Fahamu athari zinazoweza kujitokeza binamu wakioana

Picha ya pete mbili za ndoa
Maelezo ya picha, Picha ya pete mbili za ndoa
Ndoa za binamu: Ni ushahidi mpya unaoeleza sababu za watoto kuzaliwa na matatizo ya afya

Uani mwa nyumba iliyoko Bradford dada watatu wanaonekana wakipiga soga.

Mtaalam wa ulimbwende amekaa kwa kochi tayari kuwapamba warembo hawa.

Shangwe na nderemo zimetapakaa kila mahali kote chumbani.

Dada hawa wanajiandaa kwa harusi ya mmoja wa familia itakayofanyika mwishoni mwa wiki wiki, ambayo bibi na bwana harusi ni binamu.

Kwa wengi ndoa za aina hii zinawastaajabisha lakini kwa familia hii na baadhi ya maeneo ya Bradford ni kitu cha kawaida.

Ayesha mwenye umri wa miaka 28 ni mkubwa kuliko wenzake pia aliolewa na binamu yake mwaka 2017.

Kwasasa ana watoto wawili na anatuelezea anafurahia ndoa yake na haikuwa jambo geni kuolewa na binamu yake.

Mama yao mwenye asili ya Pakistani alifikiria mabinti zake wote watatu wataingia kwenye ndoa za aina hii.

Lakini Salina mwenye umri wa miaka 26, ambaye ni mdogo kuliko wote anasema alivunja dhana hii na kuolewa kwenye ndoa ya 'mapenzi', kwa kuchagua mwenza ambaye hawana uhusiano wowote wa kindugu.

Salina anatuambia hulka yake ni mchangamfu na aliyejaa maono , na kuolewa na binamu yake hakupendelea kabisa.

Kisha kuna Malika, dada aliyemfuata Salina kwasasa hana mchumba lakini ameapa hataolewa na mwanaume ndugu, kama binamu.

" Nilimwambia mama yngu, si wakejeli dada zangu lakini kuolewa na binamu hapana" Malika anatuarifu.

Anatueleza kupata elimu kumemfungua macho na kumpa fursa nyingi.

" Awali ingekuwa unaendelea na masomo ungejikuta bado unafikiria kuolewa lakini kwa sasa mambo ni tofauti".

Takwimu za kutisha

Uingereza na pia Ulaya ndoa za binamu zimeendelea kuangaziwa zaidi haswa na madaktari ambao wanaonya kuwa ndoa za binamu na ndugu wa karibu zaidi, watoto wanaozaliwa huwa na matatizo ya afya.

Na sasa kuna takwimu za kutamausha kutoka Bradford ambazo zinatonesha kidonda zaidi.

Wataalam katika Chuo cha mjini wanaingia katika mafunzo na tathmini mwaka wa 18.

Ni utafiti wa kiafya ambao ni mkubwa kuwahi kutokea .

Kati ya mwaka 2007 hadi 2010 walisajili watoto 13,000 ambao wamewafuatilia tangu wadogo mpaka kuingia wabaleghe.

Zaidi ya mmoja kati ya sita wanaofuatiliwa wazazi wao ni binamu, wengi wakitoka jamii ya Pakistani iliyoko Bradford na kuufanya utafiti huu kuwa muhimu zaidi kubaini athari za ndoa kati ya binamu.

Njia ya wazi ambayo wazazi wawili wanaoshirikiana damu wanaweza kuongeza hatari ya afya kwa mtoto ni kupitia ugonjwa wa kurithi, kama vile selimundu na uvimbe kwenye kizazi.

Kulingana na nadharia ya Gregor Mendel, ikiwa wazazi wote wawili wana jeni ya ugonjwa huo, kuna nafasi moja kwa nne kwamba mtoto wao atarithi hali hiyo.

Wakati wazazi ni binamu, kuna uwezekano mkubwa kwa wote wawili kuwa wana jeni za ugonjwa huo.

Mtoto wa binamu wa kwanza ana asilimia 6 ya uwezekano wa kurithi ugonjwa wa kimaumbile, ikilinganishwa na asilimia 3 ya mtoto aliyezaliwa na wazazi ambao sio binu.

Hata hivyo, utafiti wa Bradford ulitazama suala hili kwa mtazamo mpana zaidi na kutoa mwangaza mpya.

Watafiti hawakuchunguza tu kama mtoto alikuwa na ugonjwa wa kimaumbile, bali walijumuisha data nyingi, zikijumuisha maendeleo ya usemi na lugha ya watoto, mara kwa mara ya huduma za afya, na ufanisi wao shuleni.

Walitumia mfano wa kihesabu kuondoa athari za umaskini na elimu ya wazazi, ili kujikita katika athari za "consanguinity," neno la kisayansi linalomaanisha kuwa wazazi ni wa familia moja.

Pia unaweza kusoma:

Waligundua kuwa iwapo umaskini wa familia umedhibitiwa, mtoto wa binamu wa kwanza eneo la Bradford alikuwa na nafasi ya asilimia 11% kuwa matatizo ya kuzungumza, ikilinganishwa na asilimia 7% ya watoto waliozaliwa na wazazi ambao hawahusiani kwa damu.

Pia waligundua kuwa watoto waliozaliwa na binamu wa kwanza walitembelea mara nyingi hospitali kwa matibabu ukilinganisha na waliozaliwa kwa ndoa za kawaida - wanne licha ya watatu kila mwaka.

Neil Small profesa katika chuo cha Bradford na muanzilishi wa tathmini hiyo anasema iwapo watoto wote wanamatatizo ya kimaumbile walitembelea hospitali '' haimaniishi huduma za matabibu zinahitajika zaidi kwa watoto waliozaliwa na wanandoa ambao wanahusiana.''

Utafiti huu anasema '' ni muhimu kwasababu unatoa fursa ya namna ya kukabiliana na kulenga mikakati ya kuepusha na kutibu magonjwa yanayotokana na hali hii.''

Wasiwasi waibuka

Utafiti mmoja katika jamii moja ya Bradford haiwakilishi Uingereza kwa ujumla.

Hata hivyo, imeibua wasiwasi miongoni mwa wanasayansi ambao pia umechochea wabunge kufuatilia kiundani hasa Ulaya.

Kwa mfano, Norway, ndoa za binamu wa kwanza zilipigwa marufuku na nchini Uswidi , marufuku ya ndoa hizo yataanza kutekelezwa mwaka ujao.

Richard Holden

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Richard Holden (pichani) amependekeza mswada wa kuharamisha ndoa za binamu akiongezea kwa orodha za ndoa zilizopigwa marufuku

Nchini Uingereza, mbunge Richard Holden amependekeza mswada wa kuharamisha ndoa za binamu akiongezea kwa orodha za ndoa zilizopigwa marufuku.

Lakini serikali imesema haina mpango wowote wa kupiga marufuku aina hiyo ya ndoa.

Kwa sasa, Uingereza inafuata sera ya kutoa ushauri wa jeni ambapo wanandoa wa binamu wa kwanza wanaelimishwa hatari ya kupata watoto na kuhamasisha kufanyiwa uangalizi zaidi wakati ni wajawazito.

Wakosoaji wa sera hii wanaeleza kuwa kwanini nchi hiyo igharamike kutoa ushauri badala ya kupiga marufuku au kuweka vikwazo vingi ili kukabiliana na ndoa za aina hii?

Kuoana kwa binamu wa kwanza sio jambo geni Uingereza.

Kiongozi Charles Darwin alioa binamu wake wa kwanza , Emma Wedgwood.

Mtoto wao wa kiume Sir George Darwin aliendelea na kueleza ndoa za binamu zinajumuisha moja kati ya 20 katika mahusiano ya kikabaila karne ya 19.

Malkia Victoria alioa binamu wake wa kwanza mwanamfalme Albert.

Kufikia karne ya 20 ndoa za binamu zilipungua hadi asilimia 1%.


Ni picha ya nguo za kitamaduni za Asia Kusini

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ndoa ya binamu ni jambo la kawaida sana hasa katika nchi za Mashariki ya Kati, Asia ya Kusini, na Afrika Kaskazini

Athari za ndoa za binamu

Kwa wale wanataka kupiga marufuku ndoa za binamu wanaeleza hatari ya wanandoa kuzaa watoto walio na matatizo ya kimaumbile.

Kama vile mbunge wa Richard Holden anasema ni kuwa watoto waliozaliwa kutokana na ndoa hizi hufariki mapema ukilinganisha na watoto waliozaliwa kutokana na ndoa zilizozoeleka.

Mtafiti Patrick Nash anasema kinachomshinikiza nakutaka ndoa za aina hii ziharamishwe ni watoto wanaozaliwa wanakabiliwa na matatizo ya kiafya.

'' kupiga marufuku ndoa za binamu kutaimarisha afya ya umma na kuepukana na matatizo yakudhibiti magonjwa ya vinasaba''.

Picha ya kawaida ya Sam Oddie

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Profesa Sam Oddie amehudumu Bradford kwa zaidi ya miaka 20 na ameshuhudiwa visa vingi vya magonjwa yanayosababishwa na jeni

Profesa Sam Oddie ambaye anahudumu kama mtafiti katika hospitali ya rufaa ya Bradford ameshuhudia matatizo ya jeni.

''Nimeona matatizo ya ngozi, ugonjwa wa akili, na pia hali hatarishi ya viungo kulegea miongoni mwa watoto''.

Akiongezea kuwa changamoto hizi za kiafya zinashuhudiwa zaidi eneo la Bradford ukilinganisha na maeneo mengine.

Anakumbuka kisa kimoja ambapo familia imepoteza watoto kadhaa kutokana na matatizo ya jeni.

Haikuwa rahisi kwa familia hii kukubali msiba huo uliotokea kila mara.

Mahusiano ya Vinasaba

Profesa Oddie pia ameeleza kinachosibu jamii za Bradford sio tu ndoa za binamu pekee bali watu kuoana katika jamii moja.

Huwa ni rahisi ndani ya jamii kuwa wanachimbuko moja na wana jeni zinazofanana hata kama sio binamu wa kwanza.

Ndoa za watu wa jamii moja pia huleta changamoto za kimaumbile kwa watoto wanaozaliwa .

Nguvu ya elimu

Badala ya kupiga marufuku , anasisitiza nguvu ya kuelimisha kuhusu jeni na vinasaba.

Kwa miaka mingi kumekuwa na hamasa katika jamii ya Pakistani kuhusu hatari ya kuoana kwa binamu .

Wanandoa huanza kuelimishwa kabla yakupata ujauzito na baada ili kuwatayarisha saikolojia kitakachofuata baada ya kujifungua.


Mwanamke akipita karibu na Msikiti Mkuu wa Al-Jamia Suffa-Tul-Islam huko Bradford, Uingereza

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bradford imekuwa na kampeni za muda mrefu za kuongeza ufahamu wa hatari za kijenetiki ndani ya jamii ya Pakistani

Huko Bradford, baadhi ya watu wanabadilisha mitazamo kuhusu ndoa za binamu kutokana na kuongezeka kwa uelewa wa hatari za kiafya.

Salina, ambaye alioa kwa mapenzi, anasema mabadiliko hayo yanatokea polepole.

Mallika, dada yake, anasisitiza kuwa mitandao ya kijamii imechangia kupanua mtazamo wa watu.

Hata Ayesha, ambaye yupo katika ndoa ya binamu, anasema hafikiri watoto wake wataoa binamu zao.

Alikubaliana na hatari za kijenetiki na kusema kuwa kama mtoto atazaliwa na ulemavu, itatokea bila kujali kama ni ndoa ya binamu au la.

Pia unaweza kusoma:

'Ndoa za kulazimishwa'

Kando na matatizo ya afya kuna baadi ya sababu watu wanataka zipigwe marufuku: inachochea ndoa za kulazimishwa.

Ikiwa baadhi ya wanawake wakimbizi hulazimishwa kuolewa na wanafamilia.

Kulingana na Tonje Egedius ambaye ni mwanahabari wa masuala haya ndoa hizi za binamu huwa zinachukuliwa ni za kulinda hadhi ya familia na wakati mwingi maovu yanayotokana na kulinda hadhi inasababisha unyanyasaji.

Pia ndoa hizi pia zinatumika kubagua watu katika jamii inakuwa familia moja inaoana ili wasitangamane na wanajamii wengine.

Wanawake wengi wakiolewa kwa ndoa za aina hii hujipata wakitegemea kiuchumi familia na kupigwa marufuku kwa ndoa hizi kutawaepusha wanawake kunyanyaswa kiuchumi na wawe wakujitegemea.

Wataalam wanasema hata kama marufuku itatekelezwa, baadhi ya wanandoa wataendelea kuoana na binamu zao kupitia ndoa haramu na ambazo hazijasajiliwa - na kwamba wanawake katika ndoa hizo wanaweza kuhisi hawana tena ulinzi wa serikali ikiwa uhusiano huo utaharibika.

Nazir Afzal
Maelezo ya picha, Nazir Afzal (pichani) anaamini kuwa sheria ikitungwa huenda ikasalimisha wale wanaolazimishwa kuoa binamu wao

Aliyekuwa mwendesha mashtaka mkuu wa Uingereza Nazir Afzal, anasema sheria kamilifu zikibuniwa zitalinda watu wanaolazimishwa kuingia kwa ndoa za binamu.

Hata hivyo amependekeza kuwa kuna umuhimu wa kuheshimu mila za jamii fulani na mapenzi ya mtu binafsi.

Kwa upana, anapendekeza serikali inapaswa kuwa na mikakati ya kuelimisha na kuchunguza jeni za wanandoa wanaoingia katika ndoa hizo kuliko kupiga marufuku.

Kuchochea mgawanyiko

Kwa wengine, wazo la kupiga marufuku ndoa za binamu wanazichukulia kama kubagua jamii za walio wachache .

Karma Nirvana ambaye amekuwa akifanya kazi za misaada anasema kupiga marufuku ndoa za binamu zinaweza kutafsiriwa na chuki na kuweka uhasama miongoni mwa jamii.

Mswada wa Richard Holden uko katika awamu ya pili bungeni.

Ikikosa uungwaji mkono na serikali huenda haitapenya lakini matukio yanayoendelea Scandinavia imechochea ndoa za binamu kujadiliwa sana.

Tukirejea familia tuliokutana nayo hapo awali iliyoko Bradforth mtaalam wa ulimbwende anamalizia kuwapamba madada hao watatu wanaohudhuria harusi wikendi.

Ayesha ambaye ameolewa na binamu wake anavuta kumbukumbu kuhusu ndoa yake inayoelekea mwaka wa 8 .

'' Tumekuwa na changamoto, na panda shuka nikiwa na mume wangu lakini cha msingi tunafurahia kuoana.''

'' nadhani pia ndoa zilizoanza kwa mapenzi zinapitia changamoto labda zitofautiane kidogo''.

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid