Je, 'mapatano ya Pasaka' ya Putin ni ya mashaka au nafasi ya kufikia amani?

Chanzo cha picha, Reuters
Mwezi uliopita utawala wa Trump nchini Marekani ulipendekeza wazo la kusitisha mapigano kwa siku 30.
Ukraine ilikubali. Urusi haikufanya hivyo. Au tuseme, ilikuja na orodha ndefu ya masharti.
Badala ya siku 30, Kremlin iliamua saa 30. Siku ya Jumamosi, Rais Vladimir Putin alitangaza mapatano ya Pasaka ya upande mmoja nchini Ukraine hadi saa sita usiku Jumapili usiku huko Moscow.
Alisema alikuwa akitekeleza hatua hiyo kwa kuzingatia maslahi ya "kibinadamu".
Madai kama hayo yametiliwa shaka nchini Ukraine zaidi ya miaka mitatu katika vita vya Urusi dhidi ya nchi hiyo.
Katika mitandao ya kijamii Jumapili asubuhi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alichapisha kwamba "jeshi la Urusi linajaribu kuleta taswira ya jumla ya kusitisha mapigano, wakati katika baadhi ya maeneo bado wanaendelea na majaribio ya pekee ya kuendeleza mashambulizi na kuisababishia Ukraine hasara."
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilikuwa na mtazamo tofauti.
Katika taarifa yake, ilisema kwamba "wanajeshi wote wa Urusi katika eneo la operesheni maalumu ya kijeshi [neno la Urusi la uvamizi wa Ukraine] kutoka 18:00 saa za Moscow mnamo 19 Aprili.
Jeshi la Urusi pia liliishutumu Ukraine kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Je, kusitisha mapigano ya Pasaka ya Urusi ni hatua ya kweli ya Vladimir Putin?
kuelekea kumaliza vita?
Mtazamo wa kutilia shaka ni kwamba mapatano ya saa 30 hayahusu kuifikia amani na yanahusiana zaidi na kudumisha uhusiano mzuri na White House.
Tangu Donald Trump arejee katika Ofisi ya Oval, Putin amekuwa na shughuli nyingi akijaribu kurekebisha uhusiano na Washington na kuweka njia kuelekea enzi mpya ya ushirikiano.
Hata hivyo, maoni ya hivi karibuni ya umma ya maafisa wa Marekani (ikiwa ni pamoja na Trump mwenyewe) yamependekeza kuwa utawala wa Marekani umekuwa ukikosa subira kuhusu ukosefu wa maendeleo kuhusu Ukraine. Trump ametishia kujiepusha na majaribio ya kufikia makubaliano ya amani ikiwa makubaliano hayatatekelezwa.
Kwa kutangaza usitishaji wa mapigano wa upande mmoja, ingawa ni mfupi, Kremlin inaweza kusema kuwa ni Urusi, sio Ukraine, ambayo imejitolea kwa amani. Moscow tayari inailaumu Kyiv kwa ukiukaji wa usitishaji mapigano na kuendelea kwa mapigano.
Kumbuka, usitishaji huu mfupi wa mapigano ulitangazwa kwa taarifa fupi sana. Tangazo la Jumamosi litakuwa limetoa muda mfupi kwa upande wowote, Urusi au Ukraine, kujiandaa kikamilifu kwa hilo.
Lakini pia kuna maoni yenye matumaini zaidi.
"Mapatano ya Pasaka" ya Kremlin yalikuwa ya kushangaza. Lakini hayakutoka popote.
Katika wiki za hivi karibuni kumekuwa na diplomasia kali ya kimataifa kujaribu kusitisha mapigano.
Mjumbe wa Trump Steve Witkoff amekutana na Putin mara tatu ndani ya miezi miwili. Mjumbe wa kiongozi wa Kremlin Kirill Dmitriev alisafiri kwa ndege hadi Washington hivi karibuni.
Siku chache zilizopita Bw Witkoff na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio walikuwa mjini Paris kwa mazungumzo kuhusu Ukraine na Rais Emmanuel Macron. Ujumbe kutoka Ukraine ulikuwepo pia.
Je, kunaweza kuwa na fursa adimu ya kupata amani?
Licha ya ripoti za kuendelea kwa mapigano, je, usitishaji mapigano wa saa 30 unaweza kukua na kuwa jambo kubwa zaidi na la kina zaidi?
Baada ya kuonesha nia ndogo ya maelewano au makubaliano hadi kufikia hatua hii, je Putin anaweza kushawishiwa kwamba sasa ni wakati wa kuweka makubaliano?
Ni vigumu kuona hilo kwa sasa.
Kisha tena, linapokuja suala la diplomasia, hatujui mazungumzo yote yanayofanyika bila maelezo ya mikataba inayojadiliwa.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi