Uamuzi wa Trump na vitendo vya Houthi, yanavyotatiza kazi ya kutoa misaada Yemen

fg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Takriban nusu ya wakazi wa Yemen wanahitaji msaada wa kibinadamu, wakiwemo karibu watoto milioni 10
  • Author, Sally Nabil
  • Nafasi, BBC

Hanaa alipofika kazini miezi michache iliyopita, alikuta "vikomeo vya milango vimevunjwa, na bosi akiwa amezungukwa na wanausalama."

Kompyuta, simu, kamera na nyaraka zote zilichukuliwa, bosi wake alikamatwa na hatimaye akaunti ya benki ya shirika hilo ikafungiwa.

Hanaa anafanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali linalofadhiliwa na Marekani (NGO) nchini Yemen, ambalo linasaidia wanawake na kutoa mafunzo kwa watu ya jinsi ya kutatua matatizo kwa njia ya mazungumzo.

Lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, ambavyo vimedumu kwa zaidi ya muongo mmoja na kusababisha moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, vimefanya maisha kwa wafanyakazi wa NGO kuzidi kuwa hatarini.

Wafanyakazi 24 wa Umoja wa Mataifa, pamoja na wafanyakazi kutoka NGOs nyingine za ndani na kimataifa wameshikiliwa na waasi wa Houthi katika miezi michache iliyopita.

Wimbi la watu kukamatwa mwezi Januari limezidisha hali ya hofu - mtu mmoja kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani ambaye alizuiliwa alifariki akiwa kizuizini.

Hali hiyo imewaacha wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wahisi kukosa uhuru wa kutembea. Mashirika mengi, yakiwemo ya Umoja wa Mataifa, yanapunguza kazi zao, na hilo linatishia maisha kwa watu ambao tayari wako hoi kutokana na vita.

Pia unaweza kusoma

Kamata kamata ya Houth

ok

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waasi wa Houthi

Miaka kumi iliyopita, wanamgambo wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran walichukua udhibiti wa maeneo mengi ya magharibi mwa Yemen, ukiwemo mji mkuu Sanaa, kutoka serikali inayotambulika kimataifa.

Saudi Arabia ilifanya mashambulizi makali ya anga dhidi ya Houth - kwa msaada wa vifaa na ujasusi kutoka Marekani na Uingereza - kujaribu kuwazuia waasi wa Houthi kudhibiti nchi nzima.

Ni maafisa wa Houthi waliovamia ofisi ya Hanaa na kumzuilia bosi wake, na anahofia kuadhibiwa iwapo atazungumza. Kwa hivyo, kwa usalama wao, tumebadilisha majina ya Hanaa na wengine huko Yemeni tuliowahoji kwa makala hii.

Kwa kuwakamata wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, Hanaa anaamini, Wahouthi wanalenga kueneza hofu kwa umma. Lakini kinachomuumiza zaidi ni jinsi umma ulivyojibu.

"Nilipoangalia mitandao ya kijamii, nilishangaa kugundua kuwa watu wanatuona sisi ni wapelelezi," anasema.

Siku moja baada ya bosi wake kuzuiliwa, wakati Hanaa, akitazama chaneli inayounga mkono Houthi ikionyesha kile ilichokitaja kama ushahidi wa ujasusi, uliotolewa na watu tisa wa eneo hilo ambao waliwahi kufanya kazi katika ubalozi wa Marekani uliofungwa kwa muda mrefu mjini Sanaa. Watu hao walikamatwa 2021.

Kwa kuwa naye alikuwa akifanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali lililofadhiliwa na Marekani. Aliamua kuondoka nyumbani kwake kaskazini mwa Yemen.

Misaada ya Marekani

gv
Maelezo ya picha, Nchini Yemen, watu milioni 4.5 wamekimbia makazi yao, huku wengi wao wakiishi katika kambi, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Unicef.

Na sasa ana wasiwasi kwamba uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuwaweka tena Wahouthi kama shirika la kigaidi, unaweza kuwafanya kumlenga kila mtu anayefanya kazi katika miradi inayofadhiliwa na Marekani.

BBC iliwasiliana na Houthi kuuliza kuhusu hali za wahudumu wa misaada, lakini hawakupata jibu.

Misaada ya Shirika la Misaada la Marekani (USAID) imesitishwa kutokana na Rais Trump kusimamisha shughuli za shirika hilo duniani kote kutokana na madai ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha.

Shirika la Human Rights Watch (HRW) linaonya kwamba athari za sera za Rais Trump na kamata kamata ya kiholela ya Wahouthi – vitakuwa na athari kubwa katika utoaji wa misaada nchini Yemen," anasema Niku Jafarnia, mtafiti wa Yemen na Bahrain katika shirika hilo.

Kulingana na HRW, Marekani ilikuwa ikifadhili takriban thuluthi moja ya misaada ya kibinadamu nchini Yemen, sehemu kubwa ya misaada hiyo ni kupitia USAID.

Kati ya 2015 na 2021, ilitoa zaidi ya dola bilioni 3.6, na kuwa mfadhili mkubwa zaidi wa misaada ya kibinadamu nchini, kulingana na UN.

"Kukata misaada ni kama hukumu ya kifo kwetu," anasema Amal, mama wa watoto tisa. Anaishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani kaskazini mwa Yemen, pamoja na maelfu ya familia zingine.

Miaka 10 imepita tangu kupoteza nyumba yake. Amal anaiendesha familia yake kubwa yeye peke yake. Mumewe ana pumu kali, hivyo hawezi kufanya kazi. Familia hiyo ililazimika kuukimbia mji wa kaskazini baada ya mzozo kuanza.

Tangu wakati huo, maisha yamezidi kuwa mabaya kwao. Kambi hiyo, iko kwenye ardhi kavu ya jangwa. Makazi yao ni hema la plastiki lililochakaa, lisilo na viti wala vitanda ndani.

"Kama usambazaji wa huduma unaotolewa na NGOs utakatwa, watoto wangu wanaweza kufa. Hatuna kazi, hatuna mapato, hakuna kitu," anasema Amal.

Hali mbaya katika kambi

C
Maelezo ya picha, Kupata maji safi ni changamoto kubwa kwa wale wanaoishi katika kambi za watu waliokimbia makazi yao

Takriban nusu ya watu wanahitaji msaada wa kibinadamu, wakiwemo watoto karibu milioni 10, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Unicef. Umoja wa Mataifa umeiorodhesha Yemen kama moja ya nchi 10 masikini zaidi duniani.

Amal anatuambia anapokea kikapu cha chakula kila mwezi kutoka Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), lakini hudumu kwa muda wa wiki mbili.

Wanapokosa chakula, anasema chaguo pekee ni kuondoka kambini na kwenda kuomba katika mitaa ya jiji. Hupita katika migahawa na maduka, akitumaini kupata mikate au pakiti za mchele.

"Nimefunikwa na aibu, lakini je, niwaache watoto wangu wafe njaa? Sijiwezi kabisa," anaeleza Amal. "Hulia sana ninapotambua kwamba sina hata senti," anasema huku sauti yake ikiwa na uchungu.

Idadi kubwa ya watoto wanakabiliwa na tumbo la kuhara na nimonia kutokana na uchafu, utapiamlo na hali mbaya ya maisha, na hakuna dawa za kutosha.

BBC iliwasiliana na Umoja wa Mataifa ikitaka maoni kuhusu mchakato wa sasa wa usambazaji wa misaada na kukamatwa kwa wafanyakazi, lakini haikujibiwa.

Umoja wa Mataifa

RFC
Maelezo ya picha, Kliniki nchini Yemen hazina dawa za kutosha kwa ajili ya wagonjwa

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Hans Grundberg, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, alilaani kuzuiliwa kwa wafanyakazi wake kama "si tu ukiukaji wa haki za kimsingi za binadamu, pia tishio la moja kwa moja kwa Umoja wa Mataifa katika kusambaza misaada kwa watu wanaohitaji."

Pia alitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wafungwa wote, iwe kutoka Umoja wa Mataifa au kutoka NGOs zingine za ndani na za kimataifa.

Ni familia kama za Amal ambapo Hanaa na wafanyakazi wenzake wanajaribu kuzisaidia.

Amal anahofu kukosekana kwa msaada, kwa sababu ya ukosefu wa fedha na kukamatwa, kunaweza kuongeza viwango vya kutojua kusoma na kuandika.

"Sisi pekee ndio tuliobaki wakati wa kuporomoka kwa serikali, ili kuwatumikia wananchi," Hanaa anasema huku akivuta pumzi nzito.