Jinsi baadhi ya nchi za Afrika zinavyotegemea nishati kutoka Uturuki

.

Chanzo cha picha, KARPOWERSHIP

Maelezo ya picha, Meli ya Uturuki iliobeba nishati inayosambazwa barani Afrika

Zaidi ya watu milioni 100 barani Afrika wanakabiliwa na ukosefu wa nishati ya umeme huku tatizo la nishati likiendelea kuathiri mataifa tofauti ya bara hilo.

Mahitaji ya nishati yanapoongezeka, baadhi ya nchi zinageukia vyanzo vingine kama vile Kampuni ya Nishati ya Uturuki (Karpowership) - ambayo husambazia umeme nchini zinazoathirika

Kampuni hiyo yenye makao yake makuu mjini Istanbul, ina meli 40 zinazozalisha nishati, na inasambaza megawati 6,000 za umeme kwa nchi 14, zikiwemo Gambia, Ghana, Guinea-Bissau, Ivory Coast ,Msumbiji, Senegal na Sierra Leone.

Meli hizo hutumia dizeli na petroli, ambayo huwawezesha kusambaza nishati kwa ufanisi katika nchi hizi.

Meli zinazobeba kawi huegeshwa karibu na vituo vya umeme ambapo nyaya za usambazaji wa umeme katika vituo vya umeme huunganishwa n zile za meli hizo.

Ghana

Nchini Ghana, kwa mfano kampuni ya Karpowership imekuwa ikizalisha takriban robo ya nishati ya nchi hiyo kwa karibu muongo mmoja.

Taifa hilo limekuwa likikumbwa na hitilafu za umeme, zinazojulikana kama "dumsor".

Kampuni ya Umeme ya Ghana (ECG) inawadai wasambazaji umeme takriban dola bilioni 1.6, na kutolipwa kwa madeni haya kumesababisha kukatika kwa umeme kote nchini.

William Boateng, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ECG, anasema kampuni hiyo iliamua kukata umeme kwa sababu bunge la Ghana lilikataa kuheshimu mahitaji ya bili za umeme.

"Kukatwa kwa umeme kunaathiri kila mtu ambaye hatalipa na akishindwa kufanya anachopaswa kufanya, atakatiwa," Bw. Boateng aliambia shirika la habari la Reuters.

Karpowership inasema inaisaidia Ghana kutatua matatizo yake ya nishati.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Karpowership imekuwa ikizalisha robo ya nishati ya Ghana kwa karibu muongo mmoja.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Karpowership, Zeynep Harezi, aliiambia BBC kwamba "uwezo tulionao nchini Ghana umekuwa na matokeo chanya katika hali ya kijamii na kiuchumi ya wenyeji." .

"Kwa mfano, sekta ya uvuvi ya ndani, ambayo ilikumbwa na hitilafu ya umeme iliyowazuia kuvua samaki, ilinufaika pakubwa."

Hata hivyo, kukatika kwa umeme ni jambo la kawaida nchini Ghana, jambo ambalo serikali inajaribu kulikabili.

Ghana ina vyanzo muhimu vya nishati, ikiwa ni pamoja na mabwawa matatu ya kuzalisha umeme, ambayo yanachangia karibu theluthi moja ya umeme wake.

Pia ina rasilimali za mafuta na gesi, lakini bado hazitumiki.

Shirika la Umeme la Uturuki limesema linashirikiana na Shirika la Umeme la Ghana kubadilisha shughuli zake kuwa gesi asilia ili kupata gesi nchini humo.

Matumaini ni kwamba hii itatoa chanzo cha kuaminika cha umeme endelevu na wa bei nafuu.

Pia, kampuni hiyo inatumia bomba la urefu wa kilomita 11 kusafirisha gesi kutoka eneo la uchimbaji hadi kwenye kituo cha kuzalisha umeme, ambacho alisema kitaiingizia Ghana takriban dola milioni 20 kwa mwezi.

"Bomba hilo la kilomita 11 linaanzia Aboadze hadi kituo cha wanamaji cha Sekondi, ambako gesi hiyo inawaka kwa nguvu," alisema Bi Harezi.

Aliongeza: "Uendelezaji wa mabomba ya Ghana ni muhimu kwa mpito wa nishati yetu kuelekea gesi asilia ya nchi.

Tunatambua haja ya maendeleo ya muda mrefu ya miundombinu ya nje ya nchi na tutawasaidia wenzetu wakati wote.

Karpowership inasema kuwa matumizi ya gesi iliyosafishwa katika meli yake hutoa suluhisho kwa nishati nyingine za mafuta na husaidia kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni na kutoa vyanzo vya umeme na kukabiliana na suala la uhaba.

'Njia isio endelevu'

Hata hivyo, baadhi ya wataalam wa masuala ya nishati wameonya kuwa umeme unaaozalishwa na kampuni ya Karpowership sio suluhisho endelevu kwa sababu kukodi meli kunaweza kuwa ghali zaidi kuliko kituo cha kudumu cha umeme.

"Nchi za Afrika zimegeukia suluhisho hili kwa sababu linatoa suluhu la haraka na rahisi kwa tatizo la uhaba wa umeme," alisema Tony Tiyou, mtendaji mkuu wa kampuni ya nishati ya Green Renewables barani Afrika akizungumza na BBC.

"Lakini hatua hiyo haipaswi kuchukuliwa kuwa suluhu la matatizo ya nishati barani Afrika. Baada ya miaka mitano, suluhu itakuwa ghali zaidi kuliko suluhu ya kudumu. Tunachohitaji ni kwa nchi za Afrika kuwekeza katika aina tofauti za nishati, ikiwa ni pamoja na nishati mbadala - jua, upepo,na maji.

Karpowership, hata hivyo, inasema kuwa nishati inayotolewa ni ya bei rahisi zaidi.

“Ni afadhali kujenga kituo cha umeme ambacho kimedhibitiwa kabisa katika bandari yenye nguvu, kuliko kujenga kituo hicho katika nchi nyingi zinazoendelea,” alisema Bi Harezi.

Kushindwa kulipa bili za umeme

Licha ya athari za Karpowership nchini Ghana na nchi nyingine za Afrika, kampuni hiyo imelazimika kukata umeme kwa nchi nyingine kutokana na kutolipa.

Mwaka jana, Guinea-Bissau ilitumbukia gizani kwa takriban siku mbili baada ya Karpowership kukata umeme wakati nchi hiyo iliposhindwa kulipa bili za umeme za dola milioni 15.

Kukatika kwa umeme kuliathiri usambazaji wa maji ya kunywa, hospitali, na vyombo vya habari, huku kituo cha redio cha serikali Radio Nacional kikisimamisha matangazo yake.

Hata hivyo, Karpowership iliweza kurejesha nishati hiyo kwa taifa hilo baada ya serikali kulipa dola milioni sita.

Sierra Leone pia ilikumbwa na hitilafu ya umeme katika mji mkuu wa Freetown mwaka jana baada ya kampuni ya Karpowership kukata umeme kutokana na kutolipa deni la takriban dola milioni 40.

Waziri wa Nishati Isuf Baldé alisema kuna haja ya kujadili upya kandarasi ambayo nchi ina nayo na Karpowership kwa sababu bei ya kampuni hiyo imekaribia kuongezeka maradufu tangu kuanza kwa usambazaji huo.

Karpowership inasema kuwa inaendelea kujitolea kutoa nishati kwa nchi za Afrika, wakati bara hilo likiendelea kuwa moja ya soko kuu.

"Tumetia saini mikataba na mamlaka nchini Gabon ya kutoa megawati 150 za umeme kwa nchi," alisema Bi Herezi.

"Tunaamini kwamba tunaweza kusaidia Afrika katika mpito wake wa nishati na kupanua upatikanaji wa umeme kwa watu wa bara hili."

Imetafsiriwa na Seif Abdalla