'Usuhuba wa Kabila na M23' ni suluhu ya mzozo wa DRC au kivuli kipya cha vita vya muda mrefu?

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Joseph Kabila aliongoza DRC kwa miaka 18 kuanzia 2001
  • Author, Na Dinah Gahamanyi
  • Nafasi, BBC News Swahili
  • Akiripoti kutoka Nairobi

Rais wa zamani DRC Joseph Kabila amekuwa mjini Goma mashariki mwa nchi hiyo, eneo linalodhibitiwa na waasi wa M23, hatua iliyoibua maswali kuhusu hatma ya suluhu ya muda mrefu ya mzozo unaendelea nchini humo. Lakini Je, uswahiba wake na M23 una maana gani? na utaleta suluhu ya mzozo wa kivita DRC?.

Kujibu maswali haya ni vyema kukumbuka chanzo cha mzozo unaoendelea hivi sasa nchini DRC husan eneo la Mashariki mwa nchi.

Tulifikaje hapa?

g

Chanzo cha picha, AFC

Maelezo ya picha, Viongozi wa M23/AFC Kutoka kushoto kwenda kulia: Bertrand Bisimwa, Sultani Makenga na Corneille Nangaa

Baada ya kusitisha harakati zake za miaka ya nyuma, mwishoni mwa 2021, M23 ilianza kuibuka tena na iliendelea kusonga mbele kimkakati na kupata kasi zaidi mwaka 2023 na 2024.

Mapema mwaka huu, waasi wa M23 walisonga mbele na kuchukua udhibiti wa miji miwili muhimu - Goma na Bukavu. Takriban watu 8,500 wameuawa tangu mapigano yalipoongezeka mwezi Januari, kulingana na serikali ya Congo.

Kulingana na UN, Wakongo milioni 5.6 ni wakimbizi wa ndani DRC, na zaidi ya milioni 4 wanatoka katika majimbo ya mashariki ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri.

Desemba mwaka jana, mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Angola yalivunjika baada ya Rwanda kuitaka serikali ya DRC kuzungumza moja kwa moja na M23. Licha ya shinikizo la kimataifa kuongezeka, viongozi mjini Kinshasa walikataa kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na waasi.

Katika mahojiano na BBC, Waziri Mkuu wa DRC Judith Suminwa Tuluka alisema serikali yake inataka kufanya mazungumzo na nchi jirani ya Rwanda, ambayo inaituhumu kuunga mkono M23, tuhuma ambazo Rwanda imekuwa ikizikana.

Mwezi Machi, Rais wa DRC Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame walitoa wito wa "kusitishwa mara moja kwa mapigano" mashariki mwa Congo, baada ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja nchini Qatar.

Kufika kwa Joseph Kabila Goma

g
Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Joseph Kabilaalipokutana na viongozi wa dini katika eneo la Kinyogote, jiji la Goma Alhamisi

Ni vyema kukumbuka kuwa hii sio mara ya kwanza kwa Joseph Kabila kwenda Goma. Mwezi uliopita Kabila alikwenda Goma.

Katika taarifa yake wakati huo, Bw Kabila alisema kurejea kwake kumechochewa na nia ya kusaidia kutatua mzozo unaozidi kuwa mbaya wa kitaasisi na kiusalama nchini DR Congo.

Pia aliliambia jarida la Kifaransa la Jeune Afrique anataka "kuchukua jukumu la kutafuta suluhu baada ya miaka sita ya kuwa nje na mwaka mmoja uhamishoni."

Hata hivyo Tshisekedi amemshutumu Kabila hadharani kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na Alliance Fleuve Congo – muungano wa waasi ambao M23 ni sehemu yake. Kabila amekanusha tuhuma hizo.

Ben Radley, mwanauchumi na mhadhiri wa masuala ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Bath aliiamba BBC, Kabila ana uhusiano na waasi.

"Baadhi ya wachambuzi wanasema kiongozi wa AFC, Corneille Nangaa, aliyekuwa mkuu wa zamani wa Tume ya Uchaguzi chini ya Kabila na mshirika wa karibu wa Kabila, hilo huenda linamaanisha Kabila anahusika na uasi," anasema.

Kurejea kwa Kabila kumezua utata na uongozi wa Kinshasa haujafurahia hatua hii.

Waziri wa mambo ya nje Thérèse Kayikwamba Wagner, alisema serikali ya Congo haihitaji mchango wa Kabila kutatua mzozo wa usalama katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Baada ya kurejea kwa Bw Kabila mjini Goma Kinga yake iliondolewa na Seneti na Mahakama imedumisha uamuzi wa Bunge hilo kumshtaki kwa uhaini na kushiriki katika vuguvugu la uasi.

Wale walio karibu na Joseph Kabila wamefafanua uhusiano wake na M23, kuwa ni wa nia ya kutafuta amani, lakini utawala wa Kinshasa unaonekana kukerwa na usuhuba wake na utawala wa waaasi wa Goma. Msemaji wa serikali Patrick Muyaya akimshutumu kwa kutaka kupigana vita.

Je, juhudi za kikanda 'changamoto' kwa ushirika wa Kabila na M23?

g

Chanzo cha picha, YOWERI MUSEVENI / X

Maelezo ya picha, Viongozi wa kikanda walilikutana Alhamisi wiki hii Uganda kujadili amani DRC na kulaani hatua ya M23 kuunda uawala sambamba na serikali ya Kinshasa katika maeneo waliyoyateka.

Kabila anaimarisha ushirika na M23/AFC, huku mataifa ya kikanda 12 Rwanda ikiwemo, yakiwa tayari yameshtumu hatua ya waasi hao kuunda "utawala sambamba" na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao kundi la waasi la M23 limeanzisha katika sehemu za nchi hiyo ambayo limeiteka mashariki.

Katika azimio la tatu, kama ilivyo katika tamko lenye maazimio 30, washiriki wa mkutano huo walilaani "unyakuzi wa ardhi na kuanzishwa kwa serikali sambamba na vuguvugu la M23/AFC kwa usaidizi wa usaidizi kutoka nje".

Mkutano wa kilele uliofanyika Uganda Alhamisi wiki hii, ulitoa wito wa kuheshimiwa "bila kuyumba" kwa uhuru wa nchi jirani, kutovumilia au kuunga mkono makundi yoyote yenye silaha, na kuheshimiwa kwa masuala halali na maslahi ya nchi jirani, "hasa kuhusu masuala ya usalama."

Nchi hizi hizi pia zilijitolea "kutohifadhi au kulinda watu wowote wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, vitendo vya mauaji ya halaiki au uhalifu wa uchochezi, au watu waliohukumiwa na Umoja wa Mataifa".

Wamelaani kundi la waasi la FDLR linalopigana dhidi ya serikali ya Rwanda inayoendesha harakati zake mashariki mwa DRC, na kutoa wito wa kuvunjwa, pamoja na kuvunjwa kwa "makundi mengine yote ya kigeni yenye silaha", ikiwa ni pamoja na RED Tabara, ambayo inapigana dhidi ya serikali ya Gitega inayofanya kazi nchini DRC, CODECO na ADF.

Unaweza pia kusoma:

Je, Joseph Kabila anakuja kuongoza muungano wa AFC-M23?

Wale walio karibu na Joseph Kabila wanasisitiza kuwa rais huyo wa zamani wa Congo hayuko Goma kuiongoza AFC-M23. Hata hivyo, Kikaya Bin Karubi, balozi na waziri wa zamani, na mshirika wa karibu wa rais huyo wa zamani, anatoa maelezo ya kina kuhusu uhusiano wake na waasi.

"Kama Rais Kabila alivyosema katika hotuba yake, yuko tayari kufanya kazi na mtu yeyote ambaye anaipenda sana DRC," alisema Karubi, akizungumza na Patient Ligodi wa Radio Internationale (RFI), kitengo cha Afrika.

Siku ya Jumatatu, vuguvugu la M23 lilisema limefurahishwa na kwamba Kabila, 53, amewasili Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

'Kosa alilolifanya Kabila'

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anasema, kurejea kwa Rais wa zamani Joseph Kabila nchini humo, katika eneo linalodhibitiwa na waasi wanaoipinga serikali ya M23, ni hatua kubwa inayoashiria vita vinavyoweza kudumu kwa muda mrefu au vinaweza kuwa kosa alilofanya Kabila.

Profesa Jason Stearns, mwanasayansi wa kisiasa wa Marekani katika Chuo Kikuu cha Simon Fraser nchini Canada, aliiambia BBC News kwamba mustakabali wa mzozo wa mashariki mwa DRC utaamuliwa na matokeo ya mazungumzo kati ya Rwanda na DRC, ambayo kwa sasa yanaongozwa na Marekani.

Inatarajiwa kuwa mwezi ujao pande zinazohusika na mzozo wa DRC zitakutana mjini Washington kutia saini makubaliano ya amani ya kumaliza vita.

"Iwapo mazungumzo hayo yatashindwa, ikiwa hakuna makubaliano yaliyofikiwa, nadhani kuwasili kwa Kabila kungekuwa muhimu na sehemu ya maafa ya muda mrefu," anasema Profesa Stearns.

Vuguvugu la M23, linaloongozwa zaidi na Watutsi wa Congo, linasema lilichukua silaha kutetea haki za watu wa Nyamucye na kwa sababu mamlaka za DRC zilipuuza ahadi zao chini ya makubaliano ya awali ya amani.

Profesa Stearns anasema iwapo mazungumzo kati ya Rwanda na DRC yataleta makubaliano ya amani, huenda Kabila akagundua kuwa alifanya makosa.

"Lakini iwapo Marekani itafanikisha mpango wake wa kulirudisha nyuma jeshi la Rwanda na M23, uamuzi wake unaweza kuonekana kuwa ni kosa kwasababu hatua yake ya uswahiba na waasi hao inakuja wakati ambapo serikali ya Marekani inajaribu kutafuta suluhu la kudumu la mgogoro huu na ikiwa RDF [Jeshi la Wanajeshi la Rwanda] litajiondoa, Kabila atapoteza nguvu nyingi," Stearns alisema.

Kinshasa, Umoja wa Mataifa na mataifa mengi ya Magharibi zinaishutumu Rwanda kwa kusaidia waasi wa M23 katika vita hivi mashariki mwa DRC, shutuma ambazo Rwanda inazikanusha.

g

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kabila (kushoto) na Tshisekedi katika hafla ya kuapishwa kwa Tshisekedi Januari 2019, baada ya uchaguzi kukosolewa kwa udanganyifu.

Stearns anasema ingawa Kabila bado hajatangaza rasmi kujiunga na M23, kwa kuhamia eneo la udhibiti "ameweka wazi kuwa anaimarisha mahusiano na kundi hilo na kuna vyanzo vingi [vya habari] vinavyoonyesha kuwa analisaidia kundi hilo".

Profesa huyo wa chuo kikuu aliongeza kuwa ziara yake huko Goma "ilithibitisha habari ambazo tumekuwa tukisikia kwa miezi kadhaa kwamba kulikuwa na aina fulani ya ushirikiano kati ya Kabila na vuguvugu la M23".

Stearns anasema kwamba kuwasili kwa Kabila ni "muhimu" kwa sababu M23 yenyewe "ni dhaifu kwa maana kwamba ina wafuasi wachache sana mbali na watu wachache sana [wanaounga mkono M23] mashariki mwa DRC".

Anasema ingawa M23 ina mrengo wa kisiasa unaojulikana kwa jina la AFC (Alliance Fleuve Congo), haijasaidia kupata idadi kubwa ya wafuasi kwasababu AFC "pia ni mrengo dhaifu wa kisiasa".

"Ni vigumu kusema wana wafuasi wengi ndani ya jamiii pana ya Wacongo," Stearns anasema.

Lakini anasema kwamba kuwasili kwa Kabila katika vuguvugu hili, ambalo limeiteka miji mingi ya mashariki na mji mkuu Bukavu wa jimbo la Kivu Kusini, kunaweza kubadili hilo kwasababu "Joseph Kabila ni mtu mwenye nguvu sana katika siasa nchini DRC".

"Sidhani kama kuna mtu angesema kuwa yeye ni maarufu sana...umaarufu wake ulikuwa wa asilimia 20 hadi alipoondoka madarakani lakini ni mwanasiasa mkubwa - asilimia 20 [katika jambo lolote] si chochote."

"Kwahiyo nadhani kwa kujiunga na kundi hili watapata uaminifu."

Stearns anaongeza kuwa Kabila pia anaweza kuunga mkono vuguvugu la M23 na kulifanya "lionekane kama kitu zaidi ya chombo cha Rwanda tu - [na] kuwa na uhuru zaidi".

Iwapo kujiunga kwa Bw Kabila na waasi wa mashariki mwa DRC kutaleta suluhu la mzozo unaoikumba DRC au la , ni suala la kusubiri.