Kwa nini wanawake wa China hujiunga na vikundi vya ushirika kuokoa pesa?

Chanzo cha picha, Handout
- Author, Sylvia Chang
- Nafasi, BBC Chinese, Hong Kong
"Kila mwaka uishapo tulikuwa na pesa kidogo. Nilihisi kutokuwa salama lakini sikujua la kufanya," anasema Xiao Zhuo, mama wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 36 anayeishi Xiamen, jiji lililo kusini mashariki mwa China.
Wakati wa janga la Uviko 19, Xiao Zhuo na mumewe walilazimika kuchukua mishahara iliyokatwa kwa 50%. Lilikuwa pigo kubwa kwa familia yake, alikuwa na mzigo pia wa kumtunza mama yake, ambaye aligunduliwa na saratani miaka mitano iliyopita.
Imekuwa mtindo kwa vijana wa Kichina kutafuta washirika - wenye sifa sawa kwenye mtandao. Xiao Zhuo alitafuta watu ambao wana mitazamo ya kuokoa pesa.
Hashtagi ya kuokoa pesa iliibuka kwa mara ya kwanza kwenye Xiaohongshu, toleo la China la Instagram, Februari 2023. Imevutia maoni milioni 1.7, tangu wakati huo, kulingana na kampuni ya uchambuzi wa data ya Newsrank.
Wengi wa wanachama hao ni wanawake wenye umri kati ya miaka 20 na 40, huku wengi wao wakiwa ni akina mama. Wengine wanasema wanataka kuweka akiba kwa ajili ya elimu ya watoto wao, ambayo inazidi kuwagharimu.
Baada ya miaka ya sera kali ya Covid, ufufuaji wa uchumi wa China unakabiliwa na mzozo wa gharama ya pango ya majengo, kupungua kwa bei ya bidhaa, kushuka kwa uwekezaji wa kigeni na kuongezeka kwa deni la serikali za mitaa.

Chanzo cha picha, Getty Images
“Huko China, wanawake ndio huwa na jukumu la kugharamia nyumba kila siku. Kuona wanawake wengi wanaweka akiba ni kiashiria kwamba ukosefu wa ajira unaenea - sio tu miongoni mwa vijana,'' kulingana na profesa wa sera za umma Lu Xi, kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Singapore.
Kuongezeka kwa hamu ya watu binafsi kuweka akiba kutafanya iwe vigumu zaidi kwa China kusawazisha uchumi wake. Katika miongo kadhaa iliyopita, ukuaji ulichochewa na uwekezaji katika miundombinu na nyumba za bei ya chini.
Lakini kadiri uchumi wa China unavyokua, wataalamu wanasema kuna haja ya kuongeza matumizi ya ndani ili kuendeleza ukuaji.
Kujiandaa na hatari
Xiao Zhuo anahisi mwenye bahati kwamba anafanya kazi katika sekta ya nishati safi, sekta inayopanuka ambayo inaripotiwa kuchangia 40% katika ukuaji wa uchumi wa nchi mwaka jana.
Hata hivyo, anahisi analazimika "kujiandaa kwa hatari" kwani wengi wa watu katika familia na marafiki zake wanapoteza kazi - ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi katika huduma za umma kama vile hospitali na shule.
Mwezi Februari, Xiao Zhuo alijiunga na vikundi kadhaa vya kuweka pesa. Kila siku, wanachama wanapaswa kuweka bajeti na matumizi yao. Pia wanazuia kufanya manunuzi ya ghafla.
Xiao Zhuo pia amejifunza mbinu za kuweka pesa. Kwa mfano, alijifunza kuhusu programu ya simu – yenye kumfanya kila siku kuokoa kuanzia yuan 1 hadi 183. Baada ya mwaka mmoja, ataweza kuwa na akiba ya karibu yuan 34,000.
Msukumo wa kufanya manunuzi kwa Xiao Zhuo umepungua. Hapo awali, angeweka chochote alichopenda kwenye toroli kwenye duka kubwa. Lakini sasa, hutengeneza orodha ya mahitaji ya chakula tu aendapo dukani.
Mwezi mmoja baada ya kupata washirika wa kuhifadhi pesa, amepunguza matumizi yake kwa 40%. Ana matumaini ataokoa yuan 100,000 baada ya mwaka - ongezeko mara kumi kutoka hapo awali.
Wanawake wengine pia wanasema mbinu hiyo imewasaidia kuokoa pesa. Mwanachama mmoja anasema sasa anajipikia mwenyewe na amepunguza ununuzi usio wa lazima.
Mwingine anasema ameokoa zaidi kwa kujiweka bize kazini na atatafuta mambo mapya ya kumfurahisha ambavyo hayana gharama sana.

Chanzo cha picha, Handout
Fedha ni mfalme
Baadhi ya wanawake wamechagua njia ya kitamaduni zaidi ya kuhifadhi pesa nyumbani. Sio kawaida kwani China ina karibu 70% ya watu wanaotumia malipo ya simu, kulingana na Statista.
"Ninahisi salama na kuridhika kuona rundo la noti zikizidi kuwa nene," anasema Bi Chen, mwenye umri wa miaka 32, ambaye anaendesha kampuni ya urembo katika jimbo la kati la Henan.
Kila mwezi, alitoa sehemu kubwa ya mapato yake kutoka benki na kuweka pesa kwenye sanduku. Ikifika Yuan 50,000, ataweka amana ya kudumu.
Sasa pia anatumia pesa taslimu kwa ununuzi. Ni usumbufu, anasema, lakini hii ni njia yake ya kupunguza matumizi."
Huku kukiwa na kuzorota kwa uchumi, Bi Chen amepoteza idadi kubwa ya wateja na wateja wake wengi wa kawaida wamepunguza matumizi.
Bi Chen na mumewe ni watoto pekee, ikimaanisha wanapaswa kuwatunza wazazi wao wanne wazee. Anataka kuokoa angalau Yuan milioni moja kwa wanawe wawili.
Nchini China, wanaume wanatarajiwa kumiliki nyumba watakapofunga ndoa. Kwa hivyo ni kawaida kwa wazazi kununua mali kwa wana wao.
Kwa makadirio yake, familia yake inahitaji angalau yuan milioni tano kama akiba - lakini ana hofu hata hiyo haitatosha kwani sasa ni mjamzito tena.
"Hapo awali, sikuwa na mpango wowote wa kuweka akiba lakini nilikuwa na pesa. Lakini sasa kuwa na pesa mkononi kunanifanya nisiwe na wasiwasi."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah