Simba SC kwenye dhamira ya kuvunja ngome ya Berkane Afrika

a

Chanzo cha picha, Simba

  • Author, Yusuph Mazimu
  • Nafasi,
  • Akiripoti kutoka BBC Dar es Salaam

Simba SC wapo kwenye safari ya kihistoria, kwa mara ya kwanza kwa miaka 32 wameingia fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF, ikiwa ni fainali ya pili kubwa baada ya ile ya mwaka 1993, fainali za Kombe la Caf walipopoteza dhidi ya Stella Abidjan.

Lakini mbele yao safari hii ni kuta imara za RS Berkane, kiboko ya michuano hii. Kati ya misimu saba iliyopita wametinga fainali ya kombe hili la Shirikisho la CAF mara tano, na kutwaa mara mbili.

Mechi ya kwanza itapigwa Mei 17 Morocco, katika uwanja wa Manispaa ya Berkane (Stade Municipal de Berkane), uwanja unaofahamika kwa presha, na rekodi ya kibabe Afrika. Mechi ya kwanza ya fainali itapigwa Mei 17 katika kabla ya marudiano Mei 25 jijini Dar es Salaam ama Zanzibar, ikisubiriwa taarifa rasmi, kufuatia utata wa uwanja utakaotumika.

Hii si fainali ya kawaida kwa Simba. Ni nafasi ya kuandika historia, kuvunja hofu ya timu za Afrika Kaskazini, na kuweka msingi wa taji lao la kwanza kabisa la CAF. Dhamira ni moja: kuondoka Berkane wakiwa na matumaini kabla ya marudiano Dar es Salaam Mei 25.

Rekodi ya Simba SC ugenini katika michuano ya Afrika

s

Chanzo cha picha, Simba

Safari ya Simba kuelekea fainali hii haikuwa rahisi. Lakini rekodi yao ugenini msimu huu, japo si ya kuridhisha sana imefanikiwa kuwafikisha hapo walipo. Walianza katika hatua ya awali kwa kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya. Katika hatua ya makundi ugenini walicheza dhidi ya CS Constantine ya Algeria, CS Sfaxien ya Tunisia, na Bravos do Maquis ya Angola. Walipata ushindi muhimu wa 1-0 ugenini dhidi ya Sfaxien, sare dhidi ya Bravos (1-1), lakini wakapoteza dhidi ya Constantine (2-1).

Katika robo fainali walikumbana na Al Masry ya Misri na kufungwa 2-0 ugenini kabla ya kushinda nyumbani na kufuzu kwa penalti. Katika nusu fainali waliwabana Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa sare ya 0-0 ugenini, na kuhitimisha kazi nyumbani.

Sasa katika mechi zote 6 za ugenini msimu huu, Simba wamefunga mabao 3 pekee na kuruhusu mabao 5. Hata hivyo, uwezo wao wa kupata matokeo ya kiufundi na kulinda heshima ugenini, umeonyesha timu iliyokomaa kisoka na kiakili.

RS Berkane na ngome ya chuma nyumbani

s

Chanzo cha picha, Berkane

RS Berkane si wageni katika fainali za CAF, na inajivunia ngome imara iliyo nayo. Klabu hiyo ya Morocco inacheza fainali yake ya tano ya Kombe la Shirikisho la CAF katika kipindi cha miaka saba. Imecheza fainali mwaka2018, 2019, 2020, 2022 na sasa 2025 dhidi ya Simba, ikitwaa ubingwa mara mbili (2020 na 2022), pamoja na ubingwa wa CAF Super Cup mwaka 2022.

Kwa sasa pia ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu ya Morocco (Botola Pro) baada ya kuwashinda vigogo kama Wydad Casablanca na Raja Casablanca kwenye mbio za ubingwa. Si ba yenyewe ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi kuu Ya Tanzania, nyumba ya Yanga

Rekodi ya Berkane nyumbani kwenye michuano ya CAF msimu huu ni ya kutisha. Wamecheza mechi 6 katika dimba la Stade Municipal de Berkane bila kuruhusu hata bao moja:

Katika Raundi ya pili kuelekea Makundi, iliichapa 5-0 Dadje (Benin), kwenye Makundi Iliiichapa 5-0 Stellenbosch (Afrika Kusini), hawa ambao Simba walikutana nao nusu fainali, ikashinda 2-0 dhidi ya Lunda Sul (Angola),na kuichapa 1-0 Stade Malien (Mali).

Robo fainali ikashinda 1-0 dhidi ya ASEC Mimosas (Ivory Coast) kabla ya nusu fainali kuizaba CS Constantine (Algeria) 4-0.

Kwa jumla wamefunga mabao 18 nyumbani msimu huu na hawajaruhusu hata moja. Mara ya mwisho kufungwa bao nyumbani katika michuano ya CAF ilikuwa Mei 12, 2024, walipolala 2-1 dhidi ya Zamalek ya Misri kwenye fainali ya kombe hilo msimu uliopita.

Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, anakiri wazi ukubwa wa kazi iliyo mbele yao:

"Matumaini yapo lakini lazima ukweli mmoja tuuseme, mpinzani tunaokwenda kucheza naye ni mpinzani mgumu kweli kweli. Siyo mpinzani mwepesi; amechukua ubingwa mbele ya Wydad Casablanca, amechukua ubingwa mbele ya Raja Casablanca, huyu ni mpinzani wa kiwango cha kutisha mno."

Kwa hivyo, Simba wanaelekea kwenye moja ya viwanja vigumu zaidi barani Afrika.

3. Je, Simba SC inaweza kuvunja ngome ya Berkane?

s

Chanzo cha picha, Simba

Maelezo ya picha, Mlinzi wa Simba., Shomari Kapombe

Simba SC wanaingia dimbani wakiwa na dhamira kuibomoa ngome ngumu ya Berkane. Ni ngome ya chuma inayomjumuisha Adil Tahif, Abdelhak Assal, Hamza El Moussaoui, Haytam Manaout na mpinda mlango Munir Mohamedi.

Simba SC wameonyesha uwezo wa kupambana na kuhimili presha ugenini. Ni ugenini tu kutakoleta matumaini nyumbani, na kama wanataka kubeba kombe, kuipa heshima Tanzania na kuwatambia watani zao Yanga, ni kupata matokeo kwanza ugenini dhidi ya ngome ngumu ya Berkane.

Wakiwa na kikosi cha wachezaji wa kimataifa wenye uwezo wa kubadilisha matokeo. Washambuliaji Jean Ahoua (Ivory Coast), Elie Mpanzu (DR Congo), Steven Mukwala (Uganda) na Kibu Denis (Tanzania) wanabeba matumaini ya mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi.

Safu ya kiungo inajengwa na vijana wenye njaa kama Joshua Mutale (Zambia) na Yusuph Kagoma, huku ulinzi ukiwa chini ya wazoefu Che Malone (Cameroon), na manahodha Mohamed Hussein na Shomari Kapombe. Mlinda mlango Moussa Camara atakuwa na jukumu kubwa kuzuia mashambulizi ya Berkane.

Kwa Dhamira ya kuvunja ngome inaweza kuibeba, lakini uhalisia wa kuivunja ngome ya Berkane kunahitaji zaidi ya mipango, kunahitaji ujasiri, nidhamu, na kutumia kila nafasi inayojitokeza.