Je, tembe za aspirini tumaini jipya kwa wagonjwa wa saratani?

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Je, dawa ya kupunguza maumivu ya gharama nafuu ya aspirini inaweza kuzuia kuenea kwa ugonjwa kama saratani? Wanasayansi wamegundua hivyo.

Majaribio yaliyofanywa na wanasayansi kwa wanyama yameonyesha kuwa aspirini huongeza uwezo wa mfumo wa kinga kupambana na magonjwa.

Timu ya utafiti katika Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza ilionyesha kuwa ugunduzi huu wa kusisimua na usiotarajiwa unaweza kufungua upeo mpya kwa wagonjwa wa saratani kuagizwa na madaktari kutumia aspirini katika siku zijazo, lakini wakati haujafika kuchukua hatua hii, na madaktari wanashauri wagonjwa wasitumie vidonge vya aspirini bila ushauri wa matibabu.

Ikumbukwe kuwa matumizi ya aspirini ya kawaida yanaambatana na hatari fulani, hivyo majaribio ya kisayansi bado yanafanywa ili kubaini aina za wagonjwa ambao watafaidika zaidi tembe hizo.

Je, saratani hutokea vipi?

Kinachoonekana kutokea kinahusu wakati wa udhaifu katika seli za saratani, wakati seli moja inajitenga na uvimbe wa awali na inataka kuenea kwa sehemu zingine za mwili.

Mchakato huu unajulikana kama metastasis, na unahusika kwa asilimia kubwa na vifo vinavyotokana na saratani.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Sehemu ya ulinzi wa mfumo wetu wa kinga, hasa seli nyeupe za damu zinazojulikana kama T-cell, huunda safu ya ulinzi ambayo inaweza kuganda na kuharibu saratani ya metastatic inapojaribu kushika mizizi katika mwili.

Lakini utafiti huo pia umebaini kuwa sehemu nyingine ya damu, chembe chembe za damu, ambazo kazi yake ya kawaida ni kuzuia kuvuja damu, huvuruga shughuli za seli za T, na kufanya kazi yake ya kuondoa saratani kuwa ngumu zaidi.

Aspirin huvuruga seli za saratani na huondoa athari zake kwenye seli za T, na kuziruhusu kufuatilia na kuondoa seli za saratani.

"Tulichogundua ni kwamba aspirini inaweza kuwa na ufanisi, bila kutarajia, kwa kufungua nguvu ya mfumo wa kinga kutambua na kuondoa seli za saratani zinazozunguka," alielezea Rahul Roychowdhury, profesa katika Chuo Kikuu cha Cambridge.

Dawa hiyo inafikiriwa kufanya kazi vizuri katika saratani ambazo hugunduliwa mapema, na zinaweza kutumika baada ya matibabu, kama upasuaji, kusaidia mfumo wa kinga kugundua seli zozote za saratani ambazo zinaweza kuwa tayari zimeenea.

Je, aspirini inapendekezwa kama matibabu ya saratani?

Swali ambalo kwa kawaida linakuja akilini kwa mtu yeyote anayesumbuliwa na saratani ni: Je, nimezee aspirini?

"Ikiwa una saratani, usikimbilie kwenye duka la dawa kununua aspirini," anasema Mangesh Thorat, daktari wa upasuaji na mtafiti wa saratani katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London. "Lakini fikiria kwa umakini kushiriki majaribio ya kliniki yanayoendelea au ya baadaye ili kuamua ufanisi wa aspirini."

Aliongeza kuwa ingawa utafiti huo umebaini "kipande cha puzzle" kuhusu jinsi aspirini inavyofanya kazi, kuna maswali zaidi ya kujibiwa.

Aspirini inaweza kusababisha kutokwa na damu nyingi ndani ya mwili, ikiwa ni pamoja na kiharusi, hivyo faida lazima zipimwe kila wakati dhidi ya hatari zinazoweza kutokea.

Pia haijulikani ikiwa aspirini huathiri saratani zote au aina maalum tu. Aidha, utafiti huu bado unafanywa kwa wanyama, na ingawa wanasayansi wana matumaini kwamba matokeo yanaweza kutumika kwa wanadamu, hii inahitaji uthibitisho zaidi na utafiti.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Madaktari tayari wanapendekeza kwamba baadhi ya wagonjwa wenye ugonjwa wa Lynch, ambayo huongeza hatari ya aina mbalimbali za saratani, kutumia aspirini.

Hata hivyo, bado itahitaji kufanya majaribio ya kina ya kliniki ili kuamua ikiwa wagonjwa zaidi wanaweza pia kufaidika nayo.

Majaribio haya ya kliniki tayari yanaendelea, na Ruth Langley, profesa kutoka Kitengo cha Majaribio ya Kliniki ya Baraza la Utafiti wa Matibabu katika Chuo Kikuu cha London, anaongoza kuwa utafiti unafaa kuamua iwapo aspirini inaweza kuzuia saratani za mapema kurudi.

Alieleza kuwa matokeo ya utafiti huo ni ugunduzi muhimu sana kwasababu utasaidia kubaini "kundi ambalo linanufaika zaidi kwa kuchukua aspirini baada ya kugundulika kuwa na saratani."

Hata hivyo, Langley alisisitiza onyo lake juu ya hatari za kutumia aspirini, akisisitiza umuhimu wa "kushauriana na daktari kabla ya kuanza kuchukua."

Kwa muda mrefu, Roychowdhury anaamini, wanasayansi wanaweza kuendeleza dawa mpya ambazo zinachanganya faida za aspirini, lakini na zenye madhara machache ya hatari.

Unaweza pia kusoma:

"Wakati mzuri wa ugunduzi"

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Wanasayansi waligundua faida za aspirini katika kutibu saratani, maelezo ambayo yalichapishwa katika jarida la kisayansi la Nature, kwa bahati, kwani wanasayansi hawakuwa wakifanya utafiti juu ya aspirini.

Timu ya utafiti katika Chuo Kikuu cha Cambridge ilikuwa ikichunguza jinsi mfumo wa kinga unavyokabiliana na saratani wakati zinaenea mwilini.

Watafiti walitumia panya zilizobadilishwa kijenetiki na kugundua kuwa panya wasio na seti fulani ya maagizo ya maumbile walikuwa na uwezekano mdogo wa kuendeleza saratani ya metastatic.

Utafiti zaidi ulionyesha jinsi seli za T zilikuwa zinawashwa, na hii ilianza kuungana na utaratibu unaojulikana wa hatua ya aspirini katika mwili.

"Ilikuwa ni wakati wa eureka," alisema Dk Ji Yang, ambaye alifanya utafiti huo.

"Ilikuwa ugunduzi usiotarajiwa kabisa, na ilituchukua kwenye njia tofauti kabisa ya utafiti kuliko tulivyotarajia," aliongeza.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi