Je, unayajua magonjwa ya zinaa na jinsi ya kujikinga?

Chanzo cha picha, Getty Images
Magonjwa yatokanayo na maambukizi wakati wa kufanya ngono (STI), huambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kupitia kujamiiana au matendo yanayohusisha ngono.
Maambukizi yake mara nyingi hayaonyeshi dalili siku za awali na ni vigumu kuyagundua. Maambukizi yanapodhihirika na magonjwa kuanza kuonyesha dalili fulani, hapo ndipo husemwa ana ugonjwa wa zinaa (STD).
Magonjwa ya zinaa kwa kawaida huenezwa wakati wa kujamiiana, lakini wakati mwingine yanaweza kusababishwa na mgusano wa kingono wa ngozi kwa ngozi.
Baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza pia kuambukizwa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua, au kunyonyesha.
Njia nyingine ambazo magonjwa ya zinaa yanaweza kuenezwa ni kuongezewa damu au kwa kuchangia sindano.
Magonjwa ya zinaa yanaweza kusababisha athari mbaya ikiwa ni pamoja na saratani, maumivu ya muda mrefu ya nyonga, mimba nje ya kizazi na utasa.
Magonjwa ya zinaa na dalili zake

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kuna zaidi ya bakteria 30, virusi na vimelea vinavyoweza kuambukizwa kwa kujamiiana. Mtu anaweza kuwa na magonjwa mengi ya zinaa kwa wakati mmoja.
Magonjwa ya zinaa yanayojulikana zaidi ni kaswende, kisonono, klamidia na trikomonasi. Magonjwa haya yote yanatibika.
Maambukizi ya magonjwa ya zinaa kwa kawaida hayana dalili au yanaweza kuonyesha dalili kidogo sana. Na inawezekana kuwa na maambukizi bila kujua. Baadhi ya dalili ni kama:
- Kutokwa na uchafu usio wa kawaida katika uume au uke
- Kupata vidonda au dutu kwenye sehemu ya siri
- Kupata maumivu wakati wa kukojoa
- Kukojoa mara kwa mara
- Muwasho na uwekundu katika eneo la uke
- Malengelenge au vidonda ndani au pembeni ya mdomo
- Harufu mbaya isiyo ya kawaida ya uke
- Sehemu ya haja kubwa kuwasha, kuuma au kutokwa na damu
- Maumivu ya tumbo
Kwa nini magonjwa ya zinaa ni mengi?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
2020, WHO ilikadiria kuna maambukizi mapya milioni 374 ya moja ya aina nne za magonjwa ya zinaa; trikomonasi (milioni 156), klamidia (milioni 129), kisonono (milioni 82) na kaswende (milioni saba).
Zaidi ya watu milioni 490 wanakadiriwa kuishi na ugonjwa wa malengelenge katika sehemu za siri kufikia mwaka 2016, na inakadiriwa watu milioni 300 wana maambukizi ya virusi vya HPV (human papillomavirus).
Virusi vya papilloma vya binadamu (HPV) ni chanzo kikuu cha saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na saratani ya haja kubwa kwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao, kulingana na takwimu za WHO.
"Ngono ni hitaji la kibaolojia. Ni kama kula na kunywa, ni sehemu ya asili ya mwanadamu,” anasema Dkt. Teodora Elvira C. Wi, kiongozi wa taasisi ya Global HIV, Hepatitis and STIs ya WHO.
“Unafanya mapenzi na unapofanya mapenzi unaweza kupata magonjwa ya zinaa. Ndio maana idadi ya maambukizo ni kubwa sana."
Dkt. Wi pia anaeleza kuwa magonjwa ya zinaa mara nyingi hayana dalili, watu wanaweza kuambukizana bila kujua.
''Hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa imeongezeka kwa sababu ya mabadiliko ya ufanyaji wa ngono; urahisi wa kupata kufanya ngono, kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja na kuongezeka matumizi ya mitandao ya kutafuta wapenzi,'' anasema Dkt. Wi.
Ingawa tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kupungua kwa idadi ya vijana wasio katika ndoa na wanaofanya mapenzi, lakini pia kuna kupungua kwa matumizi ya kondomu.
Dkt. Wi anaeleza, ''wakati hakukuwa na matibabu ya VVU, watu walikuwa waangalifu kufanya ngono zembe, haswa bila kondomu lakini sasa watu wanaamini wanaweza kupima VVU, kunywa dawa na kupona. Kwa hiyo, matumizi ya kondomu yamepungua."
2022, watu milioni 1.3 waliambukizwa VVU, kulingana na ripoti ya WHO. Zaidi ya watu 600,000 wanafariki kila mwaka kutokana na virusi hivyo kwa sababu hawajui wana VVU na hawako kwenye matibabu, au wanaanza matibabu wakiwa wamechelewa, linasema shirika hilo.
Unawezaje kujikinga na magonjwa ya zinaa?

Chanzo cha picha, Getty Images
“Tafadhali tumia kondomu. Hiyo ndiyo itakulinda dhidi ya magonjwa ya zinaa,” Dkt. Wi anasema.
“Ikiwa utafanya ngono na mtu usiyemjua chukua tahadhari. Ni bora ujifunze jinsi ya kutumia kondomu na jinsi ya kufurahiya nayo."
Utumiaji sahihi wa kondomu za mpira hupunguza hatari, lakini haziondoa moja kwa moja hatari ya kupata magonjwa au kueneza magonjwa ya zinaa kwa mujibu wa wataalamu wa afya.
Ikiwa mtu ana mzio na kondomu za mpira, ushauri ni kutumia aina nyingine za kondomu.
Ikiwa utapata dalili za ugonjwa ya zinaa, ni muhimu kwenda kwa mhudumu wa afya mara moja ili kupimwa na kutibiwa.
“Usiende kwenye duka la dawa ambako unakwenda kujitibu mwenyewe - hilo halitakusaidia. Usipotibiwa ipasavyo, unaweza kupata madhara makubwa zaidi, kama vile utasa,” anasema Dkt. Wi.
"Kupuuza magonjwa ya zinaa kunaharibu afya; kunaweza kusababisha ugonjwa wa uvimbe kwenye fupanyonga. Kuna kesi milioni moja hadi mbili za utasa kila mwaka kutokana na maambukizi mapya ya kisonono au klamidia kwa wanawake wasiotibiwa," anasema.
''Kaswende wakati wa ujauzito husababisha madhara mabaya. Kuna kesi 355,000 kila mwaka za matatizo wakati wa kujifungua. Na husababisha vifo vya watoto wachanga 61,000 kila mwaka na HPV husababisha vifo 342,000 vya saratani ya mlango wa kizazi kila mwaka,'' anasema Wi.
Ni matibabu gani ya magonjwa ya zinaa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Maambukizi ya zinaa ambayo husababishwa na bakteria au vimelea yanaweza kutibiwa kwa dawa, lakini hakuna tiba ya magonjwa ya zinaa yanayosababishwa na virusi, kama vile herpes au HPV.
Dawa zinaweza kusaidia na kupunguza hatari ya kueneza maambukizi. Pia kuna chanjo za kuzuia HPV na hepatitis B.
Dkt. Wi anasema, ''WHO inatengeneza chanjo ya kisonono na chanjo ya matibabu ya malengelenge ya sehemu za siri, kama ile chanjo ya mRNA iliyotumiwa katika Uviko 19.''
Dkt. Wi pia anadokeza kuna juhudi za kutengeneza chanjo ya klamidia pamoja na utafiti wa njia zinazowezekana za kutengeneza chanjo ya kaswende.
“Kwa sababu ya unyanyapaa wa magonjwa ya zinaa, hayapewi kipaumbele.'' Anasisitiza, ''serikali zinapaswa kueneza huduma na kupunguza gharama za huduma za afya na kutoa ufadhili kwa ajili ya maendeleo ya vifaa vya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya ngono.''
"Magonjwa ya zinaa yamepuuzwa kabisa. Tunahitaji kupunguza unyanyapaa unaoyazunguka na kuyachukulia kama maambukizi mengine yoyote,” anasema Dtk. Wi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi