Tapeli wa mapenzi alivyowalaghai wanawake pauni 80,000

Chanzo cha picha, Other
Kundi la wanawake linawaonya wengine kufanya upelelezi kuhusu wenzi waliokutana nao kupitia programu za uchumba baada ya mikopo yenye thamani ya maelfu ya pauni kuchukuliwa kwa majina yao na mtu mmoja.
Peter Gray, mwenye umri wa miaka 35, ambaye alikutana na wanawake kwenye programu (App) ya kutafuta wachumba inaofahamika kama Tinder, alifungwa jela baada ya kuwatapeli wanawake wanne takriban pauni elfu 80.
Muathiriwa mmoja alisema Gray, kutoka West Yorkshire, "aliharibu maisha yangu" na kumwacha na maswali muhimu ya uaminifu.
Tinder ilisema "imetekeleza njia mbalimbali za kuwaonya watumiaji kuhusu uwezekano wa ulaghai".
Gray, wa Mirfield, alihukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu jela mwezi Februari na kupewa amri za zuio kuhusiana na waathiriwa.
Akiongea na Clare McDonnell wa BBC Radio 5 Live, Jessica - sio jina lake halisi - alielezea jinsi alivyokutana na Gray kwenye programu ya kutafuta wachumba mnamo 2018 baada ya kutoka katika uhusiano wa wa awali wa kimapenzi miaka sita iliyopita.
Ingawa hakuwa mtu mwenye vigezo alivyovitaka alikuwa "msikilizaji mzuri na alikuwa na kila kitu nilichohitaji wakati huo", alikumbuka.
Walipokutana kwa mara ya tatu, Jessica alikuwa katika nyumba yake na akaamka kwenda kujisaidia.
"Niliacha begi langu kwenye meza yake ya chakula, akaingia kwenye begi langu na kuchukua picha za leseni yangu ya kuendesha gari na kadi zangu zote mbili za benki," alisema.
Baadaye aligundua mikopo ya hadi thamani ya pauni 9,000 ilichukuliwa kwa jina lake.

Chanzo cha picha, Tinder
Licha ya Grey kujitolea kulipa pesa kwa muda, Jessica alienda polisi. "Sikutaka kufungwa na kijana huyu kwa miaka mitano kwa sababu hata sikumjua," alisema.
Hana, mwanamke mwingine ambaye alikutana na Gray kwenye Tinder, alimweleza kuwa mwanzoni kama mtu "mtulivu na mtatuzi," changamoto za mapenzi katika mazungumzo yao lakini alihisi kuna kitu ambacho "hakikuwa sawa".
Wiki moja baadaye, baada ya Hannah kuamua kusitisha uhusiano huo, alipokea barua ya kukubali mkopo wa pauni elfu 20 kwa jina lake.
Wawili hao walirejesha uhusiano wao miezi michache baadaye baada ya Gray kummiminia zawadi na maneno ya mahaba, hata hivyo baadaye alisitisha uhusiano wao kwa mara nyingine tena.
"Nadhani nilikuwa nimepata dalili za hatari kuhusiana na yeye ," alisema.
Vidokezo vya utapeli wa kimapenzi
- Uwe na shaka na maombi yoyote ya pesa kutoka kwa mtu ambaye hujawahi kukutana naye ana kwa ana.
- Ongea na familia au marafiki na usione aibu kuijadili uhusiano wako.
- Huenda picha za utambuisho zisiwe za kweli, kwa hivyo tafuta picha kupitia mfumo wa kidigitali wa kutafuta ili kuona kama picha zimechukuliwa kutoka kwa mtu mwingine au la.
- Fuatilia ripoti yako ya mkopo, hasa ikiwa umekuwa muathirika wa wizi wa utambulisho.
- Ulaghai unaweza kuripotiwa kwa polisi
- Usaidizi zaidi unaweza kupatikana kupitia BBC Action Line
Vyanzo: Usaidizi wa Ulaghai/Waathiriwa/Acha Ulaghai Uingereza.
Katika mahusiano yote, Grey alianzisha uhusiano wa karibu ambao ungemsaidia kutenda makosa kwa faida yake binafsi ya kifedha.
Hannah alipogundua kuwa alikuwa mjamzito, dada yake alichunguza maisha ya Grey na kumtafuta mmoja wa washirika wake wa zamani, ambaye alimuonya kuhusu maisha yake ya nyuma yaliyofichwa.
"Hakuna njia ambayo nitaruhusu mtoto alelewe mahali popote karibu na mwanadamu muovu kama huyo," Hannah alisema.
"Ulimwengu wangu ulikuwa umegawanyika mbele ya macho yangu katika mazungumzo hayo ya nusu saa."
Grey alirudia mtindo huo huo tena wakati alipokutana na Elizabeth - sio jina lake halisi - mnamo 2020.
Alituma maua nyumbani kwake, licha ya Elizabeth hakuwahi kufichua mahali alipokuwa akiishi.
Elizabeth alisema: "Nilianza kuhisi kuna udanganyifu, lakini niliendelea kufikiria, acha kuwa mjinga, unahitaji kumtafuta mtu anayekutendea vizuri."
Siku mbili kabla ya kuhamia katika nyumba yake mpya, rehani ya Elizabeth ilitolewa baada ya Gray kutumia leseni yake ya kuendesha gari kupata mkopo wa takriban £10,000 kwa jina lake.
Unaweza pia kutazama:
Jessica alisema vitendo vya Grey "vimeharibu maisha yangu kabisa" na akasema kuwa ameacha kuchukua kitambulisho na kadi za benki anapokutana na wapenzi.
"Simwamini mtu yeyote ninayekutana naye," alisema.
Elizabeth alisema: "Unafikiria mara kwa mara, huyu mtu ananiambia ukweli kumhusu au anachosema sio kweli");