Wahouthi: Je, waasi wa Yemen wana nguvu kiasi gani?

Chanzo cha picha, REUTERS
- Author, Frank Gardner
- Nafasi, BBC
Wahouthi wanaendelea kuwashangaza wanajeshi wenye nguvu zaidi duniani. Bado wanarusha makombora kwenye meli yoyote ya kimataifa wanayozingatia kuwa ina uhusiano na Marekani, Uingereza au Israel.
Mashambulizi yao yamekuwa na athari kubwa kwa biashara ya kimataifa, na kulazimisha meli kuzunguka maelfu ya maili.
Wanaonekana kutotishika na mashambulizi ya mara kwa mara ya anga yanayoongozwa na Marekani kwenye vituo vyao vya makombora na wameapa kulipiza kisasi dhidi ya rasilimali za Marekani na Uingereza.
Wahouthi ni nani?
Wahouthi wanatokana na jamii ya wachache kutoka eneo la milimani kaskazini-magharibi mwa Yemen.
Jina lao linatokana na mwanzilishi wa vuguvugu hilo, Hussein Al-Houthi. Walipigana vita kadhaa dhidi ya mtawala mwenye nguvu wa Yemen, Ali Abdullah Saleh, mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Baada ya mtawala huyo kuondolewa madarakani kwa maandamano ya Arab Spring, waliteka mji mkuu, Sana'a, na kunyakua madaraka mwaka 2014.
Saleh aliingia vitani na Houthis, lakini kisha wakamuua mara moja.
Tangu Houthi wachukue mamlaka, Yemen, taifa maskini zaidi la Kiarabu, limesambaratishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha maafa.
Takribani watu 150,000 wameuawa, mamilioni wanaishi kwa kutegemea msaada wa chakula. Kwa muda wa miaka saba Wahouthi walinusurika kampeni ya kuwaondoa madarakani, ilioongozwa na Saudi Arabia.
Kwanini wanashambulia meli?
Kuanzia katikati ya Novemba 2023 na kuendelea, Wahouthi wametumia makombora na ndege zisizo na rubani kulenga meli zinazopita bahari ya shamu.
Lengo lao ni kushambulia meli yoyote yenye uhusiano na Israel, kuonyesha kuunga mkono kwao Hamas, wakiahidi kuendeleza mashambulizi yao hadi Israel itakapomaliza mashambulio yake Gaza.
Wahouthi - ambao wengi wao wanafuata madhehebu ya Zaid ya Uislamu wa Shia katika Yemen yenye Wasunni wengi - wanawakilisha 15% tu ya Wayemen lakini wanajiona kuwa watawala halali.
Kwa muda mrefu kumekuwa na juhudi za pamoja, zikiongozwa na Umoja wa Mataifa, kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Yemen.
Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Yemen, 2015-2017, Edmund Fitton-Brown anaelezea uzoefu wake na Wahouthi wakati wa vikao vya mapatano.
"Ilikuwa changamoto kubwa. Walikuwa wakaidi, wenye uhasama, wenye hasira, wenye tabia ya kufoka, kuchelewa kufika na kususia. Walisisitiza wapewe mapokezi ya heshima na kuwepo na mirungi. Wakati wa mazungumzo ya amani walikuwa wakiwachanganya wenyeji wa mapatano nchi ya Kuwait."
Tangu waasi wa Houthi waanze mashambulizi dhidi ya meli, na Marekani na Uingereza kujibu mashambulizi kwa kushambulia vituo vyao vya makombora, kumekuwa na maandamano makubwa yaliyoidhinishwa na serikali dhidi ya nchi hizo katika mji mkuu.
Nguvu za Wahouthi

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
"Kwa kupinga kile ambacho wakaazi wengi wa kaskazini mwa Yemen wanakiona kama vikosi vya kigeni, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, na kukabiliana moja kwa moja na Israel kwa kuunga mkono Gaza," anasema mtaalamu wa Mashariki, Mohammed Al-Basha, "Wahouthi wamepata umaarufu."
Anasema, Yemen ya sasa inasalia kuwa taifa lililogawanyika, na upinzani wa kimaslahi dhidi ya Houthi uko kaskazini-mashariki mwa Yemen, Maarib, Taiz na majimbo ya kusini. Inaonekana kuna uwezekano kuwa Houthi wanaweza kuibuka washindi ikiwa kutakuwa na "uchaguzi huru na wa haki".
Kuhusu maandamano, Fitton-Brown anasema. "Huitisha maandamano, huifanya siku ya mapumziko ya kazi, wanaweka wazi kwamba unatarajiwa kuhudhuria. Wafanyakazi wao wengi waliajiriwa kwa sababu hawakuwa na kazi na walikuwa na hamu ya kupata mshahara. Katika maeneo yaliyo nje ya udhibiti wao wanachukiwa."
Wahouthi wanaonekana kuwa na droni zisizoisha na silaha nyingine za kushambulia meli, nyingi zikiwa zinatolewa na Iran na zinaingizwa kimagendo kwa boti ndogo au kuvuka mpaka.
Mvutano huu utaishaje?

Chanzo cha picha, REUTERS
Fitton-Brown anasema, "ikiwa usitishaji vita utafanyika huko Gaza, wanaweza kuchukua fursa hiyo na kutangaza ushindi, wakidai wamefikia malengo yao. Iwapo Iran itakuwa na wasiwasi kwamba vitendo vya Houthi vinaiweka Jamhuri ya Kiislamu hatarini, ina ushawishi wa kutosha kuwafanya Wahouthi kubadili mwelekeo."
Waasi wa Houthi bado wako imara licha ya kampeni za kijeshi na maeneo yao kurushiwa makombora kuharibiwa na mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Marekani.
Ni wazi kuwa wana makombora mengi, na dalili ni kwamba wanatafuta kuongeza hatari kwa mashambulizi ya makombora ya kutoka ardhini hadi angani kwa nia ya kuiangusha ndege ya kivita ya magharibi.
Kusini mwa Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden itasalia kuwa sehemu hatari kwa siku zijazo.