Waridi wa BBC: Mume wangu aliniacha na kumuoa dada yangu

mAJUTO

Chanzo cha picha, Lilian Migwi

  • Author, Anne Ngugi
  • Nafasi, BBC Swahili

Lilian Migwi, mwanamke wa miaka 30, hakuwahi kamwe kufikiria kwamba siku moja mmoja wa dada yake wa damu, aliyelelewa naye pamoja toka utotoni angemsaliti.

Hata hivyo, kama waswahili wasemavyo, umdhaniaye sie ndiye...mambo ndivyo yalivyokuwa kwani mdogo wake waliyenyonya titi moja ndiye aliyekuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yake na hatimaye kugeuka na kuwa mke wa mumewe na baba wa watoto wao wawili.

Bi Lilian kwa muda mwingi baada ya ndoa yake kuvunjika hujiuliza maswali mengi, asipate majibu ya ni kwa nini, dada yake ambaye anakiri alimpenda na kumjali kwa moyo wake wote angemgeuka na kumpokonya penzi lake.

"Mimi ni mtoto wa kwanza na aliyenisaliti ndiye dada aliyenifuatia, tumelelewa kwa upendo mwingi na wazazi wetu, mimi pia nilimpenda dada yangu na pia ninaamini kuwa wakati huo alikuwa amenipenda mno, ila kitendo alichonifanyia kiliniacha hoi nisijue cha kufanya au kumgeukia nani" asema Lilian.

Mwanadada huyu anasema kuwa hakudhania kuwa kuna siku ambayo dada yake angemtamani mume wake - anajilaumu kwa kuwa mwema kupindukia kwa dada yake kiasi cha kumfanya ampuuze na kumdhalilisha.

Lilian alikutana vipi na mume wake?

Bi Lilian anasema kuwa wakati alipokutana na mume wake, wote walikuwa wakifanya kazi katika taasisi mmoja . Kama kawaida ya mahaba mapya walipendana sana na uchumba wao ulidumu kwa miaka saba.

Wawili hao waliamua kuwa hawangeshiriki tendo la ngono hadi wafunge ndoa rasmi. ''Nilipendezwa sana na tabia za mchumba wangu hasa kwa kuwa alikuwa mcha Mungu," anasema Lilian.

Aliongeza kuwa: "Nadhani kuwa nilikuwa nampenda sana aliyekuwa mume wangu, hadi nilikuwa nimejitoa kuliko kawaida ya ubinadamu, wajua nilikuwa nasikia watu wakisema kuwa ukimpenda mtu usimpe moyo wako wote, ila mimi nahisi kuwa nilikuwa nimempa wangu wote," anakumbuka Lilian.

Ndugu zake walikuwa na ukaribu na mumewe

Kulingana na mwanadada huyu ni yeye aliyehakikisha kuwa kaka na dada zake walikuwa na uhuru wa kujieleza na ukaribu na mume wake, kwani wakati huo aliamini kuwa ni katika kujenga jamii iliyo bora , asijue kuwa kule kuwashikanisha dada zake kwa mume wake na pia kuzoeana na kutangamana mara kwa mara na wao kungezaa majonzi na kovu alilonalo mpaka sasa.

Bi Lilian anasema kuwa mume wake alipendwa mno na watu wa familia yak

Chanzo cha picha, Lilian Migwi

Bi Lilian anasema kuwa mume wake alipendwa mno na watu wa familia yake kuanzia wazazi wake, pamoja na kaka na dada zake.

''Nakumbuka mume wangu alikuwa ni mtu wa kupendeka kwa haraka hasa kutokana na tabia yake na weledi katika kuhakikisha kuwa watu walijisikia huru akiwa nao. Hili liliivutia sana familia yangu,'' anakumbuka.

"Sijutii kumkutanisha aliyekuwa mume wangu na kaka zangu, ila najutia sana na ninahisi nilikosea mno kwa kuwaleta karibu sana dada zangu na mume wangu , kwani kutokana na ukaribu huo, urafiki na mapenzi ulianza kunoga nyuma yangu bila mimi kufahamu " anaongeza Lilian.

Aliwapenda na kuwasaidia dada zake

Mwanamke huyu anasema kuwa dada zake wawili walikuwa wakiishi pamoja , wakati tayari yeye alikuwa ameanza maisha ya ndoa na mchumba wake.

Mmoja wa dada zake alikuwa chuo kikuu kimoja nchini Kenya, na pia alikua anaishi na dada yao mwingine. Kama kawaida Lilian kama dada mkubwa alikuwa anawatembelea kila wakati kuhakikisha kuwa walikuwa hawakosi chochote kwani walikuwa ni wadogo zake aliowapenda sana. Dada zake wawili walikuwa wamekodisha nyumba ndogo karibu na chuo kikuu.

"Kila mara tulikuwa tunawatembelea na kuhakikisha kuwa kila kitu ni shwari, kwa mfano tungewanunulia bidhaa mbalimbali za kukidhi mahitaji yao ya kila siku na shughuli hii niliifanikisha na mume wangu, kila mara tulikuwa tunawatembelea, kitu ambacho hadi wa leo sijaelewa ni vipi dada yangu anayenifuata alipata nambari ya simu ya mume wangu , kwani niligundua kulikuwa na mwasiliano yalikuwa yanafanyika nyuma yangu," anasema Lilian.

Bi Lilian anasema kuwa mume wake alipendwa mno na familia yake

Chanzo cha picha, Lillian Migwi

Lillian anashuku wakati alipopata ujauzito wa pili, ndipo uhusiano wa kimapenzi kati ya dada yake na mume wake ulipoanza na kunoga. Anasema kuwa mume wake alikua amemkataza kutumia mitandao ya kijamii kwa mfano WhatsApp, Facebookna mingine kwa hivyo yeye hakuwa anafahamu mengi kuhusiana na shughuli za mitandao.

"Kwa kuwa sikutaka kuharibu uhusiano wangu wa ndoa, nilikubali shingo upande na kufuta 'app' zote za mitandao ya kijamii katika simu yangu, nilikuwa na simu nzuri ambayo ingenipatia wakati mzuri katika mitandao ila niliheshimu uamuzi wa mume wangu."

Kuna wakati mmoja mume wake alimpatia simu yake ya mkononi, mara akaamua kuipekua na ndipo alipopata ujumbe kadhaa ambao uliashiria kuwa alikuwa anatuma fedha moja kwa moja kwa nambari ya dada yake, ila Lilian hakuwa na taarifa kuwa hilo lilikuwa linafanyika.

''Nilimuita mume wangu na kumuuliza waziwazi ni kwanini alikuwa anatuma pesa moja kwa moja kwa dada yangu, bila hata kuniuliza au nieleza. Nilimuuliza swali hilo kwani nilihisi kuwa kwa kufanya hivyo ni kudumisha heshima kati yake na dada zangu,'' anasema.

Majibu ya mume wake yalikuwa ni kwamba dada yake alimpigia simu na kumueleza kuwa alikuwa na jambo la dharura na alihitaji fedha, kwa hiyo hakuona shida kumtumia . Ni jambo walilozungumza na mume wake akaomba msamaha . Ila kosa hili la kutuma fedha kwa dada yake lilikuwa linajirudia kila wakati.

"Nikiwa na ujauzito wa mtoto wa pili, karibu miezi sita suala hili la mume wangu kutuma fedha kwa simu ya dada yangu lilikithiri mno hadi wakati mmoja nikaamua kuwapigia wazazi simu ili waingilie kati na tupate suluhu, ila juhudi zangu ziligonga mwamba, hakuna kilichobadilika."

Lilian anasema kuwa alimueleza mama yao mzazi kwamba amuonye dada yake aache kupokea fedha kutoka kwa mume wake, badala yake ikiwa anahitaji lolote amjulishe na yeye atalishughulikia . Ni jambo ambalo mama yake alilitekeleza na badala ya kumuonya dada mmoja alitoa ushauri kwa dada wote wawili.

Baada ya kisa hicho ilikuwa kana kwamba tabia hiyo ilikwisha na aliacha kuwasiliana naye, huku mume wake akionekana kurejea kuwa mume mwema.

Kumfumania dada yake na mume wake

Wakati akikaribia kujifungua, aliamua kurejea kijijini kuwasalimia wazazi wake , kwa hiyo alichukua siku kadhaa kwa shughuli hiyo. Simu ya mkononi aliyokuwa anaitumia haikuwa na mitandao ya kijamii kwani mume wake tayari alikuwa amemuamrisha azifute. Lilian hakuwa na habari kuhusiana na mawasiliano ya mitandao ya kijamii .

Akiwa pale nyumbani kaka yake aliichukua simu yake ya mkononi, katika pilikapilika za kurejesha mitandao, Lilian aligundua picha moja kwenye mtandao wa WhatsApp ambayo ilikuwa kwenye nambari ya dada yake - ilikuwa ni picha ya mume wake na ya dada yake ikiwa imeandikwa mandishi ya kimapenzi.

"Maandishi yalikuwa ya mapenzi tele, nilitazama maandishi hayo kwa mshanga, nilikuwa mja mzito aliyekaribia kujifungua, kwa sekunde kadhaa nilinyamaza na kubaki kinywa wazi... Sikuamini kuwa maandishi hayo yalitoka kinywani mwa mume wangu niliyemfahamu. Maandishi ambayo hakuwahi kuniambia hata katika uchumba wetu," anakumbuka Lilian.

Ni kipindi ambacho anasema hawezi kukisahau kwani kuondoka kwa mume wake kuliashiria kuwa anaanza maisha mapya.

Chanzo cha picha, Lillian Migwi

Baada ya kuvuta pumzi alimpigia mama yake mzazi simu ambaye hakuwa kijijini wakati huo, alimwelezea kuhusiana na picha zilizokuwa mtandaoni za dada na mume wake. Kwa kuwa mama alikuwa mjini alisafiri hadi nyumbani kwa dada yake Lilian ili kuelewa zaidi kuhusiana na picha hizo.

"Mama alipomuuliza dada yangu kuhusu uhusiano wake na mume wangu, dada yangu alimjibu mama kuwa hataachana na mume wangu, jambo lililomuuma mama yangu sana, kiasi cha kuwa mama alianza kumzaba makofi dada yangu kwa hasira na machozi," anasema Lilian.

Mpasuko ndani ya familia

Ni kisa kilichoiacha familia ya Lilian na mpasuko mkubwa, upande wa mume pia mashemeji walikuwa na mshangao mkubwa kuhusiana na uhusiano huo usio wa kawaida. Siku zilizofuata hapo zilikuwa zilizojaa vuta n'kuvute mume wa Lilian hakuonekana kushutushwa na yaliyokuwa yanajiri wala dada yake pia hakutetereka kuona kwamba uhusiano wao wa kimapenzi wa kisiri ulikuwa umejulikana.

Mkutano mkubwa ulipangwa kati ya wazazi wa Lilian na wazazi wa mume.. Wote walisafiri ila mume wake na dada yake hawakufika katika mkutano huo. Kuanzia wakati huo Lilian anasema kuwa mume wake aliondoka nyumbani na wakaanza kuishi na dada yake...kuanzia hapo uhusiano wao haukuwa siri tena.

Kipindi hicho Lilian alipatwa na uchungu wa kujifungua, mume wake tayari alikuwa ameanza kuishi na dada yake kama mke wa pili . Alikuwa amemtelekeza na lilian alijifungua mtoto wa kiume bila uwepo wa mume wake .

Ni kipindi ambacho anasema hawezi kukisahau kwani kuondoka kwa mume wake kuliashiria kuwa anaanza maisha mapya.

Chanzo cha picha, Lillian Migwi

Ni kipindi ambacho anasema hawezi kukisahau kwani kuondoka kwa mume wake kuliashiria kuwa anaanza maisha mapya.

Lilian hakuwa na ajira yoyote kwani mume wake alikuwa amemkataza kufanya kazi zozote ila awe mama wa nyumbani . Lakini sasa mume alikuwa hayuko na ilibidi aanze maisha ya kufanya kazi za vibarua vidogo vidogo kama vile kuwafulia watu nguo na kazi nyingine za nyumbani.

"Kufahamu kuwa mume wangu na dada yangu walianza kuishi pamoja, kulinisikitisha sana kwa kipindi cha mwaka mmoja nilipatwa na sonona mbaya mno...huzuni isiyoelezeka iliugubika moyo wangu, maswali mengi yasiyo na majibu yalinijia, huku nikipambana kulea watoto wangu wadogo pekee yangu," Lilian anakumbuka.

Msamaha

Muda mfupi baada ya Lilian kujipata bila mume na uhusiano wake na dada yake kuvunjika, Mume wa Lilian na dada yake walijaaliwa mtoto mmoja na wangali wakiishi pamoja. Ni miaka minne sasa tangu kisa hicho kutokea.

Kwa Lilian imekuwa safari ndefu ya kusamehe na kutoa machungu ya kujijua na pia kupanga maisha yake na ya watoto wake wawili.

"Kufikiria kuwa dada yangu, yaani damu yangu alinipokonya mume nilijiona mama mpumbavu sana... kwani ni mimi niliyemfungulia mlango wa kuwa huru na mume wangu kwa kufanya hivyo nilihisi najenga familia thabiti na yenye upendo, kumbe nilikuwa nachimba kaburi la kuangamia kwa ndoa yangu," asema Lilian.

Lilian anasema kuwa amewasamehe aliyekuwa mume wake na dada yake.

Chanzo cha picha, Lillian Migwi

Lilian amejitokeza kwenye vyombo vya habari nchini Kenya na kwenye mitandao ya kijamii, akizungumzia kisa hiki waziwazi . Hutoa ushauri kwa wanawake na wasichana ambao wamejikuta wamekwazwa katika mahusiano ya kimapenzi na hawana mwelekeo .

Lilian anasema kuwa amewasamehe aliyekuwa mume wake na dada yake.

Ila anasema kuwa hawajazungumza kwa muda na hatazamii kuwa watawahi kuzungumza tena maishani mwao.