Angelina Vunge: Mwafrika wa kwanza mbunge Uruguay aliyeingia nchini humo miaka 20 iliyopita bila stakabadhi halali

Chanzo cha picha, JAVIER NOCETI
Mnamo Aprili 14, 2021, Angelina Vunge alichaguliwa kama mbunge wa chama tawala cha National Party katika bunge la Uruguay .
Spika wa Bunge la wawakilishi alipompa nafasi ya kuzungumza, akasema: "Niamini ninaposema ni muhimu leo mimi kuwa hapa. Ni siku maalum sana kwangu." Huku sauti yake ikisikika kama yenye kukwaruza kwa mbali kabla ya kurejelea mjadala uliokuwa unapigiwa kura siku ile.
Haingekuwa jambo kubwa kwa mwanamke kuwa mbunge wa kiti ambacho kimeachwa na mwanaume kama haingekuwa kwa Angelina Vunge, raia wa Angola ambaye alihangaishwa kupitia ajira ya watoto , alinyanyaswa katika ndoa na kupitia manyanyaso mengine ya kingono, aliyetoroka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwake (1975 - 2002) na kuwasili Uruguay miaka 20 iliyopita bila stakabadhi halali, akiwa hajui lugha ya nchi hiyo, hakuwa na pesa wala kazi.
Na mwezi uliopita alitangazwa kuwa mbunge wa kwanza mwafrika katika bunge la Uruguay.
Vunge, 42, alizaliwa katika familia maskini katika kijiji kimoja kusini mwa Angola.
Aliishi vijiji tofauti na katika kila kijiji pamoja na kwenda shule, yeye pamoja na ndugu zake wanne walikuwa na jukumu la kutekeleza walilopewa na baba yao.
Akifanya kazi ya shamba, pia walikuwa wanakata na kubeba kuni, wanatengeneza unga na kuchukua mmea wa moringa kandokando ya mto na kusafisha nyumba iliyokuwa imejengwa kwa minyaa, mbao na udongo.
Alikwenda shuleni miguu peku
"Kama nisingesoma au nisingefanya kazi ya nyumbani ningelazimika kuelezea kwanini sijafanya, kabla sijachapwa viboko na baba. Kwanza mimi, kisha mama yangu kwasababu aliamini kuwa ikiwa nimeshindwa kufanya majukumu yangu, kosa ni la mamangu kwa kushindwa kunielekeza vyema,"Vunge alielezea BBC Mundo.
Alipitia kichapo kile kile shuleni ikiwa angeandika neno vibaya au angeshindwa kufanya hesabu. Alipiga magoti juu ya mawe mawili na kubeba vitu viwili vizito kwa mikono yake huku ikiwa imenyooshwa, amesema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Angelina, alitembea kilomita 10 kila siku kwenda shuleni akiwa miguu peku.
Akiwa na miaka minane, kwa bahati mbaya alivunja panga wakati analinoa kwa jiwe akiwa anataka kwenda kutafuta kuni. Baba yake akajua alichofanya na kama kawaida akampa kichapo cha nguvu kwanza kabla ya mama yake kuwa wa pili.
Angelia, ipo siku ambayo baada ya kufanya makosa aliamua kumfunga ndugu yake mdogo mgongoni akidhani hiyo itakuwa njia moja ya kukwepa kichapo asijue kuwa baba yake akiamua kumpiga hakuna kitakachomzuia.
Unyanyasaji aliopitia
Angelina anasema kuwa alipitia unyanyasaji kadhaa wa kingono nchini Angola na hakuwahi kusema aliyopitia kwa mtu yeyote
Anakumbuka mara ya kwanza akibakwa akiwa na umri wa miaka 4 na kijana ambaye alikuwa amechaguliwa na familia yake kama mume ambaye angemuoa "akishaanza kuota matiti."

Chanzo cha picha, JAVIER NOCETI
Angelina Vunge alinyanyaswa kingono mara kadhaa akiwa mtoto.
Unyanyasaji huo ulirejelewa akiwa na miaka 7. Familia ya Angelina ikahamia kijiji kingine na huko pia akanyanyaswa tena.
"Núñez, mwanamume aliyembaka alikuwa jamaa yake na alifanya hivyo mara nyingi, tangu nikiwa na miaka 4 na hata kukiuka baadhi ya tamaduni zilizokuwa zinakumbatiwa kijijii: kwamba wanawake wanastahili kulindwa na kuwa wanastahili kuolewa wakiwa bikra", amesema kwenye kitabu chake.
"Mwanamke anayebakwa anasalia kimya siku zote lakini cha ajabu wanaotekeleza ubakaji hakuna hata siku moja wanaadhibiwa (...) Familia yake ilikuwa wapi wakati anamlaza mkekani na kumfanya kitendo kibaya? Nililia lakani alinionya nisijaribu kusema kwa yeyote". Anasema kuna mengine ambayo atasalia nayo moyoni mwake milele.
Alishuhudia unyanyasaji katika ndoa
Akiwa na umri wa miaka, 9, tayari alikuwa ameathirika na vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na unyanyasaji kwenye ndoa, Angelina aliapa kusoma kwa bidi na kufanya kazi, nia yake ikiwa ni kuweka akiba aweze kuhamia nchi nyengine.
Mwaka mmoja kabla, alikuwa ameshuhudia kuwa mgogoro mdogo tu, baba yake alikuwa anakaribia kumpiga mama yake kiasi hata cha kutaka kumuua. Mara kadhaa, alimuona mama yake akiwa chini anagaraza, damu zinamtoka.

Chanzo cha picha, JAVIER NOCETI
Baba yao alipokuwa amekwenda kutafuta fimbo ya kuendelea kumchapa mama yake, pacha wao wa kiume, walijitahidi kumsihi baba yao aende kwa wake wengine.
Kusaka pasipoti kulimwendea mrama
Akiwa na miaka 14, alitaka kupata pasipoti yake ili ahamie nchi nyingine. Hakuwa na uwezo wa kufikia intaneti na alichofanya ni kuanza kuuliza usaidizi kwa majirani.
Lakini kosa alilofanya ni kuamini kundi fulani la wavulana waliomuahidi kumtafutia, kwasababu walikuwa na ufahamu na mchakato unavyokwenda katika ofisi ya serikali.
Siku moja mchana, walimuita nyuma ya jengo la polisi wakiwa wamemuitisha picha za pasipoti.
Lakini baada ya kuingia kwenye jengo hilo, wavulana wawili walikuwa wanamsubiri. "Funga bakuli lako, mmoja wao akaniambia, kwasababu ukipiga kelele tutaita wavulana wengi zaidi. Wakanirusha kwenye godoro tayari nikiwa ninajua nini kingefuatia
Saa kadhaa baadaye, akaondoka jengo hilo akiwa hana pasipoti na mwenye majeraha makubwa moyoni.