Wakimbizi wa Afghanistan wanaoishi Pakistan wahofia kufurushwa kwa nguvu

"Naogopa," analia Nabila.
Maisha ya msichana huyo mwenye umri wa miaka 10 yamekuwa katika nyumba yao ya chumba kimoja huko Islamabad na barabara ya mavumbi iliyo mbele yake.
Tangu Desemba, hajaenda shuleni baada ya shule hiyo kuwazuia watoto wa Ki-Afghanistan bila cheti halali cha kuzaliwa cha Pakistani. Lakini hata kama angetaka kwenda darasani, Nabila anasema isingewezekana.
"Nilikuwa nyumbani ninaummwa, kisha nikasikia polisi walikuja kutafuta watoto wa Ki-Afghanistan," analia, akieleza jinsi familia ya rafiki yake ilivyofurushwa kurudi Afghanistan.
Jina la Nabila si la kweli - majina ya Wa-Afghanistan wote waliotajwa katika makala hii yamebadilishwa kwa usalama wao.
Mji mkuu wa Pakistan Rawalpindi vinashuhudia ongezeko la kufurushwa, kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa Wa-Afghanistan, inasema Umoja wa Mataifa.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya nusu ya Wa-Afghanistan milioni tatu nchini humo hawana nyaraka halali.
Wa-Afghanistan wanaelezea maisha ya hofu ya kila wakati na mashambulizi ya kila siku katika nyumba zao kutoka kwa polisi.
Baadhi walieleza kwa BBC kwamba wanaogopa kuuawa ikiwa watarudi Afghanistan. Hii ni pamoja na familia zilizokuwa katika mpango wa Marekani wa kuhamisha ambao umeahirishwa na utawala wa Trump.
Pakistan inachoshwa na jinsi mipango ya kuhamishwa inavyochelewa, anasema Philippa Candler, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi huko Islamabad.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linasema watu 930 walifurushwa kurudi Afghanistan katika nusu ya kwanza ya mwezi Februari, mara mbili ya idadi ya watu waliondolewa wiki mbili zilizopita.
Angalau 20% ya walioondolewa Islamabad na Rawalpindi walikuwa na nyaraka kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi, wakimaanisha walikubaliwa kama watu wanaohitaji ulinzi wa kimataifa.

Lakini Pakistan si sehemu ya Mkataba wa Wakimbizi na imewahi kusema kwamba haitambui Wa-Afghanistan wanaoishi nchini humo kama wakimbizi.
Serikali imesema sera zake zinawalenga raia wa kigeni wasio halali, na tarehe ya mwisho kwao kuondoka inakaribia.
Tarehe hiyo imekuwa ikibadilika, lakini sasa imewekwa kuwa 31 Machi kwa wale wasiokuwa na visa halali, na 30 Juni kwa wale wenye hati za uhamisho.
Wa-Afghanistan wengi wanahofia kutokana na machafuko haya. Pia wanasema kuwa mchakato wa kupata visa unaweza kuwa mgumu sana.
Familia ya Nabila inadhani wana chaguo moja pekee: kujificha. Baba yake, Hamid, alihudumu katika jeshi la Afghanistan kabla ya Taliban kudhibiti madaraka mwaka 2021.
Alijibu huku akiangua kilio akielezea inavyomnyima usingizi.
"Nilihudumia nchi yangu na sasa si kitu. Kazi hiyo imenisababishia matatizo," alisema.
Familia yake haina visa, na hawako kwenye orodha ya kuhamishwa. Wanatuambia kuwa simu zao kwa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa hazijibiwi.
BBC imefikia shirika hilo kutaka kusikia maoni yake.
Serikali ya Taliban hapo awali iliambia BBC kuwa Wa-Afghanistan wote wanapaswa kurudi kwa sababu wanaweza "kuishi nchini bila hofu yoyote." Inadai kuwa wakimbizi hawa ni "wahamiaji wa kiuchumi."
Lakini ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka 2023 ilitilia shaka ahadi ya serikali ya Taliban.
Iligundua kuwa mamia ya watumishi wa zamani wa serikali na waliokuwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi walitekwa na kuuawa licha ya msamaha wa jumla.
Ahadi za serikali ya Taliban hazikuwa na tumaini kubwa kwa familia ya Nabila, hivyo walichagua kukimbia mamlaka inapowakaribia.
Majirani wanatoa hifadhi kwa kila mmoja, kwani wote wanajaribu kuepuka kurudishwa Afghanistan.
Umoja wa Mataifa uliripoti kuwa Wa-Afghanistan 1,245 walikamatwa au kuwekwa kizuizini Januari kote Pakistan, zaidi ya mara mbili ya kipindi hicho mwaka uliopita.
Nabila anasema Wa-Afghanistan hawapaswi kufurushwa. "Musifukuze Wa-Afghanistan nyumbani mwao – hatupo hapa kwa kupenda, tumelazimika kuishi hapa."
Kuna hisia ya huzuni na upweke katika nyumba yao. "Nilikuwa na rafiki ambaye alikuwa hapa baadaye alifurushwa kwenda Afghanistan," anasema mama ya Nabila, Maryam.
"Alikuwa kama dada, kama mama. Siku tuliyotengana ilikuwa siku ngumu."
Najiuliza Nabila anataka kufanya nini atakapokuwa mkubwa. "ubunifu wa mitindo," anasema, akinitazama kwa macho ya udadisi. Kila mtu katika chumba anaangua kicheko.
Msongo wa mawazo unapungua.
Mama yake anamwambia kwa sauti ya chini kuwa kuna mambo mengine mengi anayoweza kuwa, mhandisi au wakili.
Ndoto ya Nabila ya kuwa mwana mitindo ni jambo ambalo hangeweza kuliishi chini ya serikali ya Taliban.
Kwa vikwazo vilivyowekwa kwa elimu ya wasichana, mapendekezo ya mama yake pia yangekuwa vigumu kutekelezeka.
Hatua mpya
Pakistan kwa muda mrefu ina rekodi ya kupokea wakimbizi wa Afghanistan.
Lakini mashambulizi ya kuvuka mipaka yameongezeka na kuongeza mvutano kati ya majirani hawa wawili.
Pakistan inawashutumu waasi walioko Afghanistan kwa mashambulizi hayo, jambo ambalo serikali ya Taliban inalikataa.
Tangu Septemba 2023, mwaka ambao Pakistan ilianza mpango wake wa "Kurudisha raia wa kigeni waishio isivyo halali," watu 836,238 wamerudishwa Afghanistan.
Katika kipindi hiki cha sasa cha kufurushwa, baadhi ya Wa-Afghanistan wanashikiliwa kwenye kambi ya Haji huko Islamabad.
Ahmad alikuwa katika hatua za mwisho za mpango wa kuhamishwa unaosimamiwa na Marekani.
Anasema kuwa Rais Donald Trump alipoahirisha mpango huo kwa ajili ya kufanya mapitio, alipoteza tumaini lake la mwisho."
BBC imeona barua ya kazi inayodaiwa kuwa ya Ahmad kutoka kwa shirika lisilo la kiserikali Magharibi mwa Afghanistan.

Wiki chache zilizopita, alipokwenda kufanya manunuzi, alipokea simu.
Binti yake mwenye umri wa miaka mitatu alikuwa kwenye simu. "Mtoto wangu aliita, njoo baba, polisi wako hapa, polisi wanakuja mlangoni mwetu," anasema.
Alikuwa bado anasubiri uhuishaji wa visa ya mke wake, na alikuwa akiendelea kuomba polisi.
Ahmad alikimbilia nyumbani. "Nisingeweza kuwaacha." Anasema aliketi kwenye gari la abiria na alisubiri kwa saa kadhaa huku polisi wakiendeleza kamata kamata yao.
Wake na watoto wa majirani zake waliendelea kuingia kwenye gari hilo.
Ahmad alianza kupokea simu kutoka kwa waume zao, wakimuomba awaangalizie familia.
Walimbilia kwenye msitu.
Familia yake ilishikiliwa kwa siku tatu katika "mazingira magumu," anasema Ahmad, ambaye anadai walipatiwa blanketi moja kwa kila familia, na kipande kimoja cha mkate kwa siku, na simu zao zilichukuliwa.
Serikali ya Pakistan inasema inahakikisha "hakuna mtu anayenyanyasika au kudhulumiwa wakati wa mchakato wa kuwarudisha."
Tulifanya juhudi za kutembelea kambi ya Haji ili kuthibitisha maelezo ya Ahmad lakini tulizuiwa kuingia na mamlaka.
BBC ilifikia serikali ya Pakistan na polisi kwa mahojiano au tamko, lakini hakuna aliyejitokeza.

Wakihofia kushikiliwa au kufurushwa, baadhi ya familia zimechagua kuondoka Islamabad na Rawalpindi.
Wengine wanatuambia kuwa hawawezi kumudu kufanya hivyo.
Mwanamke mmoja anadai alikuwa katika hatua za mwisho za mpango wa kuhamishwa na Marekani na aliamua kuhamia Attock, na mabinti zake wawili kilomita 80 (maili 50) magharibi mwa Islamabad. "Naweza tu kumudu mkate," anasema.
BBC imeona hati inayothibitisha kwamba alifanya mahojiano na IOM mapema Januari.
Anadai familia yake bado inashuhudia uvamizi wa karibu kila siku katika mtaa wao.
Msemaji wa ubalozi wa Marekani huko Islamabad amesema kuwa wanashirikiana "kwa karibu" na serikali ya Pakistan "kuhusu hali ya raia wa Afghanistan katika kutekeleza mpango wa Marekani kuwahamisha."
Nje ya milango ya kambi ya Haji, mwanamke mmoja anasubiri. Anatuambia ana visa halali lakini ya dada yake imeisha.
Dada yake sasa anashikiliwa ndani ya kambi hiyo, pamoja na watoto wake. Maafisa hawakumruhusu kutembelea familia yake, na anahofia kuwa watafukuzwa.
Anaanza kulia, "Kama nchi yangu ingekuwa salama, kwa nini nije hapa Pakistan?
Na hata hapa hatuwezi kuishi kwa amani."
Anamwonyesha binti yake aliyeketi kwenye gari lao.
Alikuwa mwimbaji huko Afghanistan, ambapo sheria inasema wanawake hawapaswi kusikika wakizungumza nje ya nyumba zao, na kusema kuimba ni kinyume cha sheria.
Ninamgeukia binti yake na kumuuliza kama bado anaimba. Ananitazama. "Hapana."
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Ambia Hirsi