'Saratani ya koo iliondoa sauti na ndoa yangu'

- Author, Komla Adom
- Nafasi, Journalist
- Akiripoti kutoka BBC News, Accra
Kuna mamilioni ya watu wanaopambana na ugonjwa wa saratani duniani. Kaulimbiu ya Siku ya Saratani Duniani mwaka huu ni: 'United by Unique.'
Mary Amankwah Fordwor, mkunga mwandamizi katika hospitali ya kikatoliki ya St. Anthony nchini Ghana, aligundulika na saratani ya koo mwaka 2021.
"Niligundua uvimbe usio na maumivu kwenye shingo yangu ambao ulikataa kuondoka," mama huyo wa watoto wawili ameiambia BBC. Madaktari baadaye walithibitisha 'uvimbe huo aliokuwa akiutibu kwa dawa za kawaida ni saratani.
Baadaye alifanyiwa upasuaji mara 14, baadhi ya operesheni hizo zilileta matatizo, na mwishowe, sanduku lake la sauti liliondolewa. Sasa anatumia kifaa bandia cha sauti na hawezi kula tena kama hapo awali.
Kugunduliwa na saratani kulikuja muda mfupi baada ya kupandishwa cheo na kuwa mkunga wa ngazi ya juu katika hospitali aliyofanyia kazi. Saratani ilivuruga maisha yake, si tu kitaaluma bali kihisia pia, ikiwa ni pamoja na kupoteza ndoa yake ya miaka 12.
Ugonjwa wa saratani
Kila mwaka, inakadiriwa kuwa kesi milioni 1.1 za saratani hurekodiwa barani Afrika, huku watu 700,000 wakipoteza maisha kwa ugonjwa huo, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni. Hesabu ya kimataifa ni kubwa zaidi – ugonjwa huo huondoka na maisha ya watu milioni 10 kila mwaka.
"Wakati wa matibabu ya dawa na mionzi, niliona watu wakifa, kwa hivyo niliunda kundi la WhatsApp lenye watu 12, nikitumia maisha na safari yangu kuwaeleza kuwa kuna maisha baada ya saratani ya koo," ameiambia BBC.
Mary anatoa elimu juu ya masuala mbalimbali ya saratani kwa kutumia akaunti zake za TikTok, Instagram na YouTube. Pia anatembelea shule, makanisa na mashirika mengine.
"Sikujua kujipenda ni nini. Sikujua kujithamini ni nini hadi nilipopata saratani ya koo," alisema.
Madaktari wameshindwa kugundua nini kilisababisha saratani ya Mary. Lakini kulingana na WHO, "mwili hudhibiti maambukizi ya saratani kwa asilimia 90 ya watu na kuzuia maambukizi ya virusi vya magonjwa ya zinaa (papillomavirus HPV), lakini aina hatari ya virusi vya HPV, ndio sababu ya saratani ya kizazi na inahusishwa na saratani ya vulva, uke, mdomo/koo, uume na sehemu ya haja kubwa."
Mwaka 2019, HPV ilisababisha kesi 620,000 za saratani kwa wanawake na kesi 70,000 kwa wanaume ulimwenguni. Shirika la WHO la uchunguzi wa saratani duniani, linasema kwa nchini Ghana, saratani ya koo kwa mwaka 2022 ni ya 17 kwa maambukizi kati ya saratani thelathini na mbili. Na kesi mpya 227 zilirekodiwa mwaka huo na maambukizi ya miaka mitano ni 626. Barani Afrika, kesi mpya zilikuwa 10,665 mwaka huo, na maambukizi ya miaka mitano ni 28,077.
"Watu hupuuza dalili za awali - ikiwa itagunduliwa mapema, tunaweza kuizuia," anasema Dk Ama Boatemaa Prah, daktari wa sikio, pua, na koo katika hospitali ya Korlebu ya Ghana. Dalili za awali ni pamoja na sauti kukwaruza ghafla, shida katika kupumua na kumeza na mafua ya muda mrefu.
"Tulikuwa tunaona saratani ya koo miongoni mwa watu wazee lakini sasa tunaona vijana wengi chini ya umri wa miaka 40," anasema Dk Prah.
'Iliondoka na sauti na ndoa yangu'

Chanzo cha picha, Mary Amankwah Fordwor
Wakati Mary amebahatika kupata huduma za matibabu na angali hai, madaktari wanasema ni mapema mno kusema hana saratani.
"Saratani ya koo haikuondoa sauti yangu nzuri tu; pia iliondoka na ndoa yangu ya miaka 12," anasema.
Hii inamfanya kuwa mmoja wa wanawake ambao wenza wao huwaacha wakati wa mapambano yao na saratani. Utafiti wa 2014 na Chuo Kikuu cha Michigan, unasema asilimia 31 ya ndoa zinazohusisha magonjwa ya kimwili huishia kwenye talaka, huku wanaume ndio wakiwa na uwezekano mkubwa wa kuwaacha wake zao wagonjwa.
Utafiti mwingine kutoka kituo cha utafiti wa saratani cha Fred Hutchinson mwaka 2009, uliweka kiwango cha talaka wakati mwanamke ni mgonjwa wa saratani katika 20.8%, na kiwango cha 2.9% pale mwanaume anapokuwa mgonjwa wa saratani.
Wataalamu wa afya nchini Ghana wanasema hali hiyo inaendelea kuongezeka ingawa hakuna takwimu rasmi.
Mary hakosi fursa ya kujikumbusha kwamba alifanya uamuzi sahihi kwa kuchagua maisha yake badala ya ndoa. Baada ya yote, yuko pamoja na wazazi wake na watoto wake wawili - wenye umri wa miaka 11 na 8 - ambao wako pamoja naye, ingawa mwanzoni hawakuelewa aliyokuwa anapitia mama yao.
"Mama alituambia ana saratani na tulipokwenda kumtembelea baada ya kufanyiwa upasuaji, niliogopa huenda angekufa. Lakini sasa yuko pamoja nasi, na tuna furaha kubwa," anasema Emmanuella, binti yake wa miaka 8.
Dk Prah anamwelezea Mary kama faraja kwa wengine. "Yeye ni mwanamke mchangamfu kila wakati. Tunataka wagonjwa wetu waige mfano wake na wawe na matumaini ya kupambana na saratani," anasema daktari.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah