Vijana wa kiume wanaotumia picha za utupu kufanya utapeli

kj

Chanzo cha picha, Jenn

Maelezo ya picha, Jordan DeMay na Mama yake Jenn
  • Author, Joe Tidy
  • Nafasi, BBC

Kijana wa kiume alijiua saa sita tu baada ya 'walaghai' kutishia kuchapisha picha zake za utupu kwenye mitandao.

Jordan DeMay alifariki mwaka 2022 baada ya ndugu wawili Samuel na Samson Ogoshi, kutoka Logos, Nigeria, kupata picha zake za utupu baada ya kujifanya msichana mrembo wa rika lake, na kutishia kumchafua kwa kutuma picha hizo za uchi kwenye mtandao.

Mama yake DeMay, Jenn Buta, sasa anatumia ukurasa wa TikTok wa mwanawe kuwaonya vijana kuhusu wahalifu kama hao, ambao wameenea nchini Nigeria - na video zake zimetazamwa zadi ya mara milioni moja.

Polisi wa Nigeria waliambia BBC, madai kuwa hawalichukulii suala hilo kwa uzito ni ya "ujinga."

Vijana hao wa miaka 22 na 20 walitumiana picha na mazungumzo ya mapenzi na kijana huyo wa miaka 17 kwenye Instagram, walimtumia picha za uchi kabla ya kumfanya nae atume picha zake akiwa uchi.

Kisha, walimtishia kumchafua asipowapa pesa ili wasizichapishe picha hizo kwenye mtandao.

Jordan alipowaambia hawezi tena kuwatumia pesa na atajiua, vijana hao walisema: "Afadhali ufanye hivyo haraka - au tutakufanya ufanye."

Walipopelekwa Marekani, walikiri kosa na wanasubiri hukumu.

"Ilikuwa chini ya saa sita tangu Jordan alipoanza kuzungumza nao hadi alipojiua," Jenn aliambia BBC, kutoka nyumbani kwake huko Michigan, kaskazini mwa Marekani.

Pia unaweza kusoma

Ukubwa wa Tatizo

xc

Chanzo cha picha, NIGERIA POLICE

Maelezo ya picha, Samuel, 22, na Samson Ogoshi, 20, walikamatwa Lagos na wanasubiri kuhukumiwa nchini Marekani.

Tatizo hili huwapata zaidi wavulana au wanaume. Mwezi Aprili, Wanigeria wawili walikamatwa baada ya mvulana wa shule ya upili nchini Australia kujiua kwa kisa kama hicho.

Kumekuwa na ongezeko la watu wanaopata tatizo kama hili nchini Japan, kutokea Nigeria.

Pia, takwimu za uhalifu uliofanywa nchini Marekani zinaonyesha, idadi ya wahalifu wa uhalifu huu imeongezeka maradufu mwaka jana hadi kesi 26,700, ambapo wavulana wasiopungua 27 walijiua katika kipindi cha miezi miwili.

Wiki hii, maafisa kutoka Shirika la Uhalifu wa Mtandao walikutana na Mamlaka ya Uhalifu wa Mtandaoni ya Uingereza (NCA), ili kujadili jinsi ya kuboresha ushirikiano juu ya uhalifu wa mtandaoni unaolenga picha za utupu.

NCA imewaonya watoto wa shule kuhusu ongezeko la idadi ya watoto ambao wamepata matatizo hayo katika mwezi uliopita.

Ni tatizo la makundi ya wahalifu kutoka baadhi ya nchi za Afrika Magharibi na Kusini Mashariki mwa Asia.

Watafiti wa usalama wa mtandaoni wanasema uhalifu huo mara nyingi unahusishwa na wahalifu wa mtandaoni kutoka Nigeria wanaojulikana kama Yahoo Boys, walipewa jina hilo baada ya kuhusishwa na uhalifu kupitia barua pepe ya Yahoo mapema miaka ya 2000.

Na mwanzoni mwa mwaka huu, uchunguzi wa Kituo cha Utafiti wa Mtandaoni cha Marekani ulifichua jinsi baadhi ya Wanigeria wanaotumia TikTok, YouTube na Scribd wanavyopeana habari za namna ya kuwachafua watu.

Mkurugenzi wa Kituo cha Uhalifu wa Mtandaoni cha Nigeria, Uche Ifeanyi Henry, ametetea hatua wanazochukua kukabiliana na tatizo hilo:

"Watu wanadhani hakuna chochote kinachoonekana ambacho Nigeria imefanya kutatua tatizo hilo na dhana hiyo ni ujinga," anasema.

Kiasi kikubwa cha fedha ambacho serikali imetumia kujenga kituo cha kisasa cha kupambana na uhalifu wa mtandaoni kinaonyesha juhudi za kweli za kutatua tatizo hilo.

“Kuna wahalifu wengi wamefunguliwa mashtaka na wengi wamekamatwa. Wengi wa wahusika wa uhalifu huu wamekwenda kuishi katika nchi jirani kwa sababu ya hatua tunazochukua," anasema Henry.

Ukosefu wa Ajira

j
Maelezo ya picha, Mkuu wa Tume ya Kupambana na Uhalifu wa mtandaoni nchini Nigeria, Uche Ifeanyi Henry

Kuna ongezeko la watu wanaodhulumiwa mitandaoni kwa kutumia picha za utupu na dhuluma hizo hufanywa na vijana wa Nigeria.

Hata hivyo, ni tatizo linalohitaji ushirikiano wa kimataifa ili kuweza kuliondoa

Dk Tomari Sibe, kutoka kituo cha Digital Footprints nchini Nigeria, anasema utapeli wa kutumiaji picha chafu ni jambo linalokuwa miongoni mwa vijana wa nchi hiyo wanaotumia mtandao.

“Mambo yaliyosababisha haya yanahusiana na masuala ya kijamii na kiuchumi,” anasema.

“Pia kuna tatizo la ukosefu wa ajira na umaskini. Vijana hawa ambao hawana la kufanya hawafikirii matokeo mabaya ambayo yanaweza kuwapata."

SDCX

Chanzo cha picha, Jenn

Maelezo ya picha, Mamake Jordan amechapisha video kadhaa ili kutoa ufahamu kwa watu

Jenn anaendelea kutoa elimu akishirikiana na babake Jordan.

Anasema kuna baadhi ya wazazi waliowasiliana naye kutoka Marekani, Australia na Uingereza ambao aliiwashauri kuhusu watoto wao waliojiuwa kutokana na shida hii.

"Hupokea ujumbe kila siku kutoka kwa wazazi ambao wanaomba ushauri kwa sababu mtoto wao ameangukia mikononi mwao wahalifu hawa," anasema.

“Wakati mwingine, hunambia kilichotokea kwa mtoto wao. Na wakati mwingine husema, asante kwa sababu ya mkasa wa Jordan na huja kwangu niwape msaada."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah