uwanjani.
Amegharamia gharama za uwanja wa Amani, ili Simba icheze 'bure' na bila presha kama ilivyo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alivyogharamani safari za timu hiyo ilipokwenda Afrika Kusini na Morocco kucheza mechi za michuano hii. Hili ni deni nyuma ya pazia.
Kingine Mwaka 1993 wakati Simba inacheza fainali yake ya kwanza ya CAF jijini Dar es salaam dhidi ya Stella Abidjan, baba yake na Rais Hussein Mwinyi, Hayati Ally Hassan Mwinyi, 'Mzee Rukhsa' aliyekuwa rais wa awamu ya pili Tanzania wakati huo alikuwa mgeni rasmi katika mchezo huo ambao Simba ilala 2-0.
Mwinyi aliyekuwa mshabiki mkubwa Simba alihuzunika sana kwa Simba kukosa ubingwa kama ambavyo watanzania wengine walivyohuzunika.
Kwa vyovyote Simba ina deni la kulipa kwa Rais Mwinyi baba na Rais Mwinyi mtoto. Na hiyo inaleta presha nyingine kuhakikisha Simba aimuangushi Rais Mwinyi, na inakuwa katika presha ya kufuta machungu ya baba yake 'Mzee Rukhsa' ya mwaka 1993 na kumfurahisha huko aliko.
"Hatukulipa deni mbele ya Hayati Rais Ally Hassan Mwinyi na sasa tunakwenda kulipa deni mbele ya mtoto wake, Rais Dkt. Hussein Mwinyi," amesema Ahmed.
5. Presha kutoka kwa mashabiki wake

Chanzo cha picha, Simba
Presha hii ni kubwa kiasi. Matarajio ni makubwa kwa wana Simba, ingawa kuhamishwa kwa mchezo kutoka uwanja wa Mkapa kwenda Aman Zanzibar kumepunguza kiasi matumaini, kutokana na rekodi ya Simba katika uwanja wa Mkapa.
Hata hivyo wapo wenye kuamini Simba ni ubingwa tu si vinginevyo.
"Simba ina asilimia milioni 1 kuchukua ubingwa wa Afrika" hii ni moja ya kauli ya presha sana kutolewa na mshabiki na kiongozi wa zamani na timu hiyo Mwina Kaduguda.
"Hapa Berkane anapasuka goli 4, mimi nimekuwa kiongozi wa Simba 2018, Simba bingwa wa nchi hii, 2019 Simba bingwa, 2020 Simba bingwa na 2021 Simba bingwa wa nchi hii, nimetoka (uongozi) wanao (wamechukua)? anauliza Kaduguda na kuongeza "Simba akikosa ubingwa wa Afrika mwaka huu ni wao".
Sasa Kaduguda ni mmoja wa mashabiki wengi wanaozungumza maneno ya presha kwa Simba. Ukiacha watabiri na wapo wabashiri wegi wanaoonyesha kwamba Simba inachukua ubingwa.
6. Presha kutoka kwa watani zao - Yanga

Chanzo cha picha, Yanga
Katika macho ya mpinzani wao wa jadi, Yanga, matokeo ya Simba ni jambo linalojadiliwa kwa hisia kali. Kumbukumbu ya Yanga ya kushinda medali za pili za Kombe la Shirikisho la CAF mwaka 2023 bado ni silaha wanayoitumia kuwatambia Simba. Hivyo basi, Simba wakishindwa au kuambulia nafasi ya pili, watakuwa wamepoteza fursa muhimu ya kujibu mapigo hayo. Kama anavyosema shabiki wa Yanga, Rahman John, "Hii ndio nafasi pekee ya Simba kunyamazisha Afrika na mitaani; wakishindwa, kelele zitawazidi kutoka Yanga."
Aidha, kumekuwa na tabia ya mashabiki wa Yanga kuwaunga mkono wapinzani wa Simba wanapocheza na timu za kigeni, na hali kadhalika kwa Simba wanapocheza na Yanga. Hili limekuwa likionekana na kuongeza presha mpya.
Kauli ya Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, iliyotolewa Zanzibar akionya kuwa "Hapa tulipo tumevua kabisa vazi la utu, tumevua vazi la ustaarabu, hapa tumelipo tumevaa unyama kwelikweli, tusitafutiane lawama. Hatutamuonea mtu aibu, tutakuharibia mazima," inatafsiriwa na wengi kama jibu kwa kauli tata ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Arafat Hajj.
Arafat alisema alikuwa "Zanzibar kwa kazi maalum' ikiwa ni muda mfupi kabla ya mechi, ikitafsiriwa na baadhi ya mashabiki wa Simba kama fitina ya kutaka timu yao ikose ubingwa. Hivyo, mchezo huu ni wenye figisu nyingi ndani na nje ya uwanja, maneno ya ushabiki, ukiwa na uzito mkubwa wa kisaikolojia kwa Simba SC.
Presha ni kubwa mno kiufundi, kihistoria, kimazingira, na hata kijamii. Mafanikio yatawaingiza kwenye vitabu vya kumbukumbu za CAF kama timu chache za Afrika Mashariki kubeba taji la kimataifa.
Lakini wakishindwa, kumbukumbu hiyo inaweza kuwa jeraha la muda mrefu kwa klabu na mashabiki wao. Macho ya Watanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla yatakuwa kwenye fainali hii ya kusisimua na yenye presha kwa Simba.