Wahouthi ni nani na kwa nini wanashambulia meli zinazopita Bahari ya Shamu?

w

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waasi wa Houthi wamekuwa jeshi lenye nguvu nchini Yemen.

Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na roketi kwenye meli za mizigo katika Bahari ya Shamu sasa yamesababisha vikosi vinavyoongozwa na Marekani na Uingereza kufanya mashambulizi ya anga katika maeneo yaliyolenga eneo hilo.

Vikosi vya Magharibi vilichukua hatua baada ya meli kushambuliwa na Wahouthi - kundi la waasi linaloungwa mkono na Iran ambalo linadhibiti sehemu kubwa ya Yemen.

Kwanini Wahouthi wanailenga Israel?

Mashambulizi hayo yalianza baada ya kuanza kwa vita vya Israel na Hamas tarehe 7 Oktoba.

Wahouthi walitangaza kuunga mkono Hamas na kusema wangelenga meli yoyote itakayosafiri kuelekea Israel. Haijulikani wazi kwamba meli zote zilizoshambuliwa zilikuwa zikielekea huko.

Mnamo Novemba walikamata kile walichosema kuwa meli ya shehena ya Israeli .

Tangu wakati huo wameshambulia meli kadhaa za kibiashara na drones na makombora ya balestiki.

Kampuni kubwa za usafirishaji zikiwemo Kampuni ya Mediterania, Maersk, Hapag-Lloyd na kampuni ya mafuta ya BP zote zimesema zinaelekeza meli mbali na Bahari ya Shamu.

Washington imeishutumu Iran kwa "kuhusika kwa kina" katika kupanga operesheni dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nya Shamu.

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waasi wa Houthi walitoa picha zinazoonyesha wapiganaji wao wakiiteka nyara meli katika Bahari Nyekundu tarehe 2 Novemba

Novemba 2023, waasi wa Houthi waliiteka meli ya mizigo ambayo walisema ni ya Israel katika Bahari ya Shamu na kuipeleka katika eneo la pwani ya Yemen.

Israel ilisema meli hiyo haikuwa yake na hakuna Waisraeli miongoni mwa wafanyakazi wake, lakini ripoti ambazo hazijathibitishwa zilisema mmiliki wa meli hiyo anaweza kuwa ni Muisraeli.

Tangu tarehe 3 Disemba, Wahouthi wameshambulia meli kadhaa za kibiashara katika Bahari Nyekundu kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora ya yaliyorushwa kutoka pwani ya Yemen, wanayoikalia.

Meli za kivita za Marekani, Uingereza na Ufaransa zimenasa mengi ya makombora hayo, lakini meli kadhaa zimeshambuliwa.

Kampuni ya Mediterranean Shipping, kampuni kubwa zaidi ya usafirishaji duniani, ilisema inaelekeza meli zake kutotumia Bahari Nyekundu. Kampuni ya Ufaransa CMA, kampuni ya Denmark ya Maersk, Hapag-Lloyd ya Ujerumani na kampuni ya mafuta ya BP pia walifanya hivyo.

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani ilisema: "Mashambulizi haya yaliyoanzishwa na Houthis huko Yemen, yanawezeshwa kikamilifu na Iran."

Marekani imependekeza uwepo wa kikosi cha kimataifa cha wanamaji ili kulinda meli za kibiashara dhidi ya mashambulizi zaidi ya Houthi.

Houthi ni nani na lengo lao ni lipi?

Wahouthi ni kundi lenye silaha nchini Yemen la Waislamu wachache wa Kishia nchini humo, Zaidis.

Kundi hilo liliundwa katika miaka ya 1990 ili kupambana na kile walichokiona kuwa ufisadi wa rais wa wakati huo Ali Abdullah Saleh.

Jina lao ni kutoka kwa mwanzilishi wa vuguvugu hilo, Hussein al Houthi. Pia wanajiita Ansarolá au Wafuasi wa Mungu.

Baada ya uvamizi wa Iraq ulioongozwa na Marekani mwaka 2003, Wahouthi walipitisha kauli mbiu: "Mungu ni mkuu. Kifo kwa Marekani. Kifo kwa Israel. Laana kwa Wayahudi na ushindi kwa Uislamu."

Walijitangaza kuwa ni sehemu ya "mhimili wa upinzani" unaoongozwa na Iran dhidi ya Israel, Marekani na Magharibi kwa ujumla, pamoja na Hamas na Hezbollah.

''Hilo linatoa sababu kwa nini Wahouthi wanashambulia meli zinazoelekea Israel katika Ghuba,'' anasema Hisham al Omeisy, mtaalamu wa Yemen katika Taasisi ya Amani ya Ulaya.

"Sasa wanapambana na mabeberu, wanapigana na maadui wa Uislamu," anasema. "Hilo linaendana vyema na msingi wake," aliongeza.

w
Maelezo ya picha,

Jinsi Houthi walivyoyachukua maeneo ya Yemen

Waasi wa Houthi walipata nguvu kubwa ya kisiasa nchini Yemen mwanzoni mwa 2014, walipoibuka dhidi ya mrithi wa Ali Abdullah Saleh kama rais, Abd-Rabbu Mansour Hadi.

Baada ya kufikia makubaliano na Saléh, adui yao wa zamani, walikusudia kumrudisha madarakani.

Walichukua udhibiti wa jimbo la Saada kaskazini mwa Yemen na, mapema mwaka 2015, waliteka mji mkuu Sanaa, na kumlazimisha Hadi kukimbilia nje ya nchi.

f

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wahouthi walitaka kumpindua rais wa Yemen, Abd-Rabbu Mansour Hadi (kushoto), na kumrejesha Ali Abdullah Saleh (kulia).

Nani anawaunga mkono Houthi?

Waasi wa Houthi wanaungwa mkono na Hezbollah, kundi la waasi la Lebanon la Shia.

Hezbollah imewapa mafunzo makubwa ya kijeshi tangu 2014, kulingana na Kituo cha Kupambana na Ugaidi, ambayo ni taasisi ya utafiti wa kijeshi ya Marekani.

Wahouthi pia wanaichukulia Iran kama mshirika, kwa sababu Saudi Arabia ni adui wao wote. Iran inashukiwa kusambaza silaha kwa waasi wa Houthi.

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mabaki ya ndege isiyo na rubani iliyorushwa kutoka Yemen kuelekea mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abu Dhabi, mwaka 2022.

Marekani na Saudi Arabia zinasema Iran ilitoa makombora ya balistiki ambayo Wahouthi waliyarusha katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh, mwaka 2017, lakini yaliangushwa.

Saudi Arabia pia iliilaumu Iran kwa kusambaza makombora na ndege zisizo na rubani ambazo Wahouthi walizitumia kushambulia vituo vya mafuta vya Saudia 2019.

Waasi wa Houthi wamerusha maelfu ya makombora ya masafa mafupi dhidi ya Saudi Arabia na pia wameshambulia maeneo ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Usambazaji wa silaha hizi umekiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa. Iran imekana kufanya hivyo.

Je, Wahouthi wana nguvu kiasi gani?

g

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Idadi kubwa ya wakaazi wa Yemen wanaishi katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa vuguvugu la Houthi.

Serikali rasmi ni Baraza la Uongozi wa Rais. Rais Abd-Rabbu Mansur Hadi alihamisha mamlaka yake mwezi Aprili 2022 na makao yake ni mji wa Riyadh.

Hata hivyo, idadi kubwa ya watu wa Yemen wanaishi katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Houthi, na shirika hilo hukusanya ushuru katika sehemu ya kaskazini mwa nchi na pia kuchapisha pesa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linamnukuu mtaalamu anayelifuatilia kundi hilo, Ahmed al Bahri, anasema mwaka 2010 Wahouthi walikuwa na wapiganaji kati ya 100,000 na 120,000, wanaojumuisha askari wenye silaha na wafuasi wasio na silaha.

Umoja wa Mataifa pia ulisema karibu watoto 1,500 walioandikishwa na waasi wa Houthi wa Yemen walikufa katika mapigano mwaka 2020, na mamia zaidi walikufa mwaka uliofuata.

Waasi wa Houthi wanadhibiti sehemu kubwa ya pwani ya Bahari Nyekundu, ambako wamekuwa wakianzisha mashambulizi yao dhidi ya meli.

Al Omeisy anasema mashambulizi haya yamewasaidia katika mazungumzo yao ya sasa ya amani na Saudi Arabia.

"Kwa kuonyesha kwamba wanaweza kufunga Mlango-Bahari wa Mandeb katika Bahari Nyekundu, wanaweka shinikizo zaidi kwa Wasaudi wakati wa makubaliano," anasema.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Rashid Abdallah