China inasema iko wazi kwa biashara – je inaweza kuaminika kwa hili?

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchina inasema iko wazi kwa biashara – je hili linaweza kuaminiwa?
Wakati mkutano wa kila mwaka wa bunge la China ukifikia tamati baada ya wiki yenye shughuli nyingi za mikutano, pengo kubwa linatanda katika ajenda ya mwisho ya Jumatatu.
Bunge la Kitaifa la Watu wa China hukatishwa na mkutano wa Waziri Mkuu na waandishi wa habari. Lakini mwaka huu, na kwa muda uliosalia, mambo yamebadilika.
Maafisa wamesema hakukuwa na haja ya mkutano na wanahabari ikizingatiwa kulikuwa na fursa nyingine ya wao kuuliza maswali. Lakini waangalizi wengi waliona hii kama ishara nyingine ya uimarishaji na udhibiti, katika kile kilichokuwa mada ya mkutano wa Bunge, hata kama viongozi wakuu walizungumzia uwazi.
Kufutwa kwa mkutano na waandishi wa habari kunapunguza wasifu wa Waziri Mkuu Li Qiang. Ingawa tukio hilo lilipangwa, ilikuwa nafasi adimu kwa wanahabari wa kigeni kuuliza maswali na kumpa kamanda wa pili wa nchi hiyo nafasi ya kukaza misuli yake.
Katika miaka ya nyuma, kulikuwa hata na matukio ambayo hayakutarajiwa. Kwa mfano, mnamo 2020, Waziri Mkuu wa wakati huo Li Keqiang alifichua takwimu ambazo zilizua mjadala juu ya madai ya serikali kwamba ilikuwa imeondoa umaskini.
Kile kilichoonekana kama kufifia kwa uangalizi wa Waziri Mkuu, pamoja na kongamano fupi mwaka huu, zote ni dalili za mabadiliko ya kimuundo yanayoendelea ndani ya Chama cha Kikomunisti cha China (C) ambapo Rais Xi Jinping anazidi kujilimbikizia madaraka kwa gharama ya watu binafsi na taasisi, alibainisha Alfred Wu, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Singapore ambaye anasomea utawala wa China.
Lakini kwa ulimwengu wa nje, chama hicho kina nia ya kutoa taswira ya aina tofauti huku kikipambana na kupungua kwa imani ya wawekezaji wa kigeni na kuzorota kwa jumla kwa uchumi wake.
Akihutubia wanahabari wa kimataifa wiki jana, waziri wa mambo ya nje Wang Yi alisisitiza kuwa China bado ni sehemu ya kuvutia kuwekeza na kufanya biashara.
"China inasalia kuwa na nguvu kama injini ya ukuaji. 'China ijayo' bado ni China," alisema, kabla ya kutaja njia ambazo "China inafungua mlango wake kwa upana zaidi."
Mwongozo wa kiuchumi wa mwaka huu, uliotolewa na Bw Li mwanzoni mwa kikao, uliweka mipango ya kufungua maeneo zaidi kwa uwekezaji wa kigeni na kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa soko katika sekta kama vile viwanda na huduma.
Hatua hizi zimekuja baada ya wawekezaji wa kigeni kutishwa na sheria za hivi majuzi za kupinga ujasusi na ulinzi wa data, pamoja na kuzuiliwa kwa ghafla kwa wafanyabiashara wa China na wa kigeni. Uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni nchini China hivi karibuni ulipungua sana.
"Kuna ukaguzi mdogo wa kisiasa na usawa, hakuna uwazi. Hili ndilo jambo kubwa zaidi kwa wawekezaji... huwezi kutabiri kitakachotokea, kwa hivyo unaepuka hatari," alisema Dk Wu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini wiki jana Bw Wang alipuuzilia mbali wasiwasi huo. "Kueneza maoni ya kukata tamaa juu ya China kutaishia kujidhuru. Kuifikiria vibaya Uchina kutasababisha kukosa fursa," alisema, huku akilenga kuzungumza juu ya matarajio ya China.
Wang na Li walitumia mara kwa mara maneno kama "maendeleo ya hali ya juu" na "nguvu mpya za uzalishaji" kuashiria hatua mpya ya maendeleo ya China, ingawa hawakueleza kikamilifu maana yake. China inalenga kufikia lengo kubwa la ukuaji wa karibu 5% ya Pato la Taifa mwaka huu.
"Beijing inabadilisha jinsi inavyojiweka wazi kwa ulimwengu," Neil Thomas, mshirika katika siasa za Uchina kwenye Taasisi ya Sera ya Jumuiya ya Asia alisema.
Aliongeza kuwa hivi sasa inalenga kuvutia teknolojia ya hali ya juu ya kigeni na shughuli za juu za utengenezaji ili kusaidia kampuni za China katika tasnia muhimu za siku zijazo.
"Uwekezaji wa kigeni na biashara sio muhimu sana kwa uchumi wa China kuliko ilivyokuwa hapo awali, lakini Beijing bado inataka kuzuia kuondoka kwa haraka ambayo inaweza kutikisa zaidi matarajio yake ya ukuaji."

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati huo huo, viongozi walikuwa na nia ya kusisitiza lengo kuu la serikali.
"Utulivu ni wa umuhimu kwa ujumla, kwani ndio msingi wa kila kitu tunachofanya," alisema Bw Li. Kwingineko katika ripoti yake, aliweka wazi kuwa wakati China inafuatilia ukuaji, itaweka kipaumbele kwa usalama wa taifa.
Wengine wanaweza kuhoji ni kwa jinsi gani China inaweza kufikia uchumi ulio wazi unaostawi huku ikiongeza udhibiti.
Lakini "kwa mtazamo wa Beijing, hakuna ukinzani kati ya maendeleo ya hali ya juu, hasa kwa uwekezaji wa kigeni, na mahitaji makubwa ya usalama," alisema Jacob Gunter, mchambuzi mkuu wa kampuni ya Merics inayobobea katika uchumi wa China.
Kwa mfano, linapokuja suala la teknolojia muhimu ambapo makampuni ya Kichina bado hayajafikia, ingependa kuhakikisha kuwa nyingi iwezekanavyo zinazalishwa ndani ya mipaka yake, alisema Bw Gunter. Hii inapunguza hatari ya wapinzani - kama vile Marekani na washirika wake - kuiba teknolojia au kuzuia mauzo yao ya nje kwa China.
Beijing pia iliashiria itaendelea kubana maeneo yenye matatizo katika uchumi wake, kama vile sekta ya mali isiyohamishika inayoyumba na kuongeza deni la serikali za mitaa.
Bw Li aliahidi hatua zaidi za kupunguza hatari za kifedha na kuboresha usimamizi, na kukabiliana na shughuli haramu za kifedha.
Ingawa matatizo haya yamekuwepo kwa miaka kadhaa, "viwango vya madeni na kuongezeka kwa gharama za nyumba kumekuwa juu sana kiasi kwamba wanapaswa kuyatatua sasa na hawawezi kurudi nyuma", alisema Bw Gunter.
"Uchumi unafanya vibaya sana hivi sasa. Ukweli kwamba hawajarejea kuanza kukabiliana na hili linaweza kuwaathiri na hii ni kipaumbele cha muda mrefu na si kitu ambacho watakiacha."
Imefasiriwa na Asha Juma