Afghanistan: 'Nawapa watoto wangu wenye njaa dawa ili kuwasaidia kulala'

Ghulam (katikati) anasema anawapa watoto wake sita wenye njaa dawa za kuwafanya walale
Maelezo ya picha, Ghulam (katikati) anasema anawapa watoto wake sita wenye njaa dawa za kuwafanya walale.

Raia wa wa Afghanistan wanawapa watoto wao wenye njaa dawa za kuwatuliza - wengine wameuza binti zao na viungo vyao ili kujikimu kimaisha

Katika majira ya pili ya baridi tangu Taliban kuchukua mamlaka na fedha za kigeni kupigwa tanji, mamilioni ya watu wanakabiliwa na tishio la njaa.

"Watoto wetu wanaendelea kulia, na hawalali. Hatuna chakula," Abdul Wahab alisema.

"Kwa hiyo tunaenda kwenye duka la dawa, tunanunua vidonge na kuwapa watoto wetu ili wapate usingizi."

Anaishi nje kidogo ya Herat, jiji la tatu kwa ukubwa nchini humo, katika makazi ya maelfu ya nyumba ndogo za udongo ambazo zimekua kwa miongo kadhaa, zimejaa watu waliokimbia makazi yao na kukumbwa na vita na majanga ya asili.

Abdul ni miongoni mwa kundi la karibu wanaume 12 waliokusanyika karibu nasi.

Tukauliza, ni wangapi walikuwa wanawapa watoto wao dawa za kuwatuliza?

"Wengi wetu, sisi sote," walijibu.

Ghulam Hazrat aliingiza mkoni kwenye mfuko wa kanzu yake na akachomoa kipande cha vidonge.

Zilikuwa alprazolam - Dawa za kawaida za kutibu matatizo ya wasiwasi.

Vidonge vitano vya alprazolam sasa vinagharimu sawa na kipande cha mkate
Maelezo ya picha, Vidonge vitano vya alprazolam sasa vinagharimu sawa na kipande cha mkate.

Ghulam ana watoto sita, mdogo akiwa na mwaka mmoja. "Hata yeye nampatia," alisema.

Wengine walituonyesha vipande vya escilatopram na vidonge vya sertraline ambavyo walisema walikuwa wakiwapa watoto wao.

Kawaida huagizwa kutibu unyogovu na wasiwasi.

Madaktari wanasema kwamba wanapopewa watoto wadogo ambao hawapati lishe ya kutosha, dawa kama hizi zinaweza kusababisha uharibifu wa ini, pamoja na matatizo mengine kama vile uchovu wa kudumu, usingizi na matatizo ya tabia.

Wanaume katika eneo hili nje ya Herat wanatatizika kupata kazi
Maelezo ya picha, Wanaume katika eneo hili la Herat wanatatizika kupata kazi.

Katika moja la duka dawa tuligundua kwamba unaweza kununua tembe tano za dawa zinazotumiwa kwa dola senti 10 za Marekani, au bei ya kipande cha mkate.

Familia nyingi tulizokutana nazo zilikuwa zikigawana vipande vichache vya mkate kila siku.

Mwanamke mmoja alituambia walikula mkate mkavu asubuhi, na usiku waliuchovya kwenye maji ili kuufanya uwe na unyevu.

Umoja wa Mataifa umesema "janga" la kibinadamu sasa linatokea nchini Afghanistan.

Wengi wa wanaume katika eneo la Herat hufanya kazi kama vibarua wa kila siku.

Wamekuwa wakiishi maisha magumu kwa miaka mingi.

Lakini wakati Taliban walipochukua madaraka Agosti iliyopita, bila serikali mpya kutambuliwa kimataifa, fedha za kigeni zilizoingia Afghanistan zilizuiliwa na kusababisha kuporomoka kwa uchumi ambao uliwaacha wanaume bila kazi.

Siku wanapopata kazi, wanalipwa zaidi ya dola moja.

Kila mahali tulipokwenda, tulikuta watu wakilazimika kuchukua hatua kali ili kuokoa familia zao kutokana na njaa.

Ammar (sio jina lake halisi) alisema alifanyiwa upasuaji wa kutoa figo miezi mitatu iliyopita na akatuonyesha kovu la inchi tisa - alama za kushonwa zinaonekana kwenye tumbo lake. Ana umri wa miaka 20, katika kile ambacho kingekuwa kilele cha maisha yake.

Tunaficha utambulisho wake ili kumlinda. "Hakukuwa na njia ya kutoka. Nilikuwa nimesikia unaweza kuuza figo katika hospitali ya mtaani. Nilikwenda huko na kuwaambia nataka.

Wiki kadhaa baadaye nilipigiwa simu ikinitaka nije hospitali," alisema.

"Walifanya vipimo, kisha wakanidunga sindano iliyonifanya kupoteza fahamu. Niliogopa lakini sikuwa na la kufanya."

Ammar anasema aliuza figo yake miezi mitatu iliyopita
Maelezo ya picha, Ammar anasema aliuza figo yake miezi mitatu iliyopita

Ammar alilipwa dola 3,100 na sehemu kubwa ya hela hiyo alitumia kulipa pesa alizokopa kununua chakula cha familia yake.

"Tukila usiku mmoja, hatutakula mwingine. Baada ya kuuza figo yangu najiona kuwa nusu mtu. Najihisi kukosa matumaini. Maisha yakiendelea hivi ninahisi naweza kufa," alisema.

Kuuza viungo kwa pesa sio jambo geni nchini Afghanistan. Watu walikuwa wakifanya hivyo hata kabla ya Taliban kuchukua mamlaka.

Lakini sasa, hata baada ya kuchukua hatua hiyo ya kusikitisha, watu wanaona bado hawawezi kujikimu kimaisha.

Katika nyumba nyingine tulikutana na mama mdogo ambaye alisema aliuza figo yake miezi saba iliyopita. Pia alilazimika kulipa deni - pesa alizokopa ili wanyama wa kufuga nyumbani (kondoo).

Wanyama hao walikufa katika mafuriko miaka michache iliyopita na kumfanya apoteze njia zake za kujikimu.

Dola 2,700 alizopata baada ya kuuza figo hazitoshi.

"Sasa tunalazimishwa kumuuza binti yetu wa miaka miwili, watu tuliowakopa wanatunyanyasa kila siku wakisema tupatie binti yako ikiwa huwezi kutulipa," alisema.

"Nihisi kudhalilika kutokana na maisha tunayoishi. Wakati mwingine naona heri kufa kuliko kuishi hivi," mume wake alisema.

Tulisikia visa tofauti vya watu kuuza binti zao. "Nilimuuza binti yangu wa miaka mitano kwa 100,000 za Afghanistan," Nizamuddin alisema.

Hiyo ni chini ya nusu hela unazopata ukiuza figo huenda, kulingana na kile tulichopata ardhini. Akauma mdomo, macho yakamtoka. Heshima ambayo watu hapa waliishi nayo imevunjwa kutokana na njaa.

"Tunaelewa ni kinyume na sheria za Kiislamu, na kwamba tunaweka maisha ya watoto wetu hatarini, lakini hakuna njia nyingine," Abdul Ghafar, mmoja wa wakuu wa jamii hiyo, alisema.

Nazia bado anaishi na wazazi wake lakini familia yake ilimuuza alipokuwa na umri wa miaka 14
Maelezo ya picha, Nazia bado anaishi na wazazi wake lakini familia yake ilimuuza alipokuwa na umri wa miaka 14

Katika nyumba nyingine tulikutana na Nazia mwenye umri wa miaka minne, msichana mdogo mchangamfu akicheza na kaka yake Shamshullah mwenye umri wa miezi 18.

"Hatuna pesa za kununulia chakula, kwa hivyo nilitangaza msikitini kwamba nataka kumuuza binti yangu," baba yake Hazratullah alisema.

Nazia ameuzwa kwa familia nyingine kusini la Kandahar ili akaolewe. Atakapotimiza umri wa miaka 14, atakabidhiwa kwa familia yake mpya.

Kufikia sasa Hazratullah amepokea malipo mara mbili.

"Sehemu kubwa ya pesa hizo niliitumia kununua chakula, na nyingine nikatumia kumnunulia dawa mwanangu mdogo. Mwangalieni hana afya," Hazratullah alisema huku akivuta shati la Shamsullah ili kutuonyesha tumbo lake lililokuwa limevimba.

Kuongezeka kwa kasi kwa viwango vya utapiamlo ni ushahidi wa athari ya njaa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Afghanistan.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) linaelezea kuongezeka kwa asilimia 47 ikilinganishwa na mwaka jana idadi ya watoto wanaolazwa katika vituo vyao vya kutibu utapiamlo kote nchini.

Kituo cha lishe cha MSF huko Herat ndicho kituo pekee cha utapiamlo chenye vifaa vya kutosha kinachohudumia sio tu kwa Herat, lakini pia katika majimbo jirani ya Ghor na Badghis, ambapo viwango vya utapiamlo vimepanda kwa 55% katika mwaka jana.