Mzozo wa DRC: Mamia ya watu wamekamatwa na M23 katika uvamizi uliozua utata
Vuguvugu la AFC/M23 Katika mji wa Goma na vitongoji vyake , limekuwa likifanya uvamizi na na kuwakamata kwa siku kadhaa likidai kuwa watu hao wanahusika na mauaji, uporaji na utekaji nyara.
Muhtasari
- Tazama sura muhimu kwenye zulia jekundu wakati wa Tamasha la Filamu la Cannes
- Kaunti ya Nairobi yafunga kanisa la Freemason kutokana na deni la mamilioni ya pesa
- Watawala wa kijeshi nchini Mali wafuta vyama vyote vya kisiasa
- Charles Hilary: Mtangazaji nguli wa zamani wa BBC azikwa leo
- Ronaldo 'anajivunia' kuwa na mtoto wa kiume baada ya mechi ya kwanza ya Ureno
- Goma: Mamia ya watu wamekamatwa na M23 katika uvamizi uliozua utata
- 'Wazungu wa Afrika Kusini wanaokwenda Marekani ni waoga' - Ramaphosa
- Ujerumani yamkamata aliyejitangaza 'mfalme' na kupiga marufuku kundi lake lenye msimamo mkali
- Msaidizi wa Biden ajibu kitabu kinachodai walificha "kudhoofika kimwili" kwa rais wa zamani
- Familia za waathiriwa wa ajali ya ndege zawasilisha malalamiko
- Sokwe warekodiwa wakitumia dawa za mitishamba 'kujitibu'
- Trump atarajia kukutana na kiongozi wa Syria baada ya kutangaza kuwa ataondoa vikwazo
- José Mujica wa Uruguay, 'rais masikini zaidi duniani, afariki
- Zelensky aahidi 'kufanya kila kinachowezekana' kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Putin
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Tazama sura muhimu kwenye zulia jekundu wakati wa Tamasha la Filamu la Cannes
Maelezo ya video, Tazama sura muhimu kwenye zulia jekundu wakati wa Tamasha la Cannes Watu mashuhuri walijitokeza kusini mwa Ufaransa huku Tamasha la 78 la Filamu la Cannes likianza Jumanne jioni.
Kuanzia Quentin Tarantino hadi Eva Longoria na Bella Hadid - hapa kuna sura muhimu kwenye zulia jekundu nyekundu usiku wa ufunguzi.
Kaunti ya Nairobi yafunga kanisa la Freemason kutokana na deni la mamilioni ya pesa
Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Kaunti ya Nairobi imefunga Jumba la Grand Lodge linalotumika kama Ukumbi wa ibada kwa wa waumini wa Freemasons wa Afrika Mashariki lililopo katikati mwa jiji kutokana na na malimbikizo ya deni la ardhi kiasi cha Shilingi milioni 19 za Kenya
Operesheni ya utekelezaji hiyo iliyoongozwa na afisa wa Afya Suzanne Silantoi, Afisa Mkuu ofisi ya Gavana Priscilla Mahinda na Afisa Mkuu wa Makazi Lydia Mathia, ni sehemu ya kampeni pana ya kaunti inayolenga wale wanaokiuka viwango vya mapato katika mji mkuu.
"Jumba hili lina deni la zaidi ya shilingi milioni 19 katika kaunti ya Nairobi," alisema Silantoi.
Kulingana na maafisa wa kaunti, Ukumbi wa Freemasons umefungwa kufuatia taratibu zinazofaa, ikiwa ni pamoja na utoaji wa nyaraka za mahitaji na maonyo ya umma.
"Kabla ya hatua zozote kuchukuliwa, tunatoa notisi za mahitaji na kuzichapisha katika magazeti ya kila siku yanayowaagiza wamiliki wa ardhi kulipa viwango vilivyobaki," Silantoi alielezea. "Kukosa kutii kunatupa mamlaka ya kisheria ya kubana."
Afisa Mkuu Lydia Mathia alibainisha kuwa ingawa utekelezaji huo unaweza kuwasumbua wapangaji, sheria inaruhusu kaunti kukatiza huduma kwa wamiliki wa mali wasiofuata sheria.
Unaweza pia kusoma:
Wizara ya Afya ya Palestina: Mashambulio ya anga ya Israel yaua makumi ya watu kaskazini mwa Gaza
Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya Afya huko Gaza imesema kuwa idadi ya watu walioaga dunia wanaowasili hospitalini tangu alfajiri ya kuamkia leo imefikia watu 70, kufuatia mashambulizi ya anga yanayoendelea ya Israel kwenye Ukanda huo. Makumi wengine wamejeruhiwa.
Hospitali ya Indonesia iliripoti kuwa watoto 22 na wanawake 15 ni miongoni mwa waliofariki baada ya nyumba kadhaa kushambuliwa kwa mabomu huko Jabalia na kambi yake.
Wizara hiyo ilisema kuwa idadi ya kandhaa ya waathiriwa bado wako chini ya vifusi na mitaani, na kwamba ambulensi na wafanyikazi wa ulinzi wa raia hawawezi kuwafikia.
Mashambulizi hayo yametokea siku moja baada ya shambulizi la anga la Israel kulenga kile ambacho jeshi lilielezea kuwa ni ngome ya chini ya ardhini ya Hamas huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza na kuwaua makumi ya watu.
Watawala wa kijeshi nchini Mali wafuta vyama vyote vya kisiasa
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Vyama vya siasa vimekuwa vikiitaka nchi hiyo kurejea katika utawala wa kidemokrasia Kikosi cha kijeshi cha Mali kimevifuta vyama vyote vya kisiasa nchini humo huku kukiwa na msako mkali dhidi ya wapinzani tangu jeshi kunyakua mamlaka.
"Mikutano yote ya wanachama wa vyama vya siasa na mashirika yenye tabia ya kisiasa inavunjwa katika eneo la kitaifa," taarifa iliyosomwa kwenye TV ya serikali Jumanne ilisema.
Uamuzi huo ulithibitishwa na kiongozi wa kijeshi Assimi Goïta, ambaye alichukua mamlaka baada ya mapinduzi mwaka 2020 na 2021 na anatazamiwa kusalia madarakani kwa angalau miaka mingine mitano licha ya kuahidi kufanya uchaguzi.
Hatua hiyo inatarajiwa kuibua upinzani mpya kwa vyama vya siasa ambavyo vimekuwa vikidai nchi hiyo irejee kwenye utawala wa kidemokrasia.
Tangu mwaka jana, mamlaka ya kijeshi yamezidisha ukandamizaji wa shughuli za kisiasa.
Wiki iliyopita, kufuatia maandamano nadra ya kuunga mkono demokrasia, viongozi wawili wa upinzani walitekwa nyara na watu waliokuwa na silaha wakisema walikuwa maafisa wa polisi. Mamlaka haijatoa maoni yoyote kuhusu kukamatwa kwa taarifa hizo.
Unaweza pia kusoma:
Charles Hilary: Mtangazaji nguli wa zamani wa BBC azikwa leo
Chanzo cha picha, Ikulu/ Zanzibar
Mtangazaji wa zamani wa BBC Idhaa ya Kiswahili, Charles Hilary anatarajiwa amezikwa leo Jumatano kwao Zanzibar baada ya kufariki Jamapili.
Awali shughuli ya kuuaga mwili wake imefanyika Zanzibar na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar, waandishi mbali mbali wa habari pamoja na jamaa na marafiki waliomfahamu.
Wengi waliotoa rambirambi zao wamemsifu marehemu Charls Hillary kwa kuipenda kazi yake, ucheshi na upendo kwa watu.
Mhariri wa zamani wa Idhaa ya kiswahili ya BBC Tido Mhando, akitoa salamu za rambirambi za wafanyakazi wa BBC wa sasa na wa zamani alisema: ‘’Charles kwangu alikuwa ni mtu wa watu, mtu wa kuheshimu watu, mcheshi lakini mpendawatu sana’’.
Bwana Mhando aliongeza kuwa: ’’Kuwepo kwa Charles katika BBC kuliweza kujenga Idhaa na ndio maana wafanyakazi wa BBC wamenituma nije hapa na hasa kwa familia na serikali kutoa shukrani zao kwa huduma waliyoipata kutoka kwa Charles na kwamba wanajiandaa muda utakapofika weweze kutoa rambirambi zao kwa familia... kwa hiyo kwa niaba ya wenzangu, nashukuru sana kipindi kirefu cha maisha ya Charles.’’
Hilary ambaye alijizolea umaarufu Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa kazi yake ya utangazaji alifikwa na umauti akiwa ni Mkurugenzi wa idara ya mawasiliano Ikulu ya Zanzibar na msemaji mkuu wa serikali ya Zanzibar.
Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa kifo chake kilitokea katika hospitali ya Mloganzila jijini Dar Es Salaam. Taarifa kutoka kwenye familia ilieleza kuwa alikimbizwa katika hospitali hiyo baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake.
Maelezo ya picha, Michuano ya Kombe la mataifa ya Afrika nchini Equatoril Guinea, Charles Hilary anajadiliana na wachambuzi wa kandanda wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC mwaka 2015 Hilary alijiunga na BBC mwaka 2006 na kuwa sehemu muhimu ya timu ya watangazaji wa habari na pia kipindi cha Ulimwengu wa Soka kinachorusha matangazo ya mpira wa Ligi Kuu ya England kila wikendi. Alikuwa pia sehemu ya watangazaji wa awali wa matangazo ya televisheni ya Dira TV mwaka 2012. Mwaka 2015 aliondoka BBC baada ya kuhudumu kwa miaka tisa na kurejea nyumbani Tanzania.
Safari yake ya utangazaji ilianza mwanzoni mwa miaka ya 1980 akiwa na Radio Tanzania Dar Es Salaam (RTD) sasa TBC na akaibuka kuwa moja ya sauti za dhahabu katika matangazo mubashara ya mpira wa miguu wa zama zake. Mwaka 1994 alikuwa moja ya watangazaji waandamizi walioanzisha stesheni ya Radio One Sterio jijini Dar Es Salaam na akiwa hapo akapata jina lake maarufu la ‘Mzee wa Charanga’ kutokana na umaarufu wa kipindi cha muziki wa charanga ambacho alikuwa akitangaza.
Aliondoka Radio One na kujiunga na Idhaa ya Kiswahili ya DW nchini Ujerumani mwaka 2003, na alijiunga na BBC akitokea huko.
Aliporudi Tanzania alijiunga na Azam TV mwaka 2015 mpaka alipoteuliwa kuwa msemaji wa Ikulu ya Zanzibar mwaka 2021.
Ronaldo 'anajivunia' kuwa na mtoto wa kiume baada ya mechi ya kwanza ya Ureno
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Ronaldo Jr alicheza jezi namba saba ambayo baba yake amekuwa akiitumia katika maisha yake yote ya soka Cristiano Ronaldo amesema "anajivunia sana" mtoto wake mkubwa baada ya kucheza kwa mara ya kwanza katika timu ya Ureno ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 15.
Cristiano Ronaldo Jr aliingia dakika ya 54 katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Japan katika mchuano wa Croatia siku ya Jumanne.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 14 alitazamwa na nyanya/bibi yake Dolores Aveiro, mama yake Ronaldo Sr.
Iliripotiwa kwamba mawakala kutoka Manchester United klabu ya zamani ya Ronaldo Sr na vilabu vingine kadhaa vya juu vya Ulaya walihudhuria kumtazama Ronaldo Jr.
Akiwa mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or Baba yake Ronaldo alisema kwenye Instagram: "Hongera kwa mara ya kwanza kwa Ureno, mwanangu. Ninajivunia sana [ Mimi baba yako]."
Ronaldo Jr yuko Al-Nassr nchini Saudi Arabia na baba yake, ambaye alisajiliwa na klabu ya Pro League mnamo 2022.
Unaweza pia kusoma:
Goma: Mamia ya watu wamekamatwa na M23 katika uvamizi uliozua utata
Chanzo cha picha, Mitandao ya kijamii
Maelezo ya picha, Wapiganaji wa M23 wawazingira watu waliokamatwa katika msako unaoendelea kuwasaka wahalifu, wanajeshi na wapiganaji wenye silaha. Vuguvugu la AFC/M23 Katika mji wa Goma na vitongoji vyake , limekuwa likifanya uvamizi na na kuwakamata kwa siku kadhaa likidai kuwa watu hao wanahusika na mauaji, uporaji na utekaji nyara.
Wasiounga mkono kundi la M23 wanasema kuwa linawateka nyara na kujaribu kuwaajiri vijana kwa nguvu katika safu zake.
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Wapiganaji wa M23 Mwishoni mwa juma meya wa jiji la Goma Julien Katembo aliwaambia waandishi wa habari kuwa watu waliowakamata ni pamoja na "Askari wa FARDC, FDLR, Wazalendo na wahalifu wengine".
Msako wa kuwasaka na kuwakamata washukiwa uliendelea siku ya Jumatatu na Jumanne, hasa katika maeneo ya kaskazini mwa mji wa Goma, ambako vitendo vya mauaji , uporaji na utekaji nyara vimeripotiwa kwa muda.
Katika wiki chache zilizopita, zaidi ya mauaji 10 yameripotiwa katika jiji la Goma.
Unaweza pia kusoma:
‘Wazungu wa Afrika Kusini wanaokwenda Marekani ni waoga’ - Ramaphosa
Chanzo cha picha, Reuters
Rais Cyril Ramaphosa ameita kundi la Wazungu wa Afrika Kusini 59 ambao wamehamia Marekani kuwa ni "waoga", akisema "watarudi hivi karibuni".
Kundi hilo liliwasili Marekani siku ya Jumatatu baada ya Rais Donald Trump kuwapa hadhi ya ukimbizi, akisema wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi.
Lakini Ramaphosa alisema wale wanaotaka kuondoka hawakufurahishwa na juhudi za kushughulikia ukosefu wa usawa wa utawala wa kibaguzi uliopita, akitaja hatua ya kuhama kuwa "wakati wa huzuni kwao".
"Kama Waafrika Kusini, sisi ni wastahimilivu. Hatukimbii matatizo yetu. Ni lazima tukae hapa na kuyatatua. Unapokimbia wewe ni mwoga, na hicho ni kitendo cha kioga kweli," aliongeza.
Trump na mshirika wake wa karibu, Elon Musk mzaliwa wa Afrika Kusini, wamesema kulikuwa na "mauaji ya halaiki" ya wakulima wa kizungu nchini Afrika Kusini - madai ambayo yamepuuzwa.
Marekani pia imeishutumu serikali ya Afrika Kusini kwa kunyakua ardhi kutoka kwa wakulima wazungu bila kulipa fidia.
Zaidi ya miaka 30 baada ya kumalizika kwa miongo kadhaa ya utawala wa wazungu wachache wa Afrika Kusini, wakulima weusi wanamiliki sehemu ndogo tu ya mashamba bora ya nchi hiyo, huku mengi yakiwa bado mikononi mwa wazungu, na kusababisha hasira kutokana na kasi ndogo ya mabadiliko.
Mnamo mwezi Januari Rais Ramaphosa alitia saini sheria yenye utata inayoruhusu serikali kutwaa ardhi inayomilikiwa na watu binafsi bila kulipwa fidia katika hali fulani, wakati inachukuliwa kuwa "sawa na kwa maslahi ya umma".
Soma zaidi:
Ujerumani yamkamata aliyejitangaza 'mfalme' na kupiga marufuku kundi lake lenye msimamo mkali
Aliyejitangaza "mfalme" wa Ujerumani na "watawala" wake watatu wamekamatwa na kundi lao kupigwa marufuku kwa kujaribu kupindua serikali.
Peter Fitzek, 59, alikuwa miongoni mwa wale waliokamatwa katika uvamizi wa asubuhi kwenye majimbo saba siku ya Jumanne, ambayo yalihusisha takriban maafisa 800 wa usalama.
Serikali ilipiga marufuku kikundi chao, Reichsbürger, au "raia wa Reich", ambao wanataka kuanzisha Königreich Deutschland, au "Ufalme wa Ujerumani".
Alexander Dobrindt, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, alilishutumu kundi hilo kwa kujaribu "kudhoofisha utawala wa sheria" kwa kuunda taifa mbadala na kueneza "simulizi ya chuki dhidi ya Wayahudi ili kuunga mkono madai yao ya mamlaka".
Msaidizi wa Biden ajibu kitabu kinachodai walificha "kudhoofika kimwili" kwa rais wa zamani
Chanzo cha picha, Getty Images
Msaidizi wa Joe Biden amejibu kitabu kipya ambacho kinashutumu wandani wake katika Ikulu kwa kuficha "kudhoofika kimwili" kwa rais wa zamani wa Marekani wakati wa kampeni yake ya kugombea kuchaguliwa tena.
Kulingana na kitabu, Original Sin, hali ya Biden wakati wa kugombea urais mwaka 2024 ilisemekana kuwa mbaya sana hivi kwamba wasaidizi walijadili kumweka kwenye kiti cha magurudumu.
Msemaji wa Biden, 82, alisema "ushahidi wa kuzeeka sio ushahidi wa kutokuwa sawa kiuwezo wa kiakili" na akasisitiza kwamba amekuwa "rais mzuri sana".
Kitabu hicho, cha Jake Tapper wa CNN na Alex Thompson wa Axios, kinatarajiwa kutolewa tarehe 20 Mei.
Biden alisitisha ghafla kampeni yake ya kuchaguliwa tena Julai iliyopita muda mfupi baada ya utendaji wake mbaya kwenye mjadala dhidi ya Donald Trump, wa Republican.
Wadau wa mambo ya ndani ya chama walimlaumu kwa kuondoka kwenye kinyang'anyiro hicho akiwa amechelewa, na kumwacha mbadala wake, Makamu wa Rais Kamala Harris, na siku 107 kushindana na Trump, ambaye aliibuka ushindi.
Kabla ya kutolewa kwa kitabu hicho, Biden wiki jana alitoa mahojiano yake ya kwanza tangu kuondoka Ikulu ya White House kwa BBC , akisema: "Sidhani ingekuwa muhimu" ikiwa ningeondoka kwenye kinyang'anyiro mapema.
Soma zaidi:
Familia za waathiriwa wa ajali ya ndege zawasilisha malalamiko dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Jeju Air
Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya familia za waliofariki katika ajali ya ndege ya Jeju Air mwezi Disemba mwaka jana wamewasilisha malalamishi ya uhalifu dhidi ya watu 15, akiwemo waziri wa uchukuzi wa Korea Kusini na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa shirika hilo la ndege kwa uzembe wa kikazi.
Ndugu za watu 72 walioaga dunia wanataka uchunguzi wa kina zaidi ufanyike kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 179 kati ya 181 waliokuwa ndani ya ndege hiyo na kuifanya kuwa ajali mbaya zaidi ya ndege nchini Korea Kusini.
Ajali hiyo "haikuwa ya kawaida tu", wanadai, lakini "janga kubwa la raia lililosababishwa na usimamizi mbaya wa hatari zinazoweza kuzuilika".
Takriban miezi mitano sasa, mamlaka bado inachunguza kile ambacho huenda kilisababisha ndege hiyo kuanguka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan na kisha kuwaka moto.
Soma zaidi:
Sokwe warekodiwa wakitumia dawa za mitishamba 'kujitibu'
Chanzo cha picha, Elodie Freymann
Sokwe nchini Uganda wameonekana wakitumia dawa za mitishamba - kwa njia nyingi - kutibu majeraha ya wazi na mengineo.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Oxford, wakishirikiana na timu ya wenyeji katika Msitu wa Budongo, walipiga picha na kurekodi matukio ya wanyama hao wakitumia mitishamba kujipatia huduma ya kwanza, wao wenyewe na mara kwa mara kwa kila mmoja wao.
Utafiti wao unatokana na ugunduzi wa mwaka jana kwamba sokwe hutafuta na kula mimea fulani ili kujitibu.
Wanasayansi pia walikusanya miongo kadhaa ya uchunguzi wa kisayansi ili kutengeneza orodha ya njia tofauti ambazo sokwe hutumia " dawa za mitishamba kujitibu".
Watafiti wanasema utafiti huo, ambao umechapishwa katika jarida la Frontiers in Ecology and Evolution, unaongeza ushahidi kuwa jamii ya sokwe inayojumuisha nyani, orangutangu, tumbili na wengineo hutumia dawa za asili kwa njia tofauti ili kuwa na afya nzuri msituni.
Pia unaweza kusoma:
Trump atarajia kukutana na kiongozi wa Syria baada ya kutangaza kuwa ataondoa vikwazo
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa ataondoa vikwazo dhidi ya Syria, kabla ya mkutano unaotarajiwa na kiongozi wake Ahmed al-Sharaa.
Trump amekubali "kukutana" na rais wa mpito wa Syria siku ya Jumatano nchini Saudi Arabia kama sehemu ya ziara yake ya Mashariki ya Kati, Ikulu ya White House ilisema.
Tangazo la kuondolewa kwa vikwazo hivyo lilipokelewa kwa shangwe katika mji mkuu wa Syria wa Damascus, ambapo nderemo, dansi na milio ya risasi ya kusherehekea ilisikika.
Vikwazo hivyo hapo awali vilizuia ufadhili wowote wa kigeni, ikiwa ni pamoja na msaada kufika Syria na awali vilikusudiwa kuweka shinikizo kwa udikteta wa Rais aliyeondolewa madarakani Bashar al-Assad.
Trump alisema mabadiliko ya sera yataipa Syria "nafasi ya ukuu", akiambia kongamano la uwekezaji huko Riyadh ya Saudi Arabia, "ni wakati wao wa kung'aa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Asaad al-Shaibani alisherehekea uamuzi huo kama " mabadiliko muhimu kwa nchi" katika mahojiano na shirika la habari la nchi hiyo, Sana.
Nchi inatazamia mustakabali wa "utulivu, kujitosheleza na ujenzi wa kweli baada ya miaka mingi ya vita haribifu", aliongeza.
Asilimia 90 ya wakazi wa Syria waliachwa chini ya kiwango cha umaskini mwishoni mwa utawala wa Assad na serikali yake mpya imekuwa ikishinikiza kuondolewa kwa vikwazo tangu Assad alipopinduliwa mwezi Disemba.
Soma zaidi:
José Mujica wa Uruguay, 'rais masikini zaidi duniani', afariki
Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Rais wa zamani wa Uruguay José Mujica, anayejulikana kama "Pepe", amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89.
Mpiganaji huyo wa zamani ambaye alitawala Uruguay kuanzia 2010 hadi 2015 alijulikana kama "rais maskini zaidi" kwa sababu ya maisha yake ya kawaida.
Rais wa sasa Yamandu Orsi alitangaza kifo cha mtangulizi wake kwenye jukwaa la X: "asante kwa kila kitu ulichotupa na kwa upendo wako mkubwa kwa watu wako."
Chanzo cha kifo cha mwanasiasa huyo hakijajulikana lakini alikuwa akiugua saratani ya umio.
Kwa sababu ya alivyoishi kwa namna ya kawaida tu kama rais, ukosoaji wake wa ulaji na mageuzi ya kijamii aliyoyakuza - ambayo, pamoja na mambo mengine, yalimaanisha Uruguay kuwa nchi ya kwanza kuhalalisha matumizi ya bangi kama burudani - Mujica alikua mwanasiasa mashuhuri Amerika ya Kusini na kwingineko.
Umaarufu wake duniani si wa kawaida ukizingatia ni nchi yenye wakazi milioni 3.4 pekee.
Ukweli ni kwamba, ingawa wengi walimuona Mujica kama mtu nje ya tabaka la kisiasa, haikuwa hivyo.
Alisema mapenzi yake kwa siasa, pamoja na vitabu na kufanya kazi, alirithi kutoka kwa mama yake, ambaye alimlea katika makazi ya watu wa tabaka la kati huko Montevideo.
Akiwa kijana, Mujica alikuwa mwanachama wa Chama cha Kitaifa, mojawapo ya vyama vya jadi vya kisiasa nchini Uruguay, ambavyo baadaye vilikuja kuwa upinzani wa mrengo wa kati kwa serikali yake.
Mujica aliwahi kutekwa mara nne na katika mojawapo ya matukio hayo, mwaka wa 1970, alipigwa risasi sita na kukaribia kufa.
Zelensky aahidi 'kufanya kila kinachowezekana' kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Putin
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema atasafiri hadi mji mkuu wa Uturuki Ankara kukutana na rais Recep Tayyip Erdogan na atapatikana kwa mazungumzo ya moja kwa moja na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mjini Istanbul siku ya Alhamisi.
"Tutafanya kila kinachowezekana' kuhakikisha kuwa mkutano huu unafanyika," aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliopangwa kwa haraka huko Kyiv.
Urusi bado haijasema ni nani atakayesafiri kwa ndege hadi Istanbul, ila tu kwamba ingetangazwa "mara tu [Putin] atakapoona inafaa". Putin na Zelensky wenyewe hawajakutana tangu Desemba 2019.
Mazungumzo ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili mara ya mwisho yalifanyika Istanbul, Machi 2022, katika wiki za mwanzo za uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Hapo awali Putin alikuwa ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya moja kwa moja huko Uturuki "bila masharti ya awali", kabla ya Zelensky kutangaza kwamba angeenda yeye binafsi na kutarajia rais wa Urusi pia kusafiri.
Marekani pia inatarajiwa kutuma ujumbe wa ngazi ya juu.
Urusi tayari imeonya kwamba kutoa shinikizo kwa nchi yake "hakuna maana" na haikutoa kauli yake ya mwisho.
Badala yake, imetaka kuangazia suluhu la muda mrefu ambalo linashughulikia kile Urusi inachokiona kama "sababu kuu" za vita - masharti magumu yaliyotangazwa kabla ya uvamizi wa 2022 na kukataliwa mara kwa mara na Ukraine.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 14/05/2025.